Simulizi: Namtaka mpenzi wangu arudi

Simulizi: Namtaka mpenzi wangu arudi

SEHEMU YA 08

Hilo halikuwa tatizo, baada ya siku mbili wakarudi nchini Tanzania na hivyo kushiriki katika mkutano huo. Hakuwa na maisha ya wokovu lakini alipenda sana kusikiliza mahubiri. Kila alipokuwa akipata nafasi ilikuwa ni lazima kusikiliza mahubiri mbalimbali huku naye akimuomba Mungu kwamba siku moja baadaye aje kuwa mhubiri mkubwa kama alivyokuwa Benny Hinn.

Japokuwa alipenda sana dini na mahubiri lakini pia Dickson alipenda sana wanawake. Kwake, wanawake walikuwa kila kitu, aliwapenda, alipokuwa akiwaona moyo wake ulifarijika mno.
Mpaka kumaliza kidato cha sita, alikuwa amekwishatembea na wanawake wengi. Alipendwa kwa kuwa alitoka katika familia ya kitajiri lakini mbali na utajiri huo, Dickson alikuwa na sura nzuri mno.

Wanawake walimbabaikia na wengi kumuita Trey Songz kwa kuwa tu alifanana na mwanamuziki huyo kutoka nchini Marekani. Kila msichana aliyekuwa akimuona, hakutaka kumpita Dickson pasipo kumsalimia, kwao, kijana huyo aliitetemesha mioyo yao na hivyo kujikuta akilala na wanawake wengi hata wale ambao hakuwa akiwafikiria kabisa.

Siku ya kwanza ya mkutano huo mkubwa wa injili alikwenda katika Viwanja vya Jangwani huku akiendesha gari la thamani aina ya BMW X6 ya bluu. Alipofika sehemu ya kuegesha magari, akalisimamisha na kuteremka.

Watu waliokuwa pembeni wakabaki wakiliangalia gari hilo. Lilikuwa zuri mno, wengi wakatamani kumuona mtu ambaye angeteremka humo kwani wengi walihisi kwamba angeteremka mtu mzima, mwenye kitambi huku mkononi akiwa na saa ya thamani ya Rolex.

Mlango ukafunguliwa na Dickson kuteremka. Alivalia suruali nyeusi, tai nyeusi na shati jeupe huku akiwa na miwani ya macho. Kila mtu aliyemwangalia kijana huyo, alichanganyikiwa, hawakuamini kumuona kijana aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa Dickson.
 
SEHEMU YA 09

Hakutaka kujali, aliwaona wanawake wengi wakimwangalia lakini akapiga hatua na kuingia katikatika ya umati wa watu na kutulia.

Mkononi mwake alikuwa na Biblia yake, hakutaka kuzungumza na mtu yeyote, mahali hapo, alikuja kwa lengo moja la kumuabudu Mungu, hakufikiria kumfuata msichana yeyote yule japokuwa wakati mwingine moyo wake ulikuwa ukipambana vikali kumkumbusha kwamba alikuwa mkutanoni wakati macho yake yalipotua kwa wanawake warembo.

Baada ya dakika kadhaa, mkutano ukaanza rasmi. Aliyatafakari maisha yake, alijua jinsi alivyokuwa akimchukiza Mungu. Maisha yake yaliteswa na dhambi moja tu ya uzinzi ambayo ilimng’ang’ania kupita kawaida.

Alipambana na dhambi nyingine nyingi, alizishinda lakini dhambi hiyo ya uzinzi haikumuacha hata kidogo. Ilimtesa, kila alipotaka kuyabadilisha maisha yake, alianguka mara baada ya kumuona msichana mrembo.

Siku hiyo alifikiria mambo mengi, alimuomba Mungu msamaha, alihitaji kuwa msafi, hakupenda kuishi katika maisha aliyokuwa akiishi kwa sababu tu alihitaji mabadiliko kwa nguvu zote.

Aliyafumba macho yake, alikiinamisha kichwa chake chini huku akiendelea kumtafakari Mungu na maisha aliyokuwa amepitia mpaka kufikia siku hiyo. Wakati akiwa amekiinamisha kichwa chake, akasikia sauti nzuri kutoka jukwaani.

Sauti ile iliposikika tu, moyo wake ukamlipuka, akakaza moyo wake, hakutaka kuuinua uso wake kuangalia kule jukwaani ili kuona ni msichana gani aliyeitoa sauti hiyo na kuanza kuimba nyimbo za kuabudu.

Moyo wake ukashindana na akili yake. Akili ilimwambia auinue uso wake na kuyafumbua macho yake kumwangalia msichana huyo ila moyo wake ilimwambia kwamba hakutakiwa kufanya hivyo, huo ulikuwa ni muda wa kumfikiria Mungu na hivyo alitakiwa kutulia.

“Haiwezekani!” alisema na kuuinua uso wake.
Macho yake akayapeleka jukwaani, alimuona Nandy akiwa amesimama na waimbaji wengine huku akiwa ameshika kinasa sauti akiendelea kuimba. Hakumuomba vizuri kutokana na umbali aliokuwepo.

Alichokifanya Dickson ni kuanza kusogea kule karibu ya jukwaa kwa lengo la kumwangalia msichana huyo. Alipenyapenya kwa watu mpaka kufika mbele kabisa na kuanza kumwangalia nandy.
 
SEHEMU YA 10

Mbali na sauti aliyokuwa nayo, Nandy alikuwa msichana mwenye sura nzuri kupita kawaida. Dickson akajisahau kabisa kama alikuwa kwenye mkutano wa injili, akatulia na kumwangalia Nandy vizuri, sura yake ilimdatisha kupita kawaida.

“Ni msichana wa aina gani huyu?” alijiuliza huku akimwangalia Nandy ambaye alikuwa bize kumuimbia Mungu wake.

Hakutaka kuondoka mahali hapo, alibaki akiwa amesimama huku akimwangalia msichana huyo. Kichwa chake kilichanganyikiwa, kwa Nandy, hakuonekana kuwa msichana wa kumchezea na kumuacha, kichwani mwake kulikuwa na taswira ya kumuoa msichana huyo lakini si kutembea naye na kumuacha kama ilivyokuwa kwa wasichana wengine.

Mpaka Nandy anamaliza kuimba na kuteremka jukwaani, Dickson alikuwa akimwangalia. Alitembea kwa mwendo wa taratibu mpaka katika sehemu iliyoonekana kuwa maalumu kwa ajili ya waimbaji na kukaa.

Dickson alishindwa kuvumilia, hakutaka kuona akimkosa msichana huyo, alitokea kumpenda na siku hiyo ya kwanza kumuona alitamani sana kuongea naye japo kidogo.

Mkutano ulipokwisha, akasubiri, hakutaka kuondoka. Wasichana wengi walikuwa wakimwangalia, alikuwa mzuri wa sura na kila mmoja alitamani hata kuzungumza naye lakini Dickson hakutaka kuwa na habari nao, mawazo na akili yake ilikuwa kwa Nandy tu.

Alisubiri mpaka alipomuona msichana huyo yupo peke yake akipanga vitu vizuri. Kigiza kilianza kuingia, hakutaka kubaki alipokuwa, alichokifanya ni kuelekea kule Nandy alipokuwa na kumsalimia.

Kwa jinsi msichana huyo alivyoitikia, ilionyesha kabisa kwamba hakupenda kufuatwa na kusalimiwa. Akazugazuga kwa kumsifia, alipoona haeleweki akaondoka zake kuelekea garini.
“Kesho nitamfuata tena! Mpaka atanizoea tu,” alisema Dickson na kuingia garini.

Akili yake ni kama ilivurugwa, alichanganyikiwa, hakuamini kama kitendo chake cha kwenda katika mkutano ule basi angekutana na msichana mrembo kama alivyokuwa Nandy.

Alipofika nyumbani, akili yake haikuweza kutulia, alikaa chumbani huku akimfikiria Nandy kupita kawaida. Alitamani kumuona msichana huyo kwa mara nyingine, alitamani kusimama mbele yake na kuongea naye tena.
 
SEHEMU YA 11

Usiku huo ukawa wa mateso makubwa, hakula chakula chochote zaidi ya kunywa juisi tu na kulala. Asubuhi alipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumfikiria Nandy, sauti yake ilimpagawisha kupita kawaida.

Mbele yake akaanza kuona ndoto ya kuwa na msichana huyo, akaona wakiwa kanisani wakifunga ndoa na hatimaye kuwa mke na mume.

Mchana ulipofika, hakutaka kuchelewa, akaondoka na gari lake kuelekea mkutanoni. Bado wanawake waliokuwa wakimuona walishangazwa, sura yake ilimpagawisha kila mwanamke aliyekuwa akimwangalia.

Wengi wakatamani kuwa naye, wengi wakatamani kumfuata na kupiga naye stori lakini mwenzao hakuwa na mawazo nao hata kidogo, moyoni mwake kulikuwa na msichana mmoja tu, Nandy.

Dickson hakutaka kukaa nyuma, siku hiyo alitaka kumuona Nandy vizuri kabisa. Mkutano haukuwa umeanza, wasichana mbalimbali walikuwa wakiandaa viti vya watumishi wa Mungu akiwemo Nandy aliyeonekana kuwa bize hasa.

Alipomuona, mapigo yake ya moyo yakaanza kwenda kasi, siku hiyo Nandy alionekana kuwa mrembo zaidi ya jana, alionekana kuwa mrembo zaidi ya malaika. Hakukubali kuona akisimama tu pasipo kumfuata msichana huyo na kumsalimia kwani usiku uliopita, ndiye mtu pekee aliyekuwa amekisumbua kichwa chake kupita kawaida. Akaanza kumsogelea.

“Bwana Yesu asifiwe,” alimsalimia mara baada ya kumfikia. Nandy akageuka na kumwangalia.
“Amen!”
“Za tangu jana?” aliuliza Dickson, Nandy akajifanya kama kufikiria hiyo jana yake kama aliwahi kukutana na kijana huyo.
“Tangu jana?”

“Ndiyo! Nilikufuata kukusalimia na kumpa Mungu sifa zake kwa kukupa sauti nzuri,” alisema Dickson.
“Ooh! Ni nzuri tu mtumishi wa Mungu!” alisema Nandy na kuendelea na kazi yake.

“Basi sawa. Naona tumerudi kumuabudu Mungu! Leo nitakaa hapa mbele, nataka utukufu wa Mungu utakapoanza kushuka, na mimi niupate wa kwanzakwanza,” alisema Dickson na kutoa tabasamu, maneno yake yakamfanya hata Nandy kutabasamu.
“Haina shida.”
 
SEHEMU YA 12

Dickson akakaa katika kiti cha mbele kabisa huku akimwangalia Nandy ambaye alikuwa bize kufanya usafi. Alikwishaisoma akili ya msichana huyo, hakuonekana kuwa kama wasichana ambao aliwahi kutembea nao kipindi cha nyuma, Nandy alionekana msichana mwenye ari ya kumtumikia Mungu na hivyo hata kama angemwambia kwamba alikuwa akimpenda, alitakiwa kutumia lugha fulani ya kibiblia.

Akakaa kwenye kiti na kuchukua Biblia na kuanza kusoma. Yote hayo ilikuwa ni kumfanya Nady amuone kwamba naye alikuwa bize na Mungu wake. Muda mwingine alikuwa akiifunika na kuanza kumuomba Mungu.

Nandy aliyekuwa pembeni alikuwa akimwangalia kijana huyo. Kwake, alimshangaa, Dickson alikuwa na sura nzuri, alishangaa sana kumuona kijana kama huyo akimuabudu Mungu kwani vijana wengi waliokuwa katika umri wake, uzuri wake walikuwa wakiutumia kwa ajili ya kufanya kazi za kishetani tu likiwemo la kutembea na wanawake wengi.

Kwake, Dickson akaonekana kuwa mwanaume mzuri na mwenye utii hata mbele za Mungu. Alifanya kazi yake lakini naye bado kichwa chake kiliendelea kujiuliza kuhusu kijana huyo.

Alipomaliza, akaelekea chini ya jukwaa na kuanza kubadilisha nguo zake na wasichana wengine. Aliishangaa akili yake, haikufikiria kitu kingine zaidi ya kijana yule aliyekuwa amekutana naye kipindi kifupi nyuma.

Alishangaa, alimuomba Mungu amuondolee mawazo juu ya Dickson lakini hayakutoka kabisa. Alimganda akilini mwake, alichukia na wakati mwingine kuuma meno yake kwa hasira lakini Dickson hakuweza kutoka kichwani mwake.

“Mungu! Ni nini hiki? Mbona shetani anaamua kunijaribu hivi,” aliuliza Nandy huku akianza kujiimbia nyimbo mbalimbali lakini bado Dickson aliendelea kung’ang’ania kichwani mwake.
 
SEHEMU YA 13

Alipomaliza kuvaa, akatoka chini ya jukwaa na kuelekea kule walipokuwa wakikaa waimbaji. Macho yake yalikuwa yakimwangalia Dickson kwa siri, akahisi kabisa moyo wake ukianza kubadilika na upendo fulani wa ajabu ukianza kuingia moyoni mwake.

“Nandy!” aliita rafiki yake, Nandy akashtuka kama mtu aliyekuwa kwenye lindi la mawazo.
“Abeee!”
“Umemsikia mchungaji, anakuita,” alisema rafiki yake huyo.

Mawazo yake hayakuwa mkutanoni hapo, alikuwa akimwangalia Dickson na kujisahau kabisa. Haraka sana akainuka na kuanza kuelekea jukwaani. Watu wote wakaanza kushangilia akiwemo Dickson mwenyewe.

“Naomba tusimame na tutulie mbele za Mungu aliye hai,” alisema Nandy, watu wote wakasimama akiwemo Dickson ambaye macho yake hayakutulia sehemu moja, mara kwa mara alikuwa akimwangalia Nandy, na msichana huyo, mara kwa mara alikuwa akiyapitisha macho yake kwa Dickson.

“Mungu, naomba uniondolee jaribu hili, naomba umtoe kijana huyu akilini mwangu,” aliomba Nandy kimoyomoyo.
“Mungu, huyu ndiye mwanamke sahihi, naomba unipe nafasi ya kuwa naye katika maisha yangu yote,” naye Dickson aliomba.

Kukawa kama na nguvu mbili zikawa zinashindana.

JE, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 14

Kila siku wawili hao walikuwa wakikutana mkutanoni na kuzungumza kidogo kisha kuondoka. Moyo wa Dickson bado ulikuwa na uhitaji mkubwa wa kuwa na msichana huyo huku kila siku naye Nandy akimuomba Mungu ili amuondoe Dickson katika kichwa chake.

Siku zikaendelea kukatika mpaka mkutano ulipokwisha. Alichokifanya Dickson ni kumuuliza Nandy kanisa alilokuwa akisali kwa lengo la kwenda huko na kuungana naye mara moja moja.
Hilo halikuwa tatizo, akamwambia na Jumapili iliyofuata alikuwa kanisani humo akimwabudu Mungu. Bado sauti ya Nandy ilikuwa gumzo kubwa, kila mtu alikuwa akishangaa, msichana huyo alikuwa na karama ya uimbaji ambapo kila alipokuwa akisimama na kuimba, kila mtu alihisi kabisa kwamba Mungu alikuwa akimtumia katika karama yake hiyo.

Wakaendelea kuwasiliana kila walipokuwa wakikutana kanisani na hatimaye wawili hao wakawa marafiki wakubwa. Huyo ndiye akawa mvulana wa kwanza kuwa karibu naye kitu ambacho kilimfanya hata yeye mwenyewe kushangaa kwani hakuwahi kuwa karibu na mvulana yeyote zaidi ya huyo.

Baba yake hakuacha kumuonya, kila siku alimwambia mambo mengi kuhusu wanaume, aliwaambia jinsi walivyokuwa wakiwanyanyasa wanawake, alifanya hivyo kwa kuwa hakutaka kumuona binti yake akiingia kwenye uhusiano wa kimapenzi lakini la kushangaza, katika kipindi hicho akili yake haikutaka kabisa kukubaliana na maneno ya baba yake.
Alimuona Dickson kuwa mwanaume wa tofauti na wale ambao kila siku baba yake alikuwa akiwazungumzia, kwake,

Dickson alikuwa na sura ya upole kuliko mwanaume yeyote katika ulimwengu huu, hakutaka kuona akimpoteza mwanaume huyo, alihitaji ukaribu huo uendelee pasipo kuambiana kwamba walikuwa wakipendana.

Kila alipokuwa na kijana huyo, moyo wake ulijisikia tofauti kabisa, alipokuwa akikwazwa na kukutana na Dickson, alihisi mabadiliko makubwa moyoni mwake, akahisi tumaini, upendo mkubwa kuliko kitu chochote kile.

Wakati yeye akiendelea kuteseka, Dickson alikuwa akijipanga, hakutaka kumkosa msichana huyo, kwake, Nandy alikuwa kila kitu katika maisha yake na alikuwa tayari kufanya jambo lolote lile lakini si kumkosa.
 
SEHEMU YA 15

Akaamua kuachana na wanawake wake na kuamua kubaki na Nandy ambaye mpaka muda huo hakuwa amemwambia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.

Kila alipotaka kumwambia, aliogopa, hakutaka kumpoteza, kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akimuimbia Mungu, jinsi alivyokuwa akisali aliamini kabisa kwamba kama angemwambia kuhusu mambo ya mapenzi basi huo ungeweza kuwa mwisho wa urafiki wao.

“Nifanye nini? Ngoja nimtoe out, nadhani huko nitamwambia kila kitu,” alisema Dickson.
Hakutaka kuchelewa wala kukaa na jambo hilo moyoni mwake, alichokifanya mara baada ya kukutana na Nandy ni kumwambia kuhusu mtoko huo. Nandy aliposikia, akajifanya kushtuka, alitamani sana kutoka mtoko na kijana huyo lakini aliogopa ni kwa jinsi gani angeweza kumwambia.

Hakutaka kuonekana akifurahia na ndiyo maana akajifanya kushtuka kana kwamba kile alichokuwa ameambiwa kilikuwa kimemshtua mno. Hakukubali, alimkumbuka baba yake, maneno yake aliyokuwa akimwambia kuhusu wanaume yakaanza kujirudia kichwani mwake.
“Hapana! Siwezi,” alisema Nandy huku akionekana kuogopa.

“Nandy! Kwani ukitoka na mimi kuna tatizo?”
“Una uhakika kwamba utakuwa ni mtoko tu?” aliuliza Nandy.
“Ndiyo! Ni mtoko tu!”
“Kweli?”
”Naomba uniamini!”
“Hakuna kingine?”
“Wala hakuna!”

”Basi sawa. Kamwambie baba yangu anipe ruhusa,” alisema Nandy maneno yaliyomshtua Dickson.
“Nikamwambie baba yako?”
“Ndiyo!”
“Mmh! Siwezi!”
“Basi haitowezekana Dickson. Siwezi kutoka pasipo baba yangu kujua nilipo,” alisema Nandy.

Huo ulikuwa mtihani mzito kwa Dickson, hakutaka kumfuata baba yake Nandy kwani aliamini ni lazima mzee huyo angefikiria vibaya na hivyo kumwambia aachane na binti yake.
Moyo wake ukanyong’onyea, akaamua kuachana na jambo hilo na kufanya mambo mengine.

Aliendelea kukutana na Nandy kanisani, wakawa wanazungumza na kuondoka kuelekea majumbani kwao.
Nandy hakuwa na simu, walipokuwa wakiachana, hawakuwa wakiwasiliana mpaka Jumapili inayofuata.

Dickson alijaribu mara nyingi kumpa Nandy simu lakini msichana huyo hakuipokea, aliogopa, hakujua baba yake angemfikiria vipi kwani ni lazima angeulizwa maswali mengi kuhusu simu hiyo kitu ambacho kingemfanya kuonekana kuanza uhuni.
 
SEHEMU YA 16

Siku ziliendelea kwenda mbele, baada ya mwezi kukatika, Dickson hakutaka kuvumilia, akajipanga kwa lengo la kwenda kuonana na mzee Gwamaka na kumuomba ruhusa ya kumtoa Nandy mtoko.

Alikuwa akihofu moyoni mwake, hakujua kama angekubalika au kukataliwa, akapiga moyo konde na kuelekea nyumbani kwa mzee huyo. Kwa kuwa mara moja moja alikuwa akionekana kanisa, mzee Gwamaka alimzoea kidogo japokuwa ukaribu wake na Nandy ulimtia hofu kidogo.

Alipokaribishwa, akakaa kwenye kochi lililochakaa sebuleni. Akaanza kuiangalia nyumba ya kina Nandy, hakuamini kama kweli msichana aliyekuwa akimpenda, msichana aliyeyatoa maisha yake alikuwa akiishi katika nyumba kama hiyo.

Msichana mzuri kama Nandy hakutakiwa kuishi ndani ya nyumba hiyo, uzuri wake ulistahili kukaa sehemu kama Osterbay au hata Masaki lakini si hapo Kurasini tena kwenye nyumba mbovu kama hiyo.
Nandy aliogopa, mara baada ya kumkaribisha Dickson nyumbani hapo, hakutaka kukaa sebuleni, akaondoka na kuelekea chumbani kwake huku mapigo ya moyo yakimdunda kupita kawaida.

Huko, alikuwa akimuomba Mungu, alitamani mno baba yake akubaliane na Dickson na hatimaye watoke wote mtoko kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa naye karibu na aliyempenda kwa moyo wote kama kijana huyo.

Mzee Gwamaka akakaa na Dickson sebuleni, alimwangalia kijana huyo, hakuonekana kujiamini, moyo wake ulijawa hofu na muda mwingi alikuwa akimwangalia mzee huyo huku akionekana kujishtukia kupita kawaida.

“Karibu sana,” alisema mzee Gwamaka.
“Nashukuru sana!” alisema Dickson.
Wakaanza mazungumzo yao. Dickson hakutaka kumwambia mzee Gwamaka kile kilichokuwa kimemleta mahali hapo, kwanza akaanza kuzungumza naye kuhusu mahubiri ya wachungaji mbalimbali, jinsi Mungu alivyokuwa akifanya miujiza kupitia wao.

Walizungumza kuhusu ibada na hata mikutano ya injili iliyokuwa ikiendelea duniani, Dickson alitaka kuonekana kwamba alifuatilia sana mahubiri hivyo kumwambia mzee huyo kuhusu wahubiri wengi na waimbaji duniani kama Kirk Franklin, Don Moen, kundi la Hillsong kitu kilichomfanya kidogo mzee huyo kuridhika.
 
SEHEMU YA 17

“Ila pamoja na hayo yote, nimekuja kumuombea ruhusa Nandy,” alisema Dickson huku akimwangalia mzee huyo.
“Ruhusa?”
“Ndiyo!”
“Ruhusa ya nini?”

“Kutakuwa na kisherehe kidogo nyumbani, ninakwenda kuanza chuo, nimefaulu vizuri hivyo wazazi wanataka kunifanyia sherehe,” alisema Dickson.
“Kwa hiyo inahusiana vipi na Nandy?”
“Nataka ahudhurie sherehe hiyo kwa kuwa amekuwa rafiki yangu mkubwa,” alisema Dickson, mzee Gwamaka akashtuka, akamwangalia vizuri kijana huyo.

“Yaani Nandy atoke hapa, aende huko kwenu halafu arudi usiku?” aliuliza mzee huyo.
“Hapana! Itakuwa mwisho saa kumi na mbili!”
“Kijana unamchezea simba sharubu!” alisema mzee huyo.

“Mzee! Naomba uniamini na mimi nitautunza uaminifu wangu kwako. Ni ruhusa ya sherehe, hakuna kingine. Mimi si kijana mbaya kama unavyojifikiria, nimekuja kwako kuomba ruhusa kwa kuwa ninajua thamani ya wazazi, nakuahidi mzee wangu hakuna kitu chochote kibaya ambacho kitatokea,” alisema Dickson.
Siku hiyo Dickson alikuwa mnyenyekevu kuliko siku zote alizowahi kuishi katika dunia hii. Alimuomba sana mzee Gwamaka na hatimaye akakubaliana naye kwa ahadi ya kumrudisha saa kumi na mbili kama alivyokuwa amemuahidi na la zaidi, alimwambia kuwa asithubutu kumvua nguo.

“Sitoweza kufanya hivyo mzee wangu!”
“Basi ruksa umepata.”
Moyo wa Dickson ukawa na furaha tele, hakuamini kama angekubaliwa na mzee huyo kumtoa mtoko Nandy. Hakukuwa na sherehe yoyote ile bali kitu alichokitaka ni kuwa karibu na msichana huyo tu.
Alipoondoka, Nandy ndiye aliyemsindikiza, njiani, alimwambia jinsi baba yake alivyokubali kutoka naye. Nandy akafurahi kwani hata kule chumbani alipokuwa, alimuomba Mungu azungumze na baba yake na hatimaye kutoka na mvulana huyo.

Siku iliyofuata, wawili hao walikuwa katika bwawa la kuogelea katika Hoteli ya Cassanova iliyokuwa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Kwa Nandy, kila kitu alichokuwa akikiona katika hoteli hiyo alikuwa akishangaa, hakuamini kama kulikuwa na watu walikuwa wakila starehe kama ilivyokuwa kwa watu aliokutana nao ndani ya eneo la hoteli hiyo.
 
SEHEMU YA 18

Dickson hakutaka kukaa mbali na Nandy, ilikuwa ni kama alihisi kuwa angeibiwa msichana huyo. Muda wote alikuwa pamoja naye, alipokwenda kwenye bwawa la kuogelea, alihakikisha anakuwa naye na hata alipotoka, alikaa naye sehemu na kuzungumza naye.

Mpaka muda huo hakuwa ameufumbua mdomo wake kumwambia jinsi alivyojisikia moyoni mwake, alikuwa akifikiria ni kwa jinsi gani angeweza kumwambia msichana huyo na hatimaye akubaliane naye na kuingia katika uhusiano wa kimapenzi.
Waliendelea kula raha mpaka majira ya saa kumi na moja ambapo wakatoka na kuingia ndani ya gari.

Humo, bado Dickson alikuwa akijiuliza kama muda huo ulikuwa sahihi kumwambia ukweli au raha.
Kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akimuimbia Mungu na kumuabudu, moyoni mwake alihisi kabisa kwamba angemkatalia kile alichokuwa akikitaka na mwisho wa siku kuingia katika ugomvi mzito.

Akanyamaza siku hiyo, alimrudisha kwao na kurudi nyumbani. Hakuzuiliwa kufika nyumbani hapo, siku iliyofuata akarudi na kuanza kuzungumza naye.

Mzee Gwamaka aliridhia kila kitu, japokuwa alimwambia binti yake kuhusu wanaume lakini kwa Dickson ilionekana kugonga mwamba. Kijana huyo alikuwa akimfuata Nandy kwa staili ambayo hata yeye mwenyewe hakuwahi kuifikiria, alimfuata kwa unyenyekevu huku muda mwingi alipokuwa akiongea alilitaja jina la Yesu, yote hayo ilikuwa ni kuendana na mazingira ya msichana huyo aliyokuwa akiishi.

“Nandy! Kuna jambo moja muhimu sana ningependa kukwambia,” alisema Dickson huku akimwangalia Nandy usoni, uzuri wake ulizidi kuonekana.
“Jambo gani?” aliuliza.

Dickson akanyamaza kwanza. Hakujua ni kwa jinsi gani angechukuliwa mara baada ya kumwambia Nandy ukweli, akawa kama mtu aliyekuwa akijifikiria kitu fulani, alipoona kuwa Nandy alinyamaza kumsikiliza, akapiga moyo konde.

“Ninakupenda Nandy,” alisema Dickson huku kwa mbali akionekana kuweweseka.
“Unanipenda mimi?” aliuliza Nandy huku akijifanya kushtushwa, akakunja ndita kidogo, hiyo ikamuogopesha Dickson.
“No! Simaanishi unachokifikiria!

Namaanisha upendo wa Agape, kama Yesu aliowapenda wanafunzi wake,” alisema Dickson, alibadilika haraka sana kwani alihisi kwamba Nandy alikuwa amechukizwa na kile alichomwambia.
 
SEHEMU YA 19

“Kweli?”
“Ndiyo Nandy!”
“Si upendo kama ule wa Romeo aliompenda Juliet?” aliuliza Nandy.
“Nandy! Unajua...daah! Yaani sijui niseme nini...”
“Sema chochote kile, nakusikiliza.”
“Nakupenda sana.”
“Mara ya pili hiyo unaniambia!”
“Najua! Ila naomba uniamini, ninahitaji kukuoa!”

“Kunioa mimi?”
“Ndiyo! Nahitaji kukuoa wewe.”
“Kwa hiyo huo ni upendo wa Yesu aliowapenda wanafunzi wake au mwingine?”
“Nadhani huu ni wa Romeo aliompenda Juliet,” alisema Dickson na wote kuanza kucheka.
Siku hiyo wawili hao wakaingia katika uhusiano wa kimapenzi. Moyo wa Dickson ulikuwa na furaha tele, kwake, kitendo cha kuwa na msichana huyo alihisi maisha yake yakianza kukamilika tofauti na jinsi alivyokuwa kipindi cha nyuma.

Mapenzi yao yakaanza kuwa siri kubwa, waliogopa watu kufahamu kilichokuwa kikiendelea kwa kuwa kanisani msichana huyo alikuwa akiheshimika mno.
Walikuwa pamoja, na mara baada ya kuzoeana sana, ikambidi Dickson amuombe ruhusa mzee Gwamaka kwa ajili ya kumnunulia simu msichana huyo.
 
SEHEMU YA 20

Mzee Gwamaka alikataa, alizijua simu, zilikuwa na matatizo mengi, hakutaka binti yake aharibiwe na ulimwengu wa teknolojia, alimwambia Dickson kwamba jambo hilo halikuwezekana, hakutakiwa kumnunulia simu Nandy.

Waliishi hivyohivyo mpaka matokeo ya kidato cha nne yalipotoka, Nandy alifaulu vizuri na hatimaye kujiunga na Shule ya Sekondari ya Benjamini jijini Dar es Salaam huku Dickson akianza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua utabibu.

Shuleni, Nandy alikuwa mwiba mkali kwa wasichana waliojiona keki shuleni hapo. Alikuwa msichana mwenye uzuri wa ajabu ambapo kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia, alimpenda, gumzo kubwa kwa kila mtu shuleni hapo ulikuwa ni uzri wa Nandy tu.

Wanaume hawakutaka kuwa na subira, walichokifanya ni kuanza kumfuatilia kwa lengo la kumtia mikononi mwao lakini kwa Nandy, lilikuwa jambo gumu kumkubali mwanaume yeyote yule kimapenzi.

“Jamani yule demu mkali mno, ila naye mgumu kama nondo,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Nandy.

“Watu wamemfuata lakini wapi. Ana sauti nzuri ya kumtoa nyoka pangoni lakini ni mgumu sana, hivi kuna mtu anaweza kumpata yule?” aliuliza jamaa mwingine.

“Sidhani! Ila tupambaneni, mwenzenu mimi huwa siamini kama kuna demu mgumu, watu wanazaa na malkia anayewaongoza ndiyo sembuse yeye! Tuweni bize naye tu,” alisema jamaa mwingine.

Je, nini kitaendelea?
 
nzuri sana, I can't wait for another episode
 
SEHEMU YA 21

Miongoni mwa wasichana aliowahi kutembea nao Dickson alikuwa Linda Fabian. Huyu alikuwa msichana mrembo aliyekuwa akisomea sheria nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Oxford.
Linda alikuwa miongoni mwa wasichana warembo ambao walitoka kimapenzi na Dickson. Katika kipindi ambacho wawili hao walikuwa pamoja walipeana ahadi nyingi za kuwa pamoja mpaka kuja kuoana.

Kwa mapenzi motomoto ambayo Linda alipewa na Dickson, moyo wake ulichanganyikiwa na kuona kuwa katika dunia nzima hakukuwa na mwanamke mzuri kama alivyokuwa.

Dickson hakuwa na mapenzi naye, alimuonyeshea kwa kuwa aligundua kwamba msichana huyo alichanganyikiwa kwake. Walikuwa pamoja, walifanya mambo mengi pamoja na hata wakati mwingine kwenda kutembea nje ya nchi.
Walipendana, kila mtu aliyekuwa akiwaangalia aliona kabisa kwamba wawili hao wangekuwa pamoja siku moja na kutengeneza familia pamoja.

Linda alichanganyikiwa, akawaambia wazazi wake kuhusu Dickson kitu ambacho kwa kijana huyo hakupenda kabisa kuona kikitokea.
Penzi likawa wazi lakini bado Dickson alikuwa mtu wa wanawake, hakuwahi kupenda kwa moyo wa dhati, hakuwahi kumwambia mwanamke kwamba alikuwa akimpenda kutoka moyoni mwake.

Kwa uzuri wa sura aliokuwanao aliamini kwamba wanawake walimpenda wao wenyewe na kutaka kulala naye. Hakuwahi kutongoza, wanawake wote aliowahi kulala nao katika maisha yake akiwemo Linda walikuwa wakimtongoza yeye.

Alitembea na wanawake wengi, watoto wa kishua wenzake lakini mtu aliyekuwa karibu naye zaidi alikuwa Linda tu ambaye alimganda kama ruba.

Siku zikaendelea kukatika mpaka siku ambayo Linda alihisi hali ya tofauti mwilini mwake na alipokwenda kupima, akagundua kwamba alikuwa na mimba. Hilo lilimtisha,hakutaka kufanya siri, akamwambia Dickson ambaye aliruka kama ndege na kumwambia kwamba mimba haikuwa yake.

“Kumbe ni ya nani?” aliuliza Linda, kwa jinsi Dickson alivyokuwa amebadilika, hakuamini macho yake.
“Sijajua! Labda ya mwingine, huwezi kujua,” alisema Dickson.
“Kwa hiyo nilitembea na mwanaume mwingine?”
 
SEHEMU YA 22

“Kwani mimba mpaka utembee na mwanaume, hujawahi kusikia mimba inayopatikana kwenye bwawa la kuogelea? Linda, mara ya mwisho nilikuuliza kama upo kwenye siku za hatari, unakumbuka ulinijibu nini?” aliuliza Dickson.

“Kwamba sikuwa kwenye siku za hatari!” “Sasa mimba imeingiaje?”
“Dickson, sikujua kama mzunguko wangu ulibadilika,” alisema Linda.
Dickson hakutaka kukubali, hakutaka kuitwa baba kwa msichana ambaye hakuwa na ndoto zake. Wakaingia kwenye mtafaruku wa kimapenzi na baada ya kuona kuwa mwanaume huyo ameweka vikwazo, akaamua kuitoa mimba hiyo.

Moyo wa Linda ulimuuma lakini hakuwa na jinsi. Uhusiano uliendelea lakini Dickson hakuwa mtu wa kueleweka tena, wakawa kama marafiki, hakuwa mtu wa kumpigia simu Linda na kumjulia hali, kwake, hakutaka kabisa kuwa na mapenzi na msichana huyo.

Maisha yaliendelea kama kawaida mpaka Linda alipoamua kuondoka na kuelekea nchini Uingereza kusoma. Kwake, Dickson alikuwa kila kitu, hakutaka kuona akimpoteza mwanaume huyo, japokuwa aliona kabisa hapendwi lakini moyo wake uliamini kitu kimoja tu kwamba kuna siku angekuja kuwa na mwanaume huyo.

Aliendelea kusoma huku akiweka mipango yake ya muda mrefu, kwa kuwa alipokuwa akiingia mwaka wa tatu chuoni ndiyo kwanza Dickson alikuwa akianza mwaka wa kwanza jijini Dar, akaamua kutulia na kuisubiria siku ambayo aliamini kwamba mwanaume huyo angeukunjua moyo wake na kuwa naye tena.

Hakuacha kuwasiliana naye, alihakikisha anachati naye katika mitandao ya kijamii na hata kumpigia simu. Dickson hakumpenda Linda, alijitahidi kumnyamazia lakini msichana huyo hakukoma, bado imani yake ilimwambia kwamba kuna siku angekuwa na kijana huyo.

“Nimekukumbuka sana Dickson,” alisema Linda kwenye simu.
“Nashukuru sana!”
“Hivi bado unanipenda?”
“Nani? Mimi? Mbona umeniuliza hivyo?”
“Kwa kuwa nataka kujua!”

“Jamani! Sidhani kama unatakiwa kuniuliza hilo swali kwa kuwa ukweli unaujua!”
“Upi?”
“Linda! Hebu niambie, masomo yanasemaje huko?”
 
SEHEMU YA 23

Hakumpenda Linda lakini hakutaka kumwambia ukweli kwa kuwa hakupenda kumuona msichana huyo akilia mbele yake. Alitoa mimba yake kitu kilichomfanya kuamini kwamba kama angediriki kumwambia ukweli kuwa hakutaka kuwa naye basi ingekuwa balaa.
Wakati ambao Linda alikuwa akilazimisha penzi kutoka kwa Dickson ndicho kipindi ambacho kijana huyo alikuwa beneti na Nandy.

Bado maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Nandy na Dickson walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi lakini kipindi chote hicho hawakuwa wamefanya mapenzi.
Hilo halikumfanya Dickson kuumia, kwake, aliamini kwamba kuna siku Nandy angekuwa mke wake wa ndoa.

Waliendelea kuwasiliana, kila mmoja alimwambia mwenzake kwamba angekuwa mwaminifu mpaka pale ambapo wangekuja kufunga ndoa kanisani.
Hakuacha kwenda nyumbani kwa binti huyo na kuzungumza naye, aliendelea kumsisitizia upendo wa dhati uliokuwa moyoni mwake.

Baada ya Nandy kuingia kidato cha sita, Dickson akamwambia jinsi alivyokuwa akijisikia mwilini mwake. Hakutaka kufanya mapenzi na msichana yeyote yule, mtu pekee ambaye alitamani sana maishani mwake kufanya naye mapenzi alikuwa Nandy tu.

Akamwambia, msichana huyo alianza kukataakataa lakini mwisho wa siku walikuwa chumbani, kitandani huku wakiwa watupu kabisa na kuanza kufanya mapenzi.

Yalikuwa ni maumivu makali kwa Nandy, hakuwahi kukutana na mwanaume kimwili, siku hiyo hakusikia raha yoyote zaidi ya maumivu tu.

Dickson akampoza na kumwambia kwamba angezoea, na walipoendelea kufanya, Nandy akazoea, akachanganyikiwa mno kiasi kwamba hakuona kama duniani kulikuwa na wanaume wengine zaidi ya Dickson.

Siku zikaendelea kukatika mpaka Nandy alipokuja kumaliza masomo yake ya kidato cha sita na hatimaye kusubiri matokeo na kuona kama alistahili kujiunga na chuo au la.

Hapo, Dickson akamfuata tena mzee Gwamaka na kumuomba ruhusa ya kumnunulia simu Nandy, kwa kipindi hicho mzee huyo hakutaka kukataa, akakubaliana naye na hivyo kumnunulia simu msichana huyo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom