DADA WA KAZI.
SEHEMU YA TATU
NYUMBANI KWA MR BENI-CHUMBANI KWA SIA-USIKU
Sia ameketi kitandani akiibofya simu yake huku Esta yupo kitandani amelala fo fo fo, mlio wa simu wa kuingia ujumbe unasikika, “hutaki kujibu meseji zangu ila najua ipo siku tu tutakuwa karibu Sia” Sia anasoma ujumbe ule ulioingia kwenye simu yake, mara mlango unafunguliwa, anaingia Mama Esta, Sia anashtuka na kuificha ile simu chini ya mto. Mama Esta anaketi juu ya kitanda pembeni ya Sia, “enhe..naona umeamua kukaa kimya tu” anasema Mama Esta, Sia anabaki amejiinamia, wanabaki kimya kwa muda, Sia anashusha pumzi, “Dada” Sia anasema, Mama Esta anatulia kumsikiliza, Sia anashusha pumzi ndefu, “mimba ni ya Meki” anasema Sia, Mama Esta anashtuka na kubaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa, “hebu rudia tena?” anauliza Mama Esta kwa sauti ya chini, “huo ndio ukweli Dada” anasema Sia, Mama Esta anabaki kimya ameduwaa kwa sekunde kadhaa, “sikiliza Sia..tena naomba unisikilize vizuri” anasema Mama Esta, “leo iwe mwanzo na mwisho kukusikia unamtaja Mwanangu kwenye ujinga wako” anasema Mama Esta, “Meki ni mwanafunzi” anasema Mama Esta, “jiandae naenda kukata tiketi unarudi kwenu Singida” anasema Mama Esta, “nitarudi kwa nani dada na bibi yangu mlezi nilikwambia ameshafariki” anasema Sia kwa sauti ya upole na uoga, “hayo hayanihusu mimi” anasema Mama Esta huku akiinuka na kutoka, Sia anajiinamia na kutumia kanga yake kujifuta machozi yanayombubujika, mlio wa kuingia ujumbe kwenye simu unasikika, polepole Sia anainua mto na kuichukua simu yake, anaibofya na kusoma ujumbe ulioingia, “nitakusubiri bila kuchoka Sia..nitachoka siku nimekupata” Sia anamaliza kuusoma ujumbe na kuibofya simu off kuizima, anaiweka chini ya mto na kujilaza pale kitandani huku akiendelea kububujikwa machozi.
NYUMBANI KWA MR BENI-NJE-ASUBUHI.
Sia yupo kwenye kiti pembeni ya bomba la maji, chini kukiwa na nguo kadhaa ndoo na sabuni, ametulia akiwa na nguo na sabuni mkononi huku akionekana kama Mtu aliyezama kwenye mawazo mazito, “Sia” anashtushwa na sauti inayomuita upande wa pili, anatulia sekunde chache, “Shali” Sia naye anaita kwa sauti ya juu, “upo wapi wewe?” inauliza tena ile sauti, “njoo nipo huku uwani” anasema Sia, baada ya sekunde chache anafika Shali, dada, 20, akiwa na mfuko wenye vitu ndani “enhe” anasema Shali, “ndio unatoka dukani?” anauliza Sia, “ee” anaitikia Shali, “jana nilikuwa mbiombio tukashindwa kumalizia maongezi yetu” anasema Shali, “yaani Shali mwenzako nipo kwenye njia panda” anasema Sia, “Ni hiyo laki tatu ya mshahara ninayodai haijapatikana ungekuta nimeshaondoka tangu juzi” anaongeza Sia, wanabaki kimya kwa sekunde kadhaa, “ila ule ushauri wako ni mgumu sana Shali” anasema Sia, “Sia..huna namna nyingine besti” anasema Shali, “ukikubali kurudi kule kijijini hivyo umekwisha” anasema Shali, “vile nilivyokuambia ndio njia iliyobaki Siaa” anasema Shali, wanabaki kimya, Sia anashusha pumzi, “hivi hata nitaanzia wapi Shali?” anasema Sia, “simu yako iko wapi?” Shali anamuuliza Sia, “unataka kufanya nini?” anasema Sia huku akimpatia Shali ile simu kwa kusita, Shali anainyakua na kuanza kuibofya akiandika ujumbe na kuutuma, “wewe Shali..umeandika nini?” anauliza Sia baada ya kusikia mlio wa kutuma ujumbe ukitoka kwenye simu yake, “Nimemuuliza ile zawadi ipo tayari?” anasema Shali, “weee” anasema Sia kwa mshtuko, mara unasikika mlio wa kupokea ujumbe, Sia anainuka na kutaka kumpora Shali simu, Shali anakwepa na kusogea pembeni huku akibofya na kuusoma ujumbe, “siamini leo umenitumia ujumbe bebii..nimefurahi mpaka moyo umesimama kwa muda..niambie nikusubiri lini asali wa moyo wangu” Shali anausoma ujumbe kwa sauti huku Sia akiwa amesimama sambamba pembeni yake akimsikiliza, Shali anaangua kicheko, “yaani wewe” anasema Sia huku Shali akiandika tena ujumbe na kutuma, “kesho unipe mrejesho” anasema Shali huku akimpatia Sia ile simu, “umemuambiaje?” anauliza Sia huku akiipokea simu yake, “nimemwambia kesho” anasema Shali na kuondoka akimuacha Sia yupo na butwaa.
NYUMBANI KWA OBO-CHUMBANI-MCHANA.
Sia ameketi juu ya kitanda, kwenye chumba kidogo kilichosongamana kitanda, stuli, jiko la mchina, kiti cha plastiki na vikorokoro vingine kadhaa, Sia ametulia akiangalia huku na kule, mlango unafunguka, anaingia Obo akiwa na chupa ya soda na mfuko mdogo mweusi, “yaani leo siamini umekuja..mpaka nahisi kuchanganyikiwa” anasema Obo kwa bashasha huku akiwa amesimama na chupa ya soda mkononi akimshangaa Sia, Obo anaweka chupa na ule mfuko juu ya stuli, “sasa pale gengeni umemuacha nani?” anauliza Sia, “yupo Kibo yule rafiki yangu” anasema Obo huku akiifungua ile soda, “karibu” anasema Obo huku naye akiketi kwenye kiti, “siku ya leo nitaiandika kwenye kitabu changu” anasema Obo, Sia anamuangalia Obo akimshangaa, “kwa nini?” anauliza Sia, Obo anashusha pumzi, “hujui tu furaha niliyonayo moyoni kwa wewe kufika kwangu Sia” anasema Obo huku akiufungua ule mfuko wenye chips na kuku.