Shule ya sheria ya Tanzania | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Shule ya sheria ya Tanzania

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by VUTA-NKUVUTE, Feb 8, 2011.

 1. VUTA-NKUVUTE

  VUTA-NKUVUTE JF-Expert Member

  #1
  Feb 8, 2011
  Joined: Nov 25, 2010
  Messages: 5,870
  Likes Received: 6,610
  Trophy Points: 280
  SHULE YA SHERIA YA TANZANIA INAHUJUMIWA?

  Sheria ni moja ya taaluma mbalimbali zilizopo hapa nchini na kwingineko. Zipo nyingine nyingi kama vile Uhandisi, Ualimu, Uchumi, Uandishi wa habari,Siasa na Utawala. Taaluma ya Sheria ni moja kati ya taaluma muhimu sana kwa mustakabali wa nchi. Sheria ndiyo inayoongoza na kuelekeza utaratibu, kanuni na adhabu katika jamii fulani. Hata Mwenyezi Mungu kwa kutambua umuhimu wa sheria,mara tu baada ya kumaliza uumbaji,alitoa maelekezo kwa Adamu(sheria). Pia alimkabidhi Musa Amri Kumi zake zitumike kama sheria kuu popote na kwa yeyote aaminiye uwepo wake vyovyote vile. Kwa kifupi, sheria ni muhimu mno popote na kwa yeyote. Kuna makubaliano ya kimantiki kuwa kama mtu anataka kujua mfumo wa uongozi,uchungu na utamu wa maisha na ustawi wa jamii fulani, basi ajielekeze kwenye sheria za jamii husika – sheria ndio kipimo cha kila kitu(it is a measuring rod of everything).

  Katika mfumo wa elimu wa Tanzania, sheria kama taaluma husomewa ipasavyo katika Vyuo Vikuu. Tunavyo Vyuo Vikuu mbalimbali hapa Tanzania vinavyofundsha sheria. Hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Da res Salam, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo Kikuu cha Tumaini na Chuo Kikuu cha Ruaha. Mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya sheria huitwa Mwanasheria. Hii ni kwa mujibu wa tafsiri ya jumla ipatikanayo kwenye Sheria ya Mawakili, Sura Nambari 341 ya Sheria za Tanzania. Hii yamaanisha kuwa wote wenye Vyeti na Stashahada za Sheria si Wanasheria. Kwa ufupi uelewekayo, Mwanasheria lazima awe na Shahada ya Kwanza ya Sheria (‘Legum Baccalaureus-LL.B.’), na si vinginevyo.

  Yatosha kusema kuwa watu wengi – na wala si wote, wanasomea taaluma fulani (kama sheria) ili waifanyie kazi na kuifaidi. Ni vyema nikasema kuwa wapo wanasheria ambao ni Mawakili, Mahakimu, Majaji na wengineo. Mwanasheria aweza kufanya kazi zote isipokuwa mbili – za uhandisi na za udaktari! Ni wazi kuwa kwa wale wanaotaka kufaidi uanasheria wao wanahitaji kuwa Mawakili (wa Serikali au wa kujitegemea), Mahakimu, Majaji au hata Waalimu wa Sheria (ambao karibu wote ni Mawakili). Hata Chama cha Wanasheria wa Tanzania Bara (T. L. S) kinatambua Mawakili tu kama wanachama wake. Faida ya uanasheria, kwa walio wengi, yatokea pale tu mtu anapokuwa Wakili. Wakili ni nani hasa? Kwa maana ya wazi fupi Wakili ni Mwanasheria yeyote ambaye huongea kwa niaba ya mtu mwingine hasa kwenye nyanja ya mashtaka. Ni mtetezi wa mhusika wa mashtaka (ima ya jinai au madai). Kwa Tanzania, Wakili ana vigezo vyake, hatua zake, sifa zake, utawala wake na sheria yake;Sheria ya Mawakili niliyoitaja hapo mwanzo. Ingawa Mawakili Tanzania ni wachache sana ukilinganisha na mahitaji halisi, kuwa Wakili Tanzania kumefanywa kugumu kama ‘kumuona Mungu’.


  Shule ya Sheria ya Tanzania.
  Hii ni Taasisi ya kielimu ya Serikali iliyoanzishwa kwa lengo kubwa moja: kutoa mafunzo ya vitendo ya sheria kwa ajili ya kuwaandaa Wanasheria kuwa Mawakili. Imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Shule ya Sheria ya Tanzania ya mwaka 2007. Baada ya mafunzo ya kipindi kisichopungua mwaka mmoja, Mwanasheria husika anatunukiwa Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 12(1) na (2) cha Sheria tajwa. Baada ya uthibitisho wa Jaji Mkuu wa Tanzania, mtunukiwa husika anafaidi matunda ya sheria kwa kuwa Wakili wa Mahakama Kuu-hapa ni kuanzia Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi(wengi huiita isivyopasa Mahakama ya Mkoa), Mahakama Kuu hadi Mahakama ya Rufaa. Pia Mwanasheria mtunikiwa huyo anakuwa mwenye sifa za kuajiriwa kwenye utumishi wa umma. Haya ni matunda yaendayo kwa msomi huyo wa shule ya Sheria ya Tanzania tu. Wanasheria ambao hawatakuwa na uwezo wa kupata mafunzo hayo pale shule ya sheria ya Tanzania ‘wanaula wa chuya’. Wanaachwa ‘kwenye mataa’. Wanabaki sawa na wahitimu wa kidato cha sita. Wana taaluma, hawana thamani nyumbani.Hii kali,hatari na imefika mbali!

  Mwanafunzi wa shule ya sheria ya Tanzania anapaswa kusoma masomo ya darasani (ambayo karibu yote yalishasomwa wakati wa Shahada ya Kwanza ya Sheria) kwa takribani miezi mitatu kabla ya kufanya Mitihani ya kuandika.Masomo husika yamebadilishwa majina tu. Si mapya. Baada ya hapo, mwanafunzi huyo anapaswa kutumia majuma 12 katika mafunzo kwa vitendo katika Ofisi za Mawakili na Mahakamani akigawanya majuma 6 kila sehemu. Baada ya majuma hayo 12, mwanafunzi huyo anarejea shuleni kufanya mitihani mingine ya kuandika (written papers) na kuongea (oral examintions). Matokeo yakitoka na yakawa hayana mushkeli wala mawaa, mwanafunzi anakuwa mhitimu. Mhitimu anaomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imzingatie, imridhie, na kumuidhinisha kuwa Wakili.Kiapo kitafuata. Hii ni safari ndefu mno na yenye kuchosha.

  Kabla ya hapo
  Kabla ya kuanzishwa kwa shule ya Sheria ya Tanzania ambayo ilianza kufanya kazi mwaka 2008, mafunzo kwa vitendo katika mfumo wa kwenda kwa Mawakili na Mahakamani yalikuwa ni kwa semesta moja ya mwisho ya mwaka wa nne au wa tatu kutegemeana na Chuo Kikuu gani chahusika.Kwetu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilikuwa ni mwisho wa mwaka wa nne.Kila Chuo Kikuu kilikuwa na utaratibu wake juu ya mafunzo hayo kwa vitendo.Taratibu zote sasa ‘zimemezwa’ na Shule ya Sheria ya Tanzania. Baada ya hapo Mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya Sheria alikuwa akiomba kufanya mtihani wa Mawakili (Bar Examination) wakati wowote autakao na bila kunyimwa ajira za Utumishi wa umma! Mafunzo ya Sheria kwa vitendo yalikuwa ni sehemu ya Shahada ya Kwanza ya Sheria. Sasa yamepanda bei – yanajitegemea. Yamebeba safari ndefu niliyoisimulia hapo kabla. Yanagharimu sana. Mwanasheria maskini,’mwenzangu na mie’ atayasikia kwenye bomba tu-hatathubutu kuyapata. Gharama zake zote hazipungui shilingi za kitanzania milioni nne (4) – 1,590,000/= zikiwa ni za lazima na zilizobaki ni zile za ‘utajiju’.Atakosa kabisa matunda matamu yanayoendana na mafunzo hayo:Uwakili na ajira katika utumishi wa umma.Kama mtu haaminiwi kwenye utumishi wa umma atawezaje kuaminiwa kwenye sekta binafsi? Huyu hatakosa ajira sehemu zote? Taaluma na usomi wake vitakuwa vimesaidiaje?


  Maboresho makubwa, matatizo makubwa.
  Mafunzo haya kwa vitendo yameboreshwa kwa njia kuu mbili. Kwanza, darasani mawakili watarajiwa wanafunzwa na Mawakili walio tayari kwenye taaluma hiyo. Hii yawaezesha wanafunzi kupata uzoefu na changamoto ‘za motomoto’ toka kwa wakufunzi wao. Haya ni maboresho makubwa. Pili, mafunzo ya vitendo pamoja na mitihani ya mawakili havijatenganishwa tena. Hapa naamaanisha kuwa, baada ya matokeo ya mwisho, mhitimu hana haja tena ya kuomba kufanya na kusubiri mtihani wa mawakili ‘Akishasafishwa’ na Jaji Mkuu, mhitimu wa mafunzo hayo anaapishwa na Jaji Mkuu huyohuyo kuwa Wakili. Hata muda wa mafunzo kwa ujumla waonesha jinsi wahitimu wanavyokuwa wameiva kimafunzo tofauti na ile ya miezi minne tu ya mwanzo!

  Lakini, Shule ya Sheria ya Tanzania ina matatizo makubwa mno. Hadi sasa, tangu kuanzishwa kwake, Shule hii ya Sheria ya Tanzania haina miundombinu yake. Haina jengo binafsi hata moja.Shule ya Sheria ya Tanzania imekuwa bingwa wa kupanga! Kwa sasa imepangishwa majengo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya madarasa na maktaba kuendeshea mafunzo_Ofisi zake zote zimepanga katika Jengo la Ubungo Plaza.Eneo lake la ukubwa wa ekari 23 bado li pweke pale pembezoni mwa Barabara ya Sam Nujoma.Ndio kwanza Kampuni ile ya Kichina iliyojenga Uwanja wa kisasa wa Taifa iitwayo M/S Beijing Construction Engineering Group,mnamo tarehe 18/10/2010,imeingia mkataba na Wizara ya Katiba na Sheria wa ‘kuijenga’ Shule ya Sheria ya Tanzania.Ujenzi huo umepangwa kuchukua muda wa miezi 15 na utagharimu Serikali jumla ya Shilingi bilioni 16.Sina hakika kama umeshaanza.

  Pia, matokeo kwa wanafunzi wa Shule ya Sheria ya Tanzania yanachelewa kupita kiasi. Kwa mfano, wanafunzi waliomaliza mitihani yao ya mwisho Mwezi Mei mwaka huu bado hawajapata matokeo yao. Hii naiona ni dalili ya juhudi za makusudi ya kuzuia ongezeko la Mawakili. Matokeo yanapochelewa, kuapishwa kunachelewa.Tangu ‘Cohort’ ya nne inayosubiri majibu yake, Shule ya Sheria ya Tanzania ipo kwenye ‘Cohort’ ya saba. Kama matokeo yatachukua muda huo mrefu unaofanana itakuwaje? Nani anachelewesha matokeo haya? Kwa nini? Kwa faida ya nani? Yapo matatizo mengine zaidi ya haya yanayoikabili Shule ya Sheria ya Tanzania kuelekea lengo lake la kutoa mafunzo ya sheria kwa vitend


  Hitimisho
  Changamoto kwa Shule ya Sheria ya Tanzania zaweza kuwekwa pamoja kama ukosefu wa miundombinu ya kutosha, gharama za ‘kufa mtu’ za mafunzo pamoja na ratiba ngumu ya kusoma wakati wa mafunzo. Ratiba haitoi nafasi ya mtu kujisomea binafsi. Yenyewe inapelekesha tu – haijali madhara yatokeayo. Nimalizie kwa kusema kuwa matatizo haya yote yanatokana na ‘hulka’ ya Serikali yetu ya Tanzania kuwa na ‘kasi zaidi’ katika kuanzisha jambo pasi na kuwa na maandalizi ya kutosha.Hii si hulka njema kwa mustakabali wa Taifa. Pamoja na lengo jema la Shule ya Sheria ya Tanzania, taasisi hiyo yahitaji maboresho na marekebisho mujarabu. Mwisho mwishoni, kila mpenda taaluma ya Sheria anapenda kuiona taasisi hiyo ikiwa ni mkombozi kwa Wanasheria badala ya kuwa kikwazo kama ilivyo sasa.Nani anabariki kufanyika haya?
   
 2. Yohana Kilimba

  Yohana Kilimba JF-Expert Member

  #2
  Apr 27, 2016
  Joined: Dec 25, 2012
  Messages: 8,132
  Likes Received: 5,211
  Trophy Points: 280
  Naomba ufafanuzi kuhusu hili
   
Loading...