* SURA YA TATU *
Punde bwana Mtemvu aliposhuka kwenye gari, alitoa simu yake mfukoni akampigia mtu aliyemtunza kwa jina la Ninja. Aliongea naye kwa muda mfupi tu kisha akairudisha simu yake mfukoni akielekea kwenye kiti cha mgahawa mkubwa wenye jina la STEERS. Aliketi hapo akichezea simu yake kubwa nyeupe.
Ndani ya muda mfupi mhudumu alikuja na kumsikiliza, akahudumiwa. Ndani ya dakika zisizozidi kumi na tano magari mengine mawili yenye nembo za STK yakafika eneo la mgahawa. Watu wanne walishuka na kuelekea upande alipo mzee Mtemvu. Nao walisikilizwa na kuhudumiwa na wahudumu kisha maongezi yakachukua nafasi.
“Tujipongezeni jamani, hatimaye tumerudisha amani mioyoni mwetu … Cheers!” Mtemvu alibwabwaja wakagongesha glasi zao za mvinyo wakizisindikiza na matabasamu mapana usoni mwao. Waliongea maneno machache huku vicheko vikiwa vingi.
Baada ya muda waliagana na kutakiana kazi njema lakini mzee Mtemvu hakuondoka pale mgahawani. Baada ya dakika kadhaa alijumuika na kijana mmoja aliyekuwa anamuita kwa jina la Ninja. Alikuwa ni kijana mrefu mno mwenye misuli minene na kifua kikubwa kama makalio.
Alikuwa kavalia kombati la jeshi na macho akiyafunika kwa miwani kubwa ya jua. Alisalimia kisha akaketi wakaanza kuteta na mzee Mtemvu kwa sauti ya chini mno wakitazama usalama. Mzee Mtemvu aliingiza mkono mfukoni mwa koti akatoa shilingi milioni moja na kumkabidhi Ninja ambaye hakupoteza tena muda pale, akajiondoa.
Huko nyuma, mzee Mtemvu naye alitizama kushoto na kulia kisha akalifuata gari lake na kutokomea. Ila kulikuwa kuna mtu anamtizama muda wote akiwa pale mgahawani. Hakujua. Na si tu kumtizama, bali sasa alikuwa anamfuatilia hatua kwa hatua akiwa katika muonekano wa kivuli kilichoonekana pale tu mwanga wa jua ulipokiangazia.
Gari la Mtemvu, mtumishi mkubwa wa serikali, sasa liliacha lami likashika barabara ya vumbi iliyoelekea moja kwa moja na kukomea mbele ya geti kubwa jekundu lililojishikiza kwenye ukuta mrefu mnene wa rangi ya samawati. Hapo geti lilifunguka lenyewe gari likaingia na kisha geti likajifunga.
“Mpenzi, nimerudi nyumbani!” Mtemvu alipayuka baada tu ya kumaliza kuongea na dereva wake.
Nyumba ilikuwa kubwa na ya kuvutia; vigae vyekundu viliezekwa kwa juu, madirisha yake makubwa yalipachikwa vioo, chini kulitandikwa tiles, kuta zilipakwa rangi nyeupe, na bustani kubwa ya maua ya kupendeza ilitambaa mbele ya uso wa nyumba. Ilipendeza.
Mtemvu alifika mlangoni, mkewe: Mama Beatrice, akatoka na kumkumbatia.
“Karibu, mpenzi.” Alimbusu mumewe kwenye lips.
Japokuwa umri wao ulikuwa si haba, mapenzi yao hayakusita kujionyesha. Mtemvu alirudishia busu wakaingia ndani.
Walioga na kula wakajipumzisha sebuleni. Mtemvu alivalia bukta fupi rangi ya manjano na kaushi nyeupe huku mkewe, Mama Beatrice, akijisitiri kwa khanga pekee. Walikuwa wanapiga soga za hapa na pale haswa juu ya msiba wa karibuni. Watoto hawakuwepo hivyo walikuwa huru kushikana na hata kutomasana mara zingine.
Baada ya muda kidogo walinyanyuka kwa milengwa ya kueleka chumbani kujilaza. Ila kabla hajajitoa sebuleni, Mtemvu aliendea dirisha akafungua pazia na kuchungulia nje, akaliona gari lake. Alitahamaki.
“Mbona Mustafa hajaondoka?”
Alikunja sura.
“Si nimemwambia apeleke gari service?”
Mustafa, mwanaume wa makadirio ya miaka hamsini na mbili, ni miongoni mwa watu wapole wenye sauti ya chini. Ndiye mtu aliyekuwa anayempa kampani Mtemvu muda mwingi kwa kuwa naye garini.
Anamfahamu mkuu wake akiwa katika hali yoyote ile; anajua wakati ambao mkuu wake anamtaka aongee na wakati gani anaomtaka anyamaze. Zaidi ya yote anafahamu vyema siri za mkuu wake, pengine kuliko mkewe.
Mtemvu alipata shaka. Alitoka nje akalifuata gari, alipolifungua mlango akakuta Mustafa amelalia usukani. Alimuita lakini hakuitika. Alimshika begani akamvuta kumnyanyua.
La haula!
Mustafa alikuwa anamimina damu mdomoni na uso wake haukuonyesha kutojitambua. Moyo wa Mtemvu ulitetemeka na akajikuta anahisi hofu imemtambaza.
“Mustafa! Mustafa!” Aliita akimtikisa lakini Mustafa alikuwa kimya. Alimshusha kwenye gari akamlaza chini. “Mustafa! ... What is this? Mama Beatrice! Mama Beatrice!” Mtemvu aliita. Aliinamisha kichwa chake akakilaza kifuani mwa Mustafa: kifua kilikuwa kimya, tuli.
Aliponyanyua kichwa chake, mkewe – mama Beatrice – alikuwa tayari ameshafika, na msichana wa kazi – Habiba – alikuwa amesimama mlangoni. Mvulana wa kazi naye – Lupi – alikuwa amefika eneo la karibu.
“Nini baba?” Mama Beatrice alichuchumaa. “Nini kimetokea?”
“Sijui! Nimemkuta Mustafa hivi. Anatoka damu na mapigo yake ya moyo yamesimama!”
“Tumpeleke hospitali! … Au mpigie dokta wako!”
“Dada, embu niletee simu yangu hapo kwenye kochi.”
Dada, msichana mchanga mwenye umri kati ya 15 mpaka 18, aliyevalia gauni lake la pink iliyofifia na kiremba kichwani, mwembamba mrefu na mwenye uso wa upole, alielekea alipotumwa akarejea na simu ya bosi.
Mtemvu akampigia dokta.
Dokta aliwasili ndani ya dakika thelathini. Aliukagua mwili wa Mustafa kwa dakika kadhaa, akatikisa kichwa.
“Amefariki.”
“Nini kimemuua?” Mtemvu alidakia. Dokta akameza kwanza mate.
“Sijui, bado sijafahamu. Nahitaji kuufanyia uchunguzi zaidi.”
“Sawa. Acha basi nitoe taarifa polisi.”
Mtemvu alichukua simu yake akapigia polisi. Ndani ya muda mchache polisi walifika wakahoji na kufanya msako mwepesi bila ya matunda, mwili wa marehemu ulichukuliwa polisi wakaenda na daktari. Mtemvu pamoja na mkewe walirudi ndani tukio hilo bado likiwa kichwani na midomoni mwao. Walijilaza kitandani giza la usiku likazidi kudaka umri.
Ila Mtemvu hakupata usingizi.
***
Muendelezo soma hapa