Gembe
JF-Expert Member
- Sep 25, 2007
- 2,483
- 159
WAkuu heshima mbele,Je kuna mtu anafahamu ni mfanyabiashara gani anataka kuchukua eneo hilo?,Je wana bodi mnasemaje kuhusu hili la kubomolewa?.sijafika Mkoa wa Mwanza muda kujua kama kweli uwanja huo umebomolewaa.na Sitta Tumma , Mwanza
SAKATA la kuvunjwa kwa uwanja wa michezo wa Nyamagana uliopo katikati ya Jiji la Mwanza, limeanza kuchukua sura mpya, kutokana na Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani hapa kulifikisha kwa uongozi wa taifa ili utoe tamko rasmi.
Uamuzi huo umekuja baada ya CCM Mkoa kuonekana kuingia kwenye mgogoro mzito na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, baada ya chama hicho kupinga kitendo cha halmashauri hiyo, kuubomoa uwanja huo kwa ajili ya kupisha uwekezaji wa hoteli ya kitalii.
Taarifa ya CCM Mkoa kwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho taifa kwa upande wa Bara, Pius Msekwa, imeeleza kusikitishwa na kitendo cha uongozi wa jiji kuvunja uwanja huo, na kwamba hatua hiyo inakinzana na Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya kukuza na kuboresha michezo hapa nchini.
Mbali na taarifa hiyo kulaani ubomoaji wa uwanja huo, pia imeeleza kuwa uamuzi uliofikiwa na uongozi huo wa jiji, unapaswa kusitishwa mara moja ili kwenda sambamba na utekelezaji wa ilani hiyo ya uchaguzi.
Mwezi mmoja uliopita, uongozi wa Jiji la Mwanza chini ya Mkurugenzi wake, Wilson Kabwe ulianza ubomoaji wa uwanja huo, pasipo kueleza dhamira halisi ya kuuvunja, licha ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Pombe Magufuli kutoa amri ya kutovunjwa.
Habari za ndani zinaeleza kuwa, sababu ya kuvunjwa Nyamagana, inatokana na mmoja wa wafanyabiashara wakubwa jijini hapa, kupewa nafasi hiyo na jiji kwa ajili ya kujenga hoteli.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa kwa Msekwa na Mwenyekiti wa CCM Nyamagana, Athuman Zebedayo, uongozi wa jiji umekaidi amri ya kusitisha zoezi hilo la ubomoaji.
"Makamu mwenyekiti, kuna mgogoro umeanza kufukuta kati ya chama na jiji, na sababu ya yote hayo ni Uwanja wa Nyamagana ambao jiji linaubomoa bila sababu za msingi, na chama hakitaki kubomolewa kwa uwanja huo," alielezwa Msekwa.
Mwenyekiti huyo aliyekuwa akizungumza huku akionyesha dhahiri kukerwa na kitendo hicho, aliyaeleza hayo juzi kwenye Baraza la Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), jijini hapa lililokutana kwa ajili ya ugeni wa Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM taifa.
Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, huku akishangiliwa na wajumbe, Zebedayo alisema, kuvunjwa kwa uwanja huo ni sawa na kuvunjwa kwa sera na ilani ya CCM na kwamba uwanja huo ndiyo tegemeo kwa vijana kufanyia mazoezi.
Aliitumia nafasi hiyo, pia kumuomba Msekwa pamoja na Mwenyekiti wa Taifa CCM, Rais Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake ya kichama kutoa amri ya kutovunjwa kwa uwanja huo mkongwe.
"Kwa mfano, uchaguzi umekaribia na vijana tumeanza kuwabughudhi, tofauti na tulivyowaahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu, hivi tutaponea wapi? Kwa nini jiji likiuke ilani na sera za chama tawala?" alihoji Zebedayo.
Hata hivyo, habari zilizopatikana jijini hapa na kuthibitishwa na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu mkoani hapa, zimeeleza kuwa mmoja wa wana CCM mkoani hapa, ndiye anayetaka kujenga hoteli katika viwanja hivyo na kwamba kamwe chama hakitaridhia kubadilishwa matumizi ya uwanja huo.