Simulizi - Dosari (a life full of flaws)

Simulizi - Dosari (a life full of flaws)

We jamaa hii nayo ungepeleka tu huko fasihinet.com,
sio unaleta apa kuitangaza ukiona imepata umaarufu unazingua km ulivyozingua ile ya mimi na mimi.
Ungekuwa unanisaidia kuandika, ndiyo ungesema nazingua kwa haki
 
DOSARI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Uhalifu, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA TANO

★★★★★★★★★★★★★



Mazishi yake Lydia yalimalizika vyema baada ya Reuben na familia yake kuufikisha mwili kwao salama, nao wakafunga safari kurejea jijini kwao baada ya siku mbili tena. Bado, pamoja na jitihada zozote zilizowekwa kutoka kwa wapendwa wake, Larissa hakuweza kutamka neno lolote lile tangu siku aliyopata taarifa za kifo cha mama yake, na kwa kadiri kubwa jambo hilo liliendelea kuitatiza sana nafsi ya Reuben.

Wakiwa nyumbani, Reuben angejaribu kumsemesha kwa upendo, alipomuuliza kama angetaka hiki ama kile, na Larissa hakuitikia kwa njia yoyote kabisa. Kutazama mtu angetazama, kula alikula, kwenda ndani na nje alienda, yaani alitenda kwa njia kawaida kabisa ya mwili alipohitaji jambo fulani, lakini hakuonyesha hisia wala hakuzungumza na yeyote kana kwamba aliupoteza kabisa uwezo wa kuongea. Ikambidi Reuben aite tabibu wake maalumu hapo nyumbani ili kumwangalia bintiye, na hata daktari huyo alipompima, aliona kwamba mtoto alikuwa sawa kabisa kiakili na kiafya, ila tu, ni hitilafu kwenye mfumo wa saikolojia yake uliokuwa ukimzuia kuongea kutokana na mshtuko alioupata kwa sababu ya msiba.

Akiwa ameshauriwa kumpa mtoto muda tu ili hali hiyo iondoke taratibu, Reuben aliona hilo kuwa jambo gumu kwake kufanya kwa sababu hangeweza kuishi na huzuni ya kifo cha mkewe huku na mwanaye akiwa anapitia hali ngumu kwa sababu ya hilo. Larissa asingeweza kurejea shuleni akiwa namna hiyo, na masomo yangeendelea na kumwacha akae nje ya ujuzi aliotakiwa kuendelea kuupata. Mwanaume akajikuta akikabili tena vile vile vishawishi kutoka kwa mama na dada zake, waliotumia majibu ya daktari kama kigezo cha kumshinikiza awaruhusu waondoke naye kwenda kumpa mazingira mbadala na haya ili arudie hali njema. Pamoja na hayo, Reuben hakutaka kuwakubalia, na alijitia uimara kwa kufikria ni lazima ingekuwepo njia ya kumfanya Larissa azungumze tena upesi.

Haikumchukua muda mrefu kurudia kazi zake tena, yaani walipofika tu jijini na kukaa siku moja kabla ya tabibu huyo aliyeitwa kuja kumwangalia Larissa, Reuben tayari akaanza kwenda ofisini. Kulikuwa na kazi nyingi kwa upande wake katika ile kampuni, na masuala ya ujenzi wa hoteli yake bado yaliendelea, kwa hiyo aliona kujipa ubize kwa uharaka ndiyo jambo lililofaa huku akiwa makini kushughulika na ishu ya binti yake. Mgahawa wa Lydia pia uliendeleza shughuli zake, kukiwa na meneja aliyewekwa kuusimamia na kuripoti kwa Reuben mwenyewe, hivyo ni kama na huo aliushikilia pia. Mama yake na dada zake hawangechukua siku nyingi kukaa huku nao wangerudi Ulaya tena, kwa hiyo wazo walilompatia Reuben bado lilikuwa mezani kwa ajili ya uchaguzi kutoka kwake.

Kwa upande wake Paulina, baada ya kufikishwa kwenye nyumba ile ya starehe na kutambulishwa kwa bosi wake na wa wanawake wengine waliotumiwa kuingiza pesa hapo, tayari alikuwa ameshaanza kuzoeshwa mazingira ya kuwa kivutio cha wanaume wenye pesa nyingi. Baada ya kukaa kwa siku mbili tatu hapo kuzoezwa taratibu, alionyeshwa jinsi ya kutenda wakati ambapo angepata mteja maalumu ambaye angelipia pesa nono, na kwa sababu Josephina aliamua kumweka kwenye daraja la wanawake wazuri zaidi kwa ajili ya pochi nene tu, bado mwanamke huyu hakuwa amekatiwa dau lake kwa mwanaume yeyote ndani ya hizo siku.

Kuyazoea mazingira hayo kwa kufundishwa haikuwa ngumu kwa Paulina, lakini kuja kuyatenda mubashara ndiyo ingekuwa mtihani kwake. Yaani alitakiwa kuwa tayari kufanya CHOCHOTE ambacho mteja wake maalumu angetaka, na alijua ingekuwa ngumu sana kwake kwa sababu hakuwahi kufanya lolote kati ya mambo haya huko nyuma. Aliweza kuwasiliana na Roza kupitia simu ya msimamizi wa wanawake wa hapo, yaani mama lao sasa aliyewatunza, na alipewa taarifa na shangazi yake yule kwamba mama alikuwa akiendelea vizuri. Roza alisema ameshatumia karibia milioni moja aliyokopa mahali fulani ili kulipia dawa na tiba za mama yake kwa wiki chache kutokea hapa, kwa hiyo Paulina angetakiwa kuchangamka haswa ili atengeneze pesa ndefu kufidishia, na kumfanyia mama yake upasuaji.

Maisha ya mwanamke huyo kijana yalikuwa yamebadilika rangi sana, hakuwahi kujiona kuja kuwa kama malaya kuuza mwili wake kwa wanaume asiowafahamu ili tu apate faida fulani. Lakini kwa ajili ya mama yake mzazi, angeweza kuvumilia magumu yote ambayo angekabiliana nayo ingawa alielewa ni dosari nzito sana yangeuachia moyo wake, na maisha yake kwa ujumla. Alijipa matumaini kwamba kila kitu kingekuwa sawa tu kwa upande wa mzazi wake, kikubwa atengeneze pesa upesi ili asaidie kufanikisha hilo. Kwa hiyo akaendelea kuwa mtulivu tu na kujifunza utundu huu na ule, ili aje kuwajibika vyema siku ambayo angekutanishwa na mteja wake kwa mara ya kwanza...


★★★


Basi, ikiwa ni siku ya Jumatano sasa, yaani ikikaribia kuisha wiki tangu Lydia azikwe, Reuben alikuwa zake kazini akiendelea na shughuli hizi na zile kama ilivyokuwa ada. Kutokea asubuhi mpaka mida ya mchana hakuweka chochote tumboni, na alitatizwa na baadhi ya kazi alizoshughulika nazo kwa kiasi fulani. Ilikuwa kama anapatwa na hisia ya uchovu wa kiakili uliosababisha azifanye baadhi ya kazi hizo kwa basi tu, huku yeye akidhani anafanya mambo mengi vyema na kwa utaratibu. Alijitahidi kutoona lolote kati ya kazi zake kwa leo linaboa ingawa haikuwa rahisi, na alijielewa vyema ni kutokana na sababu ipi hilo lilitokea.

Jana usiku, mama yake pamoja na Cynthia walimfata tena wakiwa huko nyumbani kuongelea kuhusu suala la Larissa. Cynthia alimwonyesha taasisi fulani ya kisaikolojia kule Ulaya ambayo ingemsaidia binti upesi sana ili aweze kuzungumza tena, hasa kwa kuwa walionelea madaktari wa kisaikolojia wa hii nchi kutokuwa wazuri vya kutosha kumsaidia mtoto. Ile kwamba ya huko nje ndiyo mazuri zaidi ya kwa huku ndani. Zamu hii walimsisitiza sana kwa sababu Alhamisi ndiyo wote walikuwa wanapanga kuondoka, yaani kesho sasa, na jambo hilo lilizunguka kichwani kwa Reuben bila yeye mwenyewe kupenda hata alipojaribu kulipotezea. Vipi kama mama yake alikuwa sahihi kwa wazo hilo? Larissa angekuwa bora zaidi kwenda kukaa mbali na mazingira haya? Mbali na yeye? Ingekuwa rahisi kwake Reuben kumwachia aende?

Hakutaka kujifiikirisha kwamba kumpeleka Larissa huko ndiyo jambo ambalo lingefaa, kwa sababu alihisi ingemfanya aonekane ameshindwa kumsaidia mtoto wake mwenyewe. Alipenda kubeba na kushughulika na changamoto zake yeye kama yeye, na Larissa hakuwa kama changamoto yoyote ile; ndiye mtu pekee aliyebaki kuiweka kumbukumbu ya Lydia karibu zaidi na moyo wake. Alihofia endapo kama angekubaliana na mama na dada zake kwa wazo lao, ingefika hatua binti yake angewekwa mbali sana naye na hata kumsahau; wasiwe na ule uhusiano wenye nguvu yaani. Kwa hiyo ingawa suala hilo lilimhangaisha, msimamo wake ungekuwa pale pale tu. Na akaona ni vyema tu ndugu zake wakiondoka haraka ili asiwe chini ya huo mkazo tena.

Ikiwa ni kwenye mida ya saa nane mchana sasa, Reuben akapigiwa simu na msaidizi wake ofisini hapo kuambiwa kwamba mgeni fulani alifika kuonana naye. Alipouliza ni nani, akataarifiwa jina lake kuwa Josephina Deus. Reuben akatambua huyo kuwa Phina, naye akamwambia msaidizi wake amruhusu mwanamke huyo kuingia ofisini kwake. Alipokata simu, Reuben akanyanyuka kutoka kwenye kiti chake ili aweze kumpokea vyema dada ya rafiki yake. Hawakuwa wameonana wala kuwasiliana tangu msibani, hasa kwa sababu hakuwa na namba za Josephina. Akaelewa ni lazima Francis angekuwa amemwekekeza jinsi ya kufika hapo, kwa kuwa ni jana tu alizungumza na rafiki yake huyo alipomjulia hali pia.

Akiwa ndiyo anauekekea mlango, Reuben akasimama hapo kati baada ya mlango kufunguliwa na moja kwa moja msaidizi wake kutangulia kuingia, kisha ndiyo mgeni akafuatia. Mwanaume alibaki akimtazama Josephina kwa namna mpya, kutokana na jinsi ambavyo mwanamke huyo alijiweka kimwonekano. Alivaa kiblauzi laini chenye mikanda myembamba sana mabegani, sehemu kubwa ya juu na kifua ikionekana, na sketi fupi ya kijivu yenye kubana iliyoishia magotini ilichora shepu lake vizuri, huku miguuni akitinga viatu vyeusi vya kuchuchumia. Usoni alijiremba vizuri pia mwanamke huyu, akiweka kope fupi za urembo, lipstick nyekundu midomoni, na rasta ndefu zenye rangi ya manjano zilipendezesha kichwa chake.

Akiwa ameshikilia pochi nyekundu mkononi, Josephina akaachia tabasamu hafifu huku akizidi kumkaribia Reuben hapo alipokuwa amesimama, na mwanaume aliendelea kumtazama kwa utulivu tu, ila kwa undani aliafikiana na ukweli kwamba mwanamke huyo alikuwa na moto sana. Msaidizi wake Reuben akafunga mlango na kuondoka, na sasa Josephina akawa amesimama mbele yake mwanaume huku akimtazama kwa njia yenye upendezi. Harufu yake ya marashi ilivutia mno.

"Phina... karibu. Karibu sana," Reuben akamwambia kwa sauti tulivu.

"Asante," Josephina akasema.

Kabla Reuben hajaongea tena, mwanamke huyo akamkaribia zaidi na kisha kumkumbatia taratibu, akipapasa mgongo wa mwanaume kama anaubembeleza yaani, na Reuben akatabasamu kiasi na kurudisha kumbatio hilo vizuri.

"Za siku? Unaendeleaje?" Josephina akasema akiwa bado amemshikilia.

"Nipo salama tu. Nashukuru Mungu. Wewe?" Reuben akaongea pia.

"Niko poa. Nisamehe sijakutafuta mapema," Josephina akamwambia.

"Ah, usijali. Asante sana kwa kuja," Reuben akamwambia.

Josephina akamwachia taratibu, yaani akijitoa mgongoni kwake na kuendelea kusimama kwa ukaribu sana na mwanaume huyu, na hili likampa Reuben hisia zenye uajabu kiasi. Kumwangalia usoni kwa ukaribu namna hiyo ilikuwa jambo lililoamsha hisia ambazo hakutazamia ziamke, hivyo akamwachia kabisa na kurudi nyuma kidogo.

"Karibu. Karibu ukae," Reuben akamwonyesha kwenye sofa.

Josephina akatabasamu na kurudisha nywele zake nyuma kiasi, naye akasogea na kukaa hapo sofani. Mapaja yake yalifunuka zaidi baada ya yeye kukaa, ila halikuwa jambo zito kwa mwanaume kwa kuwa mambo ya uzungu namna hiyo alikuwa ameshayazoea kutoka kwa wanawake wengi.

Reuben akakaa hapo pia na kusema, "Unapendeza sana. Ulikuwa umetokea wapi?"

Josephina akatabasamu kiasi na kusema, "Asante. Ila niko kawaida tu mbona? Sikwenda popote. Leo niliona nije kukutembelea wewe tu."

Reuben akatikisa kichwa kuonyesha uelewa na kusema, "I see. Alikuelekeza Francis jinsi ya kufika hapa, bila shaka."

Josephina akatikisa kichwa kukubali na kusema, "Nilijisikia vibaya sikuweza kuongea na wewe tena kutokea ile siku. Ndiyo nikamwomba anielekeze ili nije kukuona."

"Oh, usijali wala. Usijisikie vibaya kwa lolote. Me niko sawa," Reuben akamwambia.

"Mlizika salama?"

"Yeah, tulimaliza... ndiyo tunajitahidi kuyasongesha maisha mbele sasa," Reuben akamwambia.

Josephina akatabasamu na kuibana midomo yake, akimtazama kwa njia yenye subira.

Reuben akamuuliza, "Mwanao hajambo?"

"Mzima. Vipi Larissa? Anaendelea vizuri?" Josephina akauliza pia.

Reuben akatazama pembeni kiufikirio.

"Ameshaanza kuongea?"

Reuben akatikisa kichwa kukanusha. "Nimeshauriwa kumwacha tu... kumpa muda yaani... ataanza tu tena kuongea," akamwambia hivyo.

"Lini?"

"Sijajua. Inaweza ikachukua muda mfupi... au mrefu."

"Masikini! Pole sana kwa hilo Reuben..." Josephina akamfariji.

"Asante. Nishapoa," Reuben akamwambia hivyo bila kuwa na uhakika kama ni kweli.

"Kwani ulikuwa umempeleka hospital... ndo' wakasema hivyo?" Josephina akauliza.

"Nilimleta daktari mmoja bingwa... akampiga check-up. Majibu ndiyo hayo, ila..." mwanaume akaishia hapo.

"Ila?" Josephina akauliza.

Reuben akamwangalia na kusema, "Ila naambiwa napaswa kumpeleka mbali ambako anaweza... ahah... akapata tiba nzuri sana... aanze kuongea haraka."

"Ni wapi?"

"London."

"Nani amekwambia hivyo?"

"Mama," Reuben akajibu kwa namna iliyoonyesha kukosa amani.

Josephina akamtazama kwa uelewa, naye akamuuliza, "Hautaki kumpeleka huko, si ndiyo?"

Reuben akatazama pembeni na kusema, "Ndiyo. Hata kama inaweza kuwa kweli, sioni haja. Naona itakuwa kupoteza gharama, na... hata hivyo sidhani kama hili ni tatizo kubwa sana. Atapona tu. Kama afya iko vizuri, atarudi tu kuwa sawa. Tutampa tu huo muda aponee huku huku..."

Josephina alikuwa akimsoma mwanaume huyu vizuri, naye akajisogeza karibu yake zaidi na kumshika pajani akisema, "Hizo siyo sababu."

Reuben akamtazama.

Josephina akamwambia, "Hutaki Larissa aende Ulaya kwa sababu unahisi ni kama atakupotea. Kama vile atakucha, si ndiyo? Unaogopa hisia ya kubaki mwenyewe."

Reuben akatikisa kichwa kukanusha na kusema, "Hapana Phina, siyo hivyo wala, ni kwamba tu...."

"Kama Lydia," Josephina akamkatisha.

Reuben akamwangalia kiumakini.

"Unahisi Larissa akienda mbali, itakuwa ni kama Lydia amekuacha kwa mara ya pili," Josephina akamwambia.

Reuben aliingiwa na hisia zilizovurugika baada ya mwanamke huyo kusema hivyo, naye akanyanyuka kutoka hapo sofani na kusimama pembeni, akiwa ametatizwa sana na maneno hayo. Josephina akatabasamu kiasi kwa namna yenye hila, naye akasimama pia na kumsogelea mwanaume huyo kwa nyuma.

"It's okay, Reuben. Nakuelewa vizuri. Hata mimi nilipatwa na hisia kama hizo baba yake Hans alipokufa... isingekuwa rahisi kumchukua mwanangu kutoka kwangu. Aende mbali? Hapana. Nisingekubali. Kwa hiyo nakuelewa," mwanamke akamsemesha kwa njia yenye kujali.

Reuben akatazama chini kwa huzuni.

"Ila inapokuja kwa Larissa, hali ni tofauti. Mtoto anaumwa Reuben, na...."

Josephina akaishia hapo baada ya kuona kiganja chake Reuben kimetetemeka kidogo. Akaelewa kwamba hisia za mwanaume huyo zilikuwa zimevurugika zaidi kutokana na maneno yake.

"Aam... naomba nisamehe kwa kukwambia hayo. Najua hatuna ukaribu sana hata hivyo, kwa hiyo sipaswi kuvuka mipaka," Josephina akaongea kwa hisia.

Reuben akamgeukia na kumwangalia usoni, naye akasema, "Haina shida. Asante tu... kwa kunielewa."

Alikuwa makini zaidi wakati huu, akijitahidi kuonyesha yuko sawa, naye Josephina akaamua sasa kufanya kilichompeleka hapo kabla ya mambo kuharibika. Akamsogelea karibu zaidi na kumshika mwanaume kiunoni, jambo lililofanya Reuben amtazame kwa hisia makini hata zaidi. Mwanamke alionyesha waziwazi lengo fulani kwa kumshika namna hiyo, na Reuben hakuwa amewaza kwamba Josephina angetaka kupeleka mambo baina yao kwa njia hiyo.

Nyuso zao zikawa karibu sasa, na Reuben akaita, "Phina..."

Josephina, akiwa anamwangalia kwa namna yenye kuamsha hamu, akabana zaidi kiuno cha mwanaume huyo kwa makucha yake na kusema, "Hauhitaji kuhisi upweke tena, Reuben. Ninaweza kukusaidia."

Reuben akakunja uso kimaswali zaidi, na kwa kauli hiyo ya Josephina, akaishika mikono yake na kuitoa kiunoni kwake kistaarabu, kisha akamwambia, "Sihitaji msaada wowote, Phina. Nimekwambia niko sawa."

Josephina akatikisa kichwa kupingana na hilo, naye akasema, "Unadanganya Reuben. Na wewe unalijua hilo."

Reuben akabaki kumwangalia kwa namna yenye kujihami.

Josephina akamsogelea karibu zaidi tena na kusema, "Ninaelewa maumivu unayopitia, ndiyo maana ninajua bado yanakupa stress sana. Kwanza Lydia, then Larissa, mama yako, hizi kazi... najua unachoka sana. Nina njia ya kukusaidia... kutuliza stress zako kwanza, ili uwe na nguvu zaidi, na I swear... hautajutia kuniruhusu nikusaidie..."

Reuben akatikisa kichwa kupingana na maneno hayo kabisa, naye akajitoa karibu yake na kusogea mpaka sehemu ya meza, akiiangalia picha ya marehemu mkewe na binti yake iliyokuwa hapo, naye akasema, "Sijui ni kwa nini unafikiri hivyo, lakini siwezi kukubaliana nawe. Ninakuheshimu Phina. Naomba tusifike huko nakoelewa unamaanisha."

Josephina akang'ata meno yake kwa kuhisi hasira kiasi, lakini akajituliza na kumwambia, "Hapana Reuben... hujanielewa vizuri. Ndiyo sababu nataka... nahitaji wewe mwenyewe ujionee maana yangu."

Reuben akabaki kimya na kutazama pembeni.

Josephina akairudia pochi yake sofani na kisha kusogea mpaka usawa wa meza, akitoa kikadi fulani ndani ya pochi hiyo, naye akasema, "Nipe tu nafasi Reuben nikuonyeshe kwamba ninaweza kukusaidia, kwa sababu sipendi kabisa kuona unaumia namna hii. Haustahili hii mikazo yote unayopitia. Please nakuomba..."

Reuben akabaki kimya tu.

Josephina akaiweka kadi hiyo mezani na kusema, "Haitakuwa kama namna ambavyo unafikiria ukiniruhusu nikuonyeshe nachomaanisha. Wewe mwenyewe ndiyo utaamua kama kinakufaa, au la. Namba yangu hiyo hapo. Anytime utakapojisikia kunitafuta, nitafute. Na mimi nitakuwa tayari."

Akiwa kimya tu bado, Reuben akainamisha uso wake kwa kuhisi kama amevunjwa moyo na mwanamke huyo.

Josephina akamsogelea karibu kwa nyuma yake na kumshika mgongoni, naye akasema, "Me naenda. Nimefurahi kukuona, na natumaini tutaonana tena. Usisahau hili Reuben. Niko hapa kwa ajili yako."

Baada ya kumwambia hivyo na kutojibiwa, mwanamke huyo akageuka na kuanza kuondoka sehemu hiyo kwa mwendo wake wenye madoido, huku Reuben akigeuka kumtazama. Alipoufikia mlango, Josephina akaufungua na kumtazama mwanaume pia, kukuta anamwangalia, naye akaibana tu midomo yake na kuondoka kutoka humo huku akihisi ni kama alipata ushindi kwa kiasi kikubwa ingawa kwa mwanzo mwanaume hakuonekana kutaka pendekezo lake. Na alikuwa shuta kweli Josephina, yaani hata wiki moja tu haikuwa imeisha tokea Reuben amzike mkewe tayari akawa ameanza mawindo! Ingembidi angoje kuona kama mtego wake wa maneno ungemnasa mwanaume huyo na kubadili akili yake.

Reuben, akiwa amebaki kusimama hapo ofisini kwake, akainamisha kichwa kwa kuhisi kuchoka kabisa. Hivi siyo alivyokuwa ametarajia ujio wa mwanamke huyo kazini hapo kuwa, yaani hata hakuelewa alichokuwa akikiwaza mpaka kumwambia yale yote. Akarudi tu kwenye kiti chake na kukaa, kiganja kikiwa usoni, mawazo lukuki kichwani,
na hali nzito mno moyoni. Angewahi kuja kupata amani kutokana na haya yote kweli?


★★


Si muda mrefu sana kupita baada ya Josephina kuwa ameondoka ofisini kwake Reuben na mwanaume huyu akawa amepigiwa simu na mmoja wa viongozi ndani ya kampuni yao hiyo. Walikuwa pamoja kwenye bodi kama wakurugenzi wa kampuni na nini, ila huyu aliyempigia akiwa kati ya wale wenye hisa za juu zaidi ndani ya kampuni, na akiwa na sauti kuu pia kati ya washiriki wote wa bodi hiyo. Kwa hiyo ni kama kusema mkubwa wake akawa amempigia simu kumwambia aende kwenye ofisi yake hapo hapo jengoni ili wazungumze kibinafsi. Reuben alijua bila shaka ingekuwa suala lililohusiana na kazi, kwa hiyo akamkubalia na kutoka ofisini kwake; moja kwa moja akipanda ghorofa lililofuata mpaka kuingia ofisini kwa mwenzake.

Mshirika huyo alikuwa mbaba msomi mwenye kitambi kizito kwelikweli, aliyeitwa Julius Ndenji, mfupi, mweusi, aliyevalia miwani pana ya macho. Reuben alimkuta akiwa ameketi kwenye kiti chake cha ofisi, ikiwa na mwonekano mzuri sana kama yake tu, naye akakaribishwa akae kitini pia ambapo wangeweza kutazamana kwa meza kuwatenganisha kutokea kati.

"Hapo vipi mzee?" Julius akamsemesha kirafiki.

"Ah, safi. Nimepita hapo nimekuta kama... sijui umebadilisha assistant?" Reuben akaongea.

"Ahaa... eeh. Kale kazuri kazuri kameondoka..."

"Wapi tena?"

"Alikuwa mwanafunzi bado, sijui ndo' ameenda full time... sielewi. Wamebadilisha, juzi ndiyo amekuja huyo mpya."

"Sawa sawa. Mambo mazuri lakini huku?"

"Fresh. Wewe?"

"Good," Reuben akajibu kwa unyoofu.

Julius akabaki kumtazama kwa utulivu.

Reuben akauliza, "So, let's get to it. Kuna ishu umesema unataka tuzungumzie..."

Julius akatikisa tu kichwa na kusema, "Yeah. Ni kuhusu wewe."

Reuben akamwangalia kwa umakini zaidi.

"Unaendeleaje?" Julius akauliza.

"Unamaanisha nini?" Reuben akauliza pia.

"I mean..." Julius akaishia tu hapo, akimwagalia kwa namna yenye maana fulani.

Reuben akalazimisha cheko ya pumzi na kusema, "Imeshaanza kuonwa ni kama Reuben ni mgonjwa sasa, eti?"

"Hakuna anayesema hivyo..."

"Ndo' nachoona una-imply. Kuna kipi kinachokufanya ufikiri labda siendelei vizuri mpaka uniulize ninaendeleaje?"

"Ilikuwa ni kama kukujulia hali tu. Kwa nini wewe uwaze hivyo?"

"Okay, basi... kama siyo hivyo... labda uniambie ulichoniitia kaka. Kuna kazi nyingi bado," Reuben akamwambia kwa heshima.

"Reuben... hauko sawa," Julius akamwambia.

Reuben akakaza macho kiumakini.

Julius akamnyooshea karatasi fulani hapo mezani, naye Reuben akaipokea na kusoma yaliyomo kwa ufupi. Alipoona ni ripoti fulani ya matokeo mabovu kutokana na kazi zilizofanywa kwa upande wake Reuben hizi siku za karibuni, mwanaume huyu akafumba macho kwa kusikitika.

"Wakati ule tupo mwanzo kabisa kuiinua kampuni, unamkumbuka yule jamaa ambaye alikuwaga anafanya kazi kitengo cha finance... nani hivi... aliyefiwa na mama yake lile ghorofa lilipoangukaga kule town?" Julius akauliza.

"Fidelis," Reuben akajibu bila kumtazama.

"Eeh, Fide. Ni vizuri unamkumbuka. Hiyo inamaanisha utakumbuka jinsi alivyorudi kazini baada ya msiba, akionekana kuwa na energy ya kutosha... lakini baadaye tukaja kuona alivyochoka... physically and emotionally, yaani... mpaka sehemu kubwa ya kazi zikavurugika kwa sababu...."

"Hii haipo kama hivyo, Julius..." Reuben akamkatiza.

"... motivation yake nzuri ilipotea kwa kadiri kubwa, najua unajua. Unakumbuka ili-cost kiasi gani cha pesa kwa vikwazo vilivyotokea kwa sababu yake?" Julius akauliza.

"Julius..."

"Nikumbushe..."

Reuben akatulia kwanza, kisha akasema, "Milioni thelathini."

"Yeah. Ikapelekea afukuzwe, awe chini ya deni kwa sababu ilionekana ameiba, wakati sisi wote tunajua haikuwa hivyo. Ni kwa sababu tu alipoteza focus kwenye..."

"Julius, naelewa unakoelekea," Reuben akamwambia.

Julius akatulia kwanza.

Reuben akasema, "Hii haiko kama hivyo. Haya... ni mambo nayoweza kurekebisha upesi. Surely, hizi ni... ni kazi zinazohitaji...."

"Focus na motivation," Julius akamkatiza pia.

Reuben akatazama pembeni.

"Reuben, huzuni huwa ina-trigger anxiety na depression ya hali ya juu ikiwa hautajipa muda wa kutosha kutuliza maumivu yako. Unataka kuikimbia hiyo hali upesi sana, ndiyo sababu ukaona uwahi kurudi kazini, lakini hiyo haikusaidii. Inakubomoa zaidi..."

"Julius..."

"Unahitaji kujipa muda, Reuben. Usiharakishe. Kila mtu anajua jinsi gani Lydia alikuwa wa muhimu kwako, na hizo kazi kufeli inaonyesha wazi kuwa your head is still not in back in the game... kwa sababu bado unatikiswa na huzuni yako. Ukilazimisha mambo, vitu vingi zaidi vitaanguka, na mimi sitataka kukuangalia unageuka kuwa Fidelis wa pili kaka'angu," Julius akamwambia kwa ustaarabu.

Reuben akatikisa kichwa kwa kusikitika sana, naye akasema, "Nitarekebisha hili. I swear. Hii ni utelezi kidogo tu. Unajua potential yangu. You know me."

"Yes, I do. Na ndiyo maana nataka kukusaidia urudi kuwa effective kama ambavyo nakufahamu, kijana wangu. Ila kwa wakati huu... naona dawa nzuri kwako ni kutulia kwanza ili hilo lifanikiwe," Julius akamwambia.

"Kwa hiyo unataka kusemaje Julius?" Reuben akauliza.

"Chukua mwezi wa kupumzika, Reuben," Julius akamwambia.

"Mwezi? Julius, come on..."

"Najaribu kukusaidia ili tusaidiane, Reuben. Ukiendelea kukaa hapa, najua utazidi ku-force vitu na mwisho wa siku...."

"Nahitaji muda ndiyo, lakini siyo kuwa nje ya kazi, ila ndani. Huo mwezi ndiyo ningeweza...."

"Nisikilize, nisikilize. Siyo... ombi. Ni jambo lililoamuliwa tayari. Unapaswa ukae nje ya kazi kwa mwezi mmoja kwanza, then urudi. Tuone itakavyokuwa," Julius akamwambia kwa ustaarabu.

Reuben akaishiwa pozi kabisa.

"Sikutaka hili jambo lisambae, kwa hiyo nitali-fix mimi mwenyewe. Naomba uende nyumbani, pumzika. Hakuna anayeelewa umuhimu wako hapa zaidi yangu, sitopenda mambo yaje kukuharibikia hapa wakati una jina zuri tayari. Hii itakufadisha sana, chukua hata... vacation. Nenda mbali, kapunge upepo, safisha akili, tuliza hisia, ninajua utarudi na nguvu zaidi..." Julius akampa ushauri huo.

Reuben akabaki kutazama pembeni tu kama vile amezubaa.

"Reuben..." Julius akaita.

Mwanaume akamgeukia.

"Umeelewa nilichosema?" Julius akauliza.

Reuben hakuwa na namna ila kutikisa kichwa kuonyesha uelewa, na hapo ndiyo Julius akampa pole kwa yote na kumsihi afuate ushauri wake ili kweli anufaike. Alihuzunika kujua alikuwa karibu kuwaangusha wenzake kwa sababu ya matokeo mabaya ya kazi alizofanya tangu arudi. Kampuni ilimpenda sana, na yeye alipenda kuwa kazini, lakini kwa sasa alihitaji kutuliza akili kwanza ili aje kufanya kazi kwa utaratibu maalumu na siyo tu kuziona kazi kama sehemu ya kuondoa mikazo yake. Ni hapo ndiyo aling'amua kwamba kweli bado hakuwa sawa, alijitahidi, lakini bado hakuwa sawa. Hivyo kama ni kuondoka kampunini kwa muda mfupi, angehitaji kwenda huko nje kuitafuta njia ambayo ingemsaidia arudie huo usawa wake.


★★


Alipoondoka huko kwenye kampuni, Reuben aliamua tu kwenda eneo lililokuwa likifanyiwa ujenzi wa hoteli yake kubwa. Kuna mahitaji mengi yaliyotakiwa kukamilishwa kwenye suala hilo, naye alipewa orodha ya vitu hivyo ili viongezwe na ujenzi uendelee. Akiwa anahisi ni kama alitoka kufukuzwa huko kazini, mwanaume alihitaji kujitia ubize na jambo fulani ili mawazo yake mengi yafifie, kwa hiyo pamoja na kwamba alikuwa bosi hapo, Reuben akavua mkoti wa suti na tai na kukunja mikono ya shati, akianza kusaidia kujenga pia sehemu kadha za jengo hilo. Walioajiriwa hapo walimshangaa sana, na mkandarasi mkuu hata akamwambia aache kufanya kazi hiyo kwa sababu iliwafanya wengine wasijisikie vizuri kumwona namna hiyo, lakini mwanaume akasisitiza kwa kuwaambia wote wawe huru, na yeye angesaidiana nao kwa kuwa alihitaji zoezi la mwili kidogo.

Kwa hiyo ikawa ni hivyo. Simu za mara kwa mara akitafutwa na watu kadhaa alizipuuzia kwa kujikita na kazi ya kunyanyua ndoo zenye zege, kupandisha mchanga kwenye ghorofa za juu, na hata kuchanganya udongo na simenti na kujiunga na mafundi kwenye mlo na kupiga story za hapa na pale ili kupisha muda na kumwondolea mkazo, lakini bado mwisho wa siku hali yake ilimrudisha kule kule tena kihisia. Ingawa alitoa jasho jingi kuzikimbia hizo hisia, zenyewe hazikutaka kumwacha. Akaona ingekuwa vyema labda akiondoka tu na kwenda kwake, labda kwa kuwa sasa alipewa muda wa kuwa nje na kazi, angeutumia zaidi kukaa na Larissa. Huenda ni kweli kuwahi kurudi kazini baada tu ya kuzika halikuwa jambo la busara kufanya, na bintiye alimhitaji kwa ukaribu zaidi kama yeye alivyomhitaji.

Alifika nyumbani kwake ikiwa ni kwenye mida ya saa mbili iliyoelekea tatu usiku. Msongamano wa magari katikati ya safari ulimfanya akawie kufika kwa sababu aliondoka huko kwenye hoteli yake jioni ya mapema tu, na ndiyo alipoingia ndani akawakuta wapendwa wake wakiwa wamekaa kwa kutulia. Mama yake pamoja na Sorange walikuwa sehemu ya sebule hapo chini wakiburudika na simu zao na maongezi, huku Cynthia akiwa huko chumbani kuandaa vitu vyake kwa ajili ya safari yao kesho. Kwa kuona jinsi Reuben alivyoonekana kuwa rafu kiasi, mama yake akauliza ni wapi alipita, lakini mwanaume hakujibu na moja kwa moja kuuliza binti yake alikuwa wapi.

Ni muda huo huo ndiyo Amina, yule dada wa kazi, akawa amefika hapo kumpokea bosi na kumsalimu, naye Reuben akageuzia swali hilo kwake. Amina akamwambia kwamba Larissa alikuwa ameshalala huko chumbani kwake baada ya kula mapema, na alitoka muda si mrefu kumwangalia na kukuta amevuta shuka kabisa. Akamuuliza bosi wake ikiwa angependa ampakulie chakula, lakini Reuben akasema alishiba na kumshukuru.

Ikabidi mama yake Reuben arudie kumuuliza mwanaume kwa kiingereza kabisa swali lile ambalo hakujibiwa, maana aliona ni kama amempuuzia. Hiyo ikamfanya Amina aondoke upesi hapo, na ndiyo mwanaume akasema alipita hotelini na kuwasaidia kidogo kwa ujenzi. Iliwashangaza wanawake, lakini kabla hata mama mtu hajaongeza swali lingine, Reuben akazielekea tu ngazi ili akajisafishe kwanza. Alihisi uchovu, lakini haukuwa wa kimwili, bali kihisia. Mama yake na dada yake walivunjika moyo kumwona namna hiyo, akiwa hajiweki karibu nao zaidi yaani, lakini hawakuwa na namna ila kumwacha tu.

Baada ya kujimwagia maji, Reuben akavalia kwa njia ya kawaida na kutoka chumbani kwake ili aelekee sebuleni kukaa na kuzungumza na mama yake, kwa kuwa hakutaka kuondoka kwao kesho iwe kwa namna yenye kuyaacha mambo katika sehemu ya sintofahamu zaidi. Hakukuwa na ubaya yeye kufanya maamuzi yaliyopingana naye, sema kwa kuwa hakuzungumza sana, labda ingeonekana amekwazika nao mno. Hivyo, akaanza kuelekea huko, na akiwa ameupita mlango wa chumbani kwake Larissa, Reuben akaamua kuufungua ili kumchungulia binti yake kwanza. Alikuwa anataka kumwona kidogo kama kawaida kwa sababu hakuweza kufanya hivyo kwa siku hii, na alipofungua mlango na kuingia, kweli akakuta binti yake akiwa amelala na kuufunika mwili wake vyema kwa shuka.

Lakini Reuben akatambua kwamba huo ulikuwa mwonekano tu. Aliposogea zaidi ndani ya chumba hicho chenye ugiza, akaona jinsi shuka kwa kule mbele kuelekea kichwa cha binti yake lilivyotoa mtikiso fulani wenye kujirudia, na alipokaza umakini wake hapo akatambua sauti ya chini sana ikitokea huko. Ikabidi aelekee upande wa kichwa chake Larissa, na alipofika karibu zaidi, akasimama na kubaki kumwangalia mtoto wake kwa hisia sana. Larissa hakuwa amesinzia. Alijifunika mpaka kichwani na kuonekana amejikunyata chini ya shuka hilo kitandani, huku akisikika kama analia. Reuben akachuchumaa na kulisogeza shuka pembeni kufunua vizuri mwili wa bintiye, na hapo ndiyo roho yake ikaingiwa na simanzi zaidi.

Larissa alijikunja sana, mwili wake ukishtuka kutokana na vilio vya sauti ya chini alivyotoa, na alichokuwa amekunjia kifuani kwake kwa mikono yote ilikuwa ni picha ndogo ya mama yake iliyowekwa ndani ya frame. Alilia kwa huzuni sana, bila kutoa sauti, lakini hali hii yote ilimfanya Reuben atambue namna ambavyo bado binti yake aliumia mno, na hakutaka wengine walione hilo. Mwanaume akamshika mtoto wake begani taratibu na kuita jina lake, naye Larissa akanyanyua kichwa juu na kumtazama. Alimwangalia kwa hisia sana, machozi yakiendelea kumtoka na kilio cha huzuni kisiweze kukata, na baba yake akajikaza tu kutoonyesha hisia zake zote kwa kuamua kupanda kitandani hapo na kukaa karibu na bintiye.

Akamvuta taratibu, na Larissa akaitikia hilo kwa kumruhusu hadi Reuben alipoweza kumweka miguuni pake, kisha akaulaza mwili wake kwenye kifua chake kwa kukumbatia. Akamwachia baba yake picha ile kiganjani, akiendelea kulia kwa sauti ya chini iliyoonyesha anajitahidi kuyakaza maumivu yake ingawa alikuwa mtoto mdogo sana, na kiukweli hii ilimtesa zaidi Reuben. Akiwa ameshikwa na simanzi nzito, akawa akimbembeleza tu mtoto wake kwa kumsugua taratibu mgongoni na kuzilaza nywele zake, huku akijizuia kutoa machozi pia kutokana na kuiangalia picha ya marehemu mkewe karibu na huzuni kuu ya binti yake mpendwa. Hisia zote za huzuni alizokuwa akijaribu kuweka kando, zikampiga zaidi kama wimbi zito sana ndani ya moyo wake.

Mwanaume huyu akaendelea kukaa na mtoto wake kwa dakika nyingi, namna hiyo hiyo, na mpaka alipokuja kutambua kwamba Larissa alikuwa ameshasinzia, ni muda wa saa zima ulikuwa umeshapita binti akiwa mikononi mwake tu. Akamshusha taratibu mtoto wake wa pekee na kumlaza pembeni, akamfunika vizuri, na kisha akakaa kwa dakika chache zaidi akimtathmini. Ilimuuma sana kutambua ni namna gani kifo cha mkewe kilimtafuna sana mtoto wao. Na mbaya zaidi, ni kama vile hakujua ni jinsi gani ya kumsaidia kutokana na yeye mwenyewe kuhangaishwa sana na hali hizi ziliizowapata. Hiyo ilimfanya ahisi yeye siyo baba mzuri, alianza mpaka kufikiria labda mama yake alikuwa sahihi; huenda kumpeleka Larissa mbali ndiyo jambo ambalo lingesaidia, lakini bado hakutaka kuafikiana na wazo hilo. Hakutaka kabisa.

Akiwa ndani ya dilemma nzito sana kutojua ashughulike vipi na huzuni ya binti yake ilhali hakuwa ameweza kuituliza ya kwake mwenyewe, Reuben akaona ni vyema tu akimwacha mtoto alale kwa sasa na yeye atoke kwenda sebuleni mara moja. Akamwacha Larissa akiwa amelala kwa usalama, naye akashuka mpaka chini na kuwakuta wapendwa wake wakiwa bado wamekaa kwa utulivu; Cynthia akiwepo pia. Mama yake na dada zake walitarajia kwamba Reuben angekwenda kujiunga nao hapo, lakini mwanaume alipowatazama tu, akaona ni kama asingeweza kupata utulivu wa kiakili kukaa nao baada ya kutikiswa kihisia na alichotoka kupitia chumbani kwa binti yake. Akawapita kabisa na kuelekea nje, akielewa wazi kwamba aliwaacha wakijiuliza anaelekea wapi.

Reuben akaenda tu mpaka ndani ya gari lake na kuliondoa hapo, ikiwa imeshaingia saa nne usiku, naye hakuelekea mbali, bali akajitoa tu kwenye hayo mazingira ya nyumbani na kwenda kuegesha eneo la nje lililokaribiana na barabara kuu. Alitulia humo kwa dakika kadhaa akijaribu kutafuta utulivu, lakini akili yake haikuacha kutangatanga. Vitu vingi vilipita kichwani, moyoni ndiyo alivurugika haswa, mpaka akawa anawaza labda alihitaji pia kumwona daktari ili aangalie endapo alihitaji msaada wa kisaikolojia pia. Hakujua kabisa afanye nini ili apate kitulizo ambacho kingemruhusu atende kwa busara ili amtoe binti yake kwenye mateso, na ndipo, wazo lile likawa limemwingia. Josephina.

Hakuelewa ni kwa nini, lakini mara ghafla tu akiwa ndani ya gari lake hapo akaanza kumwaza huyo mwanamke. Alikumbukia namna Josephina alivyomwonyesha hisia-mwenzi wakati wakiwa msibani, namna alivyomsemesha leo wakati wako ofisini, na pendekezo lake la msaada fulani aliosema angeweza kumpatia ambao ungemwondolea mikazo aliyokuwa akipitia. Aliwaza vitu vingi kuhusu kauli za mwanamke huyo, na ingawa angewazia kuuangalia upande huo kuwa jambo lisilofaa, akapatwa na hisia ya kutaka kujaribu "tiba" ambayo, kama maneno ya Josephina, ingemhitaji Reuben ajionee mwenyewe ili aelewe ni jinsi gani ingemsaidia kuondokana na mikazo yake.

Jicho la mwanaume huyu likatulia juu ya kisanduku cha kutunzia vitu vyake kadhaa alivyoweka kwenye gari hapo mbele, naye akakifungua na kuitoa ile kadi ambayo Josephina alimpatia leo ofisini. Alipoondoka kazini kwake leo alikuwa ameichukua pia na kuirushia humo, lakini hakudhani angeihitaji leo leo. Aliiangalia sana, namba ya simu ikiwa hapo na jina la mwanamke huyo, naye akaitoa simu yake na kuanza kuiandika. Kwa sekunde chache baada ya kufanya hivyo, akatulia kwanza, roho yake ikimfanya atake kusitisha kitendo cha kumpigia, lakini kichwa chake ndiyo kikamsukuma kukifanya tu hivyo hivyo. Kwa mpigo mmoja kidole chake, akawa ameitumia mawasiliano namba hiyo, nayo ikaanza kuita....

"Hallo..."

Kwa hakika sauti ya Josephina mwenyewe ikawa imesikika akisema hivyo, naye Reuben akasema, "Hallo. Phina?"

Upande wa pili, madam Phina akiwa amekaa mahali fulani na kuisikia sauti ya Reuben, akaachia tabasamu hafifu na kusema, "Reuben? Ni wewe?"

Reuben akasema, "Ndiyo, Phina. Ni mimi. I need your help."

Josephina akatabasamu kwa namna yenye kiburi zaidi kwa kuelewa sasa alikuwa anakaribia kuipata tuzo yake aliyoilenga, naye akasema, "Of course Reuben. Niko hapa kwa ajili yako. Nafurahi umenipigia."

Reuben akatikisa kichwa kiasi kama kupatwa na hisia za mara mbili tena, naye akasema, "Sijui... ni nini yaani... ila... sikuwa... sija...."

"Usiwaze lolote tena Reuben. Nilikuahidi ningekusaidia na nitafanya hivyo. Nakuomba tu ufuate nitakachokuelekeza. Sawa?" Josephina akaongea kwa njia yenye ushawishi.

Reuben akahisi aina fulani ya kitulizo japo kwa kadiri ndogo tu, naye akasema, "Okay. Niambie. Nifanye nini? Niko tayari."









★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom