SEHEMU YA 92
Roho ya mauti ilikuwa imenivaa, sikuona ubaya wa jambo lile, sikuipa nafasi akali yangu kufikiria mara mbili ama mara tatu na zaidi.
Kila kitu nilichofanya kilisukumwa kwa utashi wa hisia.
Kabla sijajiua sauti ya kimalaika ikanikumbusha “Sasa ukijua nani mwenye hasara? unamkomesha nani. Unajiua Debora anabaki duniani anaponda raha. Ujinga huo.”
Bahati mbaya ibirisi alikwisha nizingira pande zote za dunia, nilichofanya ni kuanza kuhesabu moja hadi tatu kabla ya kujiachia na kujinyongelea mbali: “Moja, mbili, tatuuuu!” nikajiachia!!. Kamba ikanibana shingoni kwa nguvu.
Nikaanza kutapatapa kwa kukosa hewa, kadiri sekunde zilivyojongea ndivyo nafsi yangu ilivyohitaji kuhema, niliishika ile kamba ili nijinasue. lakini wapi. Sikuwa na nafasi nzuri ya kujiondosha.
Uzito wa mwili ukazidi kuikaza zaidi ile kamba shingoni, nikauhisi mkojo ukinitoka na kulowanisha suruali yangu. Kila sekunde zilivyozidi kupotea ndivyo nilivyoona nguvu zikiniishia.
Hamu ya kuishi ikanirejea. Nikajitahidi kwa nguvu zangu zote ili nipige kelele za kuomba msaada, bahati mbaya sauti haikutoka.
Na hata kama sauti ingetoka, bado nisingeweza kupata msaada kwa wakati sahihi. Kamba ilikuwa imebana shingo yangu.
Muda ule ilikuwa ni usiku mkubwa, msichana wangu wa kazi na mwanangu Faraji walikuwa wakikoroma huko vyumbani mwao. “Nilikwambia usijiue, unaona sasa unakufa!!”ile sauti ya pili ilinilaumu fikirani nikiwa naipambania roho yangu.
Nikataka kusema neno ‘nisaidie’ nikajikutana nalitamka kimoyomoyo. “Jitahidi kuizua kamba usife, piga kelele.” Sauti ilinisihi. Wakati huu nikaitii sauti ile ya kimalaika.
Nikaing’ang’ania kamba kwa nguvu ili isizidi kunikaba shingoni, kadhalika nikijitahidi kupiga kelele. Bahati mbaya sauti haikutoka zaidi ya kuishia kukoroma kama chura au gari lililoishiwa mafuta.
Muda huohuo, giza la ajabu likazikumba mboni zangu, na wakati giza linagubika mbele ya ngu nikajiona naelea katika anga maili nyingi kutoka ardhini.
Halafu muda huohuo nikajiona naanguka kwa kasi kuelekea chini, ajabu nikawa sifiki. Katika anguko lile, nikabaini kwamba nilikuwa natumbukia kwenye shimo lenye giza zito. Kuzimu.
JARIBU KUTABIRI KITU GANI KITATOKEA.... . TUKUTANE KESHO HAPAHAPA