Badala ya kusikiliza ushauri kiburi cha ajabu cha huyu Mama kimetufikisha hapa. Halafu machawa bado wanataka kumtetea badala ya kujali taifa!!!
Baba Askofu Kalikawe Lwakalinda Bagonza PhD; MNANILAZIMISHA NISEME TUMEFIKAJE HAPA badala ya TUNATOKAJE HAPA?!
Nimesema mara kadhaa kuwa si muhimu kujiuliza tumefikaje hapa bali tujiulize tunatokaje hapa. Mtu mkubwa ninayemheshimu sana “kanilazimisha” niseme tumefikaje hapa. Kwa heshima yake Nasema sasa:
1. Miaka yote tuna AMANI bila Haki, hapakuwa na maandamano.
2. Miaka yote chaguzi hulalamikiwa, hapakuwa na maandamano.
3. Miaka yote wagombea huenguliwa, kura huibiwa na hakuna maandamano.
4. Miaka yote wagombea hutekwa, wakurugenzi hujificha chini ya meza na hakuna maandamano.
5. Miaka yote ufisadi, kupuuza ripoti za CAG na rushwa za uchaguzi zipo, kupora ushindi kwa mabomu kupo - bado hakuna maandamano.
6. Miaka yote Diaspora wapo, wakiunga mkono upinzani na CCM pia - bado maandamano hayapo.
7. Miaka yote wapinzani hugawanyika, huuza ushindi, hujiteka - bado maandamano hayapo.
8. Miaka yote wapinzani hujiengua na kuhamia CCM na ubambikiziaji wa kesi za uhaini umewahi kuwepo - bado maandamano hayakutokea.
9. Miaka yote viongozi wa upinzani hukamatwa, hunyimwa haki, hufungwa na kulipiwa faini - bado maandamano hatukuyaona.
10. Miaka yote tume ya uchaguzi huteuliwa na rais, huhesabu kura au hubuni matokeo na bado maandamano hayakutokea.
SASA NINI KILITOKEA MPAKA MAANDAMANO YAKATOKEA?
a) Utekaji, utesaji na mauaji ya kikatili vilishamiri sana mpaka watu kujitaja na viongozi wakakaa kimya.
b) Hoja ikapelekwa bungeni - Spika akaitupilia mbali. Kama angeipokea, utekaji ungekoma. Damu za watu zitalilia bunge lililopita.
c) Kesi zikapelekwa mahakamani (Hebeas Copus), zikatupwa. Na pale mahakama ilipokubali; Polisi wakaigomea mahakama. Majaji wetu kuweni macho. Damu isiyo na hatia ni hatari.
d) Baadhi ya Viongozi wa Dini wakapaza sauti, wakapigwa nondo na wengine makanisa yakafungwa. Waliokaa kimya, Mungu hatawakalia kimya. Mdomo haulipiwi kodi.
e) Wana diplomasia wakatishwa kwa kuwasikiliza wapinzani na wana harakati. Nijuavyo: Geneva Convention inamfanya “mbwa wa mfalme kuwa mfalme wa mbwa wote”.
f) Wana CCM walio huru na jasiri walionya na kushauri - wakapuuzwa, wakatishwa, wengine wakagombea na majina yao kukatwa.
Mwisho, wakosoaji wakaambiwa wasubiri MPAKA YESU ARUDI!
Wapendwa, mwanadamu ana kiwango fulani cha uvumilivu. Huo uvumilivu husaidiwa na matumaini kuwa kesho itakuwa bora kuliko leo. Matumaini yalitoweka kwa sababu mianya yote ya kupata haki ilifungwa. Mihimili yote iliungana kuushambulia uhuru na haki za watu na kuwakebehi (impunity).
Mwanadamu aliye maskini na kukosa haki na uhuru, ni mkatili sana. Naomba na kusihi, tujitazame. Tusiwatazame vijana au hao “wahuni”. Kuna hali mbaya ya uchumi iko njiani. Tulitazame taifa kuliko vyama vyetu. Tunaelekea kuchelewa.
Nawapongeza wote ambao wameanza kuuona ukweli. Kuna kitu hakiko sawa. Hakitaondoka kwa kukamata na kufunga watu, kuongeza askari mitaani, kufuta vyama, kulaumu mataifa ya jirani nk. Tume ya Uchaguzi imekosa uaminifu na uangalifu. Tumemwaga damu nyingi bila sababu. Wahusika wasiposikia, basi wakebishe hali za magereza yetu kwa sababu bila mabadiliko na toba, wanaofunga sasa pia watafungwa siku zijazo. Ukweli huu usiharibu urafiki wetu na wala msigeuze aibu kuwa hasira.
Hivi anayeteka na anayetekwa nani ni GAIDI?
Haya ni mawazo yangu, wewe una yako, na walioua wana yao. Waliouawa hawana maoni. TUMEWAONEA