SEHEMU YA 50
MAUMIVU ya ndani kwa ndani yalifukuta kifuani mwangu, taswira ya mke wangu akifanya mapenzi na hawara wake, ikajitengeneza akilini mwangu. Donge zito likanikaba kooni.
Pumzi zilinitoka kwa shida. Nikataka kusema kitu, nikashindwa, sauti ikagoma ndio usiulize, iligoma kabisa kutoka. “Yanii!..Yaniii…Khaaa!” nilibwabwaja. Kigugumizi kikinizonga, bila kutarajia, machozi yakanibubujika.
Shemeji Aisha alitaka kunipa pole, akasita. Akataka kusema kitu, akaghairi, mwishowe akazipiga hatua kinyonge akiniacha nikipambana na hali yangu. “Baba unalia!” mwangu niliyekuwa nimempakata miguuni, akasema, ni baada ya kuyaona machozi yakinibubujika mashavuni na kutengeneza mifereji.
Jambo lile lilinighafirisha sana, sikupenda kabisa kulia mbele ya mtoto yule mdogo. Nilimwacha sebuleni, nikaingia chumbani na kufungulia sauti kubwa ya redio, kisha nikalia mno.
Dakika 15 badaye nikahisi kuna kitu nimepunguza baada ya kilio kile. Nikaingia bafuni, nikanawa uso, nikwanywa maji, nikajiweka vizuri ili Doreen na mtoto wangu Faraji wasione mabadiliko yoyote.
Baada ya kurudi sebuleni, nikakuta Doreen amekwisha aanda chakula cha usiku na wamekaa ‘dining Room’ wananingoja.
Tukiwa tunakula, kutokuwepo kwa mke wangu na shemeji Aisha kuliifanya nyumba yangu ipooze sana. Hata kwenye meza ya chakula kulipwaya. Pamoja na maumivu niliyokuwa nayapitia muda ule, sitaki kuficha kusema ukweli huu. Upweke wa nyumba yangu, ulinifanya nimisi uwepo wa watu wale wawili.
Hata hamu ya kula sikuwa nayo. Nikaonja onja kama kuwapa hamasa ya kula wale watu wawili kisha nilijiondoa pale ‘dining room’ nikarudi sebuleni, ile naketi kitini nikamkumbuka Issa Mnally, mwandishi aliyefotoa picha za mke wangu na hawara wake wakiwa wanafanya mapenzi.
Sikuwa nimewasilina naye tangu tulipoachana kwenye fumanizi la gesti, nilimpigia simu, nikamuuliza kama picha za mke wangu na hawara wake zipo, akanijibu zipo zote, na wahariri wa gazeti lao wamefurahia upatikanaji wa habari ile.
“Kwa hiyo, habari hiyo mtaitoa kwenye Gazeti gani?”nikamuuliza nikitambua kwenye kampuni aliyokuwa akihudumu kulikuwa na magazeti mengi.