Mawaziri wazomewa
na Christopher Nyenyembe, Mbeya
MAWAZIRI wa Serikali ya Awamu ya Nne walio mkoani Mbeya kwa lengo la kukisafisha chama hicho tawala dhidi ya sumu iliyosambazwa na wapinzani, jana walijikuta wakiwa katika wakati mgumu kisiasa, baada ya mkutano wao wa hadhara kutawaliwa na miguno ya wananchi na baadaye kuzomewa.
Hali ya wananchi kutokubaliana na hoja za mawaziri hao walioandamana na makada wengine wa chama hicho wakiwamo wale waliotoka katika vyama vya upinzani ilianza kujionyesha tangu mapema kabisa.
Hata hivyo kelele za hao hao, wamekosa hoja, tunataka Karamagi ajibu hoja ndizo zilizotawala eneo ulipofanyika mkutano huo wa hadhara kwenye viwanja vya Shule ya Msingi ya Ruanda eneo la Nzovwe, nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
Hali hiyo ya kuzomea iliendelea hata wakati viongozi hao wakiwa ndani ya magari yao wakiondoka katika mkutano huo jana jioni baada ya wananchi wengi kujipanga kando ya barabara wakipiga mayowe ya hao
haoo, haoo.
Viongozi hao wa juu serikalini na ndani ya CCM waliokuwa wakiongozwa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Taifa, Aggrey Mwanri, walitumia muda mwingi wa hotuba zao kukipamba chama hicho tawala, Ilani yake ya uchaguzi na kuwaponda viongozi wa kambi ya upinzani.
Hata hivyo miguno na kuzomea kwa wananchi wakati wote wa mkutano wakati fulani ilisababisha mhamasishaji mkuu wa chama hicho na mjumbe wa Halmashauri Kuu ambaye ni kiongozi wa kikundi cha uhamasishaji cha chama hicho cha Tanzania One Theatre (ToT), John Komba, kuwataka wale wote waliokuwa hawataki kupunga mikono kuondoka.
Hatua hiyo ya Komba ambaye alikuwa ameongozana na kikundi chake kizima cha TOT ilikuja baada ya kuwataka watu kupunga mikono kuitikia nyimbo zake, hatua ambayo haikuungwa mkono na baadhi ya watu, tukio lililosababisha ajikute akitoa maneno hayo.
Huu ni mkutano wa CCM kwa hiyo kama kuna watu hapa hawataki kupunga mikono waondoke, alisema Komba.
Katika mkutano huo, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chilligati, hakupata nafasi ya kuhutubia mkutano huo kutokana na wenzake waliomtangulia kutumia muda mwingi kukanusha tuhuma zinazotolewa na wapinzani dhidi ya chama hicho tawala.
Mwana CCM pekee aliyeonyesha kuungwa mkono moja kwa moja katika mkutano huo alikuwa ni Mbunge wa Kyela, moja ya majimbo ya mkoani Mbeya, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye alipopewa nafasi ya kuzungumza alizungumzia kuhusu utekelezaji wa sera za chama hicho katika maendeleo ya nchi.
Dk. Mwakyembe alisema kuwa mtaji pekee wa CCM walionao kwa wananchi ni kutekeleza ilani ya chama hicho ili kuweza kujihakikishia ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2010 na si vinginevyo, hatua ambayo ilisababisha ashangiliwe na watu.
Naye Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Stephen Wasirra, aliyetamba kwa jina la Tyson alisifia juhudi zilizofanywa na serikali kuendeleza kilimo kwa kuingiza nchini kiasi kikubwa cha mbolea ya ruzuku.
Wassira aliyetumia muda mwingi kuziponda hoja za wapinzani kuhusu ufisadi, alisema miaka miwili kati ya mitano ambayo serikali imewekeana mkataba na wananchi, imefanya kazi kubwa ya kuboresha huduma za maji, miundombinu ya barabara, elimu na kilimo.
Huku baadhi ya watu wakionekana kutokubaliana naye kwa kutoa maneno ya; siyo kweli, Wasirra aliendelea kusema kuwa katika ziara yake ya hivi karibuni nchini Marekani, Rais Jakaya Kikwete amepatiwa dola milioni 600 kwa ajili ya kilimo na ujenzi wa barabara kuwa hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo.
Alidai kuwa ametumwa mkoani Mbeya kuja kuwabomoa wapinzani na hoja zao za ufisadi, ambao alisema wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa kueneza uongo kwa wananchi bila kutoa ushahidi wa wazi, hali ambayo inapaswa kukomeshwa kwa kuwashikisha adabu.
Hoja hizo za Wasirra zilisababisha mkazi mmoja wa Mbeya kuingia mkutano akiwa na trekta lake kama ishara ya kuwataka viongozi hao kuachana na maneno ya jukwaani na kuhimiza vitendo.
Mbali ya viongozi hao wengine waliopata fursa ya kuhutubia ni makada wapya wa chama hicho waliojiunga kutoka upinzani, Shaibu Akwilombe, Tambwe Hiza na Salim Msabaha, ambao walitumia muda mwingi kuwaponda wapinzani na kuvifananisha vyama vinne vya upinzani vilivyoanzisha ushirikiano kuwa ni sawa na paka waliofungwa mikia pamoja.
Hawa wapinzani walioungana ni sawa na paka waliofungwa mikia yao pamoja na nawaambia hawa hawajaungana, ukiwapelekea panya mbele yao kila mmoja atataka amkamate, wangojeni mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu utaona watakavyoachana, alisema Akwilombe huku akipokewa na miguno ya dhahiri kutoka kwa wananchi.
Kwa upande wake, Tambwe aliwaambia wakazi wa Mbeya kuwa amekuja mkoani humu kuwaomba msamaha kwa kuwa alipokuwa upinzani ndiye alikuwa mpika majungu mkuu dhidi ya serikali na kwamba alikuwa akiungana na wenzake kupika uongo, sasa amerudi CCM.
Wananchi wengi waliozungumza na Tanzania Daima waliuelezea mkutano huo kuwa usio na jipya na wakasema kwa kiwango kikubwa walikuwa wameshindwa kujibu hoja zilizotolewa na wapinzani siku chache zilizopita.
Katika mazingira hayo na watu kushindwa kuishangilia CCM, kiongozi wa bendi ya TOT, Kapteni Komba, aliamua kuwalazimisha watu washangilie na kuwataka wale wasiofanya hivyo wageuke nyuma na kuondoka, hali iliyozusha minongono na wengine kuamua kuondoka. Baadhi ya watu walidai kuwa huu haukuwa muda muafaka kwa chama hicho tawala kufanya mkutano huo, kwani watu wanachotarajia zaidi ni kuona utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na chama hicho kwa mujibu wa ilani yao ya uchaguzi.