SIMULIZI:JUMBA LA MUUAJI

JOTO LA MOTO

JF-Expert Member
Apr 11, 2018
758
551
MTUNZI:MSANII JOTO LA MOTO
SEHEMU YA KWANZA

MSITUNI-JIONI
Hali ya utulivu imetawala, huku sauti za Ndege na mivumo ya matawi ya miti inayopulizwa na upepo ikisikika, mara unasikika MNGURUMO WA PIKIPIKI INAYOKARIBIA.

Zinapita sekunde chache inafika PIKPIKI KUBWA NYEUSI na kusimama mita chache kutoka lilipo jumba moja la kizamani na lililochakaa lililotelekezwa kwa muda mrefu katikati ya msitu mnene.

MAKI OVA, kijana, 30, yupo juu ya Pikipiki, anavua Helmeti, akionekana mwenye wasiwasi anaangalia huku na kule.

Polepole anashuka kutoka kwa Pikipiki ile na kujongea kwenye jumba lile. anafika kwenye uwazi unaoashiria kuwa lilikuwa ni sehemu ya dirisha, anasita kwa muda wa sekunde kadhaa akiangalia huku na kule kwa makini, polepole anapanda na kuingia ndani.

NDANI YA JUMBA.
Maki ananyata polepole anafika kwenye mlango uliochoka, anausukuma pole pole na kwa umakini huku amejawa na uoga.

Mara macho ya Maki yanalipuka kwa mshtuko na uoga wa hali ya juu baada ya kuona mifupa(skeleton) ya binaadamu ikiwa kwenye muundo wa Mtu aliyeketi sakafuni na kuegemea ukutani.

Maki anatoa kitambaa mfukoni na kujifunga kuziba pua na mdomo wake kisha polepole anasogelea ilipo mifupa ile, anafika na kuchuchumaa kuangalia kwa makini.“Wee” Maki anatoa sauti kali ya mshtuko huku akiruka na kuanguka kwa mgongo baada ya kuona sehemu ya mkono wa mifupa ile kutaka kumshika usoni, “Shhh” sauti inasikika upande wa pili, Maki anageuka na kushangazwa na kundi la Mifupa(skeleton) waliosimama wakimuonesha ishara ya kuacha kelele huku wameweka kidole mdomoni, kwa haraka anajiinua kutoka pale sakafuni huku akihema kwa uoga.

Polepole anarudi nyuma, akionesha kama amechanganyikiwa, anaafika lilipo dirisha aliloingilia na kutoka kwa haraka.

NJE YA JUMBA.
Maki akiwa aliyejaa uoga anakimbilia ilipo Pikipiki na kupanda, anajaribu kuiwasha kwa mara kadhaa bila mafanikio.

Sauti ya Mtu anayeshusha pumzi kutoka nyuma yake inasikika na kumshtua, anageuka kwa haraka, na kupatwa na duwaa. ”Anko Ngabu” Maki anatamka kwa mshtuko na uoga, “umefuata nini huku?” anauliza NGABU kwa hasira, Mzee mwembamba mrefu wa miaka 80 hivi, “niliku..wa na..na pita”, anasema Maki akitoa sauti ya uoga yenye kigugumizi. “umeshajiharibia Maki” anasema Ngabu, “kwa vi..vi..pi Mjomba”, anauliza Maki, Ngabu anatikisha kichwa na kushusha pumzi, “ondoka” sauti kali na ya juu ya Ngabu inamuogofya Maki, Ngabu anaondoka kuelekea kwenye lile jumba, Maki anajaribu kuwasha Pikipiki tena, “achana na hilo dude na upotee” anasema Ngabu huku akiingia kwenye jengo.Maki anaacha Pikipiki na kuanza kukimbia.

NDANI.KWA MAKI-MCHANA
Maki ameketi kitandani akiwa anahema kwa uoga,MAINDA, Dada 25,ameketi pembeni na Glasi yenye maji mkononi, “sasa wewe huko ulifuata nini?” anauliza Mainda, “kuna taarifa nilitaka kuzihakiki” anasema Maki, “ili iweje Maki?” anauliza Mainda, “kama Watu hawathubutu kwenda huko wewe ndio unajifanya mjuaji sana ama?’ anasema Mainda. “Mainda..hili ni tatizo na ni lazima apatikane Mtu mmoja wa kutafuta ufumbuzi” anasema Maki, “kwa hiyo ndio umejitoa mhanga?” anasema Mainda na kumfanya Maki kumuangalia Mainda kwa kumkazia macho. “siogopi kitu..hakuna aliye zaidi ya Mungu kwenye hii Dunia..nataka nijue siri za lile jumba..nataka nijue siri ya Mjomba Ngabu”, anasema Maki huku akiwa amemkazia macho Mainda., Mainda anabaki ametulia kwa sekunde kadhaa, anashusha pumzi, “Maki mume wangu..nakutakia kila la kheri..ingawa najua unachokifanya ni jambo hatari”, anasema Mainda huku akimkumbatia Maki, “hilo nalijua” anasema Maki.

KATIKATI YA SHAMBA LA MIGOMBA NA KAHAWA-MCHANA
Watu kadhaa wamekusanyika.Wote wanasikiliza hotuba ya Kiongozi wa mazishi, Maki amesimama sehemu ya mwisho kwenye mkusanyiko ule, anamuona Mzee Ngabu, Mzee Ngabu anageuka na kumuona Maki, wanaangaliana kwa sekunde kadhaa.

”Ni wakati wa kurejea kwa Mungu…hii misiba inavyofululiza ni hali ya kuogofya hapa kijijini kwa kweli” anasema Kiongozi wa mazishi.

Maki anamuona Mzee Ngabu anaondoka, Maki pole pole anamfuata. Mzee Ngabu anafika mita kadhaa. “Mjomba” sauti ya Maki inaita, Mzee Ngabu anaendelea kwenda, “Mjomba Ngabu” Maki anaendelea kuita, Ngabu anaendelea kwenda, Maki anaanza kumkimbilia Ngabu, anamfikia. “bila shaka na huu msiba kuna mkono wako Mjomba”, Ngabu anasimama kwa muda akimuangalia Maki, “usinifanye nijutie kukuacha salama nilipokukuta kule juu Maki” anasema Ngabu, “usinitishe Mjomba…zama za kutishika zilishapita..kwa sasa yupo ninayemtumainia..simuogopi Binaadamu” anasema Maki, Ngabu anaondoka, Maki anabaki amesimama, “mwisho wako upo karibu Ngabu” anasema Maki kwa sauti ya chini.

...........Itaendelea.........
 
Back
Top Bottom