Bilioni 7.5 zatumika kulipa watumishi hewa - Hawa Ghasia
Uzembe unaendelea....
SERIKALI imepoteza shilingi bilioni 7.5 kwa kuwalipa watumishi hewa 2,924, Bunge limeelezwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, amewaeleza wabunge kuwa, wahusika katika wizi huo wameiba jumla ya sh 7,568, 625, 519/-.
Waajiri waliobainika kuwa na malipo mengi hewa ni pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Amesema Waziri Ghasia bungeni wakati anajibu swali la Mbunge wa Singida Kusini, Mohamed Misanga.
Mbunge huyo aliuliza, katika miaka minne kuanzia mwaka 2006, Serikali imepoteza fedha kiasi gani kwa kuwalipa watumishi hewa na ni kutoka katika Wizara na taasisi zipi. Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo alimuuliza Waziri Ghasia kuwa, waliosababisha hasara hiyo wamechukuliwa hatua gani.
Ghasia amesema, watumishi hao hewa wanalipwa mishahara kwa kuwa waajiri hawajawaondoa kwenye orodha ya malipo wakati utumishi wao umekoma.
Kwa mujibu wa Ghasia, utafiti umebanisha kuwa, watumishi hewa walikuwa ni waajiriwa serikalini lakini utumishi wao umekoma kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kustaafu, kufariki dunia, na pia kufukuzwa kazi.
Waziri Ghasia amelieleza Bunge kuwa, majina ya waliosababisha wizi huo yamepelekwa kwenye vyomvo vya ulinzi na usalama, vinalifanyia kazi suala hilo.
Mbunge wa Kisarawe, Athumani Janguo, aliuliza kwamba, uchunguzi kuhusu suala hilo utamalizika lini, na Serikali itachukua hatua gani.
Ghasia amemjibu kwamba, uhakiki katika sekta ya afya umekamilika mwaka jana, Serikali ikijiridhisha itapeleka majina kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali imepata taarifa za awali kuhusu wahusika kwenye sekta ya elimu, hivi karibuni watachukuliwa hatua za kinidhamu na kushitakiwa.
Source: Gazeti la HabariLeo