Imetolewa mara ya mwisho: 16.11.2008 0021 EAT
• Nguvu za EPA TAKUKURU 'kupiga' kambi Kisutu
Na Said Mwishehe
Majira
SIKU moja baada ya baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kutumiana kupokea rushwa kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa wa wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) , Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ina mpango wa kuweka mtego utakaowanasa wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Habari za ndani kutoka ndani ya TAKUKURU ambazo zimelifikia gazeti hili jana jioni zimeeleza kuwa taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa zimeisumbua taasisi hiyo na sasa inajipanga kuweka 'kambi' ili kuwanasa watumishi wanajipatia rushwa kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa kwa madai kuwa watawasaidia kupunguza makali ya dhamana.
Hata hivyo chanzo chetu hicho kilisema mpango wa kuweka mtego Kisutu ni wa siri.
"Wewe umeniuliza mmejipanga vipi kudhibiti vitendo vya rushwa vilivyoripoti Kisutu, nimekujibu kuwa tumejipanga sasa unataka nikueleze mipango yetu itafanyikaje! Uliona wapi askari anaanika siri za jeshi lake hadharani?" kilihoji chanzo chetu kwa sharti la jina lake kutochapishwa hadharani.
Hata hivyo chanzo hicho hakikuwa tayari kuliongelea kwa udani suala hilo kwa madai kuwa anayeweza kuzungumzia madai hayo ni Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hosea. Gazeti lili lilipomtafuta Dkt. Hosea, ili atolee ufafanuzi mpango huo simu yake ilikuwa imezimwa.
Jana vyombo vya habari karibu vyote viriripoti taarifa kuwa kuna tuhuma za kuwepo kwa rushwa katika mahakama hiyo ambapo baadhi ya watumishi wa mahakama hiyo wanatuhumiana kupokea rushwa kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa wa EPA ili kuwasaidia kupata dhamana.
Mbali ya tuhuma hizo, juzi mahakimu walikaa kikao cha dharura ambacho kiliwahusisha makarani wote kujadili mambo mbalimbali ambayo yamejitokeza tangu watuhumiwa wa EPA waanze kufikishwa mahakamani.
Habari za ndani zilieleza kuwa makarani wa mahakamani hiyo walionywa kutojihusisha na rushwa na kutahadharishwa kuwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Kikao hicho kiliitwa na uongozi wa mahakama hiyo na kuongozwa Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Bw.Ferdinand Wambali.
Pamoja na mambo mengine mahakimu wanaosikiliza kesi za EPA waliomba kupatiwa ulinzi kwa kuhofia usalama wa maisha yao kwa kuzingatia uzito wa kesi walizopangiwa kuzisikiliza.