HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA, MHESHIMIWA CHARLES N. KEENJA (MB.), KUHUSU MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA KWA MWAKA WA 2004/2005
IV. HUDUMA ZA USHAURI WA KITAALAM
51. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo na Chakula kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imeendelea kuwapatia wakulima teknolojia bora za uzalishaji ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji na tija. Katika mwaka wa 2003/2004, mkazo uliwekwa katika matumizi ya mbinu shirikishi jamii ili kuibua matatizo na kuainisha mikakati ya kuongeza tija na uzalishaji. Jumla ya shilingi milioni 167 zilitolewa na kutumika kuanzisha mashamba darasa 267 katika wilaya 41 ambazo ni Iringa, Arumeru, Mbulu, Babati, Kibaha, Bagamoyo, Temeke, Dodoma, Njombe, Bukoba, Ngara, Kasulu, Hai, Kilwa, Musoma, Serengeti, Bunda, Rungwe, Mbeya, Ulanga, Singida, Mtwara, Ukerewe, Sengerema, Magu, Mpanda, Songea, Mbinga, Shinyanga, Kahama, Igunga, Urambo, Korogwe, Lushoto, Sumbawanga, Morogoro, Kongwa, Tabora, Mpwapwa, Arusha Mjini, na Muheza. Wataalam 121, pamoja na wakuu wa wilaya 24 kutoka wilaya za mikoa ya Mara, Kigoma, Tabora, Morogoro, Pwani na Dodoma walifanya ziara za mafunzo ya wiki moja moja mkoani Singida kujifunza mbinu shirikishi jamii. Aidha, vipindi 52 vya mafunzo ya kilimo bora cha mazao na matokeo ya utafiti wa kilimo na ufugaji bora viliandaliwa na kutangazwa na Redio Tanzania. Wizara pia iliandaa mada tatu za video kuhusu kilimo cha paprika na vanila.