SIMANZI
Godwin Frimin Massawe umeondoka katika Dunia hii lakini Tutakukumbuka na Tutakuombea.Mwanangu Godwin naamini Upo kwa Mungu unatuombea zaidi kwa jinsi kifo chako kilivyotokea. Sijawahi kusikia kifo cha aina hii zaidi ya kusoma kwenye vitabu vya maisha ya watakatifu. Godiwin alihitimu Kisale secondary 2012,shule ipo mkoani Kilimanjaro wilaya ya Rombo.Alipenda kuishi maisha ya sala,kusoma bibilia kila mara na alifika mahali akasema hakuna anachokitafuta duniani zaidi ya kuishi maisha yatakayomuongoza kufika mbinguni kwa kusoma na kufuata maandiko matakatifu ya bibilia.
Alienda kufanya kazi na Wilvic labour solution kama data entry. Lakin siku moja aliamua kuacha kazi akarudi nyumbani. Alipoulizwa kwa nn alisema "anafanya kazi masaa mengii mnoo mpaka anakosa muda wa kwenda kwenye ibada,kusoma bibilia na kufanya tafakar" aliendelea kusema "kuliko niendelee na kazi ambayo inaniweka mbali na Mungu halafu nikafa naiacha bora niache nikamtumikie Mungu" Akamwambia baba yake nataka kwenda kujiunga na mabrother niwe nasali mda wote. Akapelekwa.Lakini siku moja akarudi nyumban.
Alipoulizwa akasema kule nilifikiri ni sehemu ya kusali, kuimba na kusoma bibilia mda wote kumbe hapana. Bora nirudi nifanye mda wangu wote wa sala. Siku ya jumapili alienda kanisani na hakurudi nyumbani Alitafutwa kila mahali hakupatkana,Taarifa zilipelekwa mpaka kanisan na kituo cha polisi, Ni mwezi sasa umepita.
Jana taarifa za wazee wanaopasua mbao katikati ya msitu zikasema kuna mtu ameonekana alifariki muda mrefu na ana bibilia. Taarifa zilipotufikia basi baba yake anaondoka na polisi leo kuelekea msituni wakiongozwa na wale wazee wapasua mbao.
Msitu upo Kule katangara,mwisho wa watu kuishi unaingia ndani mwendo wa masaa manne. Kuna barid kali sana na wanyama wakali pia. Ndipo wakamkuta Godiwin amepiga magoti kwenye gogo, akiwa na Rozary yake shingoni na biblia ipo chini imefunguliwa kitabu cha SIRA. Godiwin ameshaoza amebaki mifupa tuu na hatoi harufu yoyote. Amevalia nguo zake vilevile. Godiwin alienda msituni kufunga na kusali mpaka akafariki.
Polisi na baba yake wakamchukua na kumpeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti kule Huruma hospital.
Taratibu za mazishi zinaendelea.Godiwin aliamua kujitoa kutuombea na kusali na Mungu aliamua tunapomtafuta tusimkute mpaka mapenz yake yatimie.Basi ni majonzi kwa familia na wazazi na wahitimu na wanafunzi wa kisale secondary, wananchi wote wa mashati rombo,kanisa Katoliki na watanzania wote kwa ujumla.
Tumuombee Godwin wakati huu akiwa na malaika na watakatifu mbinguni makao ya kusali na kumsifu Mungu milele yote.
------------------
Mwili wa kijana mwenye umri wa miaka 25 umepatikana katika msitu wa Katangara chini yake kukiwa na Biblia, huku ukiwa umevaa rozari shingoni na umepiga magoti.
Kijana huyo, Godwin Massawe, mkazi wa Kijiji cha Msaranga wilayani Rombo ambaye alitoweka Jumapili ya Januari 20 baada ya kuaga kuwa anakwenda kanisani, mwili wake ulikutwa porini Machi Mosi.
Baba mzazi wa kijana huyo, Frimin Massawe aliliambia Mwananchi jana kuwa, baada ya mwanaye kutoweka alitoa taarifa polisi na kanisani ili asaidiwe kupatikana kwake.
“Tulipeleka taarifa polisi mpaka kanisani, lakini hatukufanikiwa. Jana (juzi) nililetewa taarifa na wazee wanaopasua mbao katikati ya msitu (wa Katangara) wakasema kuna mtu ameonekana amefariki (dunia) muda mrefu,” alisema Massawe.
Alisema watu hao walimweleza kuwa marehemu amepiga magoti akiwa na Biblia huku amevaa rozari, ndipo alipoongozana nao kwenda polisi na baadaye msituni.
“Tukafika hadi Katangara na kuingia ndani (ya msitu) mwendo wa saa nne. Kule kulikuwa na baridi kali sana na wanyama wakali, lakini bado niliona maajabu ya Mungu.”
Alisema, “Huwezi amini nilimkuta mwanangu Godwin amepiga magoti kwenye gogo akiwa na rozari yake shingoni na Biblia ipo chini imefunguliwa kitabu cha Joshua huku akiwa ameoza.”
Mzazi huyo alisema mabaki ya mwili huo yalikuwa hayatoi harufu, jambo alilodai kuwa ni ‘muujiza’.
Baba mdogo wa marehemu, Simon Massawe alisema tukio hilo limewashangaza na kama familia wameumia kwa kuwa kijana wao alikuwa mtu wa maombi muda mwingi.
“Sisi kama familia tumelipokea kwa huzuni kubwa, hatukutegemea kumkuta amekufa. Ila kama amekufa kiimani let it be (acha iwe hivyo),” alisema.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah alisema mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma iliyopo wilayani Rombo.
Mwananchi