Simulizi: Mchawi

Kweli kabisa tatizo mapenzi yalimpelekekesha ndio yalipomfikisha uko anapoenda
 
Sehemu ya 54

Tulikaa kwa robo saa kisha alitoka kijana aliyekuwa amevaa rubega la kaniki na kuzungumza maneno ambayo yalikuwa kama ya Kimakonde huku akiashilia kutuita.

Sikusimama nilimsikiliza mkalimani wangu ili kujua yule kijana anasema nini.
“Tunaitwa ndani,” mkalimani wangu alinieleza huku akinyanyuka.

Nilimfuata hadi ndani ya kilinge na kukaribishwa kwenye ngozi ya chui, tulikaa mbele yetu kulimkuta mzee aliyekuwa amekula chumvi. Kichwa na ndevu zake zilikuwa nyeupe.

Baada ya kukaa alisema neno ambalo sikulielewa, nilimtazama mkalimani wangu ambaye aliuniliuza.

“Anauliza tunatoka wapi? Nimwambie?”
Kabla sijajibu mganga alizungumza kwa lugha ya kiswahili iliyotushtua wote.
“Mnatoka Tanzania?”

“Ndiyo,” nilijibu.
“Karibuni.”
“Asante.”
Mganga alibadili lugha tukawa tunazungumza kiswahili.

“Mna shida gani?”
Nilimwelezea sababu ya mimi kufunga safari toka nyumbani Tanzania mpaka pale. Baada ya kunisililiza alitoka nje na kuchukuma tawi la mnyaa na kuja nao ndani. Kisha alikaa kwenye ngozi ambayo sikujua ya mnyama gani.

Baada ya kukaa alinipa tawi la mnyaa na kunieleza ninuie yote yanayonisibu.
Kwa vile nilikuwa nimeisha kuwa mzoefu, nilipokea na kunuia, niliyasema yote yanayonisibu.

Baada ya kunuia nilimpa tawi la mnyaa alilichukua na kulibana na mdomo kisha aliziba masikio yake kwa mikono yake na kufumba macho na kutulia bila kupumua kwa muda kisha alipumua kwa kasi na kurudia kubana tena pumzi.

Kwangu yalikuwa maajabu kwani alitulia zaidi ya dakika tatu bila kupumua kitu kilichoniogopesha na kuona mapya. Baada ya muda alitoa mikono masikioni na kubakiza tawi la mnyaa mdomoni na kuwa kama anazungumza na mtu kwa kutikisa kichwa kama kukataa wakati mwingine anakubali kwa kunyanyua kichwa juu.

Alifanya vile kwa zaidi ya robo saa kisha aliutema ule mnyaa na kuuweka kwenye ungo mdogo ulikuwa mbele yake na kusema:

“Kijana umetoka mbali kwa ajili ya mapenzi, kweli?”
“Kweli?”
“Umeua watu wa ajili ya mapenzi, kweli?”

“Mmh! Kweli,” nilisita kidogo lakini kwa vile jambo lilikuwa wazi nilishindwa kukataa. “Umepoteza mzazi na mtoto wa ajili ya mapenzi, ni kweli?” yote aliniuliza bila kunitaza macho yake yaliangalia kwenye ungo.

“Ni kweli.”
“Na safari yako ya kuja hata kusudio lako kubwa kuua, ni kweli?”
“Ni kweli.”

“Unataka uue watu wangapi?”
“Kivipi?” swali lake sikulielewa.
“Nakuuliza unata uue watu wangapi maana mpaka sasa umeua wanne?”
“Wanne?” nilishtuka kusikia nimeua wanne wakati najua wawili.
“Jibu kwanza, unataka kuua wangapi?” Mganga muda wote aliniuliza bila kunitazama.

“Kwa vile wameniulia familia yangu lazima na wao wabakie jina tu,”
“Nani kamuua baba na mtoto wako?”
“Kuna kijana mmoja alitembea na mke wangu, mimi sikukubali nikaamua kulipa kisasi.”

“Kisasi kipi?”
“Nilimuulia mbali.”
“Baada ya hapo?”
“Nasikia familia yake iliponiendea kona zote za dunia kutaka kuniua, waliponishindwa wakaamua kuimaliza familia yangu na kuua baba na mwanangu wa mwisho.”

“Baada ya hapo?”
“Nilikwenda kwa mtaalamu na kunisaidia kuzuia ndizi zilizoiva ili zisidondoke, lakini bahati mbaya moja ilikuwa imeisha dondoka. Mama na mke wangu walikuwa wafe kwa mpigo kwa msaada wako walipona.”
“Unajua kilichoiva kikikaa muda mrefu kinakuwaje?”

“Kinaoza.”
“Basi hawajafanya lolote kwa vile ndizi walizozizuia kuanguka muda si mrefu zitaanza kuoza.”
“Na zikioza?” niliuliza kwa mshtuko.
“Zitatoa wadudu.”

“Kwa hiyo?”
“Ile ilikuwa sawa na mgonjwa wa kichwa kumeza dawa ya maumivu, lazima baada ya muda maumivu yapo palepale. Kwa hiyo kifo cha pamoja kipo palepale.”
“Mungu kwangu, nitafanyaje?” niliuliza mikono kichwani.

“Nitakusaidia kuyaondoa maisha yao kwenye ndizi na kuyarudisha katika hali ya kawaida.”
“Nitashukuru sana mzee wangu, lazima niwamalize wote.”

“Ukiwamaliza wote pamoja na familia yako na wewe mwenyewe.”
“Kwa nini?”
“Unajua nani aliyeua familia yako?”
“Mzee si nimekueleza ndugu ya jirani yangu.”
“Hapana, wao hawahusiki,” jibu la mganga lilinishtua.

“Nani sasa muuaji?”
“Wewe mwenyewe.”
“Mimi?” nilishtuka kusikia vile.
“Ndiyo, hapa inaonesha wewe ndiye muhusika wa vifo vyote, kuanzia mgoni wako wa kwanza mpaka mzazi wako na mwanao.”
“Mzee! Mimi?” nilizidi kushtuka na kushanga.

“Ndiyo.”
“Mzee mimi nitauaje familia yangu kisha nije huku kutafuta msaada?”
“Kumbuka bila wewe kuanza kuua usinge poteza baba na mwanao.”
“Sasa ningefanyaje kama mtu katembea na mke wangu?”

“Zipo njia nyingi za kutatua tatizo si kuua, waganga wengi wamekuwa na tamaa ya fedha kuliko kutatua tatizo. Uliua ukiamini ndiyo suruhu ya tatizo lako lakini bado mkeo aliendelea na tabia zake chafu.Umeua tena kibao kimekugeukia mwenyewe.

“Nataka kukueleza uchawi wa kisasi una nguvu sana, hata kama nitaiteketeza familia yake, bado kuna watu wangebakia na kwenda pande za dunia, lazima wangekubaliza tu, uchawi unazidiana.”
“Sasa nifanyeje?” nilijikuta nikihamishwa kwenye dhamira yangu.
“Sikiliza siku zote vita huwa haina kikomo, pia uganga unazidiana naweza kusema mimi ni zaidi kuna mwingine akawa zaidi yangu na kuweza kukuteketeza kama pamba na moto.”

“Nimekuelewa, sasa nifanyeje mzee wangu?”
“Jiepushe kuchukua uamuzi mkubwa kila wakati bila kujua madhara yake, kama unaweza kuua basi kuna wengine wanaweza kukuua.

Mfano watu hao wangekuja kwangu kulipa kisasi cha kuuliwa ndugu yao umebakia jina. Lakini siku hizi waganga tumekuwa tuna tamaa na kuwasilikiza wateja bila kuangalia mbele atapatwa na nini. Wengine wanajua kabisa alichokufanyia ni bomu litakalokuypasukia mbele lakini kwa vile wana tamaa ya fedha wanafanya tu na kukuachia likulipukie.

Kama mwanamke hatulii mbona zipo dawa nyingi tu za kumfanya atulie. Kwa nini mkimbilie kuua?
Sawa niwaue wabaya yako, umerudi nyumbani mkeo kafanya ujinga wake utaua wangapi?”

“Mzee wangu yaani hata sijui nahitaji msaada wako,” nilijikuta nikizidi changanyikiwa nilijiuliza yule kweli mganga au ndiyo yamemshinda akaamua kunitisha. Lakini kwa upande mwingine nilikubaliana naye hakuwa tofauti na alivyo nishauri Simon.

“Kijana wangu nataka nikuase na waganga wenzangu, tujiepusheni kutoa roho ya kiumbe ovyo. Kulipa kisasi sawa, lakini hata chuki tu za kibinadamu. Mganga mzuri ni yule anayekushauri madhara ya kitu unachotaka kufanya.

“Mfano tatizo kama lako lililojirudia mara mbili bado wanaua watu. Hii ndiyo sababu hata dini zinaona kuwa waganga wa jadi ni chukizo la Mungu kwa waganga wenye tamaa na wasio zingatia taaluma.
Wamejisahau na kuendekeza tamaa kumbe kazi yetu kutibu na si kuua ovyo. Najua utashangaa mganga kama mimi kukataa kuua?”

“Hapana mzee najua nimefanya makosa naomba msaada wako,” maneno ya mganga yalinibadili na kujiona nimefanya makosa makubwa kutoa roho za watu kwa ajili ya mwanamke. Nijifikiria kama ningesikiliza rafiki yangu Simon nisingempoteza baba na mwanangu.

“Sasa hivi umeishakuwa mchawi, najua kwa dhamira yako upo tayari hata kula nyama ya mtu ili kumfurahisha mkeo. Hivi uliposikia mtu uliyemroga amekufa ulijisikiaje?”

“Kwa kweli mzee naomba unisaidie, maneno yako yamenichanganya sana hata sijui nijibu nini, moyo unaniuma sana kwa yote niliyoyatenda.”

“Sishindwi kukufanyia unachotaka, lakini mbele kuna vita kubwa ambayo itakufanya ufe kifo cha aibu. Baada ya kifo cha mwisho cha mwanao, ni baada ya kumzika mama yako na mkeo, ungekuwa chizi na usingepona kwa mganga yoyote mpaka unakufa kifo cha aibu.”
“Mungu wangu!” nilizidi kuchanganyikiwa.

“Usiseme Mungu wangu! Kuna watu katika familia ile hawafi cha mzizi wala kafara mpaka kudra ya Mungu. Lazima nao baada ya tukio la kupukutika kwa familia yao, wangepita juu chini kukumaliza. Siku zote vita haina udogo.”
“Nimekusikia mzee wangu, nifanyeje sasa?”

“Kijana wangu, sawa unampenda mkeo, tatua tatizo la mkeo si kukimbilia kuua, kama nilivyo kueleza zipo dawa nyingi na moja nitakupa hutaamini, kama mkeo akitembea tena nje njoo uvunje mikoba yangu.

“Kama haya ninayo kwambia unaona nakudanganya, nenda popote kwa mganga makini utakuta wewe ndiye uliyemuua baba yako na mwanao.
“Waganga wengi tumekuwa tunaangalia tatizo bila kuangalia chanzo cha tatizo. Matokea yake wamekuwa wanakimbilia kuua tu.

Kama ungekuwa umeonewa kweli, ningekufanyia kazi ambayo hakuna yeyote angeingiza mkono kila mtu asingekuona. Ningetengeneza kiza ambacho wangekwenda mashariki na magharibi wasingeona kitu.”

“Mzee wangu nimekusikiliza vizuri na nimekuelewa, utanisaidia vipi?”
“Nitakusaidia kuyaondoa maisha wa mama na mkeo katika ndizi kisha nitakupa dawa ya kumtuliza mkeo.

Nina imani ukiondoka hapa utatulia na mpenzi wako najua unampenda basi tatizo limekwisha ila jiepushe kupenda kuua damu ya watu nyingine ni nuksi unaweza kuandamwa na matatizo kila mganga halioni kwa vile aliyetenda kesha kufa.”
“Mzee wangu nakuapia kwa Mungu sitarudia tena nikitoka hapa nakuwa kiumbe kipya.”

“Wapo waganga wanasifika kwa kuua lakini, mimi nasifika kwa kutibu yakiwemo matatizo kama yako.”
“Nashukuru mzee wangu, nimejifunza kitu. Naamini nitakuwa mwalimu mwema kwa wengine.”

“Fanya hivyo ili tupunguze mauaji yasiyo na sababu, kazi ya Mungu tumuachie Mungu, toka nianze uganga sijawahi kuua na sitaua.”

Baada ya makubaliano mganga alituomba tukapumzike nje ili kusuburi muda wa kufanya kazi yangu. Tulitoka kwenda kukaa sehemu ambako tuliletewa maziwa na viazi vya kuchemsha.

Kwa vile tulikuwa hatujala toka asubuhi tulishambulia chakula chote. Baada ya chakula tulioneshwa sehemu ya kupumzika kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana. Kutokana na uchovu wa safari tulilala mpaka siku ya pili.

USIKOSE SEHEMU YA MWISHO ITAKAYOKUJIA KESHO.
 
Doh!

Kisa chakaribia tamati, kama movie vile
 
SEHEMU YA MWISHOOO.

Kwa vile tulikuwa hatujala toka asubuhi tulishambulia chakula chote. Baada ya chakula tulioneshwa sehemu ya kupumzika kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana. Kutokana na uchovu wa safari tulilala mpaka siku ya pili.
****

Siku baada ya kupatiwa kifungua kinywa cha uji wa maziwa na viazi, tuliitwa kilingeni, baada ya kukaribishwa na kukaa kwenye ngozi ya chui mzee Ngugude alichukua ungo na kuuweka mbele yetu ndani ya ungo kulikuwa na ndizi saba.

Mbili zilikuwa zimeoza, mbili zilikuwa zimeiva sana na kuanza kubadilika rangi na kuingia weusi kwa mbali na mbili zilikuwa zimeanza kuiva na moja ilikuwa mbichi kabisa.

“Unaziona ndizi hizi?” aliniuliza huku akinisogezea ungo mbele yangu.
“Ndiyo mzee wangu,” nilijibu huku nikizitumbulia macho.

“Umegundua nini?”
“Sijagundua kitu,” nilisema huku nikitikisa kichwa kusisitiza sijui.
“Basi hii ndiyo familia yako.”
“Familia yangu?” nilishtuka kidogo, japokuwa sikumwelewa.

“Ndiyo.”
“Una maanisha nini kusema hii ndiyo familia yangu?”
“Ulipokwenda kwa mganga alikueleza nini kuhusiana na ndizi?”
“Alisema familia yangu imetegewa uhai wake kwenye ndizi.”

“Basi ndizi zenyewe ndizo hizi, nimefanya kazi kubwa kuzivuta, kwa kweli kazi hii ilikuwa ngumu, ngumu sana. Nimekesha kwa kazi hii lakini nimefanikiwa. Kabla ya kufanya kitu chochote nilitaka uone ili niifanye hii kazi.”

“Kwa hiyo hapa panakuwaje?”
“Kazi iliyopo ni kuitoa sumu katika ndizi ili kuyafanya maisha ya familia yako yaondokane na uchawi uliotegwa kwenye ndizi.”
“Sawa mzee.”
“Unaona ndizi hizi mbili zilizooza?”
“Ndiyo.”

“Basi hizi ndizi, ndiyo baba yako na mwanao waliofariki, na hizi zilizoiva sana?”
“Ndiyo naziona.”
“Hizi ndiyo mkeo na mama yako, si unaona zilikuwa zikiendelea kuiva.”
“Ndiyo.”

“Basi zingeoza lazima ungepoteza watu wawili kwa mpigo japo ingechukua muda kutokana na kinga uliyopewa mwisho, hizi zilizoanza kuiva?”

“Ndiyo naziona.”
“Hizi ndizo wanao waliobakia, nao walikuwa wakiiva taratibu japo wasingedondoka, lakini wangeoza na kufa kwa mpigo.”

“Mungu wangu!” nilishika kichwa.
“Usishike kichwa hapa nakuonesha ubaya wa kisasi, ungeweza kufanikiwa kuongeza idadi ya vifo vya watu, lakini matokeo yake yalikuwa haya, ungeipoteza familia yako na wewe kuwa chizi,”
“Na hii ndizi mbichi?”
“Hii ndiyo wewe, ukweli walikushindwa na kukubali wameshindwa. Unaiona hii ndizi pembeni?”

“Ndiyo.”
“Unaona nini?”
“Kuna mistari mweusi kama chale.”
“Basi haya ni makombora yaliyotumwa kukuozesha. Lakini mwili wako umekuwa imara kinga iliyofanyika chini ya mti mkuu ndiyo iliyokulinda.

Kinga yako ingekuwa ya kawaida ya kuchanjwa tu ungebakia jina.”
“Sasa mzee wangu utanisaidiaje?”
“Kuhamisha sumu toka kwenye miili ya familia yako huku ukiona mwenyewe kwa macho yako.”

Alichukua ndizi mbichi nne na kuziweka kwenye ungo mwingine kisha alichukua dawa ya unga mweupe na kuzimwagia zile ndizi taratibu huku akinuiza maneno anayoyajua mwenyewe. Baada ya muda aliweka ungo wenye ndizi mbichi pembeni ya ungo wenye ndizi alizosema ndiyo familia yangu.

“Unauona ungo huu?”
“Ndiyo.”
“Una nini?”
“Una ndizi mbichi.”
“Ngapi?”
“Nne.”
“Vizuri,” alisema huku akichukua ndizi zilizooza na kuzitupa pembeni na ndizi mbichi akiiweka kwenye kikapu.
“Sasa nataka hizi ndizi ziwe kama hizi na hizi ziwe kama hizi.”

“Sawa mzee wangu.”
Aliuchukua ungo wenye ndizi mbichi na kuuweka pembeni ya ungo wenye ndizi zilizoiva na kutulia.

“Naomba macho yako yasicheze mbali asijesema nimebadili ndizi.”
Nilitumbulia macho ungo wenye ndizi mbichi, kila dakika nilishindwa kuelewa ghafla nilijikuta nikichanganyikiwa baada ya kuona ndizi zimebadilika na kuhamia ungo mwingine.
“Umeona nini?” mzee Ngugude aliniuliza.

“Sielewi.”
“Huelewi nini?”
“Naona kama ndizi zimehamia huku.”
“Hapana hazijahama bali sumu nimeitoa na sasa ndizi zilizokuwa ungo huu zimerudi katika hali ya ubichi.”
“Kwa hiyo.”

“Ubichi huo ni uhai. sasa hivi vifo katika familia yako vitatokea kwa amri ya Mungu na si mkono wa mtu.”
Baada ya kusema vile, alichukua unga mweupe na kunyunyizia. Alipomaliza alinieleza niende kuoga maji yaliyokuwa na dawa ili kuondoa mikosi ili nijiandae na safari.

Nilifanya kama alivyonielekeza baada ya kumaliza zoezi lile, alinipa unga mweupe aliyonieleza nibuye kidogo na mwingine niupulize kama kusafisha njia. Nilifanya kama alivyonielekeza kwa kubuya unga kidogo, unga ulikuwa na ladha kama unga wa ngano. Nilipoliza tulipewa ruksa ya kurudi nyumbani Tanzania.

Tulisafiri salama mpaka Mtwara na kuagana na mkalimani wangu ambaye nilimlipa kiasi tulichokubaliana, kutokana na kazi kubwa aliyofanya nilimuongeza kiasi kingine kama asante.

Kwa vile tulifika jioni sikutaka kulala pale Namoto nilikwenda kulala Mtwara mjini ili siku ya pili niondoke na mabasi ya asubuhi.
Siku ya pili asubuhi nilipanda basi kurudi Dar ili niunganishe mpaka nyumbani siku ileile.

Nikiwa ndani ya basi bado nilikuwa na maswali kuhusiana na maneno ya mzee Ngugude, niliyaona kama yanajichanganya. Kuna wakati aliniambia anaweza kuua na kuna wakati alisema hajawahi kuua kwa kweli maneno yale yalinishtua na kuona kama uwezo wa yule mzee ni mdogo tofauti na sifa zake.

Moyoni niliamini kama ningemkuta bi Nyangunda ningeweza kuwakomesha wabaya wangu. Pamoja na kukubaliana na yule mganga niliamini bado nilitakiwa kwenda ndani zaidi. Nilifika Dar jioni na kunganisha safari na kufika nyumbani saa tano usiku.

Nilipofika nyumbani nyumba ilikuwa kimya kuonesha wamelala. Nilipogonga mlango nilifuatwa na mke wa jirani yetu aliyenieleza kitu cha kushtushwa kwamba watoto wangu wako kwake. Niliulizia mama yao yupo wapi, niliambiwa yupo hospitali pamoja na mama yangu wapo chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

“Mungu wangu tatizo nini?”
“Jana waliugua ghafla, kwa kweli hata hatujui ule ni ugonjwa gani.”
“Wapo kwenye hali gani?” niliuliza macho yamenitoka pima.
“Tumuombe Mungu tu hata sijui niseme nini toka jana hatujafanikiwa kuwaona,” alisema kwa sauti ya huzuni.

Nilibakia nimesimama kwa dakika tano nisijue nifanye nini. Bila kujielewa nilijikuta nimekaa chini bila kupenda huku nikiwa na mawazo mengi kuhusiana hali ile ya kufikia mke na mzazi wangu kurudiwa tena na tatizo.

Wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa huenda mabadiliko ya mzee Ngugude ya ndizi ndiyo yaliyosababisha yote yale. Bila kuongeza neno nilinyanyuka mzimamzima ilipokuwa nimekaa na kukimbilia hospitali.

Nilikwenda moja kwa moja hadi hospitali kwenye wadi ya Wagonjwa mahututi na kuelezwa wametolewa na kurudishwa wadini ya kawaida. Nilipotaka kuwaona nilikatazwa na kuelezwa nirudi kesho yake kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana hivyo wagonjwa kwa muda ule hawakutakiwa kuamshwa.

Kauli ile sikukubaliana nayo nilijua ni kunifariji lakini mama na mke wangu walikuwa amekufa. Nilijikuta nikiangua kilio mbele ya daktari wa zamu na wauguzi kitu kilichowafanya wanishangae.
“Sasa unalia nini wakati tumekueleza uje kesho?” daktari wa zamu aliniuliza huku akionesha kunishangaa.

“Nije kesho kufanya nini ikiwa mama na mke wangu wameisha kufa?”
“Jamani mbona haya makubwa! Tumekwambia wapo salama ila sasa hivi wamelala. Kutokana na hali waliyokuja nayo ya nusu wafu tumewaacha kuangalia afya zao kwanza, bila hivyo ungewakuta nyumbani.”

“Si kweli, wamekufa ila mnanificha,” niliendelea kulia huku nimekaa chini.
“Kaka hakuna aliyekufa hebu ngoja tukawaamshe uwaone ili uridhike japokuwa si sheria kumuamsha mgonjwa aliyetulia kwa ajili ya mtu kumuona tu.”

Kauli ile ilinifanya ninyamaze kidogo, baada ya muda niliitwa na kuingia wadini. Sikuamini nilikutana na mama na mke wangu wapo kwenye hali nzuri kabisa.
“Umeamini?” daktari aliniuliza.

“Hapa nimeamini, mara nyingi mtu akiingia ICU huwa hatoki salama.”
“Haya baba waache wagonjwa wapumzike njoo kesho.”

Niliagana na wagonjwa wangu na kurudi nyumbani nikiwa na maswali mengi kuhusiana hali iliyowatokea. Nilikumbuka kitu maneno niliyoelezwa na mzee Ngugude kuwa kuna hali itatokea na kuwatisha watu lakini ni ya kawaida ni ya kuyabadili mauti kurudi katika uhai.
Mwanzo sikuelewa kutokana na kuchanganyikiwa, niliamini nilichoelezwa ndicho kilichotokea.

Baada ya siku mbili walitoka hospitali wakiwa wazima wa afya. Kitendo kile kilinifanya nibadili mawazo na kuona hakuna haja ya kuendeleza vita ya kisasi. Niliyakumbuka maneno ya marehemu baba kuwa hakuna mwanadamu mwenye uwezo kama Mungu hivyo tulitakiwa kumuabudu yeye.

Alinieleza kwa dini yake kisasi ni haki lakini kusamehe ni bora zaidi. Niliamini ule ulikuwa wakati wa mimi kujikabidhi kwa muumba ili nizaliwe upya. Niliendelea na shughuli zangu kama kawaida huku nikiwa nimejifunza vitu vingi katika maisha yangu.

Niliamini hakuna vita ndogo pia moto hauzimwi na mafuta. Siku zote tulihusiwa kusamehe ili kurudisha amani, pia unapolipa jema kwa baya, ubaya hukosa nafasi lakini ukilipa baya kwa baya vita yake haina mwisho.

Nilijifunza kitu kimoja kikubwa kuhusu mwanadamu kuingilia kazi ya Mungu, kuua ni kazi ya Mungu kuingilia kazi hiyo ni kujiingiza kwenye dhambi ya kujitakia. Uwezo wa kuumba na kuua ni wake yeye peke yake.

Hata unayemuua ukimwacha lazima atakufa tu kwa nini umuue?
Nina imani wengi mmesoma mkasa wangu tokea mwanzo mpaka leo nilipofikia tamati, napenda kuwaomba wote tusikimbilie kuua au kumroga mtu kwa ajili ya mwanamke kwa vile mke au mume bora hutoka kwa Mungu si kwa mapenzi ya mwanadamu.

Kama mwanamke si muaminifu mkanye kama ukishindwa mwache au mtenge, lakini usiue kwa ajili yake. Japo wengi tunaamini waganga wa asili ni wabaya, lakini kama watatokea waganga kama mzee Ngugude dunia itakuwa salama.
Namalizia kwa waganga wa asili, jina lenu linaweza kuwa baya kwa watu kutokana na kuonekana nyie ndiyo chanzo cha matatizo kati ya mtu na jirani yake hata familia kwa familia.

Mganga siku zote anatibu, anayeua au kumroga mtu huyo ni mchawi ni makosa kumwita mganga. Basi chagueni moja kuwa wachawi au waganga. Namalizia kwa kumuomba Mungu anisamehe kwa yote niliyoyafanya kwa ajili ya mke wangu, kwani niliisha kuwa mchawi kamili nilifikia hatua mbaya ya kuroga na kuua pia nilikuwa radhi hata kula nyama ya mtu kwa ajili ya mke wangu.

Najua hukumu yake kwangu ni kubwa lakini kupitia ukurasa huu najutia kila nilichokifanya. Nakuombeni katika mkasa huu chukueni mazuri na mabaya muyaache kwa vile kusudio la kuutua mzigo mzito uliokaa moyoni mwangu ilikuwa kuhakikisha makosa yangu hayarudiwi na mtu mwingine.

Namalizia kwa kuwashukuru wote mliokuwa nami mwanzo hadi mwisho wa mkasa huu, Mungu awabariki, asanteni.

MWISHO
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…