SoC03 Serikali za Majimbo zitaongeza Kiwango cha Uwajibikaji na Utawala Bora Nchini

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
Kawaida, kwa Tanzania ukizungumza juu ya majimbo, watu wengi hudhani ni yale yanayowakilishwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majimbo ninayozungumzia hapa, ni mikoa inayoongozwa na Wakuu wa Mikoa kwa sasa! Swala la serikali za majimbo limezungumzwa siku nyingi na mara nyingi na wanasiasa kwa kukinzana; wapo wanaoutetea kwa kutoa sababu mbalimbali, na wengine wakipinga, pia kwa kutoa sababu mbalimbali.

Mimi napendekeza mfumo wa serikali za majimbo kwa mtizamo wa Uwajibikaji na Utawala Bora, na sii kwa mtizamo wa kisiasa.
Hapa namaanisha kila mkoa kuunda serikali itakayowahudumia wananchi wake kwa ukaribu na ufanisi zaidi. Ikibidi, ile mikoa ambayo aidha ina idadi ndogo ya watu au ni midogo kijiografia, inaweza kuungana na mikoa mingine ya jiraji na kutengeneza Jimbo moja.

Ninajenga hoja kwa namna ambavyo nchi yetu inaweza kuboresha uwajibikaji na utawala bora katika kila sekta kwa kuanzisha serikali za majimbo. Rasimu kamili ya muundo wa serikali za majimbo na majukumu yake, utapaswa kuandaliwa kwa muda maalum na jopo la wataalamu wazalendo na wabobezi katika Nyanja mbalimbali, bila kuwa na ushawishi wowote wenye msukumo wa maslahi binafsi na/au wa kisiasa.

Kutokana na ukomo wa maneno katika Makala haya, nitadokeza kidogo juu ya muundo na majukumu ya serikali za majimbo.

Mabadiliko ya Kiutawala
Mfumo huu utaleta mabadiliko makubwa sana ya kiutawala, kwani kuna nafasi zitaondolewa na nyingine kuundwa. Mfano: Nafasi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zitaondolewa. Nafasi ya Mkuu wa Mkoa itajazwa na Gavana wa Jimbo, ambaye atapigiwa kura na wananchi wa Jimbo lake; nafasi ya Mkuu wa Wilaya haitajazwa, na badala yake majukumu yake yatatekelezwa na Meya au Mwenyekiti wa Halmashauri husika, pamoja na Mkurugenzi wa Jiji/Mji/Wilaya, nafasi ambazo zipo hadi sasa.

Gavana wa jimbo atakuwa na msaidizi wake ambao wote watachaguliwa na wananchi na kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Umuhimu wa Serikali za Majimbo
Kwa muda mrefu, serikali imekuwa inashughulika na mambo mengi madogomadogo kwa ufanisi mdogo, kutokana na ukweli kwamba kuna vipaumbele vingi vinavyoshindana; ambapo yangeshughulikiwa kwa karibu na kwa ufanisi na serikali za majimbo.

Mfano: Upungufu au ukosefu wa watumishi wa afya au elimu wilayani Uvinza, Kigoma unaweza kusababisha athari kwa wananchi kwa muda mrefu, kwa sababu ya kusubiri maamuzi kutoka makao makuu ya serikali jijini Dodoma. Lakini pia changamoto nyingi za miundombinu, hasa za barabara; utakuta Mbunge analia bungeni Dodoma, eti kwa sababu barabara ya kilomita moja tu haijatengewa bajeti na serikali!

Chini ya mfumo wa serikali za majimbo, mambo kama haya na mengine mengi yatapatiwa ufumbuzi kwa haraka na kwa ufanisi, kwa kuwa zipo karibu zaidi na jamii.

Inaaminika kuwa Gavana na serikali yake watawajibika vizuri kwa wananchi, kwa kuwa wamechaguliwa nao, na wanaweza kuondolewa, kama watafanya vinginenvyo.

Kwa kiasi kikubwa gharama za kufuatilia maswala ya wananchi zitapungua kwa sababu mambo mengi ambayo yangefanyika serikali kuu Dodoma, yanafanyika jimboni kwao.

Itakuwa rahisi kubaini fursa za kiuchumi jimboni na kuzifanyia kazi kwa faida ya wananchi wake, ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji ndaji na nje ya jimbo, na hata nje ya nchi.

Kinyume na mtizamo wa baadhi ya watu, serikali hizi za majimbo zitapunguza gharama za uendeshaji wa serikali, kwani kila sekta itasimamiwa na sekretarieti zitakazowajibika moja kwa moja kwa Gavana, na watumishi hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Sekretarieti hizi zipo hata sasa chini ya wakuu wa mikoa.

Baadhi ya Maswala yenye Hofu na Majibu yake

Serikali za Majimbo zitaleta Ukabila!
Baadhi ya watu, hasa wanasiasa, hujaribu kuwaaminisha watu wengi kuwa serikali za majimbo zitachochea ukabila.
Majibu: Tanzania, ina makabila takriban 120, yaliyosambaa karibu kila wilaya. Kwa mfano: Ukienda wilaya ya Chalinze utakuta makabila mbalimbali kutoka mikoa tofauti ya Tanzania, maana kila Mtazania ana haki kikatiba ya kuishi Popote nchini, ambapo anaamini atapata fursa mbalimbali za aidha kuajiriwa na/au kujiajiri. Uhuru wa kuishi Popote nchini, utasalia, hata wakati wa serikali za majimbo. Kama katika wilaya kuna makabila mchanganyiko kama nilivyoeleza hapo juu, basi katika ngazi ya jimbo, mchanganyiko wa makabila ni mkubwa zaidi.

Gharama ya Uendeshaji wa Serikali hizi ni kubwa sana! Hii ni hofu kubwa sana ambayo baadhi ya watu wamejijengea na wanajengea watu wengine wengi. Hofu hii imefanya watu wengi kuacha hata kujadili swala hili, maana wanajiuliza, kama serikali moja tu ina changamoto nyingi hivi za kifedha, itakuwaje pale kutakapokuwa na serikali nyingine nyingi za majimbo?
Majibu: Kwa sasa kuna wabunge zaidi ya 390, wakuu wa wilaya 160, na mawaziri 50. Kama bunge la Jamhuri litabaki na wabunge 80, wabunge zaidi ya 300 watarudi mikoani mwao kuwakilisha wananchi katika serikali za majimbo yao. Kama kwa sasa anagharamiwa Sh milioni 15 kwa mwezi, jimboni itakuwa nusu. Nafasi za Wakuu wa Wilaya zitakazofutwa zitaokoa takriban bilioni 100 kwa mwaka. Na mawaziri watapungua hadi kufikia 15; na hiyo kuokoa takriban Sh. bilioni 120 kwa mwaka. Kwa wabunge wakuu wa wilaya na mawaziri, jumla ya Sh. Bilioni 247 zitaokolewa kwa mwaka, na kupelekwa kuendesha serikali za majimbo.

Kielelezo Na. 1: Baraza la Mawaziri la Kwanza Tanganyika
First Tanganyika Cabinet ii.png

Chanzo: Wikipedia

Kipindi nchi hii inapata uhuru, kulikuwa na changamoto nyingi za miundombinu ya usafiri, mawasiliano, na kadhalika; lakini serikali ya mawaziri 11 ilifanya kazi kubwa.

Baadhi ya Majimbo yatakuwa Maskini kwa kuwa yana rasilimali chache! Hii nayo ni hofu kwa baadhi ya watu wakidhani majimbo yenye rasilimali nyingi, kwa mfano kama Geita yenye madini ya dhahabu, itanufaika kuliko Lindi ambayo haina rasilimali hiyo.
Majibu: Rasilimali kama hizi zitasimamiwa na jimbo husika, ambapo, kijiji chenye rasilimali hiyo kitapata sehemu ya mrahaba, Halmashauri, Serikali ya Jimbo, na Serikali Kuu zitapata mrahaba kwa uwiano utakaokubalika. Pia serikali kuu itapokea gawio katika mapato mengine ya Jimbo. Fedha ambazo serikali kuu itapokea kutoka majimboni, pamoja na mambo mengine, zitatumika kama mfuko wa Uwiano (Balancing Fund) kwa ajili ya kunyanyua majimbo yenye Uchumi mdogo.

Hitimisho
Bila kujali historia ya nchi yetu, au kuiga mfumo huu kutoka nchi nyingine, serikali za majimbo ambazo zitabuniwa na watu wazalendo, wabobevu na wasiosukumwa na maslahi yoyote binafsi ama ya kisiasa, zitakuwa muarobaini wa Uwajibikaji na Utawala Bora hapa nchini.

Marejeo

https://icma.org/articles/article/county-government-structure-kenya

Provincial Government and State Authority in South Africa on JSTOR
 
Najua watu wenye nafasi mbalimbali na wengine wanaotarajia kupata nafasi kama hizo za kazi au uongozi katika mfumo uliopo, wanaweza wasifurahie pendekezo hili; lakini ukweli ni kwamba serikali za majimbo zitaongeza uwajibikaji na utawala bora nchini!
 
Serikali za Majimbo zitamfanya Rais wa nchi kupunguza mzigo wa kufanya mambo mengi madogomadogo kama ujenzi wa shule, zahanati, barabara nk, na hivyo kupata nafasi ya kufanya mambo makubwa na ya kimkakati, kama kutafuta masoko ya bidhaa na hduma zetu nje ya nchi, kuvutia wawekezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nk.
 
Serikali za majimbo hazikwepeki, kama kweli tunataka kupiga hatua katika maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi!
 
Serikali za majimbo ni njia nzuri ya kugatua madaraka yaliorundikwa kwa mtu mmoja ambaye ni rais wa nchi!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom