Simulizi: Kwanini Umenizaa? (Sehemu 1)

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,882
KWA NINI UMENIZAA?

Na, Robert Heriel.
Taikon wa Fasihi.

" Mama! maama! maaa,,."
Aliita kwa sauti ya kukwaruza huku akimtingisha Mama yake aliyekuwa amelala. Mama aliamka kwa uchovu akamtazama mwanaye huku akijitahidi kuvuta miayo ambayo nayo ilikataa kuvutika.

" Nina Kiu ya maji Mama"
" Doso mwanangu..!"
Mama Doso alitaja jina la mwanaye kisha akakaa kimya huku akimtazama Doso kwa macho ya huruma yaliyokata tamaa. Kitambo kidogo walikuwa kimya jua kali likiwakaanga katikati ya vichaka mahali walipokuwa wamejificha.

Hawakupenda kuwa mahali pale ambapo palikuwa ni hatari kwa uhai wao. Mahali ambapo wanyama wakali wa porini wangeweza kuwadhuru.

Lakini ilikuwa ni bora zaidi kujificha kwenye vichaka vile kuliko wangebaki mjini wakauawa. Wakauawa? Ndio wakauawa na watu wenye roho za kinyama zisizo na huruma.

Kama ni kulia Doso alilia jamani. Alilia kwa siku saba mfululizo mpaka sauti ikakauka. Alitoa machozi mpaka akiba yote ya machozi ikaisha, Alichobakiza ilikuwa kuachama mdomo na kuwasha jicho ambalo lilikuwa jekundu kwa sababu ya kulia na mchanga wa jangwa lile.

" Mama nina njaa.."
Doso alifungua kinywa chake kwa mara nyingine tena, kutoa malalamiko ya njaa kwa Mama yake. Malalamiko ambayo yeye mwenyewe alijua kuwa mama yake hana chakula cha kumpa.

Hawakuwa na chakula wala hawakuwa na maji, Vyote viliishia njia walipokuwa wakikimbia kifo kilichokuwa kinawafukuza kwa hamu na famu. Mama Doso alimuangalia Mwanaye, Doso.

Wakatazamana huku macho yao yakiwa tepetepe kwa machozi ambayo yalikuwa yapo tuu mlangoni mwa macho yao.

" Doso Mwanangu, hapa hatuna kitu. Sio maji wala sio chakula. Vyote vimeisha. Hata nguvu zenyewe za kukubeba nazo zimeisha. Nakumbuka nilikubeba miezi tisa tumboni lakini leo hii siku saba nimechoka sana"

Masikini Mama Doso aliongea maneno hayo kwa uchungu usiolezeka. Midomo yake ilitetemeka. Uso wake ulijawa na sumu ya huzuni. Alimuonea huruma mwanaye. Ndio kwanza alikuwa na miaka nane anapatwa na madhila makubwa kama haya.

Doso alifumba macho akavuta pumzi nyingi kisha akaiachia taratibu huku macho yake akiyafumbua. Aligeuka upande huu na upande huu akaona jinsi ukame ulivyoharibu nchi.

Hapo akaona mifupa ya mnyama aliyekufa siku zi nyingi akiwa anashambuliwa na Nzi. Upande wa mbele mbali kidogo akaona maiti ya mtu ikiliwa na ndege wala mizoga.

Hapo uchungu ulimshika, alitaka kusimama lakini mama yake akamzuia. Alitaka akawafukuze wale ndege wasile maiti.

Doso alivuta kumbukumbu ya siku moja iliyopita. Alikumbuka jinsi watu waliovalia nguo nyeusi juu mpaka chini wakiwa wameficha nyuso zao walivyoua watu katika mji wao.

Watu wale walikuwa hawana huruma hata chembe jamani. Filamu ya kumbukumbu ilimpitia Doso akawa kama anaona tukio moja kwa moja: Alimuona mtu mmoja mrefu mwenye umbo kubwa kama pipa akiwa ameshika shoka mkononi.

Mtu yule aliingia ndani ya nyumba moja ya nyasi kisha punde akatoka akiwa amemkamata Mama mmoja na mtoto wake.

Yule mtu mwenye kutisha akamnyang'anya yule mama mtoto kisha akamtupa chini yule mtoto. Mama kuona mtoto wake katupwa chini akamkimbilia lakini kabla hajamfikia mtoto masikini shoka lilifyeka shingo yake, kiwili wili kianguka huku kichwa kikaangukia karibu na yule mtoto.

Kile kichwa bado kilikuwa kinauhai. Macho na mdomo ya kile kichwa cha yule Mama aliyekatwa vilitazamana na mtoto wake.

Doso alikiona kile kichwa kikijaribu kusema jambo bila ya sauti. Hatimaye kilifumba macho. Lile jitu lenye roho mbaya kama shetani likamsogelea yule mtoto.

Kisha likanyanyua shoka juu na kumpasua yule mtoto vipande viwili kama gogo. Hapo Doso akapiga kelele. looh! Kumbe alikuwa anakumbuka. Mama yake alimkumbatia akawa anambembeleza.

Doso akiwa amekumbatiwa na Mama yake akaanza kuimba;

"Mawingu meupe pee, mawingu meupe pee!"
Yanapepeswa pee, yanapepeswa pee!
Hurandaranda wee, huranda randa wee!
Huku na huku yee, huku na huku wee!

Mawingu wapi Mvua, Mawingu wapi upinde?
Mawingu twafa njaa, Mawingu njo tusikonde,
Twatapa tapa paa, Twatapa tapa ndee,
Huku na huku njaa, huku na kule ndee

Mawingu nibebe, unipeleke mbali,
Juu juu unibebe, chini njaa kali,
daima ni.shibe, kula isiwe swali,
Mawingu nikinge, Juu jua kali,


Doso aliweka kituo kisha akameza fumba la mate akijinasua kwenye kumbatio la Mama yake. Kisha akasima mbele ya mama yake, akamtazama, kisha akasema

" Angani naona mawingu na Jua, natamani ningezaliwa juu ya yale mawingi. Nikaishi kwenye jua lile linalowaka(analitazama akiwa amefinya macho yake kutokana na mwanga mkali wa jua). Kule nisingepata shida. Kule nisingeona njaa. Kule nisingeona watu wakiuawa kinyama kiasi kile"

Doso anaacha kuongea na kulitazama Jua kisha anamsogelea mama yake anamtazama. Mama yake anamuangalia Doso, anayashusha macho yake mpaka alipofikia mbavu za Doso. Looh! Doso alikuwa amekonda sana. Mbavu zake zilikuwa zinaonekana na kuhesabika kabisa.

" Mama! Ulinizaa ili nije kuteseka? Je ulizaa ili nije kuona watu wakifa kwa njaa? Au ulinizaa ili nije kuona wanyama wakianguka kwa kiu? Mama..!"

Doso aliongea kisha akasogelea sikio la Mama yake. Akanong'ona kwenye sikio la Mama yake:
"Haya ndio ulitaka niyaone nikija dunia? Ulitaka nione mito ya damu inayotokana na vita? Ulitaka nione watu wakidhulumiwa? Ulilenga nini Mama?"

Doso ananyamaza huku akiondoka kwenye sikio la Mama yake. Kisha anapiga hatua tano kama mtu anayeondoka. Mama yake anataka kumuuliza swali kuwa anaenda wapi lakini kabla hajamuuliza Doso anasimama na kumgeukia Mama yake.

Anatabasamu kisha anaachia kicheko kinachofanya nzi waliokuwa wakisherekea mzoga kuruka kwa kushtushwa na sauti ya kicheko cha Doso. Kisha anaanza kuimba huku akicheza:

" Mimi na Mama, leo porini,
kutwa twahama, pori kwa pori,
Dunia Gharama, siye ndiye mihuri,
usipochutama, waitwa kiburi"

Doso anaacha kuimba muda huu anacheza huku aking'ata meno yake.
"Huyo! Huyo! Huyo! Hee! Hee! Hee!"
Mama yake anamukea biti huku akimpigia makofi kumpa munkari.

Doso naye hakuwa nyuma, sasa alijibinua na kujiviringa akicheza ngoma za asili ya Kiafrika katikati ya Jangwa lenye ukame huku njaa ikiwatafuna katika matumbo yao.

Doso anainama chini kuokota kijiti na kukishika kama kipaza sauti kisha akaanza kuimba:
" Ulinizaa ili nije imba huku porini wee!
(onana) Nawe unitazamee heeee! (Onana),
Ona vichaka, tazama anga, vyote vinatazamaaa,
Jinsi navyoimba(aah) Jinsi navyo cheza(oooh), Mamaaa weee!"

Doso anaacha kuimba anacheza huku akihema kwa nguvu akiwa amechoka kutokana na kutumia nguvu nyingi kuimba. Anatweta kwa pupa huku akishika kifua chake.

Masikini Doso anaishiwa na nguvu. Akawa anapiga hatua za kichovu akiwa kalegea. Dooh! anataka kuanguka lakini Mama yake anawahi kumshika.

"Doso..! Mwanangu Doso"
"Mama.. Maama. Ulitaka nije kuona watu wanavyohangaika na magonjwa kama UKIMWI na Saratani? Ulitakaje. Mbona siku zote huniambii? Au nione jinsi ajali na majanga yakiondoa na kuharibu maisha ya watu? Maama..."

Doso aliongea akiwa kapakwata na Mama yake mapajani huku akiwa ameyatoa macho mdomo wake ukiwa umechongoka kwa kuchoka na njaa.
Kisha akasema:

"Mama Kwa nini Ulinizaa"
Hapo akafumba macho.
" Doso... Dosoo! Amka Doso. Amka nikujibu mwanangu. Amka nikuambie kwa nini nilikuzaa"

Mama Doso aliongea lakini Doso alikuwa kapoteza fahamu.

Embu tuone PART TWO kuwa Mama Doso atamjibu nini mwanae kuwa "KWA NINI ALIMZAA?"

Usikose sehemu ya pili.
Ulikuwa nami:

Robert Heriel,
Taikon wa Fasihi,
Kutoka Nyota ya Jibi,
0693322300 au 0711345431

mtot.jpg
 
Yaani baada ya kujibu utajikuta unalia tu. Yaani kuna hali nyingine usiombe upitie ni Mungu tu ndiye anayejua hatma zetu kwakweli.

Ukitaka hilo swali hilo likupe Bp uulizwe wakati wa matatizo makubwa kama maradhi, vita na njaa. Tena uulizwe na mtoto wa miaka chini ya kumi. Unaweza ukafa
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom