Sehemu ya 34
“Ni lazima ujue kila mwanamke unayemuona hapa duniani, Mungu amemuandalia mume mzuri ambaye utaishi naye kwa upendo na amani maisha yako yote, hata mkigombana, mtakuwa wepesi mno kusameheana na kusahau mliyotendeana, ila ukijilazimisha kumfuata fulani kisa pesa, kuna siku utalia na kujuta maisha yako yote,” alisema mwanamke huyo.
Maneno ya mama yake yakaingia moyoni mwake, yakamjenga na kurudi nyuma kutoka kwa Sangiwa. Yalimfungua na kumshukuru kwani alihisi endapo angemkubali mwanaume huyo, kuna siku isiyokuwa na jina angekuja kuumia mno moyoni mwake, na inawezekana matatizo yakawa makubwa mpaka kujimaliza, hivyo hakutakiwa kuwa na haraka.
Hapo, alitamani kumwambia mama yake kuhusu huyo John ila hakujua ni kwa namna gani angemuanza. Alihisi mama yake angemwambia kwamba kwa sababu alitoka jijini Dar es Salaam ndiyo maana alimpenda kumbe haikuwa hivyo.
Hakutaka kumwambia kwa wakati huo lakini alijiahidi kwamba siku moja ilikuwa ni lazima kumwambia kuhusu moyo wake, jinsi ulivyompenda mwanaume huyo ambaye hakujua aliishi wapi, alichokijua ni kwamba alikuwa akisali naye kanisa, hilo tu.
.
.
.
Je, nini kitaendelea?