Simon Matheri Ikere: Handsome aliyeitikisa Kenya....! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Simon Matheri Ikere: Handsome aliyeitikisa Kenya....!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Jun 1, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Jun 1, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Simon_Matheri%20Ikere.jpg
  Simon Matheri Ikere
  71229_01.jpg
  Mwili wake baada ya kuuawa

  matheri.jpg

  wanjiru.jpg
  Felister Wanjiru mkewe Matheri

  Siku ya Jumanne ya Februari 20, 2007 ni siku ambayo haitasahauliwa na Wakenya wengi, na hasa Polisi wa nchi hiyo. Ni siku ambayo Polisi zaidi ya 100 wa nchi hiyo kutoka kwenye kitengo maalum cha kupambana na uhalifu walifanikiwa kumuua jambazi mmoja sugu na aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba aliyejulikana kwa jina la Simon Matheri Ikere aliyekuwa na umri wa miaka 30.

  Akiwa bado ni kijana mmbichi wa umri wa miaka 30, Simon Matheri Ikere alikuwa ni jambazi hatari aliyekuwa akivuma katika viunga vya jiji la Nairobi kama mzimu kiasi cha Polisi kukiwekea kichwa chake dau la shilingi za Kenya zipatazo 150,000 kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake.

  Ilikuwa ni majira ya saa nane na nusu za usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne, Polisi zaidi ya 100 waliizingira nyumba ya Simon Matheri Ikere iliyokuwa katika eneo la Athi River takribani kilomita 30 Kusini, Mashariki mwa jiji la Nairobi.

  Katika tukio hilo ambalo lilitawaliwa na kurushiana risasi hatimaye ilibidi Polisi wamuombe mtuhumiwa ajisalimishe kwa kutoka nje ya nyumba yake ili kunusuru maisha ya watu wengine waliokuewa ndani ya nyumba ile. Simon aliamua kujisalimisha.

  Wakati anatoka nje ya nyumba yake, Polisi walimshambulia kwa risasi na kumuuwa. Polisi walifanikiwa kumuua Jambazi huyo baada ya kupata taarifa kupitia kwa raia mwema, na kwa kutumia satelaiti walifanikiwa kujua mahali alipo kupitia simu yake ya mkononi, baada ya kupata namba yake ya simu kutoka kwa raia huyo mwema.

  Msemaji wa Polisi nchini Kenya Gideon Kipunjati alisema kwamba Matheri alikuwa anatuhumiwa kwa mauaji ya watu zaidi ya 18 miongoni mwao wakiwa ni daktari bingwa wa maradhi ya ukimwi {AIDS} Prof. Job Bwayo ambaye aliuawa mwanzoni mwa mwezi huo huo wa Februari pamoja na mfanyakazi wa kimishenari wa Kimarekani aitwae Lois Anderson na binti yake Zelda White.

  Mauaji ya Wamarekani hao yalitokea mnamo Januari 2007 katika tukio la kupora gari ambapo inasemekana Matheri na wenzie ndiyo waliohusika. Kipunjati alikiri kwamba Polisi walikuwa na ushahidi wa kina wa kumhusisha Matheri na mauaji hayo.

  Naye kamanda mkuu wa Polisi wa jiji la Nairobi Njue Njagi akizungumzia tukio hilo alisema, "Leo ni siku kubwa kwa upande wa jeshi la Polisi, kwani tumefanikiwa kumuua jambazi sugu aliyekuwa akilisumbua jeshi la Polisi kwa muda mrefu."

  Kamanda Njagi aliendelea kusema, "Mtu huyu alichukulia kuuwa kama kitu cha kufurahisha [hobby} lakini kwa uwezo wa Mungu leo polisi tumeweza kuzima vitendo vyake." Kmanda huyo aliendelea kubainisha kwamba Jeshi la Polisi bado linaendelea kuwasaka majambazi wengine watano ambao ni washirika wakuu wa Matheri.

  Polisi wa nchini Kenya wanaamini kwamba Matheri alikuwa akiongoza genge la majambazi ambalo lilikuwa likiendesha uharamia katika miji mikuu ya Afrika Mashariki, ambapo wakazi wa miji hiyo kwa muda mrefu wamekuwa majeruhi wa vitendo vya ujambazi vilivyokuwa vikiendeshwa na Matheri pamoja na genge lake.

  Baada ya kumuuwa Matheri Polisi katika upekuzi walioufanya katika nyumba yake walikuta bunduki aina ya AK-47 pamoja na risasi 26. Hata hivyo upo utata uliojitokeza katika taarifa zilizonukuliwa kutoka pande mbili, yaani upande wa Polisi na mke wa Matheri kwa upande mwingine

  Kwani kwa upande wa Polisi walidai kwamba wakati wanamuuwa Matheri alitoka akiwa na bunduki aina ya AK-47 na hivyo kuwalazimisha Polisi kumuuwa ili kujihami, lakini kwa upande wa mkewe, Felister Wanjiru ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi saba wakati huo, akihojiwa na kituo cha Luninga cha KTN alidai kuwa mumewe alitoka akiwa hana silaha yoyote, tena alitoka akiwa kifua wazi akiwa amevaa kaptula, maarufu kama Bukta huku akiwa ameweka mikono yake kichwani ili kuwaonesha Polisi kwamba hakuwa na silaha yoyote, lakini kwa mshangao Polisi walimmiminia risasi mumewe na kumuuwa palepale.

  Akisimulia zaidi mkasa huo katika kituo hicho cha Luninga, Wanjiru alisema kwamba siku ya tukio alikuwa amelala na mumewe chumbani, mara akasikia michakato ya miguu nje ya nyumba yao, lakini mumewe hakuonekana kwamba alikuwa na wasiwasi, baadae walisikia sauti ya Polisi waliokuwa nje ya nyumba yao wakijitambulisha na kumtaka mumewe atoke nje na ajisalimishe haraka la sivyo wataichoma nyumba moto na kuwauwa wote waliomo ndani.

  Mumewe aliposikia hivyo alijificha chini ya mvungu wa kitanda ili kuokoa maisha yake. Baada ya kuona kwamba Polisi wanazidi kusisitiza msimamo wao, ilibidi amsihi mumewe ajisalimishe ili kuokoa maisha ya watoto wake, kwani katika nyumba ile walikuwa yeye Wanjiru na mumewe Matheri pamoja na watoto wao 6, huku Wanjiru akiwa akiwa na ujauzito wa miezi 7.

  Akizidi kusimulia, Wanjiru alisema kwamba mumewe aliamua kutii amri ya Polisi na kutoka nje huku akiwa amevaa bukta na mikono yake ikiwa nyuma ya kichwa. Alipofika nje aliamriwa apige magoti huku akiwa ameweka mikono yake nyuma ya kichwa na aache kinywa wazi, kitu ambacho alitii.

  Ndipo Polisi mmoja alipomsogelea mahali alipo na kutumbukiza mdomo wa Bunduki yake kinywani mwa Matheri na kisha kuifyatua sawia, huku kila mtu akishuhudia. Katika mauaji hayo, Polisi walikiri pia kumuuwa mtu mwingine ambaye inasemekana alikuwa ni mlinzi binafsi wa Matheri {Bodyguard}. Utata wa namna Matheri alivyouawa haukusumbua vichwa vya Wakenya walio wengi, kwani kwao hiyo haikuwa ni hoja, bali cha msingi kwao ilikuwa ni kusherehekea kuuawa kwa Matheri.

  Polisi hao walimchukua mkewe Matheri na watoto wake sita na kuwapeleka katika kituo cha Polisi cha Kilimani kwa mahojiano zaidi ili kuwasaidia Polisi kuwakamata watuhumiwa wengine wa mtandao wa ujambazi uliokuwa ukiongozwa na mumewe. Hata hivyo watoto watatu wa waliozaliwa katika ndoa ya awali ya Matheri kati ya hao sita walichukuliwa ndugu zake Matheri.

  Ndugu zake Matheri, walidai kwamba hawafahamu kwamba Wanjiru alikuwa ni mke wa Matheri kwa sababu hajawahi kukanjaga ardhi ya kijijini kwao alipozaliwa Matheri.Wanjiru alikiri kwamba watoto hao watatu aliowazaa yeye hawakuwa wa Matheri bali walizaliwa katika ndoa yake ya awali na baba wa watoto hao alifariki mwaka 2003 baada ya kuishi wote kwa miaka kumi.

  Alidai kwamba alikutana na Matheri katika eneo cha Ongata Rongai baada ya Matheri kuhamia katika nyumba iliyokuwa jirani na anapoishi. Matheri alijitambulisha kwake kama dereva Taxi na yeye Wanjiru wakati huo alikuwa ni kibarua katika shule moja katika eneo hilo. Baada ya kuanza uhusiano mwezi mmoja baadae waliamua kuishi pamoja.
  Hapo ndipo alipoanza kuhisi kwamba mpenzi wake huenda alikuwa ni Jambazi.

  Lakini alikuja kupata uhakika zaidi baada ya kuona picha yake kwenye gazeti na pia kuonyeshwa kwenye luninga akihusishwa na mauaji ya watu 11, pamoja na matukio ya ujambazi.
  Miezi mitano baadae Matheri aliamua bila kumshirikisha kuhamia katika eneo la Kitengela. Kuhama kwao kulikuwa kwa ghafla kiasi cha kuacha baadhi ya samani zao. Alimweleza kwamba kuna adui wake wa siku nyingi kutoka kijijini kwao huko Kiambu anamuwinda ili amuue kutokana na ugomvi wao wa ardhi.

  Wakiwa hapo Kitengale Matheri alimfungulia duka la bidhaa, Hawakukaa muda mrefu waliamua kuhama tena na kuhamia katika eneo la Athi River. Alitoa sababu ile ile ya kuwindwa na adui yake ili auawe. Hapo napo hawakukaa muda mrefu Matheri akataka wahame kwa sababu amepata nyumba nyingine katika eneo la Ongata Rongai, alihamisha vitanda na viti, na kuvipeleka huko. Alimwambia kwamba watalala chini. Lakini baadae akamwambia atanunua samani nyingine na kuzirudishia.

  Siku hiyo ya kuuawa kwake Matheri, yeye na watoto wake pamoja na mtu mwingine ambaye Matheri alimtambulisha kama rafikiye aitwae Muchiri, ambaye alipenda aitwe "M" walikuwa pale nyumbani na walikuwa wamelala chini kwenye mkeka pamoja na watoto wao sita.Wanjiru alisema kwamba, kuna siku alimuuliza kuhusu habari aliyoiona kwenye TV kwamba anatafutwa na Polisi kuhusiana na tuhuma za ujambazi, ndipo Matheri alipomwambia kwamba kamwe hatakufa kwa kuuawa bali kwa kifo cha kawaida. Akimnukuu, kwa maneno yake mwenyewe Matheri alisema,"Nitakufa kifo cha Mungu, lakini hakuna mtu atanipata na aniue."

  Wanjiru alisema kwamba, mara nyingi Matheri alikuwa akitumia mlango wa nyuma kila atokapo na anaporudi nyumbani. Alitumia mlango wa mbele kwa mara ya kwanza siku alipoamriwa na Polisi atoke nje ambapo aliuawa. "Hakuwahi hata siku moja kuruhusu niangalie documents zake kikiwemo kitambulisho chake, na alikuwa akienda kuoga na Pochi yake. Sikuwahi kujua jina lake kamili mpaka siku alipoitwa na Polisi atoke nje." Alisema Wanjiru.

  Inashangaza kwamba kwa miaka miwili ambayo Wanjiru na Matheri waliishi kama mke na mume lakini Wanjiru alimfahamu mumewe huyo kwa jina moja tu la Matheri.

  "Alikuwa ni mtu wa kutabasamu muda wote, alikuwa akinisikiliza kwa makini wakati nikiongea naye, na hakuwa mzungumzaji zaidi ya kuwa msikilizaji na mwelewa." Alisema Wanjiru akimwelezea Matheri.

  Katika kijiji alichozaliwa Matheri kilichopo magharibi mwa jiji la Nairobi vituo vya Luninga nchini Kenya vilikuwa vikionesha wakazi wa kijiji hicho wakishrehekea kwa nyimbo za kuwasifia Polisi kwa ushujaa wao wa kumuuwa mtu ambaye alikuwa ni tishio kwa usalama wao na mali zao.

  Hatua ya kuuawa kwa Matheri inasemekana ni katika kutii amri ya waziri wa usalama wa raia nchini Kenya, Mheshimiwa John Michuki ambaye Wakenya walimpa jina la utani la "Kimeendero" au "Crusher" ya kuwaamuru Polisi kuwauwa majambazi pale wanapoonekana kukabiliana na Polisi kwa silaha.

  Simon Matheri Ikere kijana mzuri mwenye sura ya mvuto na mpole kupindukia alikuwa ni mtoto wa nane kuzaliwa akiwa ni kitinda mimba wa familia ya Mzee Peter Ikere Gichungu aliyekuwa dereva wa malori nchini humo na mkewe Martha Wanjiru, mama wa kilokole.

  Kwa mujibu wa maelezo ya wazazi wake, Simon Matheri Ikere alizaliwa mwaka 1977 na katika kipindi chote cha utoto wake hakuwahi kuonesha tabia ya wizi. Tabia walioijua aliyokuwa nayo tangu utoto wake ni ile ya kuwa na hasira za ziada ambazo hawadhani kama ndio chanzo cha mtoto wao kuwa jambazi sugu.

  Baba yake alisema kwamba mwanaye alishindwa kuendelea na masomo ya elimu ya msingi katika shule ya msingi Kihara akiwa darasa la sita. Mzee huyo alikiri kutojua sababu hasa ya mwanaye kuacha shule akiwa darasa la sita ili hali alikuwa na maendeleo mazuri tu shuleni.

  Baada ya kumuona mwanye ameacha shule, Mzee huyo akaamua kumpeleka katika eneo la Wangige ambalo ni maarufu kwa shughuli mbalimbali za ufundi, maarufu kama Jua Kali nchini Kenya.

  Matheri alipelekwa katika eneo hilo ili akajifunze ufundi wa kuchomea vyuma {Welding}. Baba yake anakiri kwamba huenda katika eneo hilo la Wangige ndipo mwanaye alipojifunza tabia ya uchomaji wa nyumba moto {Arsonist}, ingawa hata hivyo wataalamu wanasema tabia hii ni maradhi.

  Siku moja miaka saba iliyopita ndipo vitendo hivyo vya uchomaji nyumba moto vilipoanza pamoja na usumbufu mdogo mdogo katika familia. Mzee huyo anakumbuka siku moja likuwa ametofautiana naye na kutokana na hasira zake za ziada Matheri aliamua kuchoma nyumba yake mwenyewe na kisha kutoweka.

  Kitendo cha kuchoma nyumba yake mwenyewe ambayo aliijenga kwa msaada wa baba yake, kilimuuzi sana mzazi huyo na hivyo kumfungulia mashtaka ambapo alifungwa miaka mitano jela.

  Matheri alitumikia kifungo chake cha miaka mitano katika jela yenye ulinzi mkali ya Kamiti ambayo hutumika kwa wafungwa sugu wa ujambazi. Katika kipindi ambacho alikuwa jela, huku nyuma familia yake iliishi kwa amani, ambayo hata hivyo ilitoweka mara baada ya Matheri kuachiwa huru kutokana na kumaliza kifungo chake.

  Awali wazazi wake walidhani alikuwa amebadilika kitabia kutokana na kutumikia kifungo cha miaka mitano jela, kitu ambacho haikuwa sahihi. Kumbe katika kipindi hicho ambacho alikuwa akitumikia kifungo ndipo alipo alipohitimu na kuwa jambazi sugu.

  Baba yake alikiri kwamba anaamini mwanaye alifuzu kuwa mwizi na jambazi sugu kwa kufunzwa wakati alipokuwa katika jela ya kamiti, jela ambayo hutumika kuwafunga wahalifu sugu. Baada ya kutoka jela, baba yake aliamua kumjengea mwanaye huyo nyumba mpya akiamini kwamba atakuwa amebadilika, lakini hali ilikuwa tofauti, kwani nyumba hiyo baadaye ilikuja kuchomwa moto na watu wenye hasira kali kutokana na kukerwa na vitendo vyake.

  Alipotoka jela tu Matheri alinunua bunduki aina ya AK-47 kutoka kwa wakimbizi wa Somalia na katika hali isiyo ya kawaida, alimtishia kaka yake kwa bunduki hiyo baada ya kutofautiana katika mambo ya kawaida tu.
  Baada ya mkasa huo, ilibidi familia ilifahamishe jeshi la Polisi, ambapo Polisi walianza kumtafuta. Kama vile machale yalimcheza, Matheri alitoweka haraka sana pale nyumbani kwao na akawa anakuja pale mara chache sana tena usiku wa manane.

  Pilika zake za ujambazi zilianzia katika wilaya ya Murang'a. Akiwa na washirika wake, Matheri aliendesha ujambazi katika wilaya hiyo, mpaka alipokoswakoswa kuuwawa na Polisi katika msitu mmoja ambapo walikuwa wakifuatiliwa na Polisi ambao walikuwa wanatumia mbwa wa kunusa. Katika tukio hilo washirika wake wawili waliuawa na yeye aliponea chupuchupu baada ya kujitumbukiza katika mto wenye maji yaendayo kwa kasi na kupotelea kusikojulikana.

  Baada ya tukio hili Matheri alihamishia makazi yake katika jiji la Nairobi ambapo pia alikuwa akitoka na kuingia katika miji mikuu ya Afrika Mashariki na kufanya uharamia na kisha kutoweka kutoka mji mmoja hadi mwingine ili kuwakwepa Polisi.

  Katika kipindi ambacho Matheri aliendesha uharamia katika wilaya ya Murang'a, familia yake nayo haikusalimika. Mara nyingi familia hiyo ilivamiwa na wananchi wenye hasira kali na kuchomewa nyumba ili kulipiza kisasi. Mzee Ikere alidai kwamba kila wakati mtu anapovamiwa na majambazi katika miji ya Nairobi, Mombasa, Kisumu au mji wowote, familia yake ilikuwa ikipata usumbufu mkubwa, kwani walikuwa wakipata wageni ambao huja kulipiza kisasi kwa kufanya uharibifu mkubwa ikiwa ni pamoja na kuchoma nyumba za familia hiyo.

  Ilifikia mahali hata wizi mdogo mdogo wa kuku, jina la mwanaye lilihusishwa na wizi huo, kitu ambacho haikuwa kweli. Tukio ambalo Mzee Ikere anasema hatalisahau ni pale aliposhambuliwa kwa mapanga na mikuki na watu wenye hasira kali ikiwa ni katika kulipiza kisasi, kiasi kwamba aliachwa na majeraha huku akivuja damu bila kupata msaada wowote kutoka kwa majirani zake. Ilitokea hata watu wenye magari waliotaka kumpa msada ili kumpeleka hospitalini walikuwa wakitishwa kwamba nao wangeshughulikiwa. Kutokana na usumbufu huo, ilibidi waombe msaada polisi ili familia hiyo ipate msaada wa ulinzi lakini hawakupata msaada huo.

  Hadi kufikia mwaka 2007, jina la Simon Matheri Ikere lilikuwa likivuma nchini Kenya kutokana na uhalifu aliokuwa akiundesha yeye na genge lake. Lakini kama waswahili wanavyosema, hakuna marefu yasiyo na ncha. Ilipofika Februari 20, 2007 ukawa ndio mwisho wa mtu huyu.

  Kuuawa kwa Matheri kulipokelewa kwa hisia tofauti na jamii ya Wakenya, miongoni mwao zilikuwa ni taasisi za watetezi wa haki za binadamu. Taasisi hizo ziliwashambulia Polisi kwamba walitumia kauli ya Waziri wa Usalama wa raia, Mheshimiwa Michuki vibaya. Taasisi hizo zilipinga waziwazi kuhusu kuuawa kwa Matheri na kuwashutumu Polisi kwamba hawakumtendea haki Matheri kwani alipaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa kama mhalifu mwingine yeyote.

  Naye mama yake mzazi Matheri, Martha Wanjiru akizungumza mara baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa mwanaye na Polisi, alisema kwamba, alijua kuwa ipo siku mwanaye huyo angeuawa na hatimaye siku hiyo imefika. Mama huyo alikiri kwamba ni takribani mwaka mmoja ulikuwa umepita bila ya kumwona mwanaye.

  Huku akionekana kujuta, mama huyo alisema,
  "Kama ningejua, mimba ya mwanangu huyu niliyemzaa miaka 30 iliyopita, ingezaa mtoto atakayekuja kuwa muuaji na kuniletea usumbufu mkubwa utakaoniumiza moyoni mwangu katika maisha yangu yote, hakika nisingemzaa, lakini hilo ni jambo ambalo siwezi kulifanya."

  Mama huyo anakiri kwamba kuna wakati aliwahi kumsihi mwanaye ajisalimishe mikononi mwa Polisi, kwani hiyo ndiyo njia pekee ambayo ingepelekea kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa kwa haki, lakini mwanaye hakukubali, badala yake akaendelea na vitendo vyake vya ujambazi.

  Hata hivyo hatua inayochukuliwa na Polisi nchini Kenya ya kuwauwa majambazi kama Matheri, imewagawa wakenya katika makundi mawili. Lipo kundi linaloona kama ile ilikuwa ni hatua sahihi ya kukomesha ujambazi nchini humo, na kundi jingine linaona kuwa, hiyo haikuwa ni njia sahihi ya kukomesha ujambazi.

  Je, kwa Polisi kuendesha mauaji ya namna hii kwa watu wanaoshukiwa kuwa ni majambazi sugu, hakuliweki Taifa la Kenya katika miongoni mwa nchi zinazokiuka haki za binadamu?

  Je, hali hiyo haiwezi kuufanya uhalifu kuwa wa kutisha zaidi, kwani majambazi hawatosita kuuwa wakati wanapofanya uporaji, kwa sababu wanajua hata wao wakipatikana watauawa?

  Hayo yote ni miongoni mwa maswali ambayo Wakenya wengi walikuwa wakijiuliza na bado wanajiuliza

   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 2. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #2
  Jun 1, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Haya Ni Ijumaa nyingine tena kama kawaida, nimekuja na kisa hiki kilichotokea huko kwa majirani zetu Kenya...........Sina mengi ya kuongea, naamini wote mtajifunza kutokana na kisa hiki, hususan malezi ya watoto wetu kwa ujumla.
   
 3. CPA

  CPA JF-Expert Member

  #3
  Jun 1, 2012
  Joined: Mar 1, 2011
  Messages: 734
  Likes Received: 47
  Trophy Points: 45
  Mhhhh! Simon, RIP simon, hata barabara ina mwisho. Wapi jambaz Zombi wa mbeya?
   
 4. Radical

  Radical JF-Expert Member

  #4
  Jun 1, 2012
  Joined: Jun 3, 2009
  Messages: 374
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  Kaka kisa kinasisimua kama hadithi vile...thanks!
   
 5. leroy

  leroy JF-Expert Member

  #5
  Jun 1, 2012
  Joined: Dec 8, 2010
  Messages: 834
  Likes Received: 116
  Trophy Points: 60
  Majambazi wetu wanaitwa Mafisadi....Tunawahukumu jela Miaka mitatu, halafu Wanatoka kwa msamaha wa Rais baada ya Miezi nane.
   
 6. Siri Sirini

  Siri Sirini JF-Expert Member

  #6
  Jun 1, 2012
  Joined: Mar 12, 2012
  Messages: 547
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Asante Mtambuzi, sasa nimeridhika,Dah! Kisa kinasisimua kweli, ila polisi nao walifanya vibaya kumuua, angekuwa ametoka na silaha ndo wangepambana naye,
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 7. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #7
  Jun 1, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Kisa cha wiki ijayo kitatoka nje ya Africa......................Stay tune!
   
 8. Akagando

  Akagando JF-Expert Member

  #8
  Jun 1, 2012
  Joined: May 24, 2012
  Messages: 536
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 35
  Sina cha kusema kwa sababu mzee wake ndiye aliyechangia kuaribika kwa mwanaye.

  :->SIKU ZOTE FIKIRI KABLA YA KUTENDA:-"
   
 9. Paw

  Paw Content Manager Staff Member

  #9
  Jun 1, 2012
  Joined: Nov 14, 2010
  Messages: 2,032
  Likes Received: 236
  Trophy Points: 160
  Nimeisoma kwa msisimko mkubwa.

  Jamii inapaswa kujifunza kupitia kisa hiki cha kuogofya.

  Polisi wanapaswa kutimiza wajibu wao bila kudhuru maisha,
  Wahalifu wanapaswa kujifunza pia kuwa kila wafanyacho kina ujira wake hapa hapa dunia ya wadudi.


   
 10. s

  sawabho JF-Expert Member

  #10
  Jun 1, 2012
  Joined: Feb 25, 2011
  Messages: 4,504
  Likes Received: 946
  Trophy Points: 280
  Na liwe fundisho kwa watu wote wenye tabia kama za Simon. Nawaunga mkono Polisi wa Kenya.
   
 11. a

  ammah JF-Expert Member

  #11
  Jun 1, 2012
  Joined: Oct 2, 2010
  Messages: 211
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  thanks Mtambuzi kwa kisa hiki matata...
   
 12. Smile

  Smile JF-Expert Member

  #12
  Jun 1, 2012
  Joined: Jul 18, 2011
  Messages: 15,431
  Likes Received: 194
  Trophy Points: 160
  aisee naona weekend hii itakuwa njema kwangu
   
 13. Paw

  Paw Content Manager Staff Member

  #13
  Jun 1, 2012
  Joined: Nov 14, 2010
  Messages: 2,032
  Likes Received: 236
  Trophy Points: 160
  Mh!.... how?
   
 14. cacico

  cacico JF-Expert Member

  #14
  Jun 1, 2012
  Joined: Mar 27, 2012
  Messages: 8,392
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  mi ijumaa haiwezi pita bila kusoma hizo cases zako, big up!
   
 15. A

  AZIMIO Senior Member

  #15
  Jun 1, 2012
  Joined: Jun 15, 2011
  Messages: 188
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Sasa nimeshaelewa kwa nini watu walikuwa wanakusubiri,Hingera saba kisa kizuri na kina mafunzo katika familia zetu au jamii kwa ujumla.
   
 16. TaiJike

  TaiJike JF-Expert Member

  #16
  Jun 1, 2012
  Joined: Dec 14, 2011
  Messages: 1,475
  Likes Received: 174
  Trophy Points: 160
  Siungi mkono uhalifu ama mauaji yaliyofayanwa na Matheri lakini naona huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu, haijalishi alifanya mangapi bado alikuwa na haki ya kusikilizwa, na kama ndo hivi inafanyika kenya waache unafiki waziondoe mahakama na wabakiwe na sheria mkononi kuliko unafiki kama huu.
   
 17. E

  Elizabeth Dominic Platinum Member

  #17
  Jun 1, 2012
  Joined: Dec 7, 2007
  Messages: 4,547
  Likes Received: 52
  Trophy Points: 145
  Japo naye alikuwa muuaji lakini staili ya kifo chake inatisha, kila mtu anaundwa na malezi yake one way or another tunaweza tusivipe uzito vitabia vidogo vya watoto wetu lakini vinaweza kuwa fatal hapo baadae. Mara nyingi waafrika tunadhani vitu kama hasira, msongo wa mawazo n.k sio magonjwa its about time tuyape uzito magonjwa hayo na tusichukulie kuwa watoto wetu wana act out.
  Asante Mchambuzi
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 18. maishapopote

  maishapopote JF Gold Member

  #18
  Jun 1, 2012
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 1,998
  Likes Received: 955
  Trophy Points: 280
  mkuu umenikumbusha mbali sana..matheri alikua mdogo sana kwa Zombie...ila troops ya kina matheri ndo ile ya kina Kima na simoni Kimathi ambao wamefungwa moshi....huyu matheri haingii hata kidogo kwa Zombi,Mwamajuja na wengine wa enzi zile mbeya...sasa Hv Zombie umri umekimbia na yupo Zambia alipokimbilia baada ya mkapa kusema lazima afie jela
   
 19. maishapopote

  maishapopote JF Gold Member

  #19
  Jun 1, 2012
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 1,998
  Likes Received: 955
  Trophy Points: 280
  mkuu polisi walifanya sahihi sana kuhusu matheri,,,,alikua mtu hatari sana hiyo idadi ya watu 18 sio sahihi ilikua zaidi nawajua sana hawa jamaa
   
 20. maishapopote

  maishapopote JF Gold Member

  #20
  Jun 1, 2012
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 1,998
  Likes Received: 955
  Trophy Points: 280
  Mkuu Paw,
  Bado napinga ilikua lazima matheri auawe,kwenye genge lao iko siku moja walisimamishwa na trafiki asubuhi na walikua na uwezo wa kutosimaama lakini walisimama na kumuua yule trafiki bila sababu...hebu jiulize huyo ni trafiki na alisimamisha gari bila hata kujua ni kina nani wako kwenye hiyo gari ila walimmiminia risasi kama 60 kisa kwann kawasimamisha alikua hatari sana mkuu ndo maana hata wale wadogo zao walipouawa kule moshi mwaka huo huo wa 2007 wale 14 walikamatwa kwanza na ndio wakauawa..ukiwaacha mahakama zetu unazifahamu kesho tena wako nje utafanyaje?
   
Loading...