Simulizi: Mke Wangu Juliana

Simulizi: Mke Wangu Juliana

Sehemu ya 89

John na familia yake walikaa nchini India kwa muda wa wiki moja na nusu, madaktari walifanikiwa kwa asilimia mia moja kuwatenganisha watoto wao.

Ilikuwa ni furaha ya kila mmoja, japokuwa walitumia kiasi kikubwa cha pesa za michango ya watu lakini mwisho wa siku kile walichokuwa wakikihitaji na kumuomba Mungu kila siku hatimaye kilifanikiwa.

Waliwasiliana na Deborah wakiwa hukohuko, walimshukuru kwa wema wake kwani bila mwanamke huyo wasingeweza kupata msaada mkubwa kama walioupata hasa baada ya kwenda kuzungumza na Bwana Kayore.

Baada ya wiki ya pili kuingia, wakaondoka na kurudi nchini Tanzania. Safari ilikuwa nzuri, njiani walikuwa wakicheka kwa furaha, hawakuamini kama kile walichokuwa wamekifuata nchini India kilifanikiwa kwa asilimia mia moja.

Watoto wao walikuwa na sura nzuri, walifanana nao, waliwapa majina mazuri ya Godlove na Godson, yote yakiwa na maana ya upendo mkubwa wa Mungu aliowapa na kuwakabidhi watoto hao mikononi mwao.

Baada ya saa kadhaa wakafika nchini Tanzania ambapo wakapokelewa na madaktari na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo waliwashukuru na watoto wale kupumzishwa kwa siku moja na kisha kuondoka kurudi Kijitonyama ambapo walipanga nyumba nzima.

“Ninakupenda mke wangu,” alisema John huku akimwangalia mke wake.

“Nakupenda pia!” alisema mwanamke huyo.
Maisha yakawa na furaha tele, walikaa jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili kisha kurudi mkoani Kigoma kuendelea na maisha yao.

Walipofika huko, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuonana na Deborah na mumewe na kuwashukuru kwa wema wao, waliwaambia wazi kwamba bila wao basi inawezekana kabisa watoto wao wangefariki, ila kwa msaada wao mkubwa, walitenganishwa na kuwa wazima wa afya.

“Na sisi tunakushukuru sana, kupitia matatizo yenu, mume wangu amepata kazi,” alisema Deborah huku akimwangalia John.

“Ni Mungu! Ninajifunza mambo mengi sana katika ulimwengu huu, kama unapofanya ubaya tunasema malipo ni hapahapa duniani, basi amini hata unapofanya mema malipo huwa hapahapa,” alisema John huku akiwaangalia watu hao wawili.
 
Sehemu ya 90

Walizungumza mambo mengi, baada ya kumaliza, Deborah na mumewe wakaaga na kuondoka huku mioyo yao ikiwa na furaha tele.

Baada ya kumaliza kuzungumza nao, wakampigia simu mchungaji wao na kuwaambia kila kitu kilichotokea.

Mwanaume huyo hakuwa na la kusema, katika maisha yake siku zote aliwaambia kuhusu kumtumaini Mungu kwani alikuwa muweza wa kila kitu.
“Kwa Mungu hakuna kinachoshindikana!” alisema mchungaji huyo.
“Kabisa!”

“Matatizo yetu yote, magonjwa yalimalizwa pale msalabani Goligotha alipoteswa na kufa Yesu Kristo, hatutakiwi kuwa na hofu tena, kwenye kila kitu, ni lazima tuamini matatizo yetu yaliishia pale,” alisema mchungaji huyo.

Jumapili iliyofuata, John na mkewe wakaelekea kanisani wakiwa na watoto wao. Kila mmoja alijua kilichokuwa kimetokea, kuwaona tena kanisani humo ilikuwa ni furaha ya kila mmoja.

Mama yake Juliana kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, kilichokuwa kikiendelea kilimpa furaha ya ajabu, alimshukuru Mungu kiasi kwamba alijiona alifanya hivyo kuliko mtu yeyote katika dunia hii.

Aliwapenda wajukuu zake zaidi ya kitu chochote kile, aliacha kufanya mambo yake, muda mwingi alikuwa na wajukuu hao ambao walimpa furaha ya ajabu.

John na Juliana wakaanza kutoa ushuhuda kanisani hapo, kila kitu kilichokuwa kimetokea katika safari yao ndefu ya kuwauguza watoto wao.

Waliongea mambo mengi lakini kwenye yote hayo yalibebwa na neno moja lililoitwa shukrani, yaani kumshukuru Mungu kwa mambo yote, waliamini yeye ndiye aliongea na Deborah, yeye ndiye aliyewagusa watu kuwa na moyo wa huruma na kuwasaidia kwa mambo yote yaliyotokea.

“Kwenye maisha yako, mtu anapokuwa na tatizo, wewe msaidie tu,” alisema John huku akiwaangalia washirika wa kanisa, walikuwa kimya wakimsikiliza.

“Unapomsaidia mtu, hujui ni kwa namna gani Mungu atakurudishia malipo ya wema wako. Inawezekana ukawa unasumbuliwa sana na magonjwa, lakini baada ya kuanza kuwasaidia watu wenye matatizo, magonjwa yanapotea mwilini mwako. Malipo ya Mungu si pesa tu, kuna wakati anafanya miujiza katika maisha yako kupitia afya yako!
 
Sehemu ya 91

“Unaweza kuona huumwi kama watu wengine, mambo yako yanafanikiwa, kumbe bila kujua, Mungu anakulinda kwa sababu tu unatenda wema kwa watu wenye matatizo,” alisema John huku akianza kulengwa na machozi.

“Leo kuna watu wametusaidia bila kutujua! Wamesikia tuna matatizo, wametusaidia tu. Mtu anayekusaidia si lazima awe anakufahamu, na usitake kila unayemsaidia lazima umfahamu, hapana!

“Unapoguswa kumsaidia mtu fulani, saidia, usiangalie dini, kabila ama cheo cha mtu, kuna masikini wengi wana mahitaji, wasaidie, wengine wana nguo nyingi kabatini, wanajisifu kuwa na nguo lukuki, ni ajabu wanapopita mitaani wanawaona watu wana nguo zilizochakaa na bado hawawasaidii.

“Inawezekana kuna wengine mambo yenu hayafanikiwi kwa sababu hamsaidii watu, umesoma, una vyeti vimekaa tu ndani lakini hupati kazi, yote ni kwa sababu kwa kidogo ulichonacho hutaki kuwasaidia wasivyonavyo.

“Huu ndio moyo niliotaka sana kuuona kwa kipindi kirefu, nilihitaji kujua ulimwengu wa pili watu walikuwa wakiishi vipi.

Unapokuwa kwenye ulimwengu huu, watu wanakuchukuliaje! Sikuwahi kuishi maisha haya niliyokuwa nikiishi kwa miaka miwili, nilikuwa nayasikia tu kwa sababu nilizaliwa kwenye familia ya kitajiri, baba yangu ni bilionea.

“Kwenye maisha yake aliniambia kuna siku nitatakiwa nijifunze maisha ya upande wa pili, niwe na njaa kama wengine, niteseke ili siku mtu akija na kuhitaji msaada, basi nijue aliteseka kwa kiasi gani,” alisema John na kuwafanya watu kuwa makini kanisani hapo, si hao tu bali hata mke wake.

“Nilipokwenda India kwa ajili ya watoto wangu, baba na mama yangu walikuja kutoka nchini Australia wanapoishi na kufanya biashara zao.

Waliponiona, wakanisogelea na kunipongeza, waliniangalia machoni, sikuwa John yule wa kipindi cha nyuma, nilichakaa mno, nilikonda, hilo ndilo jambo ambalo walikuwa wakilitaka sana, kunifundisha mtoto wao maisha ya upande wa pili, jinsi masikini wanavyo...” alisema John, hakumalizia sentensi yake, akanyamaza na kuanza kulia.
 
Sehemu ya 92

Kila mmoja alimshangaa John, maneno aliyoyasema hayakuaminika, mchungaji ni kama alipigwa na butwaa, yaani kanisa zima lilikuwa likimshangaa, hawakuamini maneno aliyokuwa akiyaongea mwanaume huyo.

“Au ndiyo kamari aliyoniambia alikuwa akiicheza?” alijiuliza mke wake.
Alizungumza mambo mengi mno, historia ya maisha yake, sababu iliyomfanya kwenda mkoani Kigoma na mambo mengine mengi aliyowahi kukutana nayo.

“Mpaka sasa hivi sijaelewa,” alisema jamaa mmoja.
“Kwa nini?”
“Yaani huyu John ni bilionea! Kivipi yaani mbona kama amenichanganya?” aliuliza jamaa huyo, maneno hayo yote yaliwafanya watu kumshangaa tu.

“Sisi kama watu wenye kitu kidogo ni lazima tuwasaidie wale ambao hawana kitu, leo mtu akishiba, ukimwambia kama hapa duniani kuna njaa, atakataa kwa sababu yeye ameshiba. Tunapopata tunachokitaka ni lazima tuwasaidie wale ambao hawana,” aliendelea kusema na kuendelea:

“Mungu na malaika ni roho, tunapoomba kuwaona, haimaanishi watakuja kwa njia ya roho, wanatufuata kwa njia ya mwili, inawezekana njiani ulimuona malaika anaomba akiwa kwenye mwili wa mwanaume aliyechakaa na ukampita bila kumsaidia kwa lolote lile na wakati ulikuwa na pesa nyingi tu,” alisema na kuendelea.
 
Sehemu ya 93

“Kuna wanawake wengine wanauza mbogamboga mitaani, umetoka kununua vyakula vya kupika nyumbani vya laki mbili kwa wiki nzima, unakutana na mwanamke huyu, anauza fungu la mchicha shilingi mia tatu, bila aibu unaanza kumshusha akuuzie kwa mia mbili! Tena unalalamika kabisa,” alisema John, akanyamaza, machozi yaliendelea kutitika, akachukua kitambaa chake na kuanza kujifuta.

Baada ya kumaliza wakarudi kukaa. Yeye na mke wake walikuwa wakilia tu, Juliana hakuamini alichokisikia kwa mume wake, aliamini siku zote walikuwa masikini wa kutupa kumbe haikuwa hivyo, John alikuwa na sababu zake kufanya hivyo, baba yake alimshinikiza kwa sababu alimtaka kuyajua maisha ya upande wa pili.

Baada ya ibada kumalizika, akampigia simu Deborah na kuhitaji kuonana naye, alihitaji kuzungumza naye mambo mengi mbele ya wazazi wake kabla ya kuondoka na kwenda kuishi Dar es Salaam.
“Kwenda kuishi Dar es Salaam?” aliuliza Deborah.

“Ndiyo!”
“Kwa nini unahama Kigoma?”
“Nakwenda kuishi kwangu!”
“Sijakuelewa!”
“Naomba nionane na nyie wote, wazazi wako, nitahitaji kuzungumza nao leo hii,” alisema John.

Hilo halikuwa tatizo, baada ya kukubaliana jioni ya siku hiyo wakaondoka na kuelekea nyumbani kwa mzee Abraham.

Alipofika na kumwangalia, hakuamini macho yake, mzee Abraham alikonda mno, hakuwa kama alivyokuwa, hakushangaa kwa sababu alijua kila kitu kilichokuwa kimetokea.
“TRA si mchezo!” alisema John, alikuwa akimwambia Deborah.
“Umejuaje?” aliuliza, John hakujibu, akaachia tabasamu tu.

Wakasalimiana na kuanza kuzungumza nao. Hakutaka watu hao waombe msamaha, yeye ndiye akajifanya kuwa na kosa, si kwamba alikosewa bali yeye ndiye aliwakosea.
Deborah alishangaa, hakujua John alijuaje hayo yote. Akakaa chini na kuwaangalia watu hao, aliporidhika akaanza kuzungumza nao.

“Naomba mnisamehe kwa sababu sikutaka kuishi kama ambavyo nilitakiwa kuishi, inawezekana ndiyo sababu ya nyie kunichukia,” alisema John.
“Unamaanisha nini?” akauliza mama yake Deborah.

“Naomba niwahadithie kidogo historia ya maisha yangu, baada ya hapo nitakujibu swali hilo uliloniuliza,” alisema John na hapo ndipo akaanza kuwasimulia watu hao historia ya maisha yake mpaka kufikia hatua ya kwenda mkoani Kigoma.
 
Mkuu mbona kila mtu anatoa hisia zake za moyoni. Nami ngoja nifatilie


Sent from my iPhone using JamiiForums
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom