Mimi nadhani kuwapa pesa tu haiwezi kuwasaidia kujikwamua kiuchumi au kuwapa nafuu ya kudumu kwa matatizo yao. Kinachotakiwa ni kuweka mikakati ya kusaidia juhudi zao za uzalishaji ili ziweze kutoa tija kwa manufaa yao na ya Taifa kwa ujumla.
Kwa mfano, serikali inatakiwa kujenga miundombinu bora zaidi kwa kuhakikisha;
1. Barabara nzuri zinafika sehemu kubwa vijijini, ili kuwezesha huduma mbalimbali kuwafikia walengwa kwa urahisi badala ya kujenga miundombinu hiyo mijini peke yake.
2. Serikali inatakiwa kutafuta masoko ya mazao yoyote yanayozalishwa vijijini ili kuwapatia kipato wananchi huko
3. Serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa mazao ya wanavijiji kote nchini yanapata soko lililo fair na si kuruhusu kudhulumiwa na wafanya biashara kama ilivyo sasa
4. Serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa, wananchi wa vijijini wanapata pembejeo na malighafi nyinginezo kwa urahisi na kwa bei nafuu ili kuwawezesha kuzalisha kwa kiasi kikubwa na kwa tija zaidi.
Kama wananchi wa vijijini wakipatiwa pesa tu, mathalan shilingi 50 elfu uliyoipendekeza, baada ya muda mfupi pesa hiyo haitatosha na watahitaji pesa zaidi. Lakini vilevile, kama wakiona wanapewa pesa bila kufanya jitihada yoyote, wataamua kuacha kujitahidi kuzalisha na hivyo kuwafanya wawe masikini zaidi.
Inatakiwa serikali kuwa makini sana kwa kuboresha maisha ya vijijini ili watu wengi zaidi wavutiwe kuishi huko na kuzalisha zaidi. Hii inawezekana kabisa.