Sakata la uchakachuaji mafuta | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Sakata la uchakachuaji mafuta

Discussion in 'JF Chit-Chat' started by makerubi, Apr 15, 2011.

 1. m

  makerubi Member

  #1
  Apr 15, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 81
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  KIBAO kimewageukia wafanyabiashara wakubwa wa mafuta nchini baada ya kudaiwa wamekuwa mstari wa mbele katika kufanya vitendo vya uchakachuaji, imeelezwa. MZALENDO ilielezwa kuwa kelele zilizokuwa zikipigwa na baadhi ya wafanyabiashara hao hivi karibuni ni kiini macho chenye lengo la kutaka kuwapumbaza watu na kuficha ukweli. “Nimeshangazwa sana na baadhi ya wafanyabiasha hao kusema hawahusiki na uchakachuaji…baadhi wamefungua vituo njiani kwa ajili ya kazi hiyo na kuwa wanaendelea kufanya hivyo hadi sasa,” kilisema chanzo chetu. Ilielezwa kuwa mmoja wa wafanyabiashara hao amekuwa akisafirisha lori zima la mafuta ya taa hadi kwenye kituo chake kilichopo Dodoma na kuyapunguza kidogo kidogo kwa kuyachanganya na dizeli hadi yanapoisha.
  “Malori yake yanapopita anapunguza dizeli kiasi na kufidia na mafuta ya taa hadi yanapoisha na kujikuta dizeli aliyokuwa akipunguza inaweza kujaza lori, hivyo analijaza na kulirudisha Dar es Salaam kuuza,” alisema ofisa mwandamizi katika sekta ya mafuta.
  Ofisa huyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema kwa kiasi kikubwa mfanyabiashara huyo ndiye shehena zake zimekuwa zikikataliwa katika nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kutokana na kuchakachuliwa.
  Alisema baadhi ya wafanya biashara hao (majina tunayahifadhi) wana vituo vya mafuta ambavyo chini vina uwezo wa kuhifadhi lita nyingi kiasi cha kutia shaka lengo la kuwa na hifadhi kubwa namna hiyo.
  Ofisa huyo alisema kilichofanywa na baadhi ya wafanyabiashara hao ni kutaka kudanganya umma, ili hali wenyewe bado wanaendeleza vitendo vya uchakachuaji mafuta.
  Alisema badala ya kurudisha ushuru woto wa mafuta ya taa ambao ni tofauti ya sh. 450 na ushuru wa mafuta ya dizeli, mafuta ya taa yatozwe ushuru wa sh. 250, jambo litakalofanya wahusika kushindwa kufanya uchakachuaji.
  “Kwa sasa ushuru ni tofauti kwa sh. 450 ambapo kwa kila lita tajiri huchukua sh. 250 na dereva sh. 200, hivyo ushuru ukiongezwa kwa sh. 250, biashara ya uchakachuaji itakuwa ngumu na hivyo kufa kabisa,” alisema ofisa huyo.
  Kuibuka kwa mambo hayo kumetokea siku chache baada ya kuwepo madai kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na askari polisi ni miongoni mwa wanaotajwa kuhusika kuunda genge la uchakachuaji mafuta na kusababisha kuyumbisha uchumi wa taifa.
  Uchakachuaji huo wa mafuta umekuwa ukisababisha taifa kupoteza kiasi cha sh. bilioni 25 hadi 36 kila mwezi.
  Madai hayo yalibainika wiki hii katika Ofisi Ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi na Umoja wa Wasafirishaji Shehena kwa Barabara Tanzania (TATOA).
  Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Fulgence Bube, alisema kuwa suala la uchakachuaji mafuta linawahusisha watu wakubwa nchini na ambao wapo katika maeneo tofauti ya barabara kuu iendayo mikoa ya Kanda ya Ziwa.
  Bube alisema wachakachuaji hao walikuwa na tabia ya kuteka malori katika eneo la Kibaha na Chalinze kwa kuunda mtandao na madereva wa malori ili waibe mafuta vizuri.
  Kutokana na unyeti wa jambo hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba aliunda kamati ndogo ya bunge ya nishati na madini kubaini kiini cha tatizo la uchakachuaji mafuta nchini.
  Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni Yussuf Abdallah Nassir, Selemani Zedi, John Mnyika, Mariam Kisangi, Suleiman Nchambis, Khalfan Aeshi na Salim Ali na ambayo imepewa muda wa mwezi mmoja na itakuwa chini ya Charles Mwijage.
  Sakata la uchakachuaji mafuta liliibuliwa bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2007 na mbunge Ahamed Shabiby (Gairo – CCM) ambaye alieleza madhara na jinsi vitendo hivyo vinavyofanyika na huo ukawa mwanzo wa kutumika kwa neno uchakachuaji hadi sasa. TAFAKARI
   
Loading...