WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema ugomvi wa wanasiasa katika jumuia hiyo hauwezi kuathiri shughuli za kibiashara na uchumi wa Tanzania kwa kuwa wafanyabiashara wanaangalia faida zaidi katika shughuli zao.
Sitta alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua athari za kiuchumi zitakazopatikana baada ya kuwapo kwa taarifa ya wafanyabiashara wa Rwanda kutaka kupitisha mizigo yao katika bandari ya Mombasa badala ya ile ya Dar es Salaam.
Alisema kuwa taarifa ya wafanyabiashara wa Rwanda kuazimia kutumia bandari ya Mombasa si za ukweli na kwamba wanaofanya hivyo ni wale waliokosa zabuni mbalimbali ambazo pia hakuzitaja ni zabuni ya nini.
"Mimi ninachojua suala la hapa ni uchumi. Huu ugomvi wa wanasiasa wawili hauwezi kuwakimbiza wafanyabiashara na ukiangalia wanaopitisha mizigo ni wafanyabiashara na si serikali zinazolumbana," alisema.
Aliongeza kuwa migongano baina ya nchi na nchi haiepukiki hususan zilizo jirani na kuita hali hiyo ya mpito huku akisisitiza kuwa maelewano baina ya Tanzania na Rwanda yatarejea muda si mrefu.
Waziri Sitta alisema umbali kati ya Mombasa na Kigali ni kilometa 2300 na kutoka Dar es Salaam hadi Kigali ni kilometa 1400, suala alilodai wafanyabiashara wataangalia umbali katika kutafuta faida ya kazi wanazozifanya.
Alieleza kuwa mkakati mwingine wa kuwafanya wafanyabishara wazidi kuitumia bandari ya Dar es Salaam ni kupunguza vizuizi vya njiani kutoka 15 vya sasa hadi vitatu.
Alisema kuwa na vizingiti vingi barabarani ni tatizo huku akiwashangaa askari wanaosimamisha magari yenye lakiri ambazo hawawezi kuzifungua na kueleza hali hiyo ni kero kwa madereva na wafanyabiashara.
Juzi, msemaji wa Chama cha mizigo nchini (Tatoa) Elias Lukumay, aliiambia kamati ya Bunge ya Bajeti kuwa nchi za Rwanda na Uganda zimekubaliana kutumia bandari ya Mombasa kutokana na urasimu unaodaiwa kuwepo katika bandari ya Dar es Salaam.
Alisema nchi hizo zimekubaliana kuanza kutumia bandari ya Mombasa kuanzia Septemba mwaka huu.
Uamuzi huo wa Rwanda na Uganda unatafsiriwa kuwa unatokana na msigano wa kisiasa ulioibuka hivi karibuni baina ya Rais Jakaya Kikwete na Paul Kagame wa Rwanda baada ya ushauri wake wa kumtaka Kagame akutane na waasi kwa ajili ya kujadili amani ya taifa lao