SEHEMU YA 98
“Mwanaume kujiua kwa sababu ya mpenzi ni udhaifu mkubwa sana Faraji.”
Afande Mirumbe alizidi kunipasha, kauli yake ilizidi kunifanya nijione mpuuzi. “Siwezi tena kufanya huo ujinga afaande”nilimjibu uso wangu ukionesha kujutia sana.
Alinifungulia pingu akanitaka niwe naripoti kila siku kituo cha polisi hadi pale atakaporidhishwa na mienendo yangu. Jioni ya siku hiyohiyo, niliruhusiwa, nikarudi nyumbani.
Suala langu likawa gumzo mtaani na kwa marafiki. Mama yangu pamoja na dada za zangu walipopata habari zile, kwa kweli walihuzinika sana. Ilikuwa ni aibu kubwa kwa upande wangu. Kutaka kujiua kisa kutoswa na mwanamke. Ilikuwa ni fedheha.
Siku zilikwenda, miezi ikayoyoma. Sikuwahi kumwona wala kuwasiliana tena na Debora, nilikuwa nikiugulia ndani kwa ndani, safari hii nilikuwa tayari kufa kijerumani, lakini sio kutwaa uhai wangu mwenyewe.
Katika hicho hicho kipindi, nikajikuta napata hasara kubwa kwenye miradi yangu ya biashara, nilifunga maduka yangu mawili ya nguo yaliyokuwa pale Kinondni studio, pia saluni zote za sinza nikafanga kutokana na hasaea kubwa.
Nikabakia na duka moja tu la vipodozi ambalo lilikuwa Posta mtaa wa Azikiwe. Mapenzi yalikuwa yamevuruga mno maisha yangu, hata haiba yangu nayo ilinyauka.
Katika kipindi hicho hicho mke wangu wa zamani Nasra, naye alikuwa akijaribu kunioneshea upendo mkubwa kila alipokuwa akija kumwona mwanawe pale kwangu.
Ajabu ni kwamba, moyo wangu kwakwe ulikuwa wa baridi mno, kila nilipofikiria kuwa chanzo cha matatizo yale kilitokana na yeye, sio tu sikumpenda bali nilimchukia!. “Siwezi kuwa na wewe Nasra, sina hisia tena juu yako.” Siku moja nilimwambia, baada ya kujaribu kunishawishi.
“Lakini mwanetu anahitaji malezi ya baba na mama.” “Hilo ulitakiwa ulifahamu tangu mwanzo.” “Usifikirie mabaya yangu tu Faraji, kumbuka mimi naye ni binadamu.” “Hata kama Nasra, lakini dhambi ya usaliti haivumiliki.” “Tafadhali niko chini yako.”
Kila wakati Nasra alisema neno nisamehe, ikafikia hatua nikahisi huenda Nasra anakazana kuniomba msamaha katika kipindi kile kigumu kwangu akiamini inaweza kuwa faida kwakwe kwa kuwa nilikuwa napitia nyakati ninazo hitaji faraja.