Simulizi Binafsi: Ninavyomkumbuka Rais wa Awamu ya Tatu Mzee Benjamin Mkapa

Dr Mathew Togolani Mndeme

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
201
808
UTANGULIZI:
Kwa neema ya Mungu nimefanikiwa kuishi kwenye uongozi wa marais wote 5 wa nchi yetu hadi sasa nikiwa tayari na uwezo wa kuelewa kinachoendelea duniani (kwa sehemu). Kwa kuwa nina shahuku (enthusiasm) kubwa na uongozi na dhana nzima ya kutumikia watu (ambayo siasa ni sehemu yake) nimefuatilia na kujihifadhia kumbukumbu nyingi za marais wote watano. Katika hizo leo ninawiwa kusimulia kidogo ninavyomkumbuka Rais wa awamu ya tatu Mzee Mkapa, ambaye kwa huzuni kubwa ametutoka kwa kutushtukiza.

Kabla ya kusimulia ninavyomkumbuka Mzee Mkapa, niweke wazi maslahi yangu kwamba, pamoja na udhaifu wake kama mwanadamu na makosa kadhaa ya kiungozi ambayo yeye mwenyewe aliyakiri na kayaandika kwenye kitabu chake, nilivutiwa sana na uwezo wake wa kiungozi, kiakili, kufikiri kibunifu, kujieleza, na kuchambua mambo. Hivyo unaposoma jua hili ni simulizi langu nilitoalo bila kurejea maandiko yake, masimulizi ya watu wengine, au taarifa nyingine zinazomhusu. Kumbukumbu na mtizamo wangu vinaweza kutofautina na wengine.

1595719951269.png

SIMULIZI LA JUMLA
Mzee Mkapa alisikika sana kipindi akiwa waziri wa sayansi na elimu ya juu, nafasi aliyoishika kabla ya kuwa Rais wa nchi. Akiwa wizara hii kulikua na harakati nyingi za wanazuoni na wanafunzi wa vyuo vikuu ingawa tulikua na vyuo vikuu viwili tu, UDSM na SUA. Wanazuoni na wanafunzi wa vyuo vikuu walikua wana sauti kubwa kwenye undeshaji wa nchi na walikua chimbuko kubwa la fikra pana, tafakuri tunduizu, hoja chokonozi, mawazo mbadala, mitazamo fikirishi, na mabadiliko ya kimfumo.

Mzee Mkapa alipogombea urais kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995. Kugombea kwake kuna upekee maana kama ilivyokua mwaka 2015 kwenye uteuzi wa rais wa sasa, Mzee Mkapa hakua miongoni mwa “waliokua na majina makubwa” miongoni mwa wagombea wengi wa CCM. Alipita kwenye mchakato mgumu kwa kuungwa mkono na Baba wa Taifa na alimnadi nchi nzima. Ingawa hakukua na mitandao kijamii na TV ziliwafiki wachache, tuliokua vijijini tulifuatilia vema kampeni zake dhidi ya Mzee Mrema kupitia vifaa vya kisasa tulivyokua navyo almaarufu kama “Radio ya Mkulima” iliyotufaa sana kusikiliza RTD na Radio One.

Alipoanza majukumu yake ya urais, alitumia muda mwingi akiwa Ikulu bila kufanya ziara nje wala mikoani hadi alianza kulaumiwa. Alitumia muda mwingi kusoma, kujipanga, kupata taarifa sahihi, na kutunga sera na mikakati ya kuitoa nchi katika hali ngumu iliyokuwepo kipindi kile. Kipindi kile rushwa ilikua imetapakaa na kukumbatiwa kuliko Korona; hali ya uchumi ilikua ICU; mapato ya serikali yalikua haba; taifa lilikua na madeni ya kutisha; na mfumuko wa bei ulikua kama 30%. Aliingia madarakani na kaulimbiu yake ya “UWAZI NA UKWELI” na kati ya mambo ya kwanza kufanya aliunde tume ya kuchunguza hali ya rushwa iliyoongozwa na Jaji Warioba.

Matokeo ya tume ya Wariaoba hayakushughulikiwa kisheria. Nilipofuatilia chanzo changu kilinijulisha (ingawa sikuweza kuthibitisha) kwamba Mzee Mkapa alipomaliza kusoma ripoti ya tume ya Warioba, “aliomba apewe kinywaji atulize akili” kwa sababu ilimchanganya. Niliambiwa alishindwa kuamua aanzie wapi kwani kama angeamua kuchukua hatua za kisheria ni watu wachache sana kwenye taasisi za umma na waliokua kwenye serikali yake wangepona. Ingawa hakuchukua hatua za kisheria ninashawishika alitumia ripoti ile kama kichocheo cha kuanza kujenga taasisi imara za kuendesha nchi. Taasisi nyingi na mifumo tuliyonayo sasa ama alianzisha yeye au zina msingi katika uongozi wake.

Mzee Mkapa aliingia madarakini nikiwa ndio nimemaliza darasa la saba. Hivyo alianza mwaka wake wa kwanza wa urais nikiwa kidato cha kwanza. Tarehe 11 June 1996, shule ya Ilboru ilikua inatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Tulifanya maandalizi makubwa kwa miezi kadhaa kwa ajili maadhimisho yale na Rais Mkapa ndio alikua anakuja kama mgeni rasmi. Tukiwa tumejiandaa kumpokea, asabuhi habari ikaletwa shuleni kwamba Rais asingeweza kufika kwa kua kumetokea ajali mbaya ya meli ya MV Bukoba, hivyo kuna msiba wa kitaifa. Pamoja na huzuni kubwa ya msiba, moyo ulinyong’onyea sana kukosa kumwona Mzee Mkapa.

Mzee Mkapa alipokuja na sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma, jambo hili lilimkera Baba wa Taifa na kwa ubaba wake alimkosoa hadharani maana aliona hatukua na maandalizi ya kutosha kutekeleza mpango ule. Jambo hili lilikua kinyume kabisa na sera ya ujamaa na kujitegemea iliyokua kama Imani kwa Mwalimu Nyerere. Moja ya vitu vilivyonigusa ni adabu ya Mzee Mkapa kwani pmoja na nguvu zote kama Rais wa nchi, sikuwahi kumsikia akijibizana na Mwalim Nyerere. Alifunga kinywa chake akiheshimu maoni ya maonyo ya Baba wa Taifa huku akiendelea kutekeleza majukumu yake. Mzee Mkapa alikua na uwezo mkubwa wa kudhibiti kinywa chake alipoamua.

Mwaka 1997 nilikua miongoni mwa wanafunzi tulioshinda pale uwanja wa Amri Abeid Karuma tukimsubiri na baadaye kumsikiliza Mzee Mkapa, Moi na Museveni wakifufua upya Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokua mautini kwa miaka 20. Mafanikio haya yalikua ni mfanikio ya kidiplomasia ya pekee kwani mahusiano ya nchi zetu yalidorora kwa muda mrefu. Pia, nilikua miongoni mwa wanafunzi tuolishinda kwa masaa Zaidi ya sita barabarini chini ya ulinzi wa kutisha tukisubiri msafara wake na rais Bill Clinton alipokuja pale AICC Arusha. Nakumbuka tulisikitika kwamba pamoja na kushinda na njaa barabarani Clinton alipopita hatukumwona kwa sura na alitumia muda usiozidi masaa mawili pale AICC na kuondoka nchini.

Nakumbuka mwaka 1998 Mzee Mkapa alipata tatizo la kiafya lilipelekea kutibiwa nchini Marekani kwa muda. Akiwa kule, Baba wa taifa akaumwa na kulazwa hospitali ya Mtakatifu Thomas pale London. Hospitali hii ilipata umaarufu mkubwa sana Tanzania ingawa wengi wetu huenda ndio tuliisikia kwa mara ya kwanza. Siku ya kwanza nilipofika jiji la London, hospital hii ilikua miongoni mwa maeneo niliyoyatembelea nikiwaza uwepo wa Baba wa Taifa mule ndani.

Mzee Mkapa alipokua anarudi nyumbani akitokea Marekani, alipitia London kumwona Mwalimu na akatujulisha hali ya maendeleo yake. Ingawa alitupa matumaini, maelezo na sura yake yalidhihirisha hali ilikua sio njema. Siku chache baadaye, akiwa mwenye huzuni kubwa, akalijulisha taifa kuwa Baba wa Taifa amefariki. Siwezi kusimulia hisia tulizopata siku ile maana ilikua kama vile maisha yamesimama kusikia Mwalimu amefariki. Tulisikiliza habari hii tukiwa ukumbi wa mikutano wa shule na ilikua siku chache kabla ya mitihani ya taifa ya kumaliza kidato cha nne kuanza, hivyo iliahirishwa kusubiri msiba umalizike. ITV ilirusha msiba ule “live” na ninakumbuka siku Rubani Masawe alipoishusha Ndege ya Air Tanzania pale JK Nyerere International Airport kipindi kile ukiitwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Ni ngumu kuelezea tulivyokua tunajisikia tukisubiri ndege ile na ilipoanza kujitokeza angani wengi tulilia. Ajabu hisia zile zimenijia na machozi yananitoka nikiandika kumbukizi hili. Mzee Mkapa aliongoza maandamo yaliyompitisha Baba wa Taifa barabara za Dar es Salaam akiwa mwenye majonzi makubwa. Msiba ule ulimtesa sana Mzee Mkapa.

Mzee Mkapa alihabatika kua na uwezo mkubwa wa akili, kufikiri, kuchambua na kujenga hoja. Vitu hivi viliboreshwa sana na uwezo wake ya kusoma na kujisomea. Nakumbuka mwaka 2005 moja ya majengo ya Ikulu ya Magogoni lilipata ajali ya moto na kupelekea maktaba yake binafsi kuungua. Jambo lile lilimuhuzunisha sana Mzee Mkapa kwani sehebu ya hazina yake ya vitabu iliteketea. Enzi zile anagombea urais tuliambiwa akiwa mwanafunzi pale sekondari ya Pugu alisoma vitabu vyote vilivyokua maktaba ya shule (sikuthibitisha). Alipokua rais wasaidizi wake walipata wakati mgumu maana hakua Rais wa kukaririshwa taarifa na wasaidizi bila kuzisoma na kuhoji. Vyanzo vyangu vilikua vinaniambia Mzee Mkapa alikua anasoma kila repoti inayofika mezani kwake bila kujali ukubwa wake. Hivyo alifanya maamuzi yake mengi akiwa na taarifa za kutosha kuhusu jambo husika. Sifa hii pamoja na uzuri wake, ilikua ina shida kwa upande mwingine kwani alipokua akijiridhisha kwa jambo lolote, alilisimamia kwa nguvu zote hata kama lilikua na shida.

Kaama sehemu ya mkakati wake wa kuteleza sera yake ya uwazi na ukweli kwa vitendo, Mzee Mkapa alianzisha utaratibu wa kuongea na taifa kila mwezi kupitia vyombo vya habari. Ulikua ni mkakati wa kuwasiliana na taifa kwa mambo ya msingi kama vile sera, uendeshaji wa nchi, kutoa taarifa mbalimbali, mabadiliko ya sheria, ujenzi wa mifumo, hali ya uchumi, siasa, nk. Aliamini katika utaasisi na mamlaka ya wananchi. Aliamini katika kushirikisha wananchi katika shughuli za maendeleo na uendeshaji wa taifa. Hotuba zile zilikua na mambo mengi ya muhim hivyo zilipochapishwa kwenye vitabu tarkibani miaka 10 iliyopita, nilijinunulia nakala zangu.

Nilipenda kumwona Mzee Mkapa kutokana na “style” yake ya “kutembea na kuongea kibabe”. Alikua “mbabe” mwenye roho ya utumishi na asiyependa kuonea mtu. Nilipenda ubabe wa kauli zake zilizokua na mamlaka na ujasiri wa kifikra, tafakuri na uelewa wa mambo. Mzee Mkapa hakua anatembea na ulinzi mkubwa lakini alipokuwepo nguvu ya mamlaka yake ilikua nhahiri. Nilipenda sana kuona msafara wake. Nakumbuka nikiwa nafanya kazi pale AICC Arusha ambapo alikua anakuja mara nyingi kwenye mikutano, nilikua naacha shughuli za kazi na kuhakikisha natizama ujio wake na kuondoka kwake. Nilitamani kukutana na kufanya mazungumzo au kufanya kazi karibu naye hivyo nikashawishika niingie kwenye “mafunzo maalumu ya kijeshi” ili nipate upenyo wa kufanya kazi karibu naye. Pamoja na kubadilisha mawazo ya kuingia kwenye “mafunzo ya kijeshi” kwa sababu kadhaa, yeye ndio aliyenishawishi sana kupenda nadharia na mikakati ya kijeshi mambo ninayofuatilia na kujifunza hadi leo.

Nilifuatilia ziara zake nje ya nchi na kazi kubwa aliyoifanya kwenye jumuia za kimataifa kwenye sera za kusamehewa madeni, kupambana na UKWIMWI, na utandawazi. Uzalendo wake kwa Afrika, kujieleza kwake, na maarifa yake viliwavutia hata mabeberu ambao hakua na simile ya kutofautiana nao kwenye mambo ya msingi. Nakumbuka baada ya tatizo la kisiasa kule Zanzibar lililopekelea baadhi ya misaada kusitishwa na wafadhili kusema hawatatusaidia kugharamia uchaguzi mkuu, Mzee Mkapa aliwajibu kwa ubabe kabisa kwamba hatutawapigia magoti na uchaguzi wetu tunaendesha kwa gharama zetu. Hakutaka tuingiliewe uhuru wetu kwa kigezo cha umaskini na aliamini tunaweza kumaliza shida zetu wenyewe.

Pamoja na ujuzi wake mkubwa wa lugha ya kingereza, Mzee Mkapa alikipenda sana Kiswahili na alikiongea kwa ufahasa mkubwa. Yako maneno kadhaa ya Kiswahili kama utandawazi, asasi, mshikadau/mdau, ukata, nk ambayo amana yalirasimishwa au yalijulikana na wengi katika kipindi chake kwa kua alikua anayatumia kwenye hotuba zake. Siku namaliza shahada ya kwanza, alijumuika pamoja nasi akitunukiwa shadaha ya heshima ya uzamivu na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa kukikuza Kiswahili.

Mzee Mkapa aliipa elimu umuhim mkubwa sana na aliheshimu sana tafakuri za kitaalamu. Pamoja na hayo “wasomi walimkoma” maana hakupenda na hakuana uvumilia wa kusikia hoja dhaifu au zisozo na mashiko. Vyuo vikuu vya binafsi vingi vilianza wakati wake, alipanua wigo kwenye vyuo vya umma, alianzisha msingi wa ujenzi wa shule za kata uliongeza shule za sekondari kwa kasi kubwa na mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa (MEMKWA). Alizungukwa na wasomi wabobezi kama washauri wake. Mmoja wao ni Profesa Amani aliyenifundisha uchumi hasa uchambuzi wa uchumi mdogo (Microeconomics Analysis). Namkumbuka alivyokua anakuja darasani akitokea Ikulu na kuegesha gari lake karibu na ukumbi wa Nkurumah alipokua anatufundisha. Alikua anakuja darasani mkononi akiwa ameshika chakipeke yake lakini alifundisha somo kwa upana sana na huwezi kutomwelewa. Akimaliza kufundisha ukaenda kusoma vitabu vya uchumi kwenye alichofundisha utadhani yeye ndio aliviandika.

NILIPATA NAFASI YA KUMPINGA
Pamoja na kuvutiwa sana na uongozi wa Mzee Mkapa, nilihusika kumpinga alipokosea. Baba wa Taifa alinifundisha kupinga inapolazimu, lakini kwa hoja. Moja ya nyakati hizo ni mwaka 2004 nikiwa mwaka wa kwanza chuo kikuu. Serikali ilileta sharia ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu ambayo ilipitishwa na bunge kwa mtindo wa mwendokasi na bila kutushirikisha na tulikuja kugundua sharia ile kwa sehemu kubwa ilinakiliwa kutoka Ghana. Kwa fikra na malezi ya kijama tuliyokua nayo, ilikua ngumu sana kuelewa sera ya serikali kutukopesha ada tena kwa masharti ya kulipa kama mkopo wa kibenki. Tuliiona ni sheria ya kibeberu. Tulipoona hatusikilizwi, tukaanzisha mgomo wa kutoingia madarasani na kuandamana. Tulivumiliwa kwa siku kama 3 hivi. Siku ya mwisho majira ya saa 9 mchana, ikatoka amri kwamba tumepewa masaa mawili kila mwanafunzi awe ametowe ndani ya eneo la chuo na wale jamaa wa kugawa vichapo cha mbwa koko walikua tayari kuanza kazi.

Inahitaji Makala tofauti kuelezea tukio lile kwani wanafunzi wengi hawakujua hata kwa nini tunafukuzwa kwani hawakua wanafuatilia yaliyokua yanaendelea kuhusu uanzishwaji wa bodi (unajua tena utamaduni yetu, wengi hatufuatilii kujua “issues”, tunasubiri habari za kusimuliwa). Mimi nilikua nakaa chumba kimoja na spika wa bunge la wanafunzi pale UDSM (sasa ni hakimu mfawidhi) hivyo niliielewa ile sharia kwa undani na madhaifu yake. Tulikua na hoja kadhaa lakini mojawapo “tuliyoipa uzito” tulisema tukiikubali bodi ya mikopo wadada wenye degree hawataolewa maana itakua ngumu kuoa mke ambaye unamlipia mahari na deni la bodi ya mkopo. Pia wakaka huenda tungekosa wake maana wasingetaka kuelewa na wadaiwa. Sisi wakaka ingelazimu tutafute wake wenye vyeti na diploma za ualimu maana hawana madeni na wadada wangejijua na degree zao za kukopeshwa.

Baada ya kufukuzwa chuo tuliendelea kudai kuandamana kupinga sharia ile na wiki ilifuata tuliruhusiwa kuandamana kwa wale tuliokua tumebaki Dar. Tulianzia maandamano pale Chuo cha Ardhi, tukakata kona kuingia Sam Mujoma hadi Ubongo. Tulipofika mataa tukakata kushoto tukiitamalaki Morogoro Road. Tulipofika pale Magomeni kwenye junction ya Kawawa Road nikawaona wanasiasa kadhaa wa upinzani wametokea kusikojulikana kwenye magari wakajiunga nasi kumalizia safari ya kueelekea viwanja vya Jangwani. Mmoja wao alikua Mh James Mbatia mwenyekiti wa NCCR, kipindi kile akiwa na jina kubwa. Tulipofika Jangwani tukaanza kuhutubiana tukipigwa na jua na njaa kali. Nakumbuka niliondoka pale kama saa kumi na moja jioni nikiwa hoi nimechoka, nina njaa, kiu kali, na nimepigwa na jua vya kutosha. Ila nilijisikia raha kupinga sera ya Rais ninayemkubali na kwamba nimeshiriki kutetea haki yetu ya msingi ya kujieleza. Mzee Mkapa aliruhusu watoa vichapo watusindikize na kutulinda ingawa tulikua na hofu kubwa wangeweza kutugeuka. Kwa “ubabe uleule nilioupenda toka kwake” baada tu yay ale maandamano, Kesho yake Mzee Mkapa akatia saini ile sharia kuanza kutekelezwa halafu akapanda ndege kuelekea ubeberuni kwenye moja ya ziara chache alizokua anafanya.

HITIMISHO.
Namkumbuka Mzee Mkapa kwa mengi sana kwani mabadiliko mengi yaliyofanyika chini ya uongozi wake yalinikuta nikiwa mwanafunzi wa sekondari na shahada ya kwanza; kipindi ambacho niliguswa na mambo mengi ya kisera na kisheria. Pia nilipiga kura kwa mara ya kwanza katika uongozi wake. Alikua mmoja ya watu niliotamani kukutana nao kwa mazungumzo na kujifunza toka kwao. Hata binti niliyomchumbia alijua hilo siku za mwanzo kabisa za kumwinda. Hivyo nimesikitika sana kuona amelela mauti bila ya kupata nafasi hiyo. Nakumbuka fursa mbili ambazo nilikua nikutane naye na ikashindikana. Mojawapo niliandaliwa kabisa kua mmoja ya watu wa kupokea mgeni mashuhuri bila kujulishwa niliyekua nimpokee ni Mzee Mkapa. Muda wa kumpokea nikajikuta siko eneo husika na nikakosa nafasi ile. Tukio lile lilinitesa sana. Kati ya mipango yangu ya miezi michache baadaye nilipanga kutafuta nafasi ya kukutana naye pamoja na Mzee Pius Msekwa ambaye nilishawasiliana naye kuhusu mkakati wangu wa kuandika kitabu cha mambo fulanifulani. Ninasikitika kwamba nimekosa nafasi hii na sitaipata tena.

Mzee Mkapa hakua mtimilifu ila alikua kiongozi aliyeitumikia nchi yetu kwa bidii, alikua mzalendo, alitujengea fursa, na alitetea maslahi ya uafrika wetu kwa nguvu kubwa. Aliamini watu aliowapa majukumu ya kumsaidia na aliwapa nafasi ya kutumia mamlaka aliyowapa na uwezo wao wa kufanya kazi. Si hii ni ya muhim sana kwa kiongozi mwenye maono makubwa ingawa wako waliotumia kuamikana huko kujinufaisha na kumwangusha. Nakumbuka alipokaribia kuondoka Ikulu alikua ana programmes za kuagana na makundi kadhaa ya kijamii. Mojawapo ya ninazozikumbuka ni alipokutana na watu wa sekta binafsi. Jioni ile alipopewa nafasi ya kusema neno aliongea mambo machache na sentensi moja haijawahi kunitoa kichwani. Aliwaambia kwa lugha ya kimombo kwamba, “I might have not been the best president you would expect, but I was your president anyway” (inawezekana sikua rais mzuri sana, lakini viwavyo vyvote vile, nilikua rais wenu). Tumepoteza kiongozi ambaye hakuona aibu kukiri makosa yake na kukubali na kubadili mitizamo yako alipopata taarifa na uelewa sahihi au bora zaidi.

Buriani Benjamin William mtoto wa Mkapa na kiongozi wa taifa letu.
Buriani mwanafunzi mtiifu wa Mwalimu Nyerere, na mpigania haki ya kujitawala na kujitegemea.
Buriani mtoto wa Kimakonde, mwanapinduzi na uliyetumikia taifa lako kwa uaminifu;
Buriani mzalengo wa kweli na mpigania uhuru wa waafrika.
Buruniani mume wa Mama Anna Mkapa uliyeandamana naye hadi mauti yako.
Buriani mpenda amani na mpatanishi wa kimataifa.
Buriani Rais Mstaafu na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania.

Tutakuenzi Mzee Ben na kuwasimulia watoto wetu habari za uongozi na tuumishi wako.

Bwana alimtoa Ben mtoto wa Mkapa na Bwana amemtwaa, Jina la Bwana libarikiwe kwa maisha na utumishi wake.

Imeandikwa na Mathew Togolani Mndeme (mmtogolani@gmail.com)
 

Attachments

  • 1595719924560.png
    1595719924560.png
    184 KB · Views: 4
Nimemsikia Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu enzi ya utawala wa Mkapa kwa miaka kumi akimuelezea Mzee Mkapa anasema alikuwa ni mtu wa uwazi na ukweli, kama ukimpelekea ushauri lazima umueleweshe, akiukubali atakwambia hapo hapo sawa, na kama akiukataa atakwambia hapo hapo jambo lako haliwezekani, kwa kifupi huyu mzee alikuwa hazunguki mbuyu.

Vile vile Sumaye ameelezea majanga yaliyolikumba taifa enzi za utawala wa Mkapa;

- Majanga kama ajali ya MV Bukoba, iliyochukua roho zaidi ya watu mia minne.

- Ukame ( anasema ulikuwa mkali mpaka pale mto Ruvu unapoungana na bahari mtu angeweza kutembea kwa miguu na asilowane, baadhi ya ofisi za kibalozi zikaondoa watumishi wake nchini kwa kusema ukosefu wa maji ni hatari kwa usalama wao).

- Baada ya ukame mwaka uliofuata zikaja mvua za El Nino, hizi nazo ziliharibu miundo mbinu karibia nchi nzima.

- Pia pakawepo na ajali ya treni iliyotokea Dodoma na kuchukua uhai wa watu karibia mia tatu na themanini.

Vile vile Mzee Sumaye anasema tukio lililomsikitisha Mzee Mkapa wakati wa utawala wake ni machafuko yaliyotokea Pemba mwaka 2001, Sumaye anasema wao kama serikali walipokea taaeifa kwamba huko Pemba kuna wananchi wamemkata askari polisi na kumchinja hadharani, baada ya hapo, wananchi wale wakawa wanaelekea kituo cha polisi kupora silaha, hivyo polisi wenyewe baada ya kupata hizo taarifa ndio wakaamua kwenda huko kuzima ile hali iliyokuwa ikitokea.

Hapa Mzee Sumaye alishindwa kuthibitisha kama ni kweli askari polisi alichinjwa au zilikuwa ni taarifa za uongo zilizoifikia serikali, lakini kwa namna tukio hilo lilivyomsononesha Mzee Mkapa, ni dhahiri hizo taarifa hazikuwa za kweli.
 
Back
Top Bottom