BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,006
Posted Date::4/22/2008
Rudisheni nyumba zote za serikali
Na Prof. Abdallah J. Saffari
Mwananchi
HABARI kubwa katika ukurasa wa mbele wa gazeti moja la kila siku, Aprili 5, 2008 ilisema, "Mjadala wa Nyumba za Serikali Waibuka Tena."
Ilielezwa kuwa mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), atatoa hoja binafsi katika kikao cha 11 cha Bunge kutaka watu ambao si wafanyakazi wa serikali ambao wameuziwa nyumba za serikali wanyang'anywe nyumba hizo. Nafikiri anataka wakishanyang'anywa wauziwe watumishi wa serikali badala ya kuzirejesha serikalini!
Mbunge pia alitaka kuwa baada ya hoja yake mjadala kuhusu nyumba hizo za serikali ufungwe rasmi. Anaogopa nini? Umma usiendelee kudai nyumba zao?
Kila viongozi duniani huweza kuteleza katika uamuzi na vitendo vyao.
Lakini kwa hakika kabisa wengi wanahisi uamuzi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na wenzake kuuza nyumba za watumishi wa serikali ni wa kidhalimu, kifisadi na umestaajabisha kupindukia. Ndiyo maana kila uchao magazeti huwa na barua au makala kupinga uamuzi huo hadi leo. Wanauliza, kwani ndio mwisho wa kuwa na watumishi wa serikali Tanzania?
Watu mashuhuri ambao wamepinga uamuzi huo ni pamoja na Herman Kirighini aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi na Nyumba katika serikali ya awamu ya pili na marehemu Prof. Thedeus Bugingo.
Gazeti jingine la kila siku, Machi 12, 2008, liliandika makala fupi thabiti aliyoiita, �Rais anza kurejesha nyumba yako serikalini.� Makala hiyo inaelezwa kuwa baada ya kujichukulia nyumba ya serikali iliyopo Sea View, Upanga, Dar es Salaam Rais mstaafu Mkapa aliwaruhusu wenzake wachukue nyumba walizokuwa wanakaa kuficha dhuluma hiyo. Nyumba nyingine zilikarabatiwa kwa mamilioni kabla ya kuuzwa kwa bei poa. Rais Kikwete naye akaambulia yake Mtaa wa Ursino, Ada Estate, Dar es Salaam ambayo hadi sasa hajairejesha serikalini.
Nyumba za watumishi wa serikali zilianza kujengwa na watawala wa Kijerumani na Waingereza. Chache ziliongezwa katika awamu ya kwanza ya utawala chini ya Mwalimu Nyerere. Ziko za daraja la tatu, pili na kwanza kulingana na nyadhifa za watumishi wa serikali. Nyumba hizo takriban sio chini ya 10,000 (elfu kumi) ziko maeneo mazuri sana mikoa yote Tanzania. Mashuhuri zaidi ni zile zilizopo Upanga na Oysterbay, Dar es Salaam.
Nyumba hizo zilijengwa jirani na ofisi za serikali kurahisisha usafiri. Na azma yake kubwa ni kuondoa kero ya makazi, gharama za kuwalipia kodi za kupanga na kuwavutia wafanyakazi ili wafikie ufanisi kiutendaji. Kila mtumishi wa serikali alisubiri kwa hamu siku ya kuhamia kwenye nyumba nzuri za serikali.
Hata siku moja Mwalimu Nyerere asingefikiria kuziuza nyumba hizo kwa yeyote yule. Na inasadikiwa kuwa mara mbili Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi akikataa wazo la kuziuza nyumba hizo. Ila Mkapa aliona sawa tu! Baada ya kujichukulia ile ya Sea View aliona bora asilaumiwe peke yake. Ndipo nyumba za serikali zikauzwa kwa mawaziri, majaji, makatibu wakuu, wakurugenzi, wakuu wa jeshi, polisi magereza n.k.
Yasemekana jaji mmoja alifanya sherehe kufurahia kuuziwa nyumba ya dezo! Kama walionufaika ndio hao, wananchi watalalamikia wapi? Kama viongozi wako mbele kukiuka katiba ya nchi (ibara 9 (c ) kupora mali ya umma, wananchi wende wapi? Hawawezi kupata haki kwa kupeleka madai ya kurejeshewa nyumba hizo mahakamani ambapo waamuzi wengi ndio wanufaika wakubwa wa ufisadi huo! Jaji mwingine mstaafu tayari ameipangisha nyumba yake, iliyoko kwenye mandhari nzuri ya bahari, kwa shirika la mawakili mashuhuri Dar es Salaam.
Sababu za kuuza nyumba hizo hazikuwekwa bayana. Inadaiwa eti ni kuwasaidia watumishi wa serikali kuwa na nyumba. Mara nyingine inasemekana eti ni mzigo kwa serikali kuzimiliki na kuzihudumia nyumba hizo. Hoja hizi zote ni chapwa kwa sababu watumishi waandamizi wengi walikuwa na nyumba zao au wangeweza kuwa nazo kutokana na vipato vyao au kwa mikopo. Kuthibitisha hilo ni kuwa nyumba nyingi tayari zimevunjwa kama pale kwenye kona ya Barabara ya Kaunda, Oysterbay, Dar es Salaam au karibu na Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.
Na wengine wengi waliouziwa wamezipangisha baada ya kustaafu na kuwakosesha wale warithi wa nyadhifa zao mahali pa kukaa. Kwa mfano Kamishna Mkuu wa zamani wa Magereza aliishia kukaa kwake, nje kabisa ya jiji, kwa vile nyumba aliyostahili kuhamia Oysterbay iliuzwa kwa Kamishna Mkuu aliyemtangulia.
Waajiriwa wengi wapya na wale wanaohamishwa hufikia mahotelini au kukodiwa nyumba binafsi kwa gharama ya zaidi ya laki tatu kwa siku au mamilioni ya fedha kwa mwezi (kwa nyumba nzima).
Pia sio kweli kwamba serikali ilikuwa inapata hasara kuzimiliki na kuzihudumia nyumba hizi. Baadhi yake zilihitaji matengenezo kidogo tu kama vile inavyokarabatiwa ofisi ya Kodi ya Mapato Mtaa wa Samora, Dar es Salaam. Kuna baadhi ya majengo mengi Dar es Salaam yamekarabatiwa vizuri tu kwa matumizi kama jengo la Halmashauri ya Jiji na Boma la Zamani Mtaa wa Sokoine, Dar es Salaam.
Kuhusu kujenga nyumba mpya inathibitisha dhahiri kwamba serikali ilikuwa na uwezo wa kuzikarabati nyumba zake kwani ilikuwa rahisi zaidi kufanya hivyo kuliko kujenga nyumba mpya. Kweli ni uroho tu wa kuzichukua nyumba zile na tamaa ya kuhodhi maeneo mazuri makubwa karibu na jiji.
Kwa kuishiwa na hoja za kutetea uamuzi wao John Pombe Magufuli, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi wakati huo alibaki kutoa kauli za vijembe na dharau. �Nyie mwaona wivu,� na �Mlie tu!
Inasemekana Serikali ya Awamu ya Tatu ilikusudia hata kuuza jengo la Wizara ya Ardhi ili ijengwe hoteli kwenye mandhari nzuri ya bandari. Jitihada zikaanzishwa makao makuu ya Wizara hiyo yajengwe Dodoma. Bahati tu wafanyakazi wazalendo wakafanya mbinu kuzorotesha utekelezaji wa ufisadi huo.
Ni katika awamu hiyo hiyo majengo ya ghorofa ya Shirika la Posta na Simu yaliuzwa kwa mtu binafsi. Wapangaji wa Shirika wakatupwa nje kama mbwa koko!
Kwa hiyo tunarejea tulipoanzia kwa kumueleza Mbunge Kimaro kuwa, Kama mvuvi vua, usichezee mashua.� Kwa bahati mbaya wabunge na hata viongozi wa upinzani wamekaa kimya muda wote mintarafu suala la kuporwa kwa nyumba za serikali.
Hoja iliyopo sio kurejesha nyumba zilizouzwa kwa watu ambao sio watumishi wa serikali. Kwani kwa kufanya hivyo zitauzwa tena kwa watumishi wa serikali wateule.
Kama kweli mbunge ni mzalendo basi adai nyumba zote za serikali zilizouzwa zirejeshwe serikalini. Waliouziwa warejeshewe fedha zao. Vinginevyo dhoruba ya umma itazirejesha nyumba hizo, kama si leo, basi kesho! Hakuna haja ya kuunda Tume kuhusu jambo hili, ambayo itapoteza muda na fedha za umma.
Profesa Abdallah Safari ni Profesa wa Sheria na Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania