Suley2019
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 1,811
- 4,533
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imesema ina nia ya kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria ya ndoa 1971 katika Bunge hili la Bajeti linaloendelea, ili kuweka umri wa miaka 18 kama umri wa chini wa kuolewa na kuoa.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema hayo leo Ofisi kwake, Mtumba Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Jukwaa la Wakurugenzi Wanawake waliowakilisha Mashirika takribani 400 yanayotetea haki za Wanawake, Wasichana na Watoto Nchini Tanzania.
Wakurugenzi kutoka Jukwaa la Wakurugenzi Wanawake wametumia fursa hiyo kumhakikishia Waziri na Ofisi yake ushirikiano katika kuhakikisha mchakato huo unapelekea kuwa na sheria nzuri yenye mlengo wa kujinsia kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwa Watoto hasa Watoto wa kike.
Kwa mujibu wa sheria ya ndoa inayotumika sasa ya mwaka 1971 (kifungu namba 13), Mtoto wa kike anaweza kuolewa kuanzia umri wa 14 kwa ridhaa ya Mahakama na kifungu namba 17 kinasema anaweza kuolewa kwa miaka 15 kwa ridhaa ya Wazazi lakini sheria hiyohiyo inasema Mtoto wa kiume ananza kuoa kuanzia umri wa miaka 18.