Simulizi: Mke Wangu Juliana

Simulizi: Mke Wangu Juliana

Sehemu ya 100.

Akamwambia kama ingewezekana basi waende pamoja mpaka kwao, akaombe ruhusa yeye mwenyewe. Lilikuwa suala la kijinga mno lakini kwa sababu alimpenda sana msichana huyo, alikuwa tayari kwa kila kitu.

Amanda akakataa na kumwambia siku nyingine lingekuwa suala zuri ila si kwa siku hiyo. Wakaachana na jambo hilo na kuendelea kupiga stori kuhusu mambo mengine.

“Unaniangalia sana mpaka najisikia aibu!” alisema Amanda huku akiangalia chini.
“Najaribu kuutafakari uzuri wako! Nimeanza kushikwa na wasiwasi na vitabu vyetu vya dini,” alisema John.

“Kwa sababu gani?”
“Kwamba sisi wote tumeumbwa! Ni kweli tumeumbwa wote ama wengine wameshushwa tu hapa duniani?” aliuliza huku akitoa tabasamu pana, naye Amanda akatabasamu.
“Hebu acha masihara bhana na wewe!” alisema Amanda.
“Nisikilize Amanda. Kuna kitu ninahitaji kukwambia!”

“Ila kisihusu mapenzi?”
“Hahaha! Kwa sababu gani?”
“Nimeshaanza kuziona dalili! John! Sipendi mapenzi!” “Kwa sababu gani?”

“Yanatesa sana!”
“Unamaanisha wanaume wote ni watesaji?” aliuliza.
“Ndiyo! Nyie wanaume mnafanana!”
“Amanda.....”

“Unasemaje! Una la kujitetea?”
“Unajua kama Adolf Hitler aliwaua Wayahudi zaidi ya milioni mia moja?” aliuliza huku akimwangalia.

“Ndiyo! Nilisoma kwenye historia!”
“Sawa! Mpaka leo baba yako ameua watu wangapi?” aliuliza.

“Mh! Kwa nini unauliza hivyo?”
“Wanaume wote tunafanana kumbuka!”
Amanda hakujibu kitu, hapohapo akaanza kucheka, alijua John alimaanisha nini, alitegwa bila kujua kabla alichokuwa akimaanisha mwanaume huyo.

“Wanaume hatufanani, wanaume wote si wabaya! Leo kuna wanawake wanasema wanaume wanafanana lakini kila siku wanaongoza kuhudhuria harusi za wenzao! Sasa wale wanaoolewa, wanaolewa na akina nani?” aliuliza John, Amanda akabaki kimya.

John akaanza kumpa somo la mahusiano ambalo msichana huyo hakuwahi kulisikia kwa mwanaume yeyote yule. Alimwambia mambo mengi kuhusu hayo mahusiano na mwanaume ambaye alitakiwa kuwa naye.

Amanda alikuwa kimya, ni kama alikuwa darasani huku akimsikiliza mwalimu ambaye alimfundisha somo ambalo baadaye lingekuja kumsaidia kufaulu mitihani yake.
 
Sehemu ya 101.

“Binadamu wote tunakosea, lakini wote tuna nafasi ya kujirekebisha! Inawezekana kabisa nikawa mwanaume mbaya sana kwako, ila haimaanishi nitakuwa mbaya hivyo milele, hakuna mtu anayetaka kuwa mbaya, ubaya unakuja ghafla, wakati mwingine unaondoka,” alisema John huku akimwangalia msichana huyo.

“Hujawahi kuona siku moja umechukua uamuzi mbaya wa kumuumiza mtu fulani halafu unaanza kujuta? Hutokea kwenye maisha yetu, na kama kungekuwa na mtu ambaye anakuona wakati unamfanyia mtu huyo ubaya huo, angesema wewe ni mbaya, kumbe ni hali tu ambayo imetokea na baadaye ulijuta kwa nini ulifanya hivyo,” alisema John.

“Unamaanisha nini?”
“Kitu cha kwanza unachotakiwa kujua ni kwamba mwanaume hajakamilika, sisi ni binadamu na si malaika. Mwanamke unapoamua kuingia kwenye uhusiano na sisi, unategemea kupata maisha mazuri milele bila kujua kuna wakati ubinadamu unatuingia na kuanza kufanya maamuzi ya kijinga kabisa,” alisema John.

“Unamaanisha usaliti?”
“Usaliti, wivu, hasira na mambo mengine ni ukamilifu wa binadamu. Leo nikikusaliti haimaanishi mimi ni mbaya sana kwa kuwa utampata mwingine naye atakusaliti vilevile. Kuna makosa tukiyafanya yanadhihirisha kwamba sisi ni binadamu,” alisema John.
“Mh!”

“Hakuna ndoa ambayo wanandoa hawatofautiani! Ni lazima hilo litokee, wanaonyesha ukamilifu wao kama binadamu. Inawezekana sisi tungekuwa malaika tusingekuwa na mambo kama hayo!” alisema John.

“Unamaanisha na wewe pia unaweza kusaliti?”
“Hahaha! Amanda! Kwenye ndoa usaliti upo, ila si unasaliti mpaka mwenzako anajua kwamba unamsaliti!” alisema John.
“Mh! Wanaume nyie!”

“Nisikilize Amanda! Mwanaume anaweza kusaliti na mke usijue, ila mwanamke anaposaliti anataka mwanaume wake ajue, huwa hamsaliti kwa kupenda, wakati mwingine mnafanya kwa makusudi kabisa, ili tujue, tuumie halafu muone tutafanya nini,” alisema John.

“Nyie wanaume si watu wa kuwaamini kabisa.”
“Ndiyo! Upo sahihi! Mimi mwenyewe sitaki uniamini tukiwa kwenye uhusiano!” alisema John.
“Kwa sababu gani?”
 
Sehemu ya 102.

“Nichukulie kama binadamu, kwamba naweza kukusaliti, kukuumiza au kufanya upuuzi mwingine wa kijinga. Ukitaka uniamini kwa kuniona mimi ni malaika, jua siku ambayo nitakusaliti ama kukufanyia ubaya mwingine ni lazima utajiua kwa sababu uliniamini kupita kawaida,” alisema John.
“Mh!”

“Na ndiyo maana hata wanafunzi wanajiua baada ya kufeli!”
“Yaani weweeee...”

“Kwa kuwa tangu kidato cha kwanza walikuwa wanafunzi wa kwanza darasani, waliamini hawatokuja kufeli, hawakujua kwamba nao ni bindamu kama wengine. Inapotokea wanafeli, wanachukua uamuzi mbaya, kwenye maisha yao hawakuwa na neno kufeli, waliishi na neno kufaulu tu,” alisema.

“Aya baba nimekuelewa. Yote hayo unamaanisha nini?”
“Ninakuhitaji!”
“Unanihitaji mimi?”
“Ndiyo! Ninakuhitaji baada ya kukupenda sana!”

“Kwa nini mimi?”
“Hahaha! Ushawahi kuambiwa hivyo na mwanaume mwingine?” “Ndiyo!”
“Ulijiuliza kwa nini wewe tu?”
“Hapana!”

“Unahisi kwa nini mwanaume huyo alikwambia wewe na tena na mimi nimekuja kukwambia wewe kwa mara nyingine?” aliuliza John, swali aliloulizwa, akaligeuza.

“Yaani sina hata jibu.”
“Kwa sababu ni mzuri! Unajiheshimu, unaonekana kuwa msichana tofauti sana unapokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi!”
“Umejuaje?”

“Unaonekana tu, ila ninahitaji nijue kama nipo sahihi na ndiyo maana nimekufuata na kuhitaji kwenye uhusiano na wewe,” alisema John.

Amanda alibaki kimya kwa muda, alimwangalia John, muda wote huo mwanaume huyo alikuwa akizungumza huku tabasamu likiwa usoni mwake.

Kumkataa mwanaume kama huyo lilikuwa jambo gumu, alikuwa na akili na maisha yake yalionekana kuwa mazuri kuliko hata wengine waliowahi kumfuata.

Na hicho ndicho alichokifikiria sana, kumuacha mwanaume kama huyo apite lilionekana kuwa kosa kubwa hivyo akajifanya kugomagoma lakini mwisho kabisa akakubaliana kuwa naye.

Kwa John ilikuwa ni furaha, hakuamini kama alikubaliwa na msichana huyo. Alimpenda, moyo wake ulimwambia kwamba kuna siku moja angemuoa na kuwa mke wake wa ndoa.
 
Sehemu ya 103.

Huku akifikiria maisha ya raha tu mbele yake, hakufikiria kuhusu maumivu ambayo yangekuja hapo baadaye.

Kwa zaidi ya dakika hamsini, akatokea kumwamini Amanda kwamba angempa furaha, hakukumbuka maneno aliyoyasema dakika chache zilizopita kwamba binadamu hakukamilika, alikuwa na mapungufu kwa kuwa hakuwa malaika.

Hakuhisi kama kungekuwa na maumivu kwenye upande wa pili wa mahusiano yao, alichokuwa akikifikiria ni furaha ambayo angekuwa nayo baada ya kuwa na Amanda.
|
| “Tina upo wapi?” “Nipo huku Samaki Samaki, Mlimani City!”

“Unafanya nini mbona mapema hivyo?”
“Kuna jamaa nimekuja kumuona, ila ananiweka sana! Wewe upo wapi?”

“Nipo hapa Mwenge ITV tunaweza kuonana?”
“Kuna ishu gani?”
“Njoo tuongee mara moja, halafu nitakutoa.”
“Mh! Aya nakuja!”

Yalikuwa ni mazungumzo kwa njia ya simu baina ya wasichana wawili, Amanda na Christina. Wasichana hao wawili walikuwa marafiki wakubwa, ilikuwa kazi ngumu sana kumuona mmojawapo pasipo mwingine.

Walimaliza wote Chuo cha IFM mwaka huo na katika kipindi hicho walikuwa wakitafuta ajira katika taasisi mbalimbali kwa ajili ya maisha yao.

Ukaribu wao ulikuwa mkubwa, kwa siku za karibu hawakuwa wameonana kutokana na maisha yao kuwa na changamoto nyingi za ajira.

Amanda aliamua kumpigia simu rafiki yake huyo kwa lengo la kuonana na kuzungumza. Kulikuwa na jambo muhimu ambalo alihitaji sana ushauri wake kabla ya kufanya maamuzi yake binafsi.

Walikubaliana waonane Mwenge, ITV na ndani ya dakika kadhaa walikaa kwenye kimgahawa kidogo na kuanza kuzungumza.

Alichohitaji kusema Amanda ni kuhusu John, alikutana na mwanaume huyo, alimuelewa kwa sababu alikuwa mzuri wa sura, alimpagawisha zaidi kwa sababu alikuwa na pesa.
Amanda akamwambia Christina kuhusu John, msichana huyo alibaki kimya akimsikiliza mwenzake.

Kile alichokisikia hakuamini, moyo wake ulichoma kwa sababu kila siku rafiki yake huyo ndiye alikuwa akifuatwa na wanaume wazuri, wenye pesa tofauti na yeye.
Alimsikiliza kwa makini. Ushauri ambao aliuhitaji muda huo ni kuhusu huyo John na mwanaume mwingine aliyeitwa kwa jina la Martin.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom