Rudisheni nyumba zote za serikali

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,886
Posted Date::4/22/2008
Rudisheni nyumba zote za serikali
Na Prof. Abdallah J. Saffari
Mwananchi

HABARI kubwa katika ukurasa wa mbele wa gazeti moja la kila siku, Aprili 5, 2008 ilisema, "Mjadala wa Nyumba za Serikali Waibuka Tena."

Ilielezwa kuwa mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), atatoa hoja binafsi katika kikao cha 11 cha Bunge kutaka watu ambao si wafanyakazi wa serikali ambao wameuziwa nyumba za serikali wanyang'anywe nyumba hizo. Nafikiri anataka wakishanyang'anywa wauziwe watumishi wa serikali badala ya kuzirejesha serikalini!

Mbunge pia alitaka kuwa baada ya hoja yake mjadala kuhusu nyumba hizo za serikali ufungwe rasmi. Anaogopa nini? Umma usiendelee kudai nyumba zao?

Kila viongozi duniani huweza kuteleza katika uamuzi na vitendo vyao.

Lakini kwa hakika kabisa wengi wanahisi uamuzi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na wenzake kuuza nyumba za watumishi wa serikali ni wa kidhalimu, kifisadi na umestaajabisha kupindukia. Ndiyo maana kila uchao magazeti huwa na barua au makala kupinga uamuzi huo hadi leo. Wanauliza, kwani ndio mwisho wa kuwa na watumishi wa serikali Tanzania?

Watu mashuhuri ambao wamepinga uamuzi huo ni pamoja na Herman Kirighini aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi na Nyumba katika serikali ya awamu ya pili na marehemu Prof. Thedeus Bugingo.

Gazeti jingine la kila siku, Machi 12, 2008, liliandika makala fupi thabiti aliyoiita, �Rais anza kurejesha nyumba yako serikalini.� Makala hiyo inaelezwa kuwa baada ya kujichukulia nyumba ya serikali iliyopo Sea View, Upanga, Dar es Salaam Rais mstaafu Mkapa aliwaruhusu wenzake wachukue nyumba walizokuwa wanakaa kuficha dhuluma hiyo. Nyumba nyingine zilikarabatiwa kwa mamilioni kabla ya kuuzwa kwa bei poa. Rais Kikwete naye akaambulia yake Mtaa wa Ursino, Ada Estate, Dar es Salaam ambayo hadi sasa hajairejesha serikalini.

Nyumba za watumishi wa serikali zilianza kujengwa na watawala wa Kijerumani na Waingereza. Chache ziliongezwa katika awamu ya kwanza ya utawala chini ya Mwalimu Nyerere. Ziko za daraja la tatu, pili na kwanza kulingana na nyadhifa za watumishi wa serikali. Nyumba hizo takriban sio chini ya 10,000 (elfu kumi) ziko maeneo mazuri sana mikoa yote Tanzania. Mashuhuri zaidi ni zile zilizopo Upanga na Oysterbay, Dar es Salaam.

Nyumba hizo zilijengwa jirani na ofisi za serikali kurahisisha usafiri. Na azma yake kubwa ni kuondoa kero ya makazi, gharama za kuwalipia kodi za kupanga na kuwavutia wafanyakazi ili wafikie ufanisi kiutendaji. Kila mtumishi wa serikali alisubiri kwa hamu siku ya kuhamia kwenye nyumba nzuri za serikali.

Hata siku moja Mwalimu Nyerere asingefikiria kuziuza nyumba hizo kwa yeyote yule. Na inasadikiwa kuwa mara mbili Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi akikataa wazo la kuziuza nyumba hizo. Ila Mkapa aliona sawa tu! Baada ya kujichukulia ile ya Sea View aliona bora asilaumiwe peke yake. Ndipo nyumba za serikali zikauzwa kwa mawaziri, majaji, makatibu wakuu, wakurugenzi, wakuu wa jeshi, polisi magereza n.k.

Yasemekana jaji mmoja alifanya sherehe kufurahia kuuziwa nyumba ya dezo! Kama walionufaika ndio hao, wananchi watalalamikia wapi? Kama viongozi wako mbele kukiuka katiba ya nchi (ibara 9 (c ) kupora mali ya umma, wananchi wende wapi? Hawawezi kupata haki kwa kupeleka madai ya kurejeshewa nyumba hizo mahakamani ambapo waamuzi wengi ndio wanufaika wakubwa wa ufisadi huo! Jaji mwingine mstaafu tayari ameipangisha nyumba yake, iliyoko kwenye mandhari nzuri ya bahari, kwa shirika la mawakili mashuhuri Dar es Salaam.

Sababu za kuuza nyumba hizo hazikuwekwa bayana. Inadaiwa eti ni kuwasaidia watumishi wa serikali kuwa na nyumba. Mara nyingine inasemekana eti ni mzigo kwa serikali kuzimiliki na kuzihudumia nyumba hizo. Hoja hizi zote ni chapwa kwa sababu watumishi waandamizi wengi walikuwa na nyumba zao au wangeweza kuwa nazo kutokana na vipato vyao au kwa mikopo. Kuthibitisha hilo ni kuwa nyumba nyingi tayari zimevunjwa kama pale kwenye kona ya Barabara ya Kaunda, Oysterbay, Dar es Salaam au karibu na Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.

Na wengine wengi waliouziwa wamezipangisha baada ya kustaafu na kuwakosesha wale warithi wa nyadhifa zao mahali pa kukaa. Kwa mfano Kamishna Mkuu wa zamani wa Magereza aliishia kukaa kwake, nje kabisa ya jiji, kwa vile nyumba aliyostahili kuhamia Oysterbay iliuzwa kwa Kamishna Mkuu aliyemtangulia.

Waajiriwa wengi wapya na wale wanaohamishwa hufikia mahotelini au kukodiwa nyumba binafsi kwa gharama ya zaidi ya laki tatu kwa siku au mamilioni ya fedha kwa mwezi (kwa nyumba nzima).

Pia sio kweli kwamba serikali ilikuwa inapata hasara kuzimiliki na kuzihudumia nyumba hizi. Baadhi yake zilihitaji matengenezo kidogo tu kama vile inavyokarabatiwa ofisi ya Kodi ya Mapato Mtaa wa Samora, Dar es Salaam. Kuna baadhi ya majengo mengi Dar es Salaam yamekarabatiwa vizuri tu kwa matumizi kama jengo la Halmashauri ya Jiji na Boma la Zamani Mtaa wa Sokoine, Dar es Salaam.

Kuhusu kujenga nyumba mpya inathibitisha dhahiri kwamba serikali ilikuwa na uwezo wa kuzikarabati nyumba zake kwani ilikuwa rahisi zaidi kufanya hivyo kuliko kujenga nyumba mpya. Kweli ni uroho tu wa kuzichukua nyumba zile na tamaa ya kuhodhi maeneo mazuri makubwa karibu na jiji.

Kwa kuishiwa na hoja za kutetea uamuzi wao John Pombe Magufuli, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi wakati huo alibaki kutoa kauli za vijembe na dharau. �Nyie mwaona wivu,� na �Mlie tu!

Inasemekana Serikali ya Awamu ya Tatu ilikusudia hata kuuza jengo la Wizara ya Ardhi ili ijengwe hoteli kwenye mandhari nzuri ya bandari. Jitihada zikaanzishwa makao makuu ya Wizara hiyo yajengwe Dodoma. Bahati tu wafanyakazi wazalendo wakafanya mbinu kuzorotesha utekelezaji wa ufisadi huo.

Ni katika awamu hiyo hiyo majengo ya ghorofa ya Shirika la Posta na Simu yaliuzwa kwa mtu binafsi. Wapangaji wa Shirika wakatupwa nje kama mbwa koko!

Kwa hiyo tunarejea tulipoanzia kwa kumueleza Mbunge Kimaro kuwa, Kama mvuvi vua, usichezee mashua.� Kwa bahati mbaya wabunge na hata viongozi wa upinzani wamekaa kimya muda wote mintarafu suala la kuporwa kwa nyumba za serikali.

Hoja iliyopo sio kurejesha nyumba zilizouzwa kwa watu ambao sio watumishi wa serikali. Kwani kwa kufanya hivyo zitauzwa tena kwa watumishi wa serikali wateule.

Kama kweli mbunge ni mzalendo basi adai nyumba zote za serikali zilizouzwa zirejeshwe serikalini. Waliouziwa warejeshewe fedha zao. Vinginevyo dhoruba ya umma itazirejesha nyumba hizo, kama si leo, basi kesho! Hakuna haja ya kuunda Tume kuhusu jambo hili, ambayo itapoteza muda na fedha za umma.

Profesa Abdallah Safari ni Profesa wa Sheria na Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania
 
Hapa ndipo nachefuka sana na Magufuri ambaye ni mkono wa kulia wa MKAPA kwenye hili.
 
Nyumba za serikali zilizouzwa zarejeshwa
Mwandishi Wetu, Dodoma
Daily News; Friday,April 25, 2008 @21:01

WIZARA ya Maendeleo ya Miundombinu, imekiri kuwapo na kasoro zilizojitokeza kwenye mchakato wa uuzaji wa nyumba za serikali na tayari watu wanne waliouziwa nyumba kinyume cha taratibu wamezirudisha na saba zisizostahili kuuzwa pia zimerudishwa.

Naibu Waziri, Dk. Milton Mahanga aliyasema hayo bungeni jana wakati akichangia hoja binafsi ya Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), aliyoiwasilisha akitaka kurejeshwa kwa nyumba hizo kwa sababu ziliuzwa kinyume cha taratibu.

Katika kuchangia hoja hiyo, Dk. Mahanga alikiri kuwa kweli zilijitokeza kasoro kwenye mchakato wa kuuza nyumba hizo na Tume iliundwa na inaendelea na kazi. Kwa mujibu wa Mahanga, kuna watu ambao hawakustahili kuuziwa nyumba lakini wakauziwa. Tayari nyumba nne zimerudishwa.

Vile vile alisema kuna nyumba zisizostahili kuuzwa ziliuzwa na kwamba tayari saba zimesharudishwa na mchakato unaendelea. Pia alisema nyumba za Halmashauri hazikupaswa kuuzwa na 14 zimegundulika.

Katika maelezo kuhusu hoja yake iliyochangiwa na zaidi ya wabunge 14, Mbunge huyo wa Vunjo, aliiwakia Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kuuza nyumba za serikali. "Hapa Mheshimiwa Spika, Je, Serikali hiyo ya Awamu ya Tatu ilipouza hizo nyumba ilitegemea hapatakuwapo tena serikali nyingine na watumishi," alihoji Kimaro.

Alisema haiwezekani nyumba ambayo ni rasilimali ya Taifa kwa Watanzania wote, ikauzwa kwa Sh milioni 15 badala ya Sh milioni 200 wakati wananchi wenye mali wakiambiwa wachange wajenge madarasa, nyumba za walimu na zahanati.

Aliitaka Wizara husika itoe orodha ya wafanyakazi wanaolipwa kwa kukosa nyumba baada ya zile za awali kuuzwa na ionyeshe ni kiasi gani cha fedha kinalipwa hotelini kwa kuwaweka watumishi waliokosa nyumba.

Wabunge walipitisha hoja ya nyumba za serikali zilizouzwa kinyume cha utaratibu, zirejeshwe kwenye umiliki wake huku baadhi wakishutumu hatua ya kuziuza kwa kile walichosema ziliwanufaisha viongozi.

Kutokana na hoja hiyo, Bunge limeazimia serikali itoe orodha ya nyumba zake ambazo ziliuzwa kwa watu ambao si watumishi wa serikali na pia zile ambazo hazikupaswa kuuzwa kutokana na unyeti wa kazi za watumishi wa serikali wanaostahili kuzitumia.

Pia limeazimia serikali ichukue hatua kwa wale ambao hawajalipia na mikataba yao ya kuuziwa irejewe kuhakikisha malipo hayo yanalipwa mara moja ama mikataba inafutwa na nyumba kurejeshwa serikalini.

Miongoni mwa wabunge waliochangia, wengi walielezea kukerwa kwao kwa kile walichosema asilimia kubwa ya waliouziwa ni viongozi na watu wenye fedha. Mbunge wa Bukene, Teddy Kasella-Bantu (CCM), alipendekeza waliouziwa nyumba hizo waongeze fedha kwa vile ziliuzwa kwa bei ndogo.

Mbunge huyo alipendekeza pia watu wasio watumishi wa serikali waliopewa nyumba, wazirudishe na hatua zichukuliwe dhidi ya walioidhinisha watu hao kupewa nyumba hizo.

"Hii ya kutoa nyumba kwa watu wasio watumishi ni rushwa. Zirudi serikalini na aliyeidhinisha achukuliwe hatua. Tuendelee kutoa chuya ili mwaka 2010 tupate mchele safi," alisema Kasella-Bantu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya (CCM) alisema ugawaji huo wa nyumba unarudisha matabaka miongoni mwa wafanyakazi. Mpesya alisema wakubwa ndiyo walionufaika na hatua hiyo.

"Hawa ndiyo wenye magari yenye bendera yanayowaambia wananchi pisha apite. Huu ni unyanyasaji, ni uporaji wa mali ya umma," alisema Mpesya. Kwa mujibu wa Mbunge huyo, mwaka 2002 Baraza la Mawaziri liliamua kupitia Waraka Namba 7 wa mwaka huo ya kuwa nyumba za serikali wauziwe watumishi bila kuangalia bei ya soko na bei ya kiwanja. Hata hivyo, Dk. Mahanga alisema ni Waraka wa mwaka 2001.
 
Sasa naona Magufuli nae ajiuzulu, ingawa ufisadi wake si wa kuiba mabilioni, lakini adha yake kwa serekali ni kubwa.
Walimuuzia Mke wa Mangula Philipo ambaye hakuwa entitled officer, pili aliwapa Nduguze na Girl friend a Hse.
 
Hapa ndipo nachefuka sana na Magufuri ambaye ni mkono wa kulia wa MKAPA kwenye hili.

Yawezekana Magufuli alikuwa ni Bangusilo tu.Hapa najaribu kuwaza kama mwanadamu ambaye nawajibika kwa kiongozi mmoja mkuu tena mbabe,dikteta na ambaye maamuzi yote yanapitia mezani kwake.Isitoshe kutimiza wajibu wako wa kazi unaapa ofisi kwake na ndiye aliyekupa huo upendeleo na pia una wajibika kwake .Ukijitutumua kukaidi uamuzi ambao ametoa kukirimu rafiki zake anaokaa nao baa kwenye viti virefu,basi ni rahisi kula sumu au kukodishiwa majambawazi.

Ni Heri uwaziri nao wawe wanagombea tunawapigia kura,Na taasisi nyingine waachiwe wachague viongozi wao kwa utashi wao.Mkuu wa kaya aondolewe madaraka haya kuchagua Mawaziri,wakuu wilaya,wakurugenzi,jaji mkuu,mkuu wa majeshi,mkuu wa usalama wa Taifa,Mkuu wa polisi n.k
 
Nyumba za serikali zilizouzwa zarejeshwa
Mwandishi Wetu, Dodoma
Daily News; Friday,April 25, 2008 @21:01

WIZARA ya Maendeleo ya Miundombinu, imekiri kuwapo na kasoro zilizojitokeza kwenye mchakato wa uuzaji wa nyumba za serikali na tayari watu wanne waliouziwa nyumba kinyume cha taratibu wamezirudisha na saba zisizostahili kuuzwa pia zimerudishwa.

Naibu Waziri, Dk. Milton Mahanga aliyasema hayo bungeni jana wakati akichangia hoja binafsi ya Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), aliyoiwasilisha akitaka kurejeshwa kwa nyumba hizo kwa sababu ziliuzwa kinyume cha taratibu.

Katika kuchangia hoja hiyo, Dk. Mahanga alikiri kuwa kweli zilijitokeza kasoro kwenye mchakato wa kuuza nyumba hizo na Tume iliundwa na inaendelea na kazi. Kwa mujibu wa Mahanga, kuna watu ambao hawakustahili kuuziwa nyumba lakini wakauziwa. Tayari nyumba nne zimerudishwa.

Vile vile alisema kuna nyumba zisizostahili kuuzwa ziliuzwa na kwamba tayari saba zimesharudishwa na mchakato unaendelea. Pia alisema nyumba za Halmashauri hazikupaswa kuuzwa na 14 zimegundulika.

Katika maelezo kuhusu hoja yake iliyochangiwa na zaidi ya wabunge 14, Mbunge huyo wa Vunjo, aliiwakia Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kuuza nyumba za serikali. “Hapa Mheshimiwa Spika, Je, Serikali hiyo ya Awamu ya Tatu ilipouza hizo nyumba ilitegemea hapatakuwapo tena serikali nyingine na watumishi,” alihoji Kimaro.

Alisema haiwezekani nyumba ambayo ni rasilimali ya Taifa kwa Watanzania wote, ikauzwa kwa Sh milioni 15 badala ya Sh milioni 200 wakati wananchi wenye mali wakiambiwa wachange wajenge madarasa, nyumba za walimu na zahanati.

Aliitaka Wizara husika itoe orodha ya wafanyakazi wanaolipwa kwa kukosa nyumba baada ya zile za awali kuuzwa na ionyeshe ni kiasi gani cha fedha kinalipwa hotelini kwa kuwaweka watumishi waliokosa nyumba.

Wabunge walipitisha hoja ya nyumba za serikali zilizouzwa kinyume cha utaratibu, zirejeshwe kwenye umiliki wake huku baadhi wakishutumu hatua ya kuziuza kwa kile walichosema ziliwanufaisha viongozi.

Kutokana na hoja hiyo, Bunge limeazimia serikali itoe orodha ya nyumba zake ambazo ziliuzwa kwa watu ambao si watumishi wa serikali na pia zile ambazo hazikupaswa kuuzwa kutokana na unyeti wa kazi za watumishi wa serikali wanaostahili kuzitumia.

Pia limeazimia serikali ichukue hatua kwa wale ambao hawajalipia na mikataba yao ya kuuziwa irejewe kuhakikisha malipo hayo yanalipwa mara moja ama mikataba inafutwa na nyumba kurejeshwa serikalini.

Miongoni mwa wabunge waliochangia, wengi walielezea kukerwa kwao kwa kile walichosema asilimia kubwa ya waliouziwa ni viongozi na watu wenye fedha. Mbunge wa Bukene, Teddy Kasella-Bantu (CCM), alipendekeza waliouziwa nyumba hizo waongeze fedha kwa vile ziliuzwa kwa bei ndogo.

Mbunge huyo alipendekeza pia watu wasio watumishi wa serikali waliopewa nyumba, wazirudishe na hatua zichukuliwe dhidi ya walioidhinisha watu hao kupewa nyumba hizo.

“Hii ya kutoa nyumba kwa watu wasio watumishi ni rushwa. Zirudi serikalini na aliyeidhinisha achukuliwe hatua. Tuendelee kutoa chuya ili mwaka 2010 tupate mchele safi,” alisema Kasella-Bantu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya (CCM) alisema ugawaji huo wa nyumba unarudisha matabaka miongoni mwa wafanyakazi. Mpesya alisema wakubwa ndiyo walionufaika na hatua hiyo.

“Hawa ndiyo wenye magari yenye bendera yanayowaambia wananchi pisha apite. Huu ni unyanyasaji, ni uporaji wa mali ya umma,” alisema Mpesya. Kwa mujibu wa Mbunge huyo, mwaka 2002 Baraza la Mawaziri liliamua kupitia Waraka Namba 7 wa mwaka huo ya kuwa nyumba za serikali wauziwe watumishi bila kuangalia bei ya soko na bei ya kiwanja. Hata hivyo, Dk. Mahanga alisema ni Waraka wa mwaka 2001.


Interesting. Mbunge wa vunjo nafikiri anaelewa kuwa alipata kura chini ya 50% kwa sababu ya wapinzani kupigana vijembe kwa hiyo inabidi awajibike sana otherwise atakuja kukikosa kiti chake.

Cha kushangaza ni kuwa eti imeundwa Tume kuchunguza urudishwaji nyumba lakini ilishindikana kuunda tume kumchunguza Mkapa. Lipi linahitaji tume, hili la kupekua tu vitabu na kujua ipi iliuzwa bei poa na ipi mtendaji wake amepangishiwa au lile la Mkapa na Kiwira, Radargate au hata ile list of shame?
 
Bunge laridhia nyumba kurejeshwa

na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

BUNGE limepitisha azimio la kurejeshwa serikalini mara moja kwa nyumba zote zilizouzwa kinyume cha taratibu wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

Mbali ya hilo, Bunge limeiagiza serikali kutekeleza agizo la mwaka juzi lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete, la kurejeshwa kwa nyumba zote za walizouziwa watumishi wa umma ambazo ziko katika maeneo nyeti.

Bunge katika azimio lake hilo lililotokana na hoja binafsi ya Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), limeitaka serikali kuvunja mikataba ya kuwauzia nyumba wale wote walioshindwa kulipa kwa wakati malipo yanayotokana na uuzwaji huo wa nyumba, ambao kwa miaka mingi umesababisha manung'uniko mengi kutoka kwa wananchi mbalimbali.

Hoja hiyo binafsi ya Kimaro iliyosomwa bungeni juzi, iliamsha hisia za wabunge wengi, ambao takriban wote waliiunga mkono wakieleza namna uamuzi huo wa kuuzwa kwa nyumba za serikali uliofikiwa wakati John Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi.

Mbali ya wabunge hao kuunga mkono, serikali katika maelezo yake yaliyosomwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Miundombinu, Makongoro Mahanga iliunga mkono pia hoja hiyo ya Kimaro na kuahidi kutekeleza maamuzi ya Bunge.

Mahanga katika mchango wake alikiri kubainika kwa kasoro kadhaa katika uendeshaji wa zoezi zima la kuuzwa kwa nyumba hizo, na kwamba tayari nyumba zipatazo 25 zilikuwa zimewekwa katika orodha ya kurejeshwa.

Kwa mujibu wa Mahanga, Tume ya Rais ya kufuatilia uuzwaji wa nyumba hizo, imebaini kuwapo kwa nyumba saba katika maeneo nyeti ambazo zinapaswa kurejeshwa, wakati nyumba nne nyingine zilibainika kuuzwa kwa watu ambao hawakuwa watumishi wa umma wakati wakizinunua.

Mbali ya hilo, alisema nyumba nyingine 14 zilizokuwa mali ya halmashauri mbalimbali nchini ambazo ziliuzwa kwa makosa, nazo zimeshaainishwa tayari kurejeshwa.

Aidha, naibu waziri huyo alisema wanunuzi wengine 193 walikuwa wameshindwa kutekeleza makubaliano ya kimkataba ya kulipa madeni yaliyotokana na kununua kwao nyumba hizo, na tayari serikali ilikuwa imewapa hadi Mei 21, mwaka huu kulipa, vinginevyo nazo zitarejeshwa.

Mbali ya hilo, Mahanga alisema hadi hivi sasa, serikali ilikuwa imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 32 kutokana na mauzo ya nyumba zote 7,921 ilizoziuza kwa watumishi wake, huku kiasi kingine cha shilingi bilioni 27 kikiwa bado hakijarejeshwa.

Pamoja na kuuza nyumba hizo, Mahanga alisema hadi hivi sasa serikali bado inatakiwa kujenga nyumba za ziada zipatazo 339 nchi nzima kwa ajili ya watumishi wake.

Awali katika hoja yake binafsi, Kimaro alibainisha kuwa, mwaka 2002 Baraza la Mawaziri la kipindi hicho lilipitisha waraka namba 7 wa mwaka 2002 na kuridhia kuwa nyumba za serikali ziuzwe kwa watumishi bila kuangalia bei ya soko na bei ya kiwanja.

Alisema kutokana na waraka huo, Bunge lilitangaziwa Juni 2007 kuwa, jumla ya nyumba 7,921 zilikuwa zimeuzwa kwa gharama ya sh bilioni 59.1, ambapo mpaka wakati huo ni sh bilioni 29.1 tu ndizo zilikuwa zimekwishalipwa.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, nyumba hizo za serikali ziliuzwa bila kuwepo kwa nyumba nyingine kwa ajili ya watumishi wa serikali, na kuhoji iwapo serikali ya wakati huo haikujua kuwa kutakuwa na serikali nyingine tena na watumishi?

Katika hoja hiyo, pia Kimaro alibainisha kuwa bei ya nyumba hizo ilikuwa ndogo kulinganisha na thamani ya kwenye soko, jambo ambalo liliitia serikali hasara, na kutoa mfano wa nyumba yenye thamani ya sh milioni 200 ikiuwa kwa sh milioni 15.

Alisema inaonekana kuwa viongozi waliopendekeza kuuzwa kwa nyumba hizo, wao ndio walikuwa na mahitaji ya nyumba walizokuwa wakiishi, kwani hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kuwa, wafanyakazi wa wizara mbalimbali walituma maombi ya kuuziwa nyumba walizokuwa wakiishi.

Aliitaka serikali kutoa orodha ya watu wote waliouziwa nyumba na kubainisha maeneo zilipo, ili hatua zichukuliwe kwa kuanza na wizara, mikoa na baadaye wilaya.

Alisema ingawa rais alikwishatoa agizo kuhusu nyumba za serikali zilizouzwa kinyume cha utaratibu, na zile zilizouzwa kwa watu wasio watumishi wa serikali kwamba zirejeshwe serikalini, lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Bukene, Tedi Kassela–Bantu (CCM), alisema kuwa yeye anaiunga mkono hoja hiyo kwani wapo watumishi wengi wa serikali ambao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, bila kuwa na makazi wakati watu wasio watumishi wakiishi kwenye nyumba za serikali.

Mbunge huyo aliitaka serikali iwanyang'anye watu hao wasio watumishi wa serikali ambao waliuziwa nyumba na kutowarudishia fedha walizotoa wakati wa ununuzi kwani walikwenda kinyume cha sheria.

Alisema mbali na kuwanyang'anya watu hao nyumba, pia wanapaswa kubanwa na waeleze walizipataje ili wachukuliwe hatua za kisheria, kwani hiyo ni rushwa moja kwa moja.

"Hapa huwezi kusema kuwa hakukuwa na rushwa kwa kuwa haiwezekani mtu asiye mtumishi wa serikali auziwe nyumba ya serikali wakati wapo watumishi wa serikali wasio na nyumba," alisema mbunge huyo wa Bukene.

Pia aliishangaa serikali kuuza nyumba nzuri na za heshima zilizopo katika eneo la Kilimani mjini Dodoma na kwenda kujenga nyumba za bei nafuu na zisizoridhisha katika eneo la Kisasa mjini hapa, ambapo pia alisema mpaka sasa nyumba hizo za Kisasa zimelipiwa sh bilioni 4 kati ya sh bilioni 13 zilizopaswa kutolewa.

Naye mbunge wa Arusha Mjini, Felix Mrema (CCM), alipingana na hoja hiyo na kusema kwamba kuwanyang'anya nyumba watu hao si kuwatendea haki.

Alisema kuwa wapo watumishi wengi ambao kwa sasa wamestaafu na hawana kipato chochote, hivyo kwa kunyang'anywa nyumba hizo, watabaki bila makazi na kuendelea kuwa masikini kuliko walivyo sasa.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya (CCM), alisema kuwa zoezi hilo lilikuwa la upendeleo na lilifanywa na vigogo kwa manufaa yao binafsi, kwani maamuzi hayo hayakupitishwa na Bunge, na akasema ana hakika iko siku nyumba zote hizo zitarejeshwa.

Alisema kuwa hakukuwa na suala la utawala bora katika uuzaji wake, kwani nyumba za serikali ni mali ya Watanzania wote na si watu wachache kama wao walivyodhani.

Mbunge huyo alisema anaiunga mkono hoja hiyo na kuelezea masikitiko yake kuhusu kupuuzwa kwa Watanzania na rasilimali za nchi kutumiwa na watu wachache kwa manufaa yao, wakati wengine wakiwa hawana taarifa kuwa rasilimali za nchi zimeuzwa.

Mpesya alisema wakubwa ndio waliofaidika ingawa wanakaa kwenye nyumba zenye viyoyozi na magari, lakini waliona ni vema kidogo kilichopo cha Watanzania pia wanufaike nacho wao kisa walikuwepo madarakani jambo ambalo si sahihi.
 
Ahsante sana Kimaro, twashukuru wabunge
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

SISI wa Tanzania Daima, kama walivyo wananchi wengine kwa mamilioni wanaoipenda nchi yao, tuna kila sababu ya kushangilia ushindi tulioupata bungeni jana.


Hata hivyo, wakati tukishangilia ushindi huo, tuna kila sababu vile vile kwanza kumshukuru Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM) na wabunge takriban wote waliounga mkono hoja yake binafsi aliyoitoa bungeni juzi, kuhusu kurejeshwa kwa nyumba za serikali zilizouzwa kwa watumishi wa umma mwaka 2002.

Kwetu sisi wa Tanzania Daima, Kimaro ni shujaa wetu katika mapambano ambayo kimsingi tulishiriki kikamilifu kuyasimamia kwa dhati, na hata mara moja hatukupata kuyumba katika hili.

Kwa zaidi ya mara 12 kupitia katika tahariri ya gazeti hili, katika kipindi cha kati ya mwaka juzi, mwaka jana na mwaka huu pia, tuliandika bayana kwamba, msimamo wetu ulikuwa thabiti; kurejeshwa kwa nyumba zote zilizouzwa kwa watumishi wa umma kwa waraka namba 7 wa Baraza la Mawaziri la mwaka 2002.

Ni jambo la faraja kwamba, Kimaro alisikia kilio cha Watanzania, na akakisikia kilio chetu, hata akaamua kuandaa hoja binafsi, ambayo jana wabunge waliipitisha kwa azimio.

Kimaro katika hoja yake hiyo ambayo iliungwa mkono na wabunge takriban wote waliochangia kwa maandishi na kwa mdomo, ikiwamo serikali yenyewe, alieleza waziwazi kupinga uamuzi huo wa serikali.

Kwa hoja yake hiyo, Kimaro aliamsha hisia za wabunge wengi, ambao takriban wote waliiunga mkono, wakieleza namna uamuzi huo wa kuuzwa kwa nyumba za serikali uliofikiwa wakati John Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, ulivyofanywa pasipo kuzingatia maslahi ya taifa.

Katika hoja hiyo, pia Kimaro alibainisha kuwa bei ya nyumba hizo ilikuwa ndogo kulinganisha na thamani ya kwenye soko, jambo ambalo liliitia serikali hasara, na kutoa mfano wa nyumba yenye thamani ya sh milioni 200 ikiuzwa kwa sh milioni 15.

Alisema inaonekana kuwa viongozi waliopendekeza kuuzwa kwa nyumba hizo, wao ndio walikuwa na mahitaji ya nyumba walizokuwa wakiishi, kwani hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kuwa, wafanyakazi wa wizara mbalimbali walituma maombi ya kuuziwa nyumba walizokuwa wakiishi.

Aliitaka serikali kutoa orodha ya watu wote waliouziwa nyumba na kubainisha maeneo zilipo, ili hatua zichukuliwe kwa kuanza na wizara, mikoa na baadaye wilaya.

Alisema ingawa rais alikwishatoa agizo kuhusu nyumba za serikali zilizouzwa kinyume cha utaratibu, na zile zilizouzwa kwa watu wasio watumishi wa serikali, kwamba zirejeshwe serikalini, lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Alichokisema Kimaro kiliungwa mkono na wabunge wengi na Mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya katika hatua moja, aliwaonya wale walionunua nyumba hizo kukaa wakijua kuwa siku moja zote zitarejeshwa kwa wananchi.

Ingawa kauli hiyo ya Mpesya haikuingizwa katika azimio la Bunge ambalo kwa kiwango fulani limefanikisha kurejeshwa kwa baadhi tu ya nyumba, sisi wa Tanzania Daima, tunaamini kwa dhati kwamba, huo ni mwanzo tu wa mapambano haya ya kutaka kurejeshwa kwa nyumba zote, zilizokuwa za serikali.

Tunasema hivi kwa sababu ya msimamo wetu ulio bayana, na ambao tunafurahi kwamba umeonekana kuungwa mkono na wabunge wengi, wa kutambua kuwa uamuzi wa kuuza nyumba za serikali kwa watumishi ulifanywa si kwa maslahi ya taifa, bali kwa sababu ya ubinafsi usiomithilika wa viongozi wengi wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

Ni kwa kutambua hilo, ndiyo maana wakati tukimpongeza Kimaro na Bunge zima kwa ujasiri wa kuthubutu na kuweka mbele maslahi ya kweli ya taifa, tunapenda kusema bayana kwamba, hoja binafsi ya mbunge huyo ni mwanzo tu wa ngoma.
 
Yawezekana Magufuli alikuwa ni Bangusilo tu.Hapa najaribu kuwaza kama mwanadamu ambaye nawajibika kwa kiongozi mmoja mkuu tena mbabe,dikteta na ambaye maamuzi yote yanapitia mezani kwake.Isitoshe kutimiza wajibu wako wa kazi unaapa ofisi kwake na ndiye aliyekupa huo upendeleo na pia una wajibika kwake .Ukijitutumua kukaidi uamuzi ambao ametoa kukirimu rafiki zake anaokaa nao baa kwenye viti virefu,basi ni rahisi kula sumu au kukodishiwa majambawazi.

Ni Heri uwaziri nao wawe wanagombea tunawapigia kura,Na taasisi nyingine waachiwe wachague viongozi wao kwa utashi wao.Mkuu wa kaya aondolewe madaraka haya kuchagua Mawaziri,wakuu wilaya,wakurugenzi,jaji mkuu,mkuu wa majeshi,mkuu wa usalama wa Taifa,Mkuu wa polisi n.k

Hakuwa bangusilo alihusika na Msabaha alikuwa BANGUSILO na akatoka nae amfuate Msabaha.
 
Anybody who knows anything about real estate will tell you that the value of a house is its location.It is unbelivable that houses in the best location were sold for a song.There was absolute corruption involved in the sale of these houses,and even casual inquires leave alone investigations, will reveal that businessmen were sold goverment houses eg.Jango Master in Arusha
 
Katika vitu ambavyo vimewahi kunikera maishani, ni kuuzwa kwa nyumba za serikali OYSTERBAY. Walaaniwe wote waliohusika.Sisi tuliosoma sasa hivi tunaishi Tandale, na waliostaafu wanayakodisha kwa wazungu.
 
Hapa ndipo nachefuka sana na Magufuri ambaye ni mkono wa kulia wa MKAPA kwenye hili.

Hili lilikuwa dili la BWM na Magufuli hakuwa na jinsi isipokuwa kufuata upepo. Issue hii ilielezwa sana enzi za BCS.
 
Katika vitu ambavyo vimewahi kunikera maishani, ni kuuzwa kwa nyumba za serikali OYSTERBAY. Walaaniwe wote waliohusika.Sisi tuliosoma sasa hivi tunaishi Tandale, na waliostaafu wanayakodisha kwa wazungu.

Mwanakwetu, hata mie hilo linanikera sana. Tuombe Mungu tuje pata kiongozi atakayeamua kuzirejesha nyumba hizo Serikalini kwa nguvu ama kama atakuwa mstaarabu kidogo kwa kuwalipa fidia wale waliozi-renovate kama ambavyo wanalipwa fidia wananchi wanaohamishwa kwenye makazi yao kupisha ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege n.k. Haiwezekani akina 'Ndullu' watumie mabilioni ya fedha kujenga nyumba mpya wakati Oysterbay zilikuwepo nyumba ambazo zilijengwa na kukaliwa na Wazungu tunaowaiga kimaendeleo.
 
Hizi nyumba nina uhakika hazikugawiwa kwa upendeleo na ufisadi, maana hata mi shangazi yangu ( a very seniour civil servant) alipata hapo kinondoni. waacheni bwana wametumikia taifa kwa miaka zaidi ya 40, hawana kitu unafikiri wataenda wapi mkisema arudishe hiyo nyumba? tuwe na moyo wa huruma hasa kwa hawa watumishi watiifu wa taifa letu.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom