GE2025 Serikali yatoa bilioni 19.99 kujenga Stendi Kuu ya mabasi Babati

GE2025 Serikali yatoa bilioni 19.99 kujenga Stendi Kuu ya mabasi Babati

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Nipe Maji

JF-Expert Member
Joined
Mar 25, 2025
Posts
335
Reaction score
190
Kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Babati kuhusu ujenzi wa stendi kuu ya mabasi sasa kimesikika, baada ya Serikali kutoa shilingi bilioni 19.99 kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa stendi hiyo, ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15.

Akizungumza leo, Julai 24, katika hafla ya kumkabidhi mkandarasi mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, alisema mradi huo una umuhimu mkubwa kwani utachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa mkoa huo na kuongeza fursa za ajira na biashara.

Sendiga amesema ujenzi wa stendi hiyo unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 27, 2026, na kukabidhiwa rasmi kwa wananchi wa Babati. Alibainisha kuwa Halmashauri ya Mji wa Babati ni miongoni mwa Halmashauri 15 pekee kati ya 184 nchini zilizopata fursa ya kupata mradi wa aina hiyo.

Amewataka wataalamu wa Halmashauri pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha wanasimamia mradi huo kikamilifu ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa. Pia alimtaka mkandarasi kuhakikisha anawaajiri wazawa kwa kazi zisizohitaji utaalamu maalum ili kuwashirikisha wananchi moja kwa moja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Shabaan Mpendu, ameeleza kuwa stendi hiyo ya kisasa itajumuisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la utawala, vibanda vya maduka 60, vibanda 12 vya mama lishe, vibanda 16 vya kukatia tiketi, vibanda 3 vya walinzi, kibanda cha kukusanyia taka, kibanda cha jenereta, jengo la vyoo, msikiti mmoja na mnara wa tenki la maji moja.

Aidha, Mpendu ameongeza kuwa mradi huo pia utahusisha ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 4.7 pamoja na mitaro ya kupitisha maji yenye urefu wa kilometa 8.15, yote ikiwa ni sehemu ya bajeti ya shilingi bilioni 19.99 iliyotolewa na Serikali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Wesons Engineers, Mugore Chambili, ambayo imepewa kandarasi ya kutekeleza mradi huo, aliahidi kuwa kampuni yake itaukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora wa viwango vinavyohitajika.

1753359220602.png

 
Back
Top Bottom