SADC yajadili umuhimu wa rasilimali watu na fedha katika maendeleo ya viwanda

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Tamko la Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu uwekezaji katika Rasilimali Watu uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Julai 2023, litakuwa sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaondelea Jijini Luanda, Angola.

Kauli hiyo ilitolewa Agosti 13, 2023 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax wakati anaongea na vyombo vya habari pembezoni mwa mkutano huo.

IMG_8270.jpeg

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akifuatilia hotuba za ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika Luanda, Angola tarehe 17 Agosti 2023.

IMG_8271.jpeg
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC aliyemaliza muda wake ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Antipas Nyamwisi (kulia) akikabidhi uenyekiti wa baraza hilo kwa Waziri wa Uhusiano wa Nje wa Angola, Téte António.

Dkt. Tax amesema kuwa Tamko la Dar es Salaam limeainisha masuala mbalimbali ya utekelezaji kwa ajili ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu. Masuala hayo yameendelea kujadiliwa katika Mkutano wa 43 wa SADC ili kuhakikisha kuwa, katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu ambayo inahusu umuhimu wa rasilimali watu na fedha katika maendeleo endelevu ya viwanda, tamko la Dar es Salaam linakuwa sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu hiyo.

“Suala la uwekezaji katika rasilimali watu, suala la uendelezaji wa rasilimali watu katika kuendeleza uchumi, ni vitu ambavyo tunaendelea kuvisukuma kama ilivyokuwa kwa Rais wetu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo uliofanyika Tanzania,” Dkt. Tax alisema.

Awali, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Elias Magosi alisisitiza umuhimu wa Nchi za SADC kuondoa vikwazo vinavyorejesha nyuma kasi ya muingiliano, uendelezaji wa viwanda na upatikanaji wa masoko ya bidhaa baina ya nchi hizo na nje ya nchi hizo.

Uondoaji wa vikwazo hivyo, imeelezwa kuwa utaifanya Kanda ya SADC kuwa katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda wa 2020-2030 na dira ya kanda hiyo ya 2050.

Alisema kuwa, licha ya changamoto zinazoikabili dunia, kama mabadiliko ya tabianchi na mgogoro wa Urusi na Ukraine ambazo zimesababisha athari nyingi kwenye Kanda ya SADC, Jumuiya hiyo imefanikiwa kuziwezesha nchi wanachama kupata masoko ya kikanda na kimataifa. Nchi zilizonufaika na masoko hayo ni pamoja na Tanzania ambayo ilipata soko la maparachichi katika nchi za China, India na Afrika Kusini.

Magosi aliendelea kueleza kuwa, kwa uratibu wa Sekretarieti ya SADC, nchi wanachama zimefanikiwa kupunguza msongamano wa magari, muda na gharama za usafirishaji katika baadhi ya mipaka, hususan yenye vituo vya pamoja vya mipakani (one stop border post-OSBP) kama Nakonde/Tunduma kwenye mpaka wa Tanzania na Zambia.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliopangwa kufanyika Agosti 17, 2023. Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, ilishuhudiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikikabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri kwa Angola.

4a298849-40f2-43c1-9d00-60bb6f93f633.jpg

Waheshimiwa Mawaziri wa SADC wakiendelea na mkutano wao ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika Luanda, Angola tarehe 17 Agosti 2023.
 
Back
Top Bottom