Shetani anatumia mbinu kubwa 10 kutuangamiza

Shetani anatumia mbinu kubwa 10 kutuangamiza

John Achila Mukumwa

Senior Member
Joined
Jan 4, 2024
Posts
126
Reaction score
257
Shetani anatumia mbinu kubwa 10 kutuangamiza

Maandiko katika kitabu cha Zaburi 119:105, yanasema:
Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu”.

Hakika tukilifahamu Neno la Mungu, hata tukifungiwa katika chumba chenye giza tukapewa mshumaa na Biblia tu, tutaweza kueleza mambo yote yanayoendelea, na kazi zote za shetani azifanyazo duniani, bila hata kuhadithiwa na mtu yeyote.

Kumbe hatuhitaji shuhuda kutoka kuzimu ili kutusaidia sisi kufahamu utendaji kazi wa shetani. Biblia imeweka wazi mambo yote. Kwa msaada wa Neno la Mungu, tunaweza kuona mbinu kubwa 10 ambazo shetani anajishughulisha nazo.

Kushitaki watakaifu
Ufunuo 12, unasema:10 “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, YEYE AWASHITAKIYE mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.
11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”.

Leo umekuwa mtakatifu kwa kumwamini mwana wa Mungu. Lakini fahamu kuwa shetani bado hajakata tamaa ya kufuatilia nyendo zako, na akipata kosa tu, kazi yake ni kulipeleka mbele za Mungu ili uhukumiwe. Anapeleka mashtaka usiku na mchana. Lakini ashukuruwe Mungu, tulio ndani ya Kristo, pale anapokwenda kutushitaki, hapo hapo ameketi mwombezi wetu Yesu Kristo, kututetea. Hivyo ni jukumu letu kuziweka njia zetu katika mstari ulionyooka ili adui akose la kutushitaki nalo.

Kuzuia kazi ya Mungu
Maandiko katika kitabu cha 1Wathesalonike 2:18 yanasema:
“Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia”.
Ni jambo la kawaida kukutana na shetani uso kwa uso, unapojaribu kuieneza kazi ya Mungu. Hiyo ni moja ya kazi zake duniani. Mtume Paulo alizuiwa na jeshi la mapepo alipokuwa akienda kuhubiri Injili Thesalonike. Hata sasa, anayafanya mambo hayo hayo. Hivyo, nawe pia ukiwa umevaa zile silaha zote zinazozungumziwa katika Waefeso 6, usiogope kusimama. Kwa sababu aliyesimama upande wetu ni mkuu kuliko aliye upande wao. Utakutana na visa na mawimbi ya ajabu njiani, lakini usiogope. Aliyekutuma atakuwa pembeni yako.

Kuleta majaribu

Hii pia ni mbinu anayoitumia shetani kila siku kwa waaminio, ili kuwadondosha , na kuwafanya wauone ukristo kuwa ni mgumu, na mwisho wa siku wakate tamaa, na waiache njia ya wokovu.
Tunaona yalitokea kwa Ayubu. Yalitokea kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Yalitokea kwa mitume, na yatatokea na kwetu.

Waebrania 11:36 inasema:“wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani". Lakini ashukuriwe Mungu, ambaye anatupa nguvu ya kuyashinda. Kwa sababu biblia inaweka wazi kabisa, mtu yeyote atakayeingia katika PENDO la Kristo, hakuna kitu chochote kitakachoweza kumtenganisha nalo.
Kumbuka kuwa, mtu yeyote aliye nje ya Kristo hajaribiwi, wala asijidanganye kusema anapitia majaribu, atajaribiwa na nini wakati yupo tayari kwenye dhambi? Kinyume chake, yeye ndiye anafanyika chombo cha shetani kuwajaribu watu wa Mungu.

Kuleta magonjwa
Luka 13:16: “Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?”
Huyu ni mwanamke aliyefunguliwa na Bwana Yesu siku ya sabato, ambapo pepo la udhaifu lilimsababishia ulemavu wa kudumu wa mgongo (yaani kibiongo).

Hii ni kutuonyesha kuwa sababu ya magonjwa mengi yanayowapata watu leo hii ni kazi ya shetani. Yeye ndiye anayehusika na magonjwa na matatizo yote.

Lakini tumaini lipo, na tiba na kinga vile vile ipo, kwa yeyote amwaminiye Kristo. Kwa sababu maandiko yanasema katika Isaya 53:4, "Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa".
Kwa kupigwa kwake, sisi tulipona.

Kuua
Yohana 8:44 "Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo". Hii ni mbinu nyingine kubwa ya shetani kuangamiza kote kote, yaani mwilini na rohoni.

Ni muhimu kufahamu kuwa shetani hakupendi hata kidogo, ni rehema za Mungu tu, zinatushikilia wewe na mimi
. Zinakushikilia wewe ambaye bado upo kwenye dhambi, ungeshakufa siku nyingi. Biblia inasema shetani asili yake ni uuaji, tangu mwanzo alikuwa hivyo. Na ndicho chanzo cha mauaji unayoyaona yanaendelea duniani.

Kudanganya
Katika Yohana 8:44: “…..wala (shetani) hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo”.
Kudanganya ni mbinu inayomletea shetani matunda makubwa. Anachofanya yeye, hakuzuii kumwabudu Mungu, wala kwenda kanisani. Bali, anakuhubiria njia zake za uongo, ili umwabudu yeye pasipo wewe kujua, ukidhani unamwabudu Mungu. Au anakushawishi ufanye kitu fulani, ukidhani ni chema kumbe unamkosea Mungu, na mwisho wa siku unakufa. Unajikuta upo kuzimu, mpango wake umekamilika juu yako. Na ndiyo maana tumeonywa kila siku, tuijue KWELI ili tuwe huru, na KWELI ni NENO LA MUNGU.
Katika zama tulizopo, udanganyifu wa ibilisi umezidi kuongezeka. Tuombe Mungu atusaidie, huku na sisi wenyewe tukionyesha bidii kumtafuta Mungu.

Kupofusha
Kitabu cha 2Wakorintho 4, kinasema: 3 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; 4 ambao ndani yao Mungu wa dunia hii amepofusha fikra zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”.
Unaweza ukajiuliza, ni kwa nini watu wengi wanasikia injili, wanaziona kazi za Mungu waziwazi, akifanya ishara na miujiza. Wanajua kabisa Mungu yupo, lakini bado hawataki kubadilika. Ni kwa sababu wametaka wenyewe kuwa chini ya shetani. Hivyo, na shetani naye akatumia fursa hiyo kuwapofusha fikira zao moja kwa moja, wasiiamini injili wakapona.

Na anafanya hayo akishirikiana na wakuu wake wa giza, pamoja na mapepo yote. Hivyo, ikiwa wewe ni mmojawapo wa watu wasiosikia injili, jichunguze tena, na uamue kubadilika. Mgeukie Bwana akupake dawa kwenye macho yako upate kuona.

Kunyakua Neno la Mungu
Mathayo 13, inasema: 18 “Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. 19 Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.”

Hapa napo shetani amewekeza sana, na amefanikiwa pakubwa. Akishaona mtu fulani anaonyesha uelekeo wa kutaka kuamini, alipohubiriwa injili, ilipomchoma, yeye anachohakikisha ni kuwa anapambana kwa kila namna kuliondoa lile Neno ndani ya mtu yule. Ndiyo hapo utakuta mtu anakosa muda wa kutafari lile Neno alilofundishwa. Badala yake shetani atamletea vitu mbadala vya kujishuhulisha navyo, kama vile muvi, mpira, michezo, tv, kuchati, mihangaiko, miziki, nk. Mwisho wa siku anasahau kile alichopandiwa ndani yake, na baadaye anarudia hali yake ya mwanzo, na kuwa kama mtu ambaye hajawahi kusikia Neno la Mungu kabisa. Hiyo ni njama kubwa sana shetani anayoitumia kuiondoa mbegu iliyopandwa ndani ya mtu.

Kujigeuza na kuwa mfano wa malaika wa nuru
Hebu tuangalie 2Wakorintho 11: 13 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. 14 Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. 15 Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao".
Ni tabia ya shetani kujigeuza na kujifanya malaika mtakatifu. Hivyo, anawarithisha na watoto wake kazi hiyo hiyo. Ndiyo maana katikati ya kanisa la Mungu, leo hii utaona manabii wengi wa uongo na mitume na watumishi wa uongo, humo humo.

Kufanya ishara na miujiza ya uongo
Tazama 2Timotheo 3:8-9, inavyosema: 8 Ni kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa (Misri), vivyo hivyo na watu hawa wanavyopingana na ile kweli, ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa mambo ya imani. 9 Lakini hawataendelea sana, maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa dhahiri ".

Tufahamu kuwa Shetani yuko katika mapambano makali dhidi ya mwanadamu. Ndiyo kazi kubwa na muhimu kwake, aliyo nayo. Kazi hiyo huifanya kwa mbinu mbalimbali.

Mbinu anazotumia Shetani ni pamoja na zifuatazo:
1. Kushitaki watakatifu kwa Mungu
2. Kuzuia kazi ya Mungu
3. Kuleta majaribu
4. Kuleta magonjwa
5. Kuua
6. Kudanganya
7. Kupofusha
8. Kunyakua Neno la Mungu
9. Kujigeuza na kuwa mfano wa malaika wa nuru
10. Kufanya ishara na miujiza ya uongo


Upo katika hatari kubwa sana ya kuangamia na kuishia kuzimu.

Kinga tulishapewa, nayo ni YESU KRISTO. Amwaminiye yeye, shetani kwake ni kama kikaragosi kisichoweza kumfanya lolote, wala kumdhuru. Lakini ukiwa nje ya Kristo shetani kwako ni mungu wako, atakufanya anachotaka na anavyotaka.
 
Thibifisha Mungu na Shetani wapo kweli, si wahusika wa hadithi ya kutungwa na watu tu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom