Sheikh Shaban Rashid Msuya, mwanafunzi wa sheikh Hassan Bin Ameir 1950s

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,916
30,259
SHEIKH SHABAN RASHID MSUYA MWANAFUNZI WA SHEIKH HASSAN BIN AMEIR 1950s

John Iliffe anasema historia ya TANU nyingi ipo kwa watu.

Hili mimi nimelishudia mara nyingi.

Aliyonieleza Sheikh Shaban Rashid Msuya jioni moja tukiwa tumekaa kwenye ukumbi wake Ugweno Kata ya Kifula sikuyategemea.

Awali alinipitisha katika historia ya chuo alichoasisi Chuo cha Mbale hapo Ugweno kwa msaada wa Mangi Minja.

Chuo hiki nilionyeshwa wakati tunapanda juu nyumbani kwake kijiji cha Kisanjuni.
Haya yalikuwa na nafasi kubwa katika mazungumzo yetu.

Lakini ilikuwa historia nyingine aliyonieleza yeye mwenyewe kwa hakika akiwa hajui uzito wake ndiyo mimi kwanza iliinistua sana na baada ya mshtuko kuondoka maneno yake yalinifurahisha kupita kiasi.

Nilikuwa kwenye safari ya utafiti Kilimanjaro na mwenyeji wangu Moshi Sheikh Yusuf Lasenga alinipitisha sehemu nyingi Kilimanjaro kuonana na Waislam.

Nilijifunza mengi na yeye Sheikh Lasenga alinifunza mengi kuhusu Uislam Kilimanajro toka enzi na enzi.

Sheikh Lasenga alinifikisha Usangi Kirongwe nyumbani kwa Sheikh Shaban Rashid Msuya ambae alipata kuwa Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika safari yangu hii nilikutana na masheikh wengi lakini Sheikh Shaban alinivutia zaidi.

Kwanza nilishangazwa na lafidhi yake ya Kiswahili.

Hakuwa anazungumza kwa lafidhi ya watu wa Kaskazini.

Nikamuuliza imekuwaje hivyo.

Sheikh Shaban akaniambia kuwa baada ya kumaliza kusoma Qur'an hapo Ugweno akiwa bado mtoto mdogo baba yake alimpeleka Dar es Salaam aende akasome kwa masheikh mbalimbali.
Hii ilikuwaiaka ya 1950.

Hivi ndivyo alivyokuja kuangukia kwa Sheikh Mzee Ali Comorian.

Sheikh Mzee Ali Comorian alianza kumsomesha na Sheikh Shaban anakumbuka kuwa wakati yuko na Sheikh Mzee Ali Comorian ilikuwa ni wakati ule anafanya tafsiri ya Barzanji kitabu kiichokuja kuwa maarufu sana miaka ile ya 1950 hadi 1960.

Sheikh Mzee Ali Comorian alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Hassan bin Ameir alipogundua uwezo wa kijana Shaban ndiyo akampeleka kusoma kwa mwalimu wake Sheikh Hassan bin Ameir, Mufti wa Tanganyika.

Tulikuwa tumemaliza mazungumzo yetu na jua lilikuwa linaelekea kuzama lakini mimi nikawa nimechukuliwa na mazungumzo ya Sheikh Shaban akinieleza maisha ya kila siku ya Dar es Salaam yeye akiwa mwanafunzi kijana.

Sheikh Lasenga akawa ananikumbusha kuwa tuna safari ndefu ya kurejea Moshi kabla jua halijazama na yeye asingependa kushuka milima ya Usangi katika mwanga hafifu.

Tujitayarisha kuaga nikamuuliza Sheikh Shaban kama alipata kushuhudia harakati za Sheikh Hassan bin Ameir wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

"Nakumbuka safari ya kwanza ya Mwalimu Nyerere UNO mwaka wa 1955, Sheikh alinichukua mimi na wenzangu kwenda Al Jamiatul Islamiyya kwani kulikuwa na sherehe ya kumuaga Nyerere.

Sisi vijana wa madras ndiyo tuliokuwa pale kugawa soda, sambusa na keki kwa wageni waliokuja pale kumuaga Nyerere."

Hakika historia ya TANU ipo katika vifua vya watu wengi ambao wakati meingine wala huwategemei kuwa waliona historia yote ya kupigania uhuru kwa macho yao ikijifunua mbele yao.

PICHA:
1. Sheikh Shaban Rashid Msuya
2. Sheikh Hassan bin katikatiTewa Said Tewa Rais wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) na kulia na Julius Kambarage Nyerere Rais wa Tanzania katika sherehe ya kuweka jiwe la msingi wa Chuo Kikuu Cha Waislam 1968.
3. Kaburi la Sheikh Hassan bin Ameir, Makunduchi, Zanzibar.

Screenshot_20220524-000831_Facebook.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom