Samatta aponda hukumu ya mgombea binafsi

August

JF-Expert Member
Jun 18, 2007
8,396
4,056
19 December 2010

Leon Bahati


JAJI Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, ameiponda hukumu iliyotolewa na jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufani kuhusu suala la mgombea binafsi akisema imeonyesha kuwa sasa mhimili huo unayumbishwa na wanasiasa.

Katika hukumu ya rufaa ya serikali dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuruhusu mgombea binafsi iliyotolewa mwezi Juni, jopo hilo lilisema kuwa mahakama haina mamlaka ya kuamua juu ya hoja ya mgombea binafsi kwa kuwa ni suala la kisiasa na kuliagiza Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutafuta ufumbuzi wake.

Kesi hiyo ilifunguliwa na kiongozi wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye aliitaka mahakama kubatilisha kipengele kinachozuia mgombea binafsi akisema sheria hiyo inakiuka katiba.

Lakini Jaji Samata, ambaye baada ya kustaafu nafasi yake ilichukuliwa na Jaji Agustino Ramadhan, aliielezea hukumu hiyo kuwa inaashiria kuwa mhimili huo sasa unakwepa kutekeleza wajibu wake kwa kutolitolea uamuzi suala lililo ndani ya mamlaka yake.

Samatta aliweka wazi kwamba suala hilo la mgombea binafsi linahusu uhuru kwenye uchaguzi.

Alifafanua kuwa uhuru huo wa uchaguzi unahusu suala la kikatiba na wala siyo la moja kwa moja la kisiasa, kwa maana hiyo jopo hilo lilikosea katika kufikia uamuzi huo.

"Ninachojua ni kwamba malalamiko yoyote yanayohusu mabadiliko ya kifungu chochote cha katiba au kuamua kuhusu haki kwenye uchaguzi ni suala la kisheria na sio jambo tu tunaloweza kulielezea ni la kisiasa," alibainisha Samatta na kuongeza:

"Hebu tujaribu kukubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Rufani kuwa suala la mgombea binafsi lilikuwa la kisiasa. Mtazamo huo nafikiri utamfanya mtu kujiuliza.

"Kwa nini mahakama iliamua kujiingiza katika jambo hili la kisiasa hata kutoa ushauri kwa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali namna ya kuamua mambo ya siasa?"


Hukumu inayolalamikiwa iliyosomwa na Jaji Ramadhan aliyeongoza jopo la majaji saba waliosikiliza rufaa hiyo.

Wengine katika jopo hilo walikuwa Eusebio Munuo, Januari Msofe, Benard Luanda, Mbarouk Mbarouk, Nathalia Kimaro na Sauda Mjasiri.

Katika hukumu hiyo, Ramadhani alisema Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na hoja za serikali baada ya kuzingatia ushauri wa wataalamu wa mambo ya sheria hususan wa masuala ya katiba.

Alisema mahakama haina mamlaka ya kutangaza ibara yoyote kuwa ni kinyume cha katiba na kwamba mamlaka hayo yako chini ya Bunge, ambalo ni chombo cha kutunga sheria, tena kwa kufuata utaratibu ulioelezwa katika katiba yenyewe.

Alieleza kutokana na hukumu hiyo ni dhahiri mahakama si mlinzi wa matakwa ya watu, bali hilo ni jukumu la wabunge waliochaguliwa.

Kwa sababu hiyo akasema kuwepo kwa mgongano wa vifungu vya katiba, Bunge ndilo linalopaswa kulishugulikia na si mahakama isipokuwa tu pale ilipopewa mamlaka haya yaliyoelezwa, ambayo hata hivyo haina.

"Baada ya kusema hayo yote, ni dhahiri kuwa hatuwezi kusema kisheria kuwa mgombea binafsi ni ruksa. Hilo ni eneo la utawala wa Bunge kurekebisha katiba kwa mujibu wa kifungu cha 98 (1)," alisema Jaji Ramadhani wakati akisoma hukumu hiyo.

Hukumu hiyo ilihitimishwa kwa mahakama kushauri pande zote, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bunge kuamua suala hilo kwa kuwa lina muegemeo wa kisiasa.

Lakini ikashauri uamuzi wao kutambua kuwa kwa mujibu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, haki ya mtu kushiriki katika uchaguzi haipaswi kuwekewa mipaka bila sababu za msingi, ikiwa ni pamoja na kumtaka mgombea kuwa mwanachama wa chama cha siasa.

Hukumu hiyo ilitengua uamuzi wa Mahakama Kuu iliyokubaliana na hoja za Mchungaji Mtikila kuwa sheria inayozuia mgombea binafsi inakiuka katiba ya nchi.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 2006 na majaji watatu wa Mahakama Kuu, Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo, iliipa serikali miezi sita kuweka kifungu kinachoruhusu kuwepo kwa mgombea wa aina hiyo.

Maoni ya Samata yametolewa katika kipindi ambacho wanasheria, hasa majaji, wanaonekana kuongezeka ujasiri na kuikosoa serikali bila ya woga, huku wengi wao wakiwa miongoni mwa vinara wanaotaka katiba iandikwe upya baada ya kujitokeza kasoro kadhaa kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Kasi ya madai ya katiba mpya iliongezeka baada ya Chadema kususia matokeo ya uchaguzi wa rais na wabunge wake kuamua kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kuhutubia.

Chadema haitambui matokeo ya uchaguzi wa rais na imeweka hoja mezani ikitaka kuandikwa upya kwa katiba, kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza utangazaji wa matokeo ya rais na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.
 
Hii hukumu iliwatia aibu sana wasomi wetu majaji kwa kutoa hukumu ya aibu kwa profession yao ili mradi wawafurahishe mabwana zao wanasiasa.
 
there is no sepatarion of power kwa mahakama kuamua kusema ili ni swala la kisiasa lipelekwe bungeni. hii ni kesi ya kwanza ambayo imefikia mahakama ya rufaa na hakuna hukumu iliyotolewa, its a shame. we real need a new constitution.
 
Usinikumbushe huu upuuzi. Huwa sitaki hata kusikia juu yake. Hii ndiyo kumbukumbu ametuachia Ramadhani A (CJ as he then was)
 
Back
Top Bottom