Tupio la VII – Mama Mchungaji
Mama Mchugaji, kama watu walivyo zoea kumwita ingawaje yeye mwenyewe ndiye mchungaji wa Kanisa la ‘kilokole’ maeneo ya Kihonda Morogoro, alikuwa anasifika sana kwa huduma zake nzuri za maombezi. Kanisa lake lilijaa waumini wengi wanawake na wanaume kiasi.
Alikuwa ni msomi wa theolojia na mwenye nguvu katika huduma yake ya maombezi ambapo alikuwa akitoa watu mbalimbali mapepo na kufanya huduma za ufunguzi wa vifungo mbalimbali.
Ilikuwa siku ya Jumatano jioni, siku tatu baada ya kufanya maombi pale KKKT, ndipo tulipofika katika Kanisa la mama Mchungaji. Tukiwa pamoja na waumini wengine, na sisi wageni tukiwa tumekaribishwa kwenye viti vya mbele kabisa, ghafla mtoto Junior alianza kulia, alilia sana isivyo kawaida mara tu mama mchungaji alivyofika pale madhabahuni.
“Nikawa sina jinsi, ikanibidi nitoke nje kwa muda maana kelele zilikuwa zinaharibu utulivu uliokuwepo mle kanisani…” alisema Vailet.
“…Nilivyotoka naye nje ya kanisa tu Junior akaacha kulia, nikajuwa labda nilivyo mbembeleza ndio ametulia hivyo nikarudi ndani ya kanisa na kuketi kwenye kiti changu cha awali…”
“Junior alivyo angalia mbele tu pale madhabahuni akaanza kulia tena kama mwanzo, ndipo mama mchungaji akaamuru apelekewe mtoto…”
“Mlete huku kwangu…” alisema yule mchungaji kisha kukatisha somo alilokuwa ameanza nalo na kuanza kuomba…
“Baba katika JJina la Yesu…...” aliombea weeee huku akiwa amemshika mtoto, lakini Junior hakuonesha hali ya kutulia akawa anarukaruka mikononi mwa mchungaji kwa nia ya kutaka amuachie…
Mchungaji alizidi kumg’ang’ania lakini naye mtoto alizidi kufurukuta, kukukuruka hadi ikabidi amweke chini…
Maombezi yaliendelea na waumini wengine wakapokea kila mmoja akikemea kwa mtindo wake, lakini mtoto hakukoma kulia na kuanza kufanya kama anataka kutambaa hadi ikapelekea kulala kifudifudi akitapatapa kama anaogelea kwenye maji.
Mara sauti tofauti kutokea mlango wa kanisa ikasikika, ikiimba wimbo wa kubembeleza mtoto kwa kilugha na binti kigoli akawa anatembea huku akiimba kuelekea madhabahuni.
Alikuwa ni binti mgeni kanisani mule hakuna aliye mjua, waumini waliendelea kukemea lakini sauti kama zilishuka hivi kutokana na mrindimo wa mpangilio wa sauti ile nyororo kwa lugha kama ya Kigogo hivi isiyoendana kabisa na namna ya ukemeaji mle kanisani.
Binti yule alikuwa kama darasa la saba hivi kwa kumuangalia, lakini akiwa katika mavazi ambayo yanadhihirisha kuwa ni kutoka katika familia masikini, alikuwa amevaa gauni lililofubaa ingawaje lilionekana safi.
Alielekea moja kwa moja kwa Junior pale madhabahuni huku akiendelea kuimba kilugha wimbo wa kubembelezea watoto na alipomshika tu Junior aliacha kulia, akamnyanyua na kumbeba kifuani, kisha akawa anaelekea upande wa mama Junior.
Kanisa zima likatulia na sauti ile nyororo ikasikika waziwazi na ikajulikana ni Kikaguru. Hakuacha kuimba hadi alipomkabidhi mtoto kwa mama yake kisha yeye akawa anatoka kanisani huku akiimba wimbo mwingine wa kuabudu…
“Yua Yaweh…eheheee, x2
“You are Yaweh… Alpha na Omega…”
Ulikuwa wimbo uliochanganyika Kiswahili na Kiingereza, binti alikuwa akirudia maneno hayo hayo huku akitembea tarabitu kuelekea mlango wa kutokea Kanisani…
Kanisa zima likaanza kufuatisha wimbo ule na sauti za mitetemo zikasikika wengine wakaanza kulia kwa hisia mbalimbali kasoro Mchungaji tu ambaye alikuwa mapegwa na butwaa…
Yule binti alitoka mle kanisani, huku ndani waumini waliendeleza ule wimbowa kuabudu hadi pale mama Mchungaji alipo ingilia kati kwa yeye naye kuitikia kwa sauti ya juu huku akinyoosha mkono kuashiria waache kuimba.
Ghafla akatoka mle kanisani kukimbilia nje kuangalia labda atamuona yule binti lakini haikuwa hivyo. Binti alishatokomea kusiko julikana.
Akarudi ndani ya kanisa na kuuliza kama kuna muumini anamfahamu yule binti…! Kimya kilitawala kuashiria hakuna aliyekuwa anamfahamu.
“Yule binti ana upako sana!”… Alisema mama Mchungaji.
“Natamani nijue anatoka wapi ili nimualike aje tena kanisani…” aliongea kwa kutetemeka.
Mama mchungaji hakuwa na nguvu tena ya kuendelea na misa, bali wasaidizi wake wakashika hatamu kumalizia pale mchungaji alipoachia somo wakati mtoto alipoanza kulia.
---
Wakati wa kutoka mule kanisani baada ya ibada ile ya jioni kuisha minong’ono ilianza kama kawaida ya binadamu.
Ibada iliisha mapema kuliko kawaida maana siku hiyo hakukuwa na huduma za ufunguzi kama ilivyo kawaida baada ya mama Mchungaji kutoonekana tena pale mbele madhabahuni maana aliingia chumba cha mapumziko papo hapo kanisani na kujilaza.
“Yule binti ni mtoto wa nani!?..” aliuliza mama mmoja
“Inaonekana hakuna anaye mfahamu katika sisi…” alijibu mama mwingine
“Sijui kwanini hatumfuatilia kujua anaelekea wapi pale alipokuwa anatoka…” Alisema baba mmoja
“Inaelekea ana nguvu za kuliko mchungaji…” alisikia dada mmoja akisema
“Shiiiiii, nyamaza wewe chawa wa mchungaji watatusikia….” Alisema mama mmoja kwa sauti ya chini akimkanya yule dada asiropoke.
“Kwanza alijuwaje kama mule kanisani kuna mtoto analia…” Alihoji yule dada…
“Halafu alikuwa anaimba Kikaguru, hivi si tuna waumini wakaguru humu!!?” aliuliza mama mwingine
“Eee tunaye mmoja lakini yule ni chawa wa mama Mchungaji, hatuwezi kumuuliza…”
“Sasa yule binti mbona alitoka hakuendelea kubaki kwenye ibada…?” aliuliza mama mwingine
Wakati huo kikundi hicho cha waumini kilikuwa kinaelekea eneo moja la makazi ndio wakajikuta wanapiga soga namna hiyo, kwa upande mwingine pia makundi ya waumini walijadili suala lile huku wakielekea makwao.
“…Ni kama vile alikuja kutoa yule mtoto pale mbele na kumpeleka ma mama yake kisha kuondoka, kama vile alikuja kumuokoa, si ndiyo…” alisema yule dada na wote wakaangaliana pale kisha wakaguna.
“Msigune, ndio hivyo, mimi najua hata wale wanaotoa ushuhuda ni ushuhuda wa uongo, wameandaliwa wale…” alisema tena yule dada
“We mwana we!, hebu funga domo lako!” yule mama aliye mkanya awali akarudia kumkataza asiropoke.
Majadiliano yaliendelea hadi watu walipopungua na kubadi wachache kisha hao wachache wakashika njia tofauti na njia ya mama Onesno Junior na mama Rose, wao wakawa na njia yao peke yao iliyo wapeleka moja kwa moja hadi nyumbani kwao.
“Mama Rose, wewe umejifunza nini?!” aliuliza Vai
“Mmh, Mwenzagu, makubwa!, hebu tuwe tunaudhuria haya maombi kuna mengi ya kujifunza…” Mama Rose hakujibu swali ila alipendekeza jambo.
“Tuwe kila siku jioni tunawaita wale wana maombi na wa kule kkkt kwa pamoja tufanye maombi hapa nyumbani labda tutang’amua jambo.”
Wazo lile likapita bila kupingwa na nyumba ya Vai sasa ikawa kama Kanisa, kila siku jioni kuna watu wane hadi watano walikuwa wanakuwepo kwa ajili ya maombi.
Zoezi la maombi lilipelekea kuchelewa kulala na kufanya lile tukio la mtoto kubadilishwa nepi usiku kila siku kujirudia na kuwa kama la kawaida.
“Inawezekana ni yule mtoto ndio anakuja kumbadilisha Junior nepi” Mama Rose alisema alipo shirikisha jambo lile ambalo sasa limekuwa kama la kawaida.
“Labda, lakini ngoja nifunge na kuomba kwa siku tatu ili nione kama Mungu atanionesha anayekuja kumbadili mwanangu nepi…” Vai alisema.
Baada ya siku tatu za maombi, usiku wake alishtuka usingizini na kukuta mtoto amebadilishwa nepi, nyingine zimefuliwa na mlango ulitoa sauti ile ya kufungwa kitu kilichomstua Vai.
Ni kwamba, tangia siku ile watoke kule kanisa la mama Mchungaji, Vai aliamua kutofunga mlango wake ili iwe rahisi kupata msaada kama kuna jambo limetokea. Sasa siku hiyo alipostuka usiku wakati mlango unafungwa ndipo akakimbilia kuangalia nani anayetoka mle ndani…
Kwa mbali aliona mtu mzima mwamamke akiwa amejitanda khanga akitoka, lakini aliona mgongo tu na wala hakusikia vishindo vya nyao za kutembea, na kabla ya yule mtu tupotelea mlangoni aligeuka nyuma na wakakutanisha macho…
Inaendelea…