Sehemu ya 42
“Mkeo amefika gesti, yupo na hawara wake” “Eeeeh!!” nilihamaki “Ndio, kafika yupo na bwana wake, fika fasta basi eneo la tukio tumalize kazi,” Issa alisisitiza, nilihisi kitu ndani ya kifua changu kikilipuka kama bomu.
Kitendo cha kuambiwa mke wangu alikuwa gesti na mwanaume mwingine kilinishitua sana. “Nakuja fasta Issa,” nilimwambia na kukata simu.
Sikuwa na habari tena na simu ya mama ambayo nilikuwa nimeihold, jambo pekee lililokuwa akilini mwangu ni kufika gesti ya Madrid na kushuhudia uchafu anaofanya mke wangu Nasra.
Bila kuwaaga wafanyakazi wangu, nilikurupuka na kutoka nje ya duka, nikaona nikitumia gari langu naweza kuchelewa eneo la tukio, nilichofanya ni kuchukua bodaboda.
Dakika kumi na tano badaye, nilikuwa Kinondoni, niliwasiliana na Issa akanieleza mahali walipokuwa wamebana, walikuwa kwenye glosary moja iliyokuwa mita kama 100 kutoka kwenye gesti aliyokuwa mke wangu.
“Umechalewa sana Faraji,”Issa alinipokea na lawama. “Samahani Issa, mambo ya foleni, si unajua mji wetu huu.”
“Unajua madhala ya kuchelewa hivi, inawafanya wagoni wetu wapate wasaa wa kufanya malovee,” Issa aliniambia, maneno yale yalikuwa mkuki wa moto kifuani.
“Kwa hiyo unataka kusema, hadi wasaa huu mke wangu na hawara wake watakuwa wamekwisha vunja amri ya sita?”
“Kwa muda huu watakuwa wako katikati ya raha ya penzi, hawajamaliza bado,” Issa alisema, hakujua kabisa kama maneno yale, yalikuwa ni sawa na ncha ya sindano kwenye kidonda.
“Sasa tufanyaje?” niliuliza kwa sauti ya unyonge. “Ngoja niwastue jamaa ili tuingie” “Jamaa gani” “Polisi na mwenyekiti wa mtaa”
“Kumbe hao nao wanahusika?” “Ndio, kwenye mchakato huu inaweza kutokea jinai, polisi na mwenyekiti watasimama kama mashahidi kama ikitokea hali hiyo.”
Baada ya Issa kuwasiliana na watu hao, muda mfupi badaye mzee mmoja, aliunga nasi.
Jumla tukawa watu watatu kwa maana ya waandishi wa habari wawili, mimi na yule mzee ambaye badaye nilimtambua kama mwenyekiti wa mtaa.