LEO, Watanzania kote nchini wanaadhimisha miaka 47 tangu taifa letu lipate uhuru Desemba 9, mwaka 1961, kutoka kwenye ukoloni wa Waingereza, uliotanguliwa na ukoloni wa Wajerumani.
Kwetu sisi, heri na fanaka za uhuru tunaousherehekea leo, ni matokeo ya jitihada za wahenga wetu, waliokuwa wa kwanza kutabiri ujio wa wakoloni na hatimaye wakapambana na kumwaga damu kwa manufaa ya vizazi vya leo na vijavyo.
Ni matokeo ya jitihada za mashujaa wa vita ya Maji Maji na wale wote waliopinga ukoloni katika maeneo yao, kina mtemi Mkwawa, Mirambo, Isike, Makunganya, Mangi Meri, Bwana Heri na wengineo ambao damu yao ilikuwa chachu iliyosababisha kupatikana kwa Tanzania huru.
Ni matokeo ya juhudi za waasisi wetu wa chama cha siasa cha wakati huo Tanganyika National Union (TANU), kilichopigania uhuru kwa amani na mafanikio, chini ya uongozi, wa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Baba wa Taifa huru la Tanzania.
Tunapokumbuka na kuthamini mchango wa wale wote waliotimiza wajibu wao wakati huo, tuamini kuwa nasi tunaweza kuutumia wajibu huo kama funzo, katika kukabiliana na changamoto za leo na kesho ili taifa letu lisitopee kwenye utumwa.
Ikumbukwe kuwa taifa letu mara baada ya kupata uhuru lilikuwa na ndoto kuu tatu, nazo ni kutokomeza ujinga, umaskini na maradhi kutimia kwa ndoto zote hizi kwa pamoja kungetufanya kuwa taifa lililoendelea na linalojitegemea.
Tunakiri kuwa taifa tulilonalo leo si lile la wakati wa uhuru, ni dhahiri kuwa tumepiga hatua, kijamii, kiuchumi na kisiasa amani, umoja na mshikamano, ni vielelezo vya baadhi ya mafanikio ambayo taifa limepata na kuyadumisha tangu uhuru.
Hata hivyo, hatua tuliyopiga kimaendeleo kama taifa haiwiani hata kidogo na uhuru wetu wa miaka 47, maendeleo yetu yamekuwa ya kusuasua, kwa kiasi kikubwa tumeshindwa kuutumia uhuru wetu kupunguza umaskini.
Ieleweke kuwa sisi ni moja ya nchi 10 zilizo maskini kabisa duniani, kwa kipimo cha kimataifa cha umaskini, asilimia 57.8, sawa na watu milioni 20.2, wanaishi chini ya dola moja ya Marekani kwa siku, na asilimia 89.9, sawa na watu milioni 31.5, wanaishi chini ya dola mbili za Marekani kwa siku.
Kutokana na kasi yetu ndogo ya maendeleo, tafiti zinakadiria kwamba kwa kasi ya sasa ya ukuaji wa uchumi kwa asilimia sita kwa mwaka, italichukua taifa miaka 18 zaidi kuweza kuwanyanyua wananchi kutoka kwenye wastani wa kipato cha chini ya dola moja za Marekani kwa siku hadi kufikia dola mbili za Marekani kwa siku.
Tungependa Watanzania waelewe kuwa kama hawatachukua hatua za makusudi katika kuchochea uwajibikaji na ufanisi, hata baada ya miaka hiyo 18, bado watakuwa ni maskini, kwani hata wakipata uwezo wa kuishi chini ya dola mbili kwa siku, karibu sawa na shilingi elfu mbili, hawataweza kujikimu kikamilifu.
Tunaamini kuwa ili ndoto ya uhuru iweze kutimia, kuna haja ya msingi ya kuutazama upya mfumo wetu wa utawala, kujua ni kwanini umeshindwa kutupatia maendeleo ya haraka licha kuwa na rasilimali za kutosha na uhuru wa miaka 47.
Tanzania huru yenye maendeleo na inayojitegemea inawezekana, kila mtu atimize wajibu wake.