Simulizi: Fimbo ya mbali

Simulizi: Fimbo ya mbali

JOTO LA MOTO

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2018
Posts
766
Reaction score
562
SCRIPT ZA IMA.


Ray 7.png
Irene.png


SEHEMU YA KWANZA.

TITLE:
FIMBO YA MBALI.

MTUNZI: IMA WA JONI A.K.A MSANII JOTO LA MOTO.

TEL.0788 135 198.



OFISINI KWA RAY-JIONI.
Ray na Hemedi, vijana watanashati, Ray, 32, na Hemedi, 29, wapo ofisini, Ray akiwa kwenye kiti kikubwa akitumia computer ya mezani na Hemedi akiwa kwenye moja ya viti vilivyopo mbele ya meza akisoma kadi,Ray anashusha pumzi, "hawa jamaa nao si wamechomoa" anasema Ray, "nilishakwambia bila baraka ya dingi zitaendelea kudunda" anasema Hemedi, "hamna kitu" anasema Ray, "nakwambia ukweli" anasema Hemedi, "hiyo ni proposal ya tano unadunda Ray" anasema Hemedi,"hujui unachoongea Medi" anasema Ray, wanabaki kimya kwa muda Ray akiendelea kutumia computer na Hemedi anasoma ile kadi, “sasa hii pati utaendaje na imeandikwa bibi na bwana?” anauliza Hemedi, “sio lazima kwenda bibi na bwana” anasema Ray, “lakini kila mualikwa atakuwa na mwenzake Ray” anasema Hemedi, “itabidi nikutafutie patna wa kwenda nae?” anasema Hemedi,“hebu naomba tuachane na huo mjadala Medi…maana najua unapoelekea” anasema Ray,”mimi nilichokuitia ni hiki” anasema Ray huku akiinua lap top iliyopo pembeni pale mezani na kumpatia Hemedi, “badilisha hiyo program” anasema Ray, “kama nitaipata kesho itapendeza zaidi" anasema Ray, “nitaileta asubuhi..kabla ya saa nne” anasema Hemedi, “kesho sitokuwepo ofisini..nitaenda Moshi kumuona mzee” anasema Ray, “nitaipitia kwako nikirudi” anaongeza Ray, “poa” anajibu Hemedi, “fundi wa TV ulimpata?” anauliza Ray huku anainuka, anachukua koti lake la suti nyuma ya kiti na kulivaa,“yupo kwako..ukifika utamkuta” anasema Hemedi huku anaibofya ile lap top, “sipitii home..naunganisha kwenye hiyo pati” anasema Ray huku anaweka tai yake sawa shingoni, anachukua funguo za gari kwenye droo na kuelekea mlangoni, Hemedi nae anainuka akiwa amebeba lap top na wanatoka

OFISINI KWA RAY-JIONI-NJE
Ray anaingia kwenye gari yake na kuondoka, Hemedi naye anafika kwenye gari yake, anaingia huku akiwa anabofya simu mkononi kwake, anaiweka sikioni.

NYUMBANI KWA RAY-SEBULENI SAA MOJA JIONI.
Mobeto, binti mrembo, 25, akiwa amevalia maridadi, sketi fupi laini iliyobana na kuchora vilivyo mwili wake ulioumbika vema, akiwa amejiachia kochini na glasi yenye juisi mkononi akiimalizia kwa funda moja na kuiweka glasi mezani, simu inaita, anaichukua na kuiweka sikioni, “sema Medi” anasema Mobeto, “huyu jamaa haji huko sasa hivi.. anaenda mount Meru kwenye pati” inasikika sauti ya Hemedi kwenye simu, “kwa hiyo” anauliza Mobeto, “hebu njoo home tuyapange upya” inasema sauti ya Hemedi kwenye simu, “poa” anasema Mobeto na kuitoa simu sikioni, “We mtoto” anaita Mobeto huku anainuka, baada ya sekunde mbili hivi anakuja Dulivan, kijana, 17, “bosi wako akija mwambie nitakuja kumalizia kazi kesho” anasema Mobeto, “hata kugusa hujaigusa hiyo TV” anasema Dulivan, “wewe inakuhusu nini?” anasema Mobeto, kwa ukali, “fuata maisha yako achana na yasiyokuhusu” anaongeza Mobeto huku akimnyooshea Dulivan kidole,“na ole wako umwambie Ray sijafanya kitu” anaendelea Mobeto huku akimkazia Dulivan macho, kisha anaelekea mlangoni,Dulivan anamsindikiza kwa macho huku akimng’ong’a, Mobeto anafungua mlango na kutoka, Dulivan anachukua glasi iliyoisha juisi pale mezani na kuondoka.

BARABARA YA MOSHI ARUSHA-MCHANA.
Toyota Harrier nyeupe ikiwa mwendo wa kasi inaenda na kufika getini nje ya nyumba moja nzuri, inapigwa honi geti linafunguka na gari inaingia, anateremka Ray na kuelekea mlangoni.

NYUMBANI KWA MZEE CHIRO, SEBULENI-MCHANA
Sebuleni yupo Blue, kijana, 28 Linah, dada 22, Monalisa, dada, 30 na Natasha,Mama, 60, wameketi kwenye makochi wakizungumza, mezani kuna jagi na glasi zenye juisi ya machungwa.
Ray anafika, “wasalam” Ray anasalimu, “salama bro” anajibu Blue na Mona, “vipi shem?” Linah anasalimia, “nipo poa shem” anajibu Ray huku anaketi kochini, “bro uko fasta” anasema Blue huku akiangalia saa yake “nusu saa kutoka Arusha?” anaongeza Blue kwa mshangao, “leo hakukuwa na tochi” anajibu Ray na wote wanaangua kicheko, “za Arusha?” anauliza Natasha, “nzuri tu mama..ila sio joto kama huku Moshi” anaongeza Ray, “Mzee yuko wapi?” anauliza Ray, “yupo ndani” anajibu Natasha, unasikika mlango unafunguka, “tena huyoo” anasema Natasha, sekunde chache baadae anafika Mzee Chiro, 70, akiwa amevaa fulana nyeupe na msuli na bakora mkononi akichechemea “shikamoo baba” wote wanasalimia, Mzee Chiro anabaki kimya anawaangalia, zinapita sekunde kadhaa bila kusema chochote kisha anageuza na kurudi alipotoka, Ray, Blue, Linah, Mona na Natasha wananaangaliana, Natasha anainuka na kumfuata Mzee Chiro.

NYUMBANI KWA MZEE CHIRO,CHUMBANI-MCHANA.
Natasha anaingia, Mzee Chiro ameketi juu ya kitanda “mbona umerudi tena ghafla Baba Ray na Watoto wamekuja kukuona?” Natasha anauliza,”unajua vizuri kwa nini nimerudi ndani mama Mona” anasema Mzee Chiro, Natasha anashusha pumzi, “ila sio vizuri ulivyofanya Baba Ray..Watoto wamesikia unaumwa wamekuja kukuona” anaongeza Natasha, Mzee Chiro anabaki kimya kwa muda, anashusha pumzi, “haya nakuja huko” anasema Mzee Chiro, “njoo bana..hayo mambo yenu mengine mtamalizana kwa muda wenu” anasema Natasha huku anainuka na kutoka.
Natasha anarudi sebuleni na kuketi, “Mzee anasemaje?” anauliza Ray, “anakuja..kuna kitu alisahau ndani” anamaliza kusema Natasha kisha inasikika sauti ya mlango ukifunguka, baada ya sekunde chache Mzee Chiro anafika pale sebuleni na kuketi,”Shikamoo baba” wote wanasalimia, Mzee Chiro bila kuitikia anabaki akiangalia chini, anainua kichwa, “hivi wewe Ray” Mzee Chiro anasema huku akimkazia macho Ray, “Mungu wangu” anasema Natasha kwa sauti ya chini huku akishusha pumzi “tatizo lako nini haswa?” anauliza Mzee Chiro, “jamani Baba Mona mbona hivyo tena?” anasema Natasha, “ona mdogo wako hapo” anaendelea Mzee Chiro huku akielekeza mkono kwa Blue na Linah, “amekuja na mkewe..na wana Watoto wao” anasema Mzee Chiro, muda huu wote Natasha amaejiinamia, “dada yako hapo Mona ana mume wake na Watoto” anaongeza Mzee Chiro, “kama mwenzetu upo upande wa pili si useme” anaendelea Mzee Chiro, Ray anashusha pumzi, anainuka na kuondoka, wote wanabaki wakimsindikiza Ray kwa macho anavyotoka “Ray” anaita Natasha, “muache aende” anasema Mzee Chiro, Natasha anainuka na kumfuata Ray.

NYUMBANI KWA MZEE CHIRO,NJE-MCHANA
Ray anatoka huku akitembea kwa haraka na kuingia kwenye gari na kuwasha, Natasha anatoka kwa haraka akikimbilia lilipo gari, “Ray” anaita Natasha, Ray anashusha kioo, “naomba tu umsamehe Baba yako Ray..nadhani hali yake unaiona” anasema Natasha,Ray anashusha pumzi, “Mama..nadhani nilishajieleza kila kitu vizuri kwa Mzee” anasema Ray, “wewe msamehe tu mwanangu” anasema Natasha, Ray anabaki sekunde mbili kimya, “hamna shida mama..uzuri mzee nimeshamzoea” anajibu Ray huku akiweka gia na kuondoa gari na kumuacha Natasha amesimama pale akisindikiza gari kwa macho, anatoka Mona akiwa na glasi ya juisi mkononi, anakuja hadi aliposimama Natasha, “sasa anavimba nini na amepewa ukweli” anasema Mona, Natasha anageuka na kumuangalia Mona kwa ukali, “sasa unamwambia nani?..mfuate umwambie” Natasha anasema huku anaondoka na kurudi ndani akimuacha Mona amesimama pale, Mona anapiga funda moja ya juisi kisha nae anarudi ndani.

BARABARANI YA MOSHI ARUSHA-MCHANA.
Gari ya Ray inaambaa ambaa barabarani na kuvuka kibao kinachosomeka KARIBU ARUSHA, Ray yupo garini akionekana yupo kwenye msongo wa mawazo, anaangalia saa yake kisha anachukua simu juu ya siti, anaibofya na kuiweka sikioni, “Hemedi..upo home niijie lap top?” Ray anauliza, “umeshatoka Moshi mara hii braza?” sauti ya Hemedi inasikika kwenye simu,”hivi ndio naingia Arusha” anasema Ray, “njoo tu mimi nipo kaka” sauti ya Hemedi inajibu, “poa” anasema Ray na kuitoa simu sikioni na kuirudisha pale pembeni kwenye siti ya abiria huku akiendelea kukanyaga mafuta.

NYUMBANI KWA HEMEDI-MCHANA.
Gari ya Ray inafika na kusimama, anateremka, anaenda mlangoni na kugonga, mlango unafunguliwa, anatokea Lulu, binti mrembo, 23, akiwa amejifunga kanga moja kifuani, Ray anashtuka na kubadilika usoni akionekana kushangazwa na hali anayoiona, “Hemedi yupo?” Ray anamuuliza Lulu, “yupo..karibu ndani” Lulu anajibu huku akiondoka pale mlangoni na kurudi ndani, Ray anabaki amesimama kwa muda kisha anaingia, anafika sebuleni na kuketi kwenye kochi, anabaki ametulia akiangalia muziki unaochezwa kwenye TV kubwa iliyopo mbele yake, Lulu anatokea akiwa na glasi mbili na chupa ya mvinyo, “karibu” lulu anasema huku anaweka zile glasi mezani, “Hemedi yuko wapi?” anauliza Ray, “yupo around anakuja sasa hivi?” anajibu Lulu, Ray anabaki anamshangaa Lulu kwa anavyokazana kuandaa vinywaji, “yupo huku ndani au yupo nje?” anauliza Ray, “ametoka kidogo lakini yupo njiani anarudi” Ray anashusha pumzi huku Lulu anamalizia kumimina mvinyo kwenye zile glasi, Ray anatoa simu na kuibofya, inasikika sauti ya kuashiria simu haipatikani,“ameacha mzigo wangu?” anauliza Ray, “hapana” anajibu Lulu, Ray anashusha pumzi na kuinuka, “vipi tena?” Lulu anauliza, “nitakuja wakati mwingine leo nina wageni nyumbani” anajibu Ray huku anaelekea mlangoni, “nina maongezi na wewe Ray” anasema Lulu kwa sauti iliyolegezwa ya ushawishi, “sio leo” anajibu Ray huku anafika mlangoni, anafungua mlango na kutoka, Lulu anabaki amesimama,anashusha pumzi kichovu na kujitupa kochini.

TULIZO BAR-MCHANA.
Gari ya Ray inafika na kufunga breki kali kisha anateremka kwa haraka na kuingia Bar, anasimama mlangoni kwa muda akiangalia huku na kule, anamuona Hemedi akiwa anacheza pool na wenzake, Ray anamfuata Hemedi na kumgusa begani, Hemedi anashtuka na kugeuka kumuona Ray, “naomba tuongee kidogo” anasema Ray, Hemedi anashusha pumzi, anaachia fimbo ya pool pale mezani na wanasogea mita chache kutoka pale, “unafanya michezo gani Medi?”Ray anauliza, “kivipi Ray..sikuelewi”? Hemedi anauliza huku anatoa pakiti ya sigara, anatoa sigara na kuiweka mdomoni, anatoa kiberiti cha gesi na kuiwasha, “kwa nini uliniambia upo nyumbani na hukuwepo?” anasema Ray, Hemedi anapiga pafu moja ya sigara kisha anashusha pumzi huku akiachia moshi mdomoni, “unajua tatizo lako nini Ray?” Hemedi anamwambia Ray, “huwa unapaniki hovyo” anaongeza Hemedi, “kwanza umemkuta Lulu geto?” Hemedi anauliza, “siwezi kuingia kwenye mitego yako ya kijinga Medi” anasema Ray, “Ray kama unamtosa hata demu kama Lulu basi lazima una tatizo” anasema Hemedi,”una maana gani?” anauliza Ray, “unahitaji msaada mkubwa Ray” anasema Hemedi, “isitoshe Lulu ndio kaniomba nimkutanishe na wewe Ray” anaongeza Hemedi, “sijali mtasema nini Medi..haya ni maisha yangu na nitaishi ninavyotaka” anasema Ray,”sio wewe..sio yeyote..hata baba yangu hawezi kunipangia cha kufanya” anaongeza Ray “mimi nina misimamo yangu Medi” Ray anaongeza, “misimamo gani Ray?” anasema Hemedi, “huyo Kidoti unayemtajataja yupo maili milioni moja huko” anasema Hemedi, “na sidhani hata kama kweli Kidoti ni demu wako Ray” anaongeza Hemedi, “hata kama angekuwa yupo kwenye sayari ya Mars..yule ndio chaguo langu full stop” anasema Ray, “msimamo” Hemedi anasema huku akisindikiza kwa kicheko cha kebehi, anapiga pafu moja la sigara, “naomba hiyo lap top” anasema Ray, “kazi yako tayari ila ipo home..nitaileta kwako jioni” anajibu Hemedi, Ray anaondoka, Hemedi anapiga pafu moja kisha anatoa simu anaibofya na kuiweka sikioni, “aise Mona mpango umefeli tena” anasema Hemedi, “imekuwaje?” inasikika sauti ya Mona kwenye simu, “sijui..namsubiri Lulu anipe stori” anasema Hemedi, “na tangu nimejuana na Ray sijawahi kumuona amevimba kiasi hiki..nusura tushikane mashati” anaongeza Hemedi, “pole” anasikika Mona kwenye simu,”ok narudi Arusha leo jioni nitakucheki..tutamnasa tu” anaongeza Mona kwenye simu, “poa” anasema Hemedi na kuitoa simu sikioni, kisha anaendelea kupiga pafu sigara yake.

NYUMBANI KWA RAY-USIKU.
Ray yupo sebuleni amechuchumaa ilipo TV akiibofya hapa na pale huku TV screen ikionyesha tu maandishi,”Duli” Ray anaita huku anainuka, anakuja Dulivan,”fundi amesema TV ina tatizo gani?” anauliza Ray, “alisema anataka mpaka wewe uwepo ndio atengeneze” Ray anashtuka, “ndivyo alivyosema mpaka mimi niwepo?” anauliza Ray, “hata mimi sikumuelewa yule dada bro” anasema Dulivan, “alikuwa ni mdada?” anauliza Ray kwa mshangao,”ndio bro” anajibu Dulivan, Ray anashusha pumzi na kujishika kiuno, “na leo ndio fainali ya Arsenal na barca” anasema Ray huku akielekea kochini na kuketi kwa muda kisha anachukua simu na kuibofya.

SK HOTEL CHUMBANI-USIKU.
Hemedi na Kajala, dada mrembo,25, wameketi juu ya kitanda wakiangalia video kwenye I pad, simu inaita, Hemedi anaichukua anaibofya na kuiweka sikioni, “sema Ray” Hemedi anatamka kwa bashasha, “hivi fundi wa TV uliyemtuma ni wa kike?” anauliza Ray, “kwani haiwezekani mwanamke kuwa fundi Ray?” anauliza Hemedi, “ok..sasa huyo fundi wako hakufanya chochote kwa hiyo inabidi nije kwako kucheki hii mechi” sauti ya Ray inasikika kwenye simu,“sipo home..nipo mahali kwenye kikao na client muhimu sana” anasema Hemedi, “we nenda tu funguo utazikuta pale kwenye..” anasema Hemedi kabla ya kukatishwa na sauti ya Ray, “hapana kama haupo home basi” anasema Ray, “au si uende pale City Bar wana bonge la screen” anasema Hemedi, “hapana siwezi kwenda kwenye lile danguro mimi” inasema sauti ya Ray, “ngoja tu nitafute namna nyingine“ inaongeza sauti ya Ray kwenye simu, “Ok poa kaka” anasema Hemedi na kuitoa simu sikioni, “ni Ray?” anauliza Kajala, “jamaa anaipenda Arsenal kuliko chakula” anasema Hemedi, “hivi ni kweli jamaa jongoo hapandi mtungi?” anauliza Kajala, “ndio mimi na Mona tupo kwenye utafiti" anasema Hemedi, huku akijiweka vizuri kuendelea kuangalia video inayocheza kwenye I pad aliyoishika Kajala.

NYUMBANI KWA RAY-USIKU.
Ray amejilaza kochini akiangalia mpira kwenye simu yake, “goli..dah” anapayuka Ray huku anainuka pale kochini, “Duli” Ray anaita huku anasimama na kuvaa jaketi lililokuwa pembeni, Dulivan anakuja, “fungua geti itabidi niende tu City bar kuangalia hii mechi” Ray anasema huku kwa haraka akielekea mlangoni na kutoka Dulivan akimfuata.
 

Attachments

  • Hmedi copy.jpg
    Hmedi copy.jpg
    75.5 KB · Views: 99
SEHEMU YA PILI
CITY BAR-USIKU.
Ray anaingia Bar, watu kadhaa wapo ukumbini wakiangalia mechi, anasimama anaangalia huku na kule kisha anakwenda kuketi kwenye siti anayoiona huku macho yote yakiwa kwenye TV kubwa iliyopo mbele ikionesha mechi ya Baca na Arsenal.

Airinpol, binti mrembo, 26, akiwa na warembo wenzake, Feti na Berta wameketi kaunta, Airinpol akiwa anavuta sigara huku akionekana kuwa kinara wa maongezi huku Berta na Feti wakimsikiliza, Fetty anamuona Ray na kumgusa Airinpol na kumuonyesha kwa Ray, Airinpol anageuka na kumuangalia Ray,“mamaaa..yule kaka namjua” anasema Airinpol kwa shahuku, “acha umbea Airini” anasema Beti, huku Airinpol akiiminyia sigara kwenye ashtray , “najua hata anapoishi” anaongeza Airinpol huku anainuka, anatoa bazoka kwenye mkoba wake na kuitia mdomoni, “leo ni leo ameingia kwenye kumi na nane zangu” anasema Airinpol huku akielekea alipoketi Ray.

Ray ameketi ametulia, anakuja Muhudumu,”kaka karibu” anasema Muhuhudumu, Ray anashtuka na kugeuka kwa Muhudumu “niletee tonic water baridi” anasema Ray huku akitoa noti ya elfu kumi na kumpa Muhudumu, Muhudumu anaondoka, Airinpol anafika kwa Ray, “kaka mambo?” Airinpol anamsalimu, Ray anashtuka na kugeuka huku akimshangaa Airinpol, “najua unachotarajia kwangu dada lakini utanisamehe..nimekuja tu kuangalia mpira basi” Ray anamaliza kusema na kurudisha macho kuangalia TV, Airinpol anabaki amesimama, Muhudumu anakuja na soda na glasi na kuweka mezani na kufungua, “basi naomba uninunulie kinywaji” anasema Airinpol huku akimshika Muhudumu mkono kumzuia asiondoke, Ray anageuka kumuangalia tena Airinpol huku akimshangaa, Ray anashusha pumzi, “ok mpe anachotaka” Ray anamwambia Muhudumu, “savanna baridi” Airinpol anamwambia Muhudumu, Muhudumu anaondoka, “Kaka ahsante” Airinpol anasema, “karibu” anajibu Ray huku macho na umakini ukiwa kwenye TV, “ahsante” anajibu Airinpol huku anavuta kiti na kuketi, Ray anashtuka na kumuangalia Airinpol anavyoketi, Ray anatikisa kichwa kisha anarudisha macho kuangalia TV.

CITY BAR-SAA NNE USIKU.
Mpira unaisha, Ray na watazamaji wengine wanapiga makofi huku wakiinuka na kuondoka mmoja baada ya mwingine, Ray anamshangaa Airinpol naye anavyopiga makofi, “na wewe unapenda soka?” Ray anamuuliza Airinpol, “sana” anajibu Airinpol, “mchezaji gani anakuvutia ulaya?” Ray anamuuliza ,Airinpol anabaki kimya kwa sekunde chache, “Chriss brown” anajibu Airinpol, Ray anashusha pumzi na kubaki anamshangaa Airinpol kisha anainuka “ndio unaondoka?” Airinpol anamuuliza Ray, “narudi kwangu” anajibu Ray, “nikusindikize?” anasema Airinpol, “wapi?” anauliza Ray, “popote unapoenda” anasema Airinpol, “dada naomba tuheshimiane..mimi nina mke na Watoto” Ray anasema, “nakujua vizuri sana Ray” anasema Airinpol, Ray anashtuka na kubaki anatoa macho akimuangalia Airinpol, Ray anashusha pumzi, “sasa fanya hivi..kwanza kanichukulie chenji pale kaunta alafu uje tuongee” Ray anamwambia Airin, Airin anaondoka, Ray anaangalia kuhakikisha Airin amefika mbali kisha naye anaondoka kwa kasi kuelekea mlangoni na kutoka. Anafika garini anaingia anapiga moto, Airin anatoka kwa haraka, “Ray chukua chenji yako” Airin anapaza sauti huku Gari linaondoka kwa kasi, Airin anabaki amesimama anajishika kiuno.

NYUMBANI KWA RAY-USIKU SAA TANO.
Ray yupo kitandani na simu sikioni, “sikia doti..huku moto unazidi kuniwakia” Ray anaongea, “Mzee anaumwa sana na mpaka sasa hatuna maelewano mazuri nae” anaongeza Ray, “sasa nifanyeje jamani Ray?” sauti ya Kidoti inasikika kwenye simu, “omba likizo hata ya wiki moja uje walau nikuvishe pete tu nipate amani” anasema Ray, “Ray hii kazi yangu ni muhimu kuliko kitu chochote” anasema Kidoti kwenye simu, “najua doti” anasema Ray, kidoti anasikika akishusha pumzi kwenye simu “ok wacha nijaribu basi alafu nitakujulisha” anasema Kidoti kwenye simu, “jitahidi mpenzi” anasema Ray, “sawa..basi usiku mwema..mimi ngoja niingie ofisini” anasikika Kidoti, “ok baby kazi njema..mwa” anasema Ray huku akimalizia na busu, anaitoa simu sikioni na kuibofya, anaiweka chini ya mto, anazima taa iliyopo juu ya meza na kulala.

DCT SUPERMARKET-SIKU ILIYOFUATA,SAA MBILI USIKU.
Ray anatoka nje ya Supermarket kubwa ya DCT huku akisukuma kigari chenye mkusanyiko wa bidhaa tofauti tofauti, anafika lilipo gari lake, anafungua mlango wa nyuma upande wa abiria na kuingiza bidhaa kisha anafunga mlango na mara anashtuka kumkuta Airin amesimama sambamba na mlango wa dereva, “mambo” anasalimia Airin huku anatafuna bazoka, Ray anashusha pumzi,“una shida gani dada?” anauliza Ray kwa sauti ya kuonyesha kuchukizwa, “nimekuletea chenji yako” anasema Airin huku akionyesha noti kadhaa za pesa kwa Ray, Ray anakaa sekunde mbili kimya, “nashukuru..lakini hizo ni za kwako naomba tu ubaki nazo” Ray anasema kisha anaingia kwenye gari na kuiwasha, gari inarudi nyuma na mara Airin anaruka na kujitupa chini huku akipiga kelele kwa nguvu,”nakufa” Ray anashtuka anasimamisha gari na kuteremka na kwenda pale alipolala Airin, na tayari wameshafika watu wengine wawili, “umenivunja mguu” Airin analia huku ameshikilia mguu wake, Ray anainama na kuushika mguu wa Airin, “sasa usipoteze muda bro utajaza watu bure tu” anasema Mtu mmoja, “mkimbize tu hospitali mengine mtajuana huko” anasema Mtu mwingine huku akianza kumnyanyua Airin, wote watatu wanasaidiana kumbeba na kwenda kumuingiza kwenye gari la Ray, Ray anaingia garini kwa haraka na kuondoa gari.

NYUMBANI KWA RAY-NJE-SAA NNE USIKU
Ray na Dulivan wapo barazani, “huyu mtu simuamini..hakikisha milango unafunga na funguo uingie nazo chumbani kwako” anasema Ray, “sawa bro” anajibu Dulivan, “na usije ukalala mazima” anasema Ray, “hata mimi nitalala nusunusu” anaongeza Ray, “sawa bro” anasema Dulivan, Ray anaingia ndani.
Airin amelala kwenye kochi sebuleni, huku akiwa na mfuko wa plastiki wenye barafu juu ya mguu wa kushoto, anaingia Ray na kufika pale alipolala Airin, “mguu unaendeleaje?” anauliza Ray, “nasikia afadhali kadri muda unavyoenda”, anasema Airin, “nakuuliza tena kwa mara ya mwisho” anasema Ray, “una uhakika hatuna haja ya kwenda hospitali?” anasema Ray,”na mimi nakujibu kwa mara ya mwisho Ray..hospitali nitaenda kesho kama mguu utaendelea kuuma” anasema Airin, Ray anaondoka, “ila sikia” anasema Airin, Ray anasimama, “nashindwa kulala vizuri hapa kwenye kochi” anasema Airin, “kwa hiyo unatakaje?” anauliza Ray, “nataka nilale chumbani” anasema Airin, “shika adabau yako” anasema Ray na kuondoka.

NYUMBANI KWA RAY-SAA SABA USIKU.
Airin yupo sebuleni kwenye kochi anajigeuza huku macho yake yakiwa wazi, zinapita sekunde kadhaa, anajitoa shuka aliyojifunika na kuinuka, na polepole anaelekea mlango wa chumba cha Ray na kuanza kugonga, anagonga mara kadhaa mlango unafunguliwa huku Ray akiwa mwenye mawenge ya usingizi machoni, “nini shida?” anauliza Ray, “naogopa sijazoea kulala mwenyewe..kunatisha” anasema Airin, “unajua dada ulipolala ndipo nilipoamkia” anasema Ray kwa ukali huku akionekana sasa usingizi umeshakata, “sishindwi kukutoa hapo nje na usiku huu” anaongeza Ray kwa ukali, Airin anabaki kimya kwa sekunde chache, “unaogopa nini mtu mzima..mimi nitalala sakafuni hebu acha ushamba wa kitoto” anasema Airin huku anamsukuma Ray pembeni na kuingia chumbani, Ray anabaki amezubaa akimuangalia Airin, Airin anaingia na kwenda kuketi juu ya kitanda, “hapo chini toka kitandani kwangu” anasema Ray kwa ukali huku akimfuata Airin na kumuinua, Kisha anachukua blangeti kitandani na kulitupa chini, Airin analichukua, analikunja na kulitandika chini na kujilaza, Ray anaketi kitandani huku anamuangalia Airin pale chini kwa muda kabla naye kujilaza kitandani na kuzima taa ya mezani.

NYUMBANI KWA RAY-SAA NANE USIKU.
Mlango wa chumba cha Ray unafunguka, anatoka Airin akiwa mtupu kama alivyozaliwa na kukimbilia choo kilicho jirani na sebuleni, anaingia na kufunga mlango kwa loki, anakuja Ray naye akiwa kama alivyozaliwa, “huo ndio ujinga gani sasa?” anasema Ray huku akifika mlango wa choo na kujaribu kuufungua, “hapana aise imetosha kalale sasa Ray” inasikika sauti ya Airin kule chooni, Ray anabaki pale mlangoni akigonga mara kadhaa, mlango wa chumba cha Dulivan unafunguka na Dulivan anatoka, “kuna nini bro?” anauliza Dulivan kwa mshangao huku akishtuka kumuona Ray akiwa mtupu, Dulivan anarudi chumbani kwake na kutoka na taulo na kumpatia Ray, “hakuna shida wewe rudi kalale” Ray anamwambia Dulivan huku akiipokea taulo na kujifunga, Dulivan anabaki amesimama, "Airin" Ray anaita huku anagonga ule mlango wa chooni, “unapoteza muda wako Ray..we kalale mimi sitoki huku mpaka asubuhi” sauti ya Airin inasikika, Ray anabaki amesimama pale kwa muda kisha polepole anaondoka kurudi chumbani.

Zinapita dakika kadhaa, mlango wa choo unafunguka polepole, Airin anatoka na kujikongoja kuelekea sebuleni, anashtuka kumuona Dulivan ameketi kochini,”naomba hiyo shuka” Airin anamwambia Dulivan huku akijibanza nyuma ya ukuta, Dulivan anachukua shuka lililo juu ya kochi na kumpatia Airin huku anaangalia pembeni, Airin anajifunga shuka na kujongea lilipo kochi, “naomba maji ya kunywa” Airin anamwambia Dulivan, Dulivan anaelekea jikoni huku Airin kichovu akiketi kochini, Dulivan anarudi na glasi yenye maji na kumpatia Airin, Airin anajiinua kochini na kunywa maji yote na kushusha pumzi nzito, kisha anamrudishia Dulivan glasi, Dulivan anapeleka glasi jikoni huku Airin kichovu akijilaza pale kochini, Dulivan anarudi, “hivi huyu kaka yako alikuwa gerezani?” Airin anauliza,”kwa nini?” anauliza Dulivan, Airin anashusha pumzi “basi..wewe nenda zako ukalale” Airin anamwambia Dulivan, Dulivan anabaki amesimama, Airin anavuta shuka na kujifunika gubigubi “naomba nizimie hiyo taa” anasema Airin, Dulivan anaenda kwenye switch na kuzima taa na kuondoka.

OFISINI KWA RAY-ASUBUHI
Ray ameketi ofisini akitumia computer, anaingia Fei, dada, 27, akiwa na faili na kuliweka mezani, “umemaliza?” anauliza Ray, “ndio bosi” anajibu Fei na kutoka, Ray anabaki kimya kwa muda kisha anachukua simu anaibofya na kuiweka sikioni, “ameshaondoka huyo kichaa” anauliza Ray, “ndio bro” sauti ya Dulivan inajibu kwenye simu, “umemchunga kama nilivyokuambia?” anauliza Ray, “kuna muda niliingia kujisaidia kutoka ndio nikakuta ameshaondoka” anasema Dulivan kwenye simu, “weee” anasema Ray kwa mshtuko huku anainuka na kutoka.

NYUMBANI KWA RAY-NDANI-ASUBUHI.
Ray anafika na kwa haraka anaelekea chumbani na kuingia, anaona baadhi ya nguo ziko chini, anaangalia ilipo droo ya kikabati cha kitandani anaona ipo wazi, huku macho yamemtoka, anaenda kwa haraka na kuanza kupekua huku akitoa vitu kadhaa kwenye droo, “shit” anatamka Ray kwa sauti ya juu, anakuja Dulivan, “vipi bro?” anauliza Dulivan, “nilijua tu yule mshenzi ana lake jambo” anasema Ray huku anaketi juu ya kitanda, “pumbavu lile likajifanya nimeligonga na gari kumbe jambazi mkubwa limekuja kuniibia” anaongeza Ray kwa hasira, “ameiba nini na nini bro” anauliza Dulivan, Ray anashusha pumzi, “kuna vitu na pesa” anasema Ray, mara simu inaita, Ray anaitoa simu mfukoni na kuiweka sikioni, “sema Medi” Ray anaongea kwa sauti ya chini,“mbona umechoka hivyo?” sauti ya Medi inauliza, “nipo powa” anasema Ray, “sasa sikia..kuna demu namuona hapa amevaa jaketi la Arsenal kama alilokutumia kidoti..na lina saini ya Henry mgongoni kama hilo la kwako” anasema Hemedi, “na ulijigamba unalo peke yako Bongo nzima” anaongeza Hemedi,“ni wapi hapo?” anasema Ray kwa mshtuko huku akiinuka, “vipi..unataka kuja kuhakikisha nini bro?” anauliza Hemedi kwenye simu, “ameingia hapa AICC..ofisi ya Watoto wetu” inasema sauti ya Hemedi, Ray anaitoa simu sikioni na kwa haraka anaondoka.

ARUSHA INTERNATIONAL CONFERENCE CENTER-ASUBUHI.
Gari ya Ray inafika AICC, anateremka na kwa haraka anaingia jengoni hadi lilipo bango linalosomeka WATOTO WETU, anasukuma mlango na kuingia, anasimama kuangalia huku na kule, anamuona Airin ameketi kwenye kiti, Ray anamuendea Airin, Airin anamuona ray na kushtuka, “njoo” Ray anasema huku anamshika Airin mkono, anamuinua na kumkokota mpaka nje, Ray anachukua mkoba wa Airin na kusachi, anatoa noti kadhaa anazihesabu, “zilikuwa laki tano..iko wapi laki moja?” mara anakuja Mama Di, Mama wa makamo, “Dada shika risiti yako” anasema Mama Di huku akimpa Airin risiti, “na huyu ni mwenzako?” Mama Di anamuuliza Airin, “ndio” anajibu Airin, “mnavyofanya ni vizuri sana kaka yangu..kuja kuchangia watoto..Mungu awajalie maana michango mnayotoa ni msaada mkubwa sana kwenye kituo chetu” anasema Mama Di, Ray anabaki ameduwaa, Mama Di anaondoka, Ray anashusha pumzi “siku nyingine ukitaka kutoa michango yako tumia pesa ulizozitolea jasho” Ray anamwambia Airin, “toa na jaketi langu mwizi wewe” Ray anasema huku akishika jaketi na kumvua Airin, "na kuanzia leo hesabu hatujawahi kuonana" anasema Ray kwa ukali na kuondoka akimuacha Airin anabaki amesimama.

MIEZI SABA BAADAE, NYUMBANI KWA RAY-MCHANA.
Ray na Natasha wameketi, “muhimize huyo mwenzako aje Ray” anasema Natasha, “mama..nampigia simu kila siku ananiambia nisubiri” anasema Ray, “baba yako na hali yake ndio anazidi kulalama kila kukicha” anasema Natasha, “haipiti siku hajatamka jina lako” anaongeza Natasha, “tuombe Mungu huo mwezi ujao aje kweli kama alivyoahidi” anasema Ray, wanabaki kimya kwa muda, Natasha anashusha pumzi “twende unipeleke kwa Mona nisichelewe kurudi moshi” anasema Natasha huku anainuka, Ray anainuka huku akichukua funguo wa gari pale juu yameza, wanatoka.

MWEZI MMOJA BAADAE, NYUMBANI KWA RAY-SAA MBILI USIKU.
Gari ya Ray inaingia, anateremka Ray kwa haraka na kwenda kuufungua mlango wa abiria, anateremka Kidoti, dada mrembo, 26, aliyeumbika vema, “karibu Bongo” anasema Ray, “niambie karibu kwako maana Bongo nimekaribia tangu jana” anasema Kidoti huku akikumbatiana na Ray, “ningekukumbatia hivi jana Mzee wako yule angeniulia pale pale airport” anasema Ray,”ndio maana ulikuwa mpole vile?” anasema Kidoti, anakuja Dulivan, “shikamoo dada kidoti” Dulivan anasalimia, “waoo” anasema kidoti kwa bashasha huku akimfuata Dulivan na kumkumbatia, “alafu nataka tuongee kitu” Kidoti anamwambia Dulivan, kisha anageuka kwa Ray,“unaweza ukatupa nafasi kidogo?” Kidoti anamwambia Ray, “ok hamna shida” anasema Ray huku akiingia ndani, Ray anaingia na kusimama dirishani kuwasikiliza Kidoti na Dulivan, “nataka nikuulize kitu mdogo wangu” Kidoti anamwambia Dulivan kwa sauti ya chini, “nilipokuwa sipo ni mwanamke gani aliwahi kuingia hapa..kuacha ndugu zake?” anauliza Kidoti, Dulivan anabaki kimya kwa muda kama anayejaribu kukumbuka jambo, “namkumbuka mmoja” anasema Dulivan, Ray anasikia na kushtuka huku akikodoa macho na kuweka mkono kichwani “niambie kila kitu mdogo wangu” Kidoti anamwambia Dulivan huku akitoa noti tatu za elfu kumi na kumpatia Dulivan, “usibakize kitu mdogo wangu” anaongeza Kidoti, “kuna siku alikuja dada mmoja akakaa mpaka usiku..baadae akamuita mwenzake” anasema Dulivan, Kidoti anakodoa macho, “kwa hiyo wakawa wawili?” anauliza Kidoti kwa mshangao, “ee” anaitikia Dulivan,”lakini cha ajabu wote wawili wakashindwa” anasema Dulivan, “wakashindwa nini?” anauliza Kidoti, “si walishindwa kurekebisha TV na walijiita mafundi TV”, Kidoti anabaki ameduwaa anamuangalia Dulivan kisha ananyakua zile noti kutoka mkononi kwa Dulivan, “lete pesa zangu” anasema Kidoti, “kwa nini?” anasema Dulivan kwa mshangao huku akimuangalia Kidoti anavyoondoka.

Ray anaketi kochini huku anashusha pumzi kama mtu aliyetua gunia la chumvi, Kidoti anaingia na kuketi kochini anamkumbatia Ray, “mmeshaongea?” Ray anauliza, “tumeshamaliza kikao” anasema Kidoti, “huniamini sio” anasema Ray, "kwa nini?" anauliza Kidoti, "si nimekusikia ukiuliza" anasema Ray, "kumbe ulikuwa unatusikiliza?'
“unajua vizuri kuwa siwezi ku cheat doti” anasema Ray, “haya..umeshinda tuufunge mjadala” anasema Kidoti, wanabaki kimya kwa muda, “enhe ratiba yetu ikoje?” Kidoti anamuuliza Ray, “ni kama tulivyopanga..tunaanzia Arusha Hotel..then Club biz kuwacheki jambo squad” anasema Ray, “good” anatamka Kidoti, “ngoja nibadili hili shati” anasema Ray huku anainuka na kuelekea chumbani na Kidoti anainuka na kumfuata.

KWA MZEE CHIRO-MCHANA
Natasha na Ray wameketi kwenye kochi, Natasha akiwa na notebook mkononi na kalamu akiandika “sasa nikwambie kitu?” anasema Natasha, “hakuna muda wa kupoteza Ray” anasema Natasha, “harusi ifanyike haraka iwezekanavyo” anaongeza Natasha, “hilo ni wazo zuri sana mama” anasema Ray,”yupo nchini mpaka lini?” anauliza Natasha, “miezi miwili” anajibu Ray,”safi” anasema Natasha, Ray anainuka, “basi mimi ngoja nirudi ofini Mama” anasema Ray, “nilisema nikuletee tu hizo habari njema” anaongeza Ray “usisahau basi kutuma hiyo hela” anasema Natasha, “siwezi kusahau mama” Ray anasema huku akielekea mlangoni na kutoka.
 
SEHEMU YA TATU.

KWA RAY OFISINI-MCHANA.
Ray yupo ofisini akiandika kwenye faili, anaingia Kidoti, Ray anashtuka na kuinua kichwa “hi baby” anasema Ray kwa bashasha, “hi” anajibu Kidoti huku akitoa tabasamu kubwa, anasogea kwa Ray na kumbusu shavuni, “ngoja nimalizie hapa chap twende zetu” anasema Ray, “no” anasema Kidoti, Ray anashtuka na kumuangalia Kidoti,“wewe nenda tu lunch baby ili mimi niende saluni” anasema Kidoti, “baby imekuwaje tena?” anauliza Ray, “hakuna muda baby na saluni nzuri ni za shida wikiend” anasema Kidoti, “nataka niende kwa Mama yako nikiwa nimetokelezea kisawasawa baby” anasema Kidoti, Ray anashusha pumzi,“ok” anasema Ray,”Kidoti anambusu tena Ray, "uwe na lunch njema babe" anasema Kidoti huku anaelekea mlangoni na kutoka, Ray anarudi kuendelea kuandika kwenye faili, mara simu inaita, Ray anaichukua simu juu ya meza na kuiangalia kwa muda, “huyu nani tena?” Ray anaongea mwenyewe, simu inaonyesha namba tu, Ray anafikiria kwa muda, anaibofya na kuiweka sikioni “hallow” anasema Ray, “mambo” inasikika sauti ya kike kwenye simu, “nani mwenzangu?” anauliza Ray, “Airin” sauti inasema, Ray anashusha pumzi“si nilikwambia usinizoee wewe mpuuzi” anag’ka Ray, “na umepata wapi namba yangu?” anauliza Ray, “usitake kujua” anajibu Airin kwenye simu, “naomba unikome we mwanamke” anasema Ray kwa ukali, “mimi nimeshakukoma sana tu..ila mwanao huku tumboni ndio anataka kukusalimia” anajibu Airin kwenye simu, “unasema nini?” anauliza Ray kwa mshtuko, “habari ndio hiyo Ray..am pregnant” anasema Airin, “ukitaka nitafute..usipotaka endelea na maisha yako tu” anamalizia Airin na simu inakatika, Ray anabaki ameduwaa macho yamemtoka, anaiweka simu mezani na polepole anaketi, anaingia Fei,“bosi” Fei anaita huku akiweka faili mezani, Ray bado ameduwaa, “Bosi” Fei anaita tena, Ray bado ametulia macho yamemtoka, “bosi” anaita tena Fei huku anaonyesha uoga, anamuangalia Ray kwa muda, “bosi una tatizo?” Fei anauliza tena lakini bado Ray ameduwaa, Fei anatoka na kwenda ofisini kwake, anachukua simu na kuibofya, anaiweka sikioni, “Hemedi hebu njoo haraka mimi bosi hapa simuelewi” Fei anasema huku akiwa kwenye hali ya uoga, anaitoa simu sikioni kisha anarudi ofisini kwa Ray na kumkuta Ray bado amezubaa.

KILIMANJARO HOTEL-JIONI.
Ray na Hemedi wameketi, kila mmoja ana glasi ya kinywaji mbele yake, wapo kimya kwa sekunde kadhaa “umebeba mwanamke wa bar na hukutumia kinga?” Hemedi anamwambia Ray, “nimekwamba ilikuwa saa nane usiku Medi“ anasema Ray, “hata kama..ungeingia jikoni uchukue hata mfuko wa mkate Ray” anasema Hemedi, Ray anageuka na kumshangaa Hemedi, “huu sio muda wa utani Medi” anasema Ray, “mimi sitanii Ray” anasema Medi na kumuangalia Ray, Hemedi anashusha pumzi,“ok..maji yameshamwagika” anasema Hemedi, “jambo la kwanza kapime ngoma” anasema Hemedi, Ray anashtuka na kumuangalia Hemedi, “habari ndio hiyo Ray” anaongeza Hemedi, “alafu tusubiri mtoto azaliwe ipimwe DNA” anasema Hemedi, Ray anashusha pumzi “Medi umempigia simu mmeongea nae na amesisitiza kuwa hakuwahi kutembea na Mwanaume bila kinga kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita” anasema Ray, “usimuamini changudoa Ray” anasema Hemedi, wanabaki kimya kwa muda, “cha muhimu jitahidi kwa hizi siku zilizobaki uilee hiyo mimba” anasema Hemedi huku akipiga funda ya kinywaji chake, "zaidi ya hapo..mwanaume umefanya ya kiume” anasema Hemedi huku akimpigapiga Ray mgongoni, “hongera men” Hemedi anaongeza.

NYUMBANI KWA MZEE CHIRO-NJE-MCHANA
Ray na Natasha wapo barazani, “mwanangu..kama yameshindikana basi..hatuwezi kulazimisha mambo” anasema Natasha, “na mbona hukuwahi kuongelea hiyo mimba?” anauliza Natasha, “yeye ndio kaniambia jana” anasema Ray, wanabaki kimya kwa sekunde kadhaa, “basi kama tayari ana mimba wewe mlete tu tuonane nae” anasema Natasha, “mkwe yeyote sisi tutampokea mwanangu” wanabaki kimya kwa muda, "natumai naye ni msomi kama Kidoti" anasema Natasha, Ray anashusha pumzi, "au ni zaidi ya Kidoti?" anaongeza Natasha, "mama hebu hayo tuyaache kwanza" anasema Ray, "basi sawa" anasema Natasha, “haya mama mimi naenda” Ray anasema huku anainuka na kuelekea kwenye gari, “kila la kheri mwanangu” Natasha anamalizia, Ray anaingia kwenye gari, anawasha na kutoka.

CITY BAR-NJE-MCHANA.
Gari ya Ray inafika nje ya bar, Ray anatoa simu na kuibofya, “uko wapi?” Ray anauliza kwenye simu baada ya sekunde kama mbili anaitoa simu sikioni na kuiweka mfukoni, anatokea Airin kutoka mlango wa bar, akiwa na mimba na sigara mdomoni, anafika kwenye gari ya Ray na kuingia, Ray anabaki anamuangalia kwa mshangao, “mambo” anasema Airin katika hali kidogo ya ulevi, “una mimba alafu bado unavuta sigara?” anauliza Ray, “na kunywa pombe?” anaongeza Ray, “wewe ulikuwa wapi siku zote..kitoto kiko bwii?” anasema Airin, Ray anabaki anamuangalia Airin kwa hasira, Ray anashusha pumzi, “tunaenda kwa Mama yangu..naomba ujiheshimu” Ray anamwambia Airin, “usikonde” anajibu Airin, huku Ray anabaki anamuangalia kwa mshangao kwa sekunde kadhaa kisha anaweka gia na gari linaondoka.

NYUMBANI KWA RAY-MCHANA.
Ray, Airin, Mona na Natasha wameketi, wote wakiwa wenye furaha, mezani kukiwa na vyakula mbalimbali, Natasha anamalizia kula kwenye sahani yake, anachukua glasi yenye maji na kunywa, “mkwe hivi ulisema unafanya kazi gani?” Natasha anauliza huku anaweka glasi ya maji mezani, “mimi?” anauliza Airin huku bado akionyesha hali ya ulevi, “ndio naongea na wewe mkwe wangu” anasema Natasha kwa bashasha, Airin anabaki kimya kwa muda huku Ray akibaki anaangalia chini, “kama Ray bado hajakwambia” anasema Airin na kutulia kwa muda, “mimi ni changudoa” anasema Airin, wote wanashtuka na kubaki wanaangaliana, “unafanya shughuli gani?” anauliza Natasha kwa mshangao huku akimkazia Airin macho, “muhudumu wa bar..nipo pale City bar” anasema Airin, Natasha anaanguka chini, Mona na Ray wanainuka kwa haraka kumsaidia Natasha, Mona anachukua gazeti lilopo pembeni na kuanza kumpepea Natasha, “unaona ujinga uliofanya?” Ray anamwambia Airin kwa ukali, “msema kweli ni mpenzi wa Mungu Ray” anajibu Airin.

NYUMBANI KWA RAY-BAADAE.
Natasha, Ray na Mona wameketi kwenye makochi, “labda nife..lakini sio hivi nikiwa hai” anasema Natasha, “ila Mama kumbuka tayari huyu ana damu yetu tumboni kwake” anasema Mona, “hata kama” anajibu Natasha kwa ukali, “Ray hawezi kuoa huyo mjinga” anasema Natasha, “Mwanangu anahitaji Mwanamke mwenye elimu na heshima yake” anasema Natasha, “sio huu uchafu” anaongeza Natasha, “na huyo Mtoto anayekuja?” anauliza Mona, “azae Mtoto atuachie aende zake” anasema Natasha, muda huu wote Ray amenyamaza kimya amejiinamia, “sipokei changudoa mimi” anaongeza Natasha, “huyo mwanao hakujua huyo ni changudoa?” anasema Mona, “nyamaza Mona” anang’aka Natasha, “naomba usinichefue” anaongeza Natasha huku akimuonyesha Mona kidole, “vimba upasuke lakini ndiye anayekuletea mjukuu” anasema Mona huku anainuka na kuondoka akimuacha Natasha anamkata jicho kwa hasira.

NYUMBANI KWA RAY,NJE-MCHANA
Mona anatoka mlangoni, Airin ameketi pembeni kwenye ukingo, Mona anaenda alipo Airin, Airin amejiinamia macho mekundu huku anatumia kanga kujifuta machozi, “Airin” Mona anaita, Airin anainua kichwa “mbona unalia” anauliza Mona, “nimesikia yote aliyosema Mama yako” anasema Airin, Mona anashtuka na kubaki kimya kwa muda, “wala usimjali mama dear” anasema Mona, “ni hasira tu zitamuisha” anaongeza Mona huku akimsaidia kumfuta Airin machozi, “labda sikutakiwa kusema vile” anasema Airin, “kilichotokea kimeshatokea Airin” anasema Mona huku amemuwekea Airin mkono mgongoni.

NYUMBANI KWA RAY, SEBULENI-MCHANA.
Ray na Natasha wameketi, “endelea na huyo Kidoti msomi achana na hii balaa” anasema Natasha, “nimekuelewa mama” anasema Ray, wanabaki kimya kwa sekunde kadhaa, “mpigie simu ajiandae wiki ijayo mlete Moshi..Baba yako amuone” anasema Natasha,“na tunaanza mipango ya harusi leo hii” anasema Natasha, “sihitaji mchango wa mtu..nitasimamia show yote mwenyewe” anaongeza Natasha, Ray anashusha pumzi.
Anaingia Mona na kuketi, “Airin amesikia yote tuliyokuwa tunaongea” anasema Mona, “hata akisikia” anasema Natasha, “yupo hapo nje?” anauliza Ray, “ameondoka sasa hivi” anasema Mona, “akafie mbali huko huyo changudoa” anasema Natasha kwa ukali, “na wewe tunaanza mipango ya harusi ya kaka yako” Natasha anamwambia Mona.

WIKI TATU BAADAE-MOSHI HOSPITAL,WODINI-MCHANA.
Mzee Chiro, Ray na Mona wameketi, Mzee Chiro akiwa amelala kitandani, anaingia Natasha, anaketi pembeni ya Ray, “Kidoti yupo njiani anakuja” Natasha anamwambia Ray, wanabaki kimya kwa sekunde chache, “nadhani hali yangu mnaiona” anasema Mzee Chiro na kukata ukimya, “na niseme tu ukweli Ray umenikatisha tamaa mwanangu” anaongeza Mzee Chiro huku analengwa machozi,”wewe ndio wa kukuachia kijiti..lakini” anasema Mzee Chiro na kusita, Natasha anamshika Ray mkono, “Mwambie sasa hivi kuhusu Kidoti” kwa sauti ya chini Natasha anamwambia Ray, Ray anashusha pumzi, “ungeniletea tu hata mtoto wa kusingiziwa Ray nikupe baraka zangu” anasema Mzee Chiro, wanabaki kimya, “mwambie” anasema Natasha huku akimsukuma Ray begani “Baba Ray ana Watoto” anaropoka Mona, Natasha, Ray na Mzee Chiro wanashtuka, Ray na Natasha wanabaki wanamshangaa Mona, Mzee Chiro kwa shida anajaribu kujiinua pale kitandani na kumuangalia Mona, kisha anamuangalia Ray, “ni kweli Ray?” anauliza Mzee Chiro, Ray anabaki ameduwaa,”baba hebu subiri” anasema Ray huku anainuka na kumshika Mona mkono na kumkokota nje, Natasha naye anatoka.

MOSHI HOSPITAL,NJE-MCHANA.
Wanatoka nje, “hivi wewe umetumwa ama?” Natasha anamuuliza Mona kwa ukali, “hayo umetoa wapi Mona” anauliza Ray, “Airin kajifungua leo asubuhi” anasema Mona, “mapacha wa kiume” anaongeza Mona, Ray anabaki ameduwaa, “ni mpaka tufanye DNA..asituletee utapeli sisi” anasema Natasha, “mkiwaona watoto sijui hata kama mtahitaji hiyo DNA”, anasema Mona, mlango unafunguka, anatoka Mzee Chiro akijikingoja , wote wanashtuka, “baba umetembea mwenyewe?” anauliza Mona kwa mshtuko, “Ray..alichosema Dada yako ni kweli?” anauliza Mzee Chiro, “Baba Ray ana Watoto mapacha wa kiume” anasema Mona, “wamezaliwa leo alfajiri” anaongeza Mona, Mzee Chiro anamuangalia Ray, anatabasamu na kumkumbatia, “Ray umeniponya mwanangu” anasema Mzee Chiro, Mzee Chiro anamuachia Ray, “naomba nikawaone hao Wajukuu wangu tafadhali” anasema Mzee Chiro, Natasha anaondoka kwa haraka huku akiitoa simu yake kwenye mkoba, anaenda lilipo gari lake, anaingia na kuondoka, Mzee Chiro anamkumbatia tena Ray, anakuja Nesi na kumuona Mzee Chiro, “huyo mzee mbona mnamsumbua?” anasema Nesi “ameinuka mwenyewe” anasema Mona, “Ray umeniponya mwanangu” anaendelea kusema Mzee Chiro huku akiwa mwenye furaha tele,“baba tutaenda Arusha kuwaona Watoto lakini mpaka turuhusiwe na Daktari” anasema Ray huku akisaidiana na Nesi kumrudisha Mzee Chiro wodini.

SIKU ILIYOFUATA-ARUSHA HOSPITALI,WODINI-MCHANA.
Ray, Natasha, Mona na Mzee Chiro wapo wodini, Airini yupo kitanndani, Mzee chiro amempakata mtoto mmoja akiwa na tabasamu tele usoni, na Ray amempakata mtoto mmoja,”nimeshapona..kuanzia sasa narudi kwenye shughuli zangu” anasema mzee Chiro huku akitabasamu, anaingia Nesi, “naomba niongee na baba wa mtoto” anasema Nesi huku amesimama pale mlangoni, Ray anainuka, Nesi na Ray wanatoka.

ARUSHA HOSPITAL,OFISI YA NESI-MCHANA.
Ray na Nesi wanaingia ofisini, “karibu uketi” anasema Nesi huku akiketi kwenye kiti,”kuna jambo lazima nikuambie” anasema Nesi huku Ray akivuta kiti na kuketi huku akimuangalia Nesi kwa makini, “kuna dada mmoja walikuja hapa jana na Mama yako” anasema Nesi huku Ray akibaki makini kumsikiliza, “na jambo la kushangaza walitaka kumpa mtumishi wetu milioni tano ili wale watoto wapotezwe” anasema Nesi, Ray anabadilika na kutoa macho, “hii hospitali hatufanyagi ujinga..tuna maadili ya kidini” anasema Nesi “mama yangu?” anauliza Ray, “Mama yako yule aliyevaa kitenge aliyepo pale wodini” anasema Nesi, Ray anabaki ameduwaa, anashusha pumzi, “na huyo dada unayemtaja yupoje?” anauliza Ray, “ana kialama hapa” anasema Nesi huku akionyesha chini kidogo ya pua yake, Ray anainamisha kichwa kama mtu aliyechoka sana, “kumpoteza walimaanisha nini?” anauliza Ray, “tusiingie sana ndani..wewe elewa tu hicho ndio kilichotokea” anasema Nesi huku anainuka na kuelekea mlangoni, “jikaze kaka” anasema Nesi, Ray anainuka kichovu, wanatoka.

ARUSHA HOSPITALI,WODINI-MCHANA.
Ray anaingia akionekana mnyonge, “vipi?” anauliza Natasha, “hamna kitu” anasema Ray huku anaketi juu ya kitanda na kuinamisha kichwa, anaingia Nesi,“muda umeisha..tutaomba mtoke..anaweza kubaki tu baba wa watoto” anasema Nesi, Mzee Chiro anampa Ray mtoto na kuinuka, Mona naye anainuka na kumpa Airin mtoto na wanatoka, wanabaki kimya kwa muda, “hongera” anasema Ray, “nashukuru” anajibu Airinpol, wanabaki kimya kwa muda, “kwa nini uliamua kufanya ile kazi ya kujiuza?” anauliza Ray, Airinpol anabaki kimya, anashusha pumzi, “ni stori ndefu Ray” anajibu Airinpol, “nilikuja mjini kufanya kazi za ndani..baadae nilifukuzwa ndio nikakutana na kampani..nikaingia huko” anasema Airipol, “kwa hiyo kati ya kazi zote ukachagua hiyo dhambi” anasema Ray, “nilichanganyikiwa na sikuwa na njia nyingine” anasema Airinpol, wanabaki kimya kwa muda, “ila nashangazwa sana na hii jamii yetu” anaema Airin, “kivipi?” anauliza Ray, “tu wepesi sana wa kuhukumu” anasema Airin, Ray anashtuka na kumuangalia Airin kwa makini, “watamuheshimu mtu anayeiba mamilioni na kusababisha maelfu ya Watu wakose dawa..chakula..au hata wapoteze maisha” anasema Airinpol, “lakini wanatuona sisi ndio wabaya na wadhambi kuliko binadamu wote”
Anasema Airin, “lakini dhambi ni dhambi Airin” anasema Ray, “najua..na ndio maana nimeshatubu na ninaachana nayo” anajibu Airin, wanabaki kimya kwa sekunde chache, “na kule nilipokukuta umepeleka pesa unahusika vipi?” anauliza Ray, Airin anashusha pumzi “nimejiwekea nadhiri ya kuchangia watoto..nimepitia hayo maisha ya mitaani..kwa hiyo nayajua” anasema Airin, “chochote ninachopata nachangia” anaongeza Airin,Ray anabaki anamuangalia, wanabaki kimya, anaingia Mona, “Kaka..Mama anakuita” Mona anamwambia Ray, Ray anainuka, anampa Mona mtoto na kutoka.

ARUSHA HOSPITALI,NJE-MCHANA.
Ray anamfuata Natasha aliyesimama mita kadhaa kutoka jengo la hospitali, Ray anafika, “mwanangu Ray kama tulivyoongea” anasema Natasha huku akimuongoza Ray na kuenda lilipo gari dogo aina ya Toyota IST, wanafika na kumkuta kidoti akiwa ametulia siti ya dereva, mlango ukiwa wazi, “mkwe” anaita Natasha kwa bashasha huku akifika garini, “sasa ni hivi” anasema Natasha, Ray anashusha pumzi nzito, “naomba mnisikilize” Ray anakatisha mazungumzo ya Natasha, wanabaki kimya, “madudu yenu yote nimeshayajua..na kunzia sasa hivi kidoti sitaki kukuona mbele ya uso wangu” anasema Ray kisha anaondoka na kuwaacha Kidoti na Natasha wanaangaliana.

OFISINI KWA RAY-MCHANA.
Ray na Hemedi wameketi, kila mmoja akiwa na glasi ya kinywaji mezani, huku Ray akiwa anatumia computer, Hemedi akiwa ameshikilia glasi yake yenye kinywaji mkononi, "hatimaye yametimia" anasema Hemedi kwa bashasha, Ray anamuangalia Hemedi huku akitoa tabasamu kubwa usoni, "bifu la miaka mitano na dingi limeisha" anasema Hemedi,"Mama na Watoto yupo nyumbani" anaongeza Hemedi, "jamaa wa SA wamekubali proposal na dili liko mezani" anaongeza Hemedi huku anasimama na kumkumbatia Ray, "my men" Hemedi anaongea kwa sauti ya juu.


MWISHO.


 
Usipende kuweka script zako hadharani, labda storyline, treatment au pitch...
Ushauri mzuri mkuu Bishop, ila Storyline au pitch ni kikazi/kibiashara zaidi ili hali mimi nataka zisomeke tu kiburudani kama zilivyo.

Nimeziandika kwa muda mrefu, hivyo nimeamua kuzi publish baadhi.
 
Ushauri mkuu Bishop, ila Storyline au pitch ni kikazi/kibiashara zaidi ili hali mimi nataka zisomeke tu kiburudani kama zilivyo.

Nimeziandika kwa muda mrefu, hivyo nimeamua kuzi publish baadhi.
Hapo kwenye nyekundu ndicho nilichokikusudia, unaweza kudhani unaweka ili kujifurahisha lakini unapaswa kufikiria upande wa pili wa shilingi, who knows, pengine ukapata dili humuhumu...

Anyway, ni mtazamo wangu tu...
 
Hapo kwenye nyekundu ndicho nilichokikusudia, unaweza kudhani unaweka ili kujifurahisha lakini unapaswa kufikiria upande wa pili wa shilingi, who knows, pengine ukapata dili humuhumu...

Anyway, ni mtazamo wangu tu...
Ni mtazamo mzuri sana Mkuu Bishop, nashukuru, ila tayari nilijiridhisha mpaka kuanza ku publish.

Kuna nitakazoendelea kuzi publish pia, ila kidogo nimezifupisha ukilinganisha na original script...nimekuwa nazo kwenye stock muda mrefu tu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom