SEHEMU YA 14
Muda wa kula chakula cha jioni ulipofika, wote walikaa pamoja na kula huku wakifurahi ila baba yao alisema amechoka sana hivyo akawahi kwenda kulala kwahiyo sebleni alibaki mama na watoto wake akaanza kuongea nao,
“Eeeeh niambieni kwanza maisha ya kuishi wenyewe? Najua haijawahi kutokea ila kipindi hiki ilibidi tu wanangu kutokana na majukumu ya hapa na pale, eeeh niambieni”
Walikaa kimya kidogo basi mama yao akaanza,
“Niambie mwanangu Erica, maisha ya kuishi wenyewe uliyaonaje?”
“Mmmh yalikuwa magumu mama”
Erick nae akadakia,
“Yani mama, usiku tunalala kwa kunywa chai na mikate jamani!”
“Kheee Angel, kweli ulikuwa unawalaza wadogo zako kwa chai na mikate!”
“Mmmh mama jamani, mimi ni dada yao ndio ila sio kusema kuwa kila jukumu nitaweza maana mimi pia bado mdogo, hebu angalia niende shule, nirudi kupika, niwafulie, nilikuwa nachoka mama”
“Mmmh dada jamani, umetufulia mara moja tu”
“Na wewe Erick, kwani kufua hamjui hadi mummpe hilo jukumu dada yenu?”
“Hapana mama, alisema mwenyewe”
Mara simu ya Angel ilianza kuita pale, basi mama yake akaangalia na kukuta jina la mpigaji limetokea Hanifa, akampa Angel na kumwambia aongee nayo, basi Angel akaipokea na kutaka kuondoka pale ili akaongee nayo ila mama yake alimshika mkono na kumwambia,
“Kaa hapo uongee nayo”
Basi Angel hakuwa na namna zaidi ya kuongea na ile simu mbele ya mama yake,
“Jamani Angel, nimekusubiri leo hujatokea kwanini jamani!”
“Tulichelewa kutoka shule”
“Basi naomba kesho uje, nipo chini ya miguu yako”
“Sawa”
Angel akakata ile simu kisha mama yake akamuuliza,
“Ulikuwa ukiongea nae nini?”
“Hanifa hakuja shule leo, alikuwa anauliza tu kama tuliwahi kutoka au la!”
“Mbona mwishoni umemjibu sawa!”
“Kaniambia Jumatatu nisisahau madaftari nyumbani ili apitie tulichosoma”
“Kwahiyo kuna kipindi huwa unasahau daftari au kitu gani?”
“Hapana mama, ila kuna masomo huwa sitembei na daftari zake mara kwa mara”
“Angel, utaona mama yako nakufatilia sana ila nina maana kubwa sana, badae utashukuru na kuona ni vyema nilikuwa nakufatilia, naielewa dunia hii ilivyoharibika, yani wanaume wakiona mtoto mzuri kama wewe lazima mate yawadondoke, sitaki mjinga yoyote aharibu maisha yako”
Angel akawa anamuangalia tu mama yake ingawa kiukweli hakupenda vile ambavyo mama yake alikuwa akimchunga, basi mama yao aliwaangalia Erick na Erica na kuwaambia,
“Ninavyomchunga dada yanu ni sawa na nyie, kwanza nadhani sharia za nyumbani kwangu mnazifahamu, sitaki marafiki wa ajabu hapa nyumbani kwangu, yani kabla hujawa na rafiki ni lazima apitie kwangu nimkague kwanza na nimuhoji maswali, kama nitaridhika nae basi atakuwa rafiki yako, vinginevyo sitaki marafiki hapa kwangu. Nahitaji nyie ndio muwe marafiki, jambo likikutaziza, mwambie mwanafamilia hapa akusaidie, mpo watatu mnatosha kabisa”
Erica akauliza,
“Kwahiyo mama na wakina Junior je?”
“Sasa wale ni marafiki? Hebu kuweni na akili, wale ni ndugu zenu, yani hapa ni ndugu tu ujinga ujinga wa kuharibu wanangu siutaki, Erica sitaki marafiki wa ajabu ajabu, halafu sitaki kusikia kuna wanaume huko wanakuchanganya akili, Erick uwe mlinzi wa dada yako, nawe Erick sitaki marafiki wa ajabu, na maswala ya wanawake sitaki kuyasikia, kwahiyo Erica utakuwa mlinzi wa kaka yako. Halafu nyie wawili mtamlinda dada yenu Angel, yani sitaki kusikia ujinga wa aina yoyote ile. Nadhani mnanielewa!”
“Tumekuelewa mama”
Walijibu kwa pamoja kisha mama yao akawaruhusu kwenda kulala.