*UNA NINI LAKINI MELISSA? – 03*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Basi Melissa akajivalia nguoze na kisha akaelekea stoo. Huko akateka chepe na kutoka ndani ya nyumba kisha akaelekea moja kwa moja kule mashariki ya mbali kukuta kaburi la Cecilia Goodwin, bibi yake Darren.
Hapo kabla hajafanya chochote akaita kwa kunong’oneza, “Tabitha!”
Kisha akaanza kuchimba kaburi.
ENDELEA
Akafukua kwanguvu ya ajabu. Alipumzika takribani mara mbili kwenye zoezi lake hilo kabla hajalimalizia kabisa. Akakuta jeneza kubwa ambalo alilitengua na chepe lake kisha akaliweka wazi.
Humo ndani yake akaukuta mwili wa Cecilia. Ulikuwa unaelekea kuharibika sasa, mikono yake imejifumbata kifuani. Akaukunjua na kisha akauketisha kitako na kusemezana nao!
Namna gani mtu aongea na wafu?
Melissa aliupiga mwili ule kofi dogo kisha akaita, “Tabitha! Tabitha! Tabitha!” mara tatu, na mara mwili ukafungua macho. Macho yaliyokuwa na rangi nyekundu kana kwamba uji wa volkani!
“Tabitha …” Melissa akasema kwa kunong’ona. “Kwanini lakini?” kisha akauliza.
“Kwanini lakini?” Akarudia tena. Saa hii macho yake yakiwa yanalenga machozi. “Nilidhani wewe utakuwa wa tofauti, Cecilia. Nilikuwa nimekosea kukuamini hivyo?”
Mwili ule ambao umefungua macho haukunena kitu. Uliendelea kumtazama Melissa ambaye alikuwa akiutazama na kuuliza kwa tija. Mwishowe Melissa alipomaliza kusema aliyokuwa anahitaji, akaurudisha mwili huo ndani ya jeneza lake, lakini kabla hajaufungia, mwili huo ukamshika mkono kwanguvu!
Ukafungua kinywa kutaka kusema jambo lakini mdomoni ukaishia kutoka upepo tu. Hakuna lililosikika. Melissa akiwa analia, akautazama. Napo asiseme tena kitu, akaenda zake. Na pasipo kurudishia kifusi alichokichotea nje, akaenda zake kumkuta Darren ndani ya nyumba.
Akanyookea bafuni na kukoga kisha akarejea sebuleni ambapo bado Darren alikuwa amejilaza. Akaketi pembeni yake alafu akalaza kichwa chake kochini akiwaza sana. Alishindwa kujizuia kutoa machozi. Kila alipoyafuta yakamiminika zaidi na zaidi. Mwisho wa siku akayaacha yamiminike kama mto.
Yakamwagikia Darren na kumwamsha. Darren akamtazama kwa kuduwaa. “Melissa, haujalala?”
Melissa hakujibu. Aliendelea kumwaga machozi. Basi Darren kwa kuguswa na moyo wa huruma, akamfariji mpenzi wake akitaka kujua ni nini kinamliza. Lakini Melissa hakuwa tayari kunena. Na kadiri Darren alipokuwa anamuuliza, akawa anapandwa na hasira.
Hatimaye alimkaba Darren na kumnyanyua juu kama sufi! Darren akapapatika akirusharusha miguu. Melissa akambamizia ukutani na kusema akiwa amefuma uso wake kwa hasira, “Nitakuua, Darren!” akarudia tena, “Nitakuua, Darren!”
Darren akatoa macho akikosa hewa. Akiwa anaelekea kujikatia roho, Melissa akambamizia kichwa ukutani, mwanaume huyo akazirai! Akamwacha aangukie chini na kisha yeye akarejea pale kitini. Akakaa hapo akiendelea kuwaza.
Akiendelea kumwaga machozi.
**
Ngo! Ngo! Ngo! Ngo! Darren alisikia sauti hiyo kwa mbali. Kichwa kilikuwa kinamuuma na bado hakuwa amefumbua macho. Macho yalikuwa mazito sana lakini akajitahidi kupandisha kope.
Alipotazama akajiona yupo sebuleni, na zaidi akiwa ameegemea ukuta. Kiuno chamuuma na pia kichwa. Kiuno ni kwasababu ya kukaa muda mrefu.
Akastaajabu akiangazaangaza. Hodi ikabishwa tena. Basi akasimama na kusonga mlangoni, hapo akakutana na mzee mmoja aliyevalia kofia ya ‘cowboy’ na overall ya jeans, mkononi amebebelea reki.
Mzee huyo mwenye sauti kavu, akasema, “Wewe kijana, ni wewe ndiye umefukua kaburi kule?”
Darren akatahamaki mzee huyo akimweleza kuwa kaburi lipo wazi. Pasipo kupoteza muda, wakaongozana mpaka huko na Darren akakuta kweli kaburi li wazi mpaka jenezani!
Akazama ndani ya shimo na kutazama jeneza. Lilikuwa limetenguliwa. Akahofia pengine itakuwa kuna vitu vimeibwa humo ndani. Basi akalifungua jeneza na kutazama mwili. Ulikuwa sawia ila macho yakiwa wazi. Akatahamaki.
Ni nini kinatokea hapa?
“Kijana ni nini kinaendelea?” akauliza yule mzee aliyekuja kumshtua Darren. Naue Darren hakuwa na jibu kwani hakuwa anajua lolote lile. Basi kwa kushirikiana na yule mzee wakafukia tena lile kaburi na alivyoenda kule ndani akampasha habari hizo Melissa. Melissa akaigiza kushtushwa.
“Inawezekanaje?”
“Sijui. Ni ajabu! Nadhani mahali hapa hapatakuwa salama tukienda. Napata mashaka sasa,” alisema Darren akiketi kitini. Akafikiria kwa muda kidogo kabla Melissa hajamkalia mapajani na kumtazama kimahaba.
“Unaonaje tukaendelea kukaa hapa kwa muda mpenzi?”
“Melissa, wewe ni mzima kweli? Vipi kazini?”
Melissa akaguna. “Kwani kazini kwenu hamna kuumwa?”
“Sijatoa taarifa hiyo!”
“Kwani hamna wanaoumwa ghafla, Darren?” Melissa akanong’oneza. Darren akasisimkwa na mwili. “Lakini Melissa …”
“Lakini kitu gani mpenzi?” Melissa akauliza akikata kiuno chake kwa mbali.
“Ni hatari!” Darren akashukiwa.
“Hatari lakini salama,” Melissa akamwambia kwa sauti laini kisha akambusu mdomoni. “Nataka kukaa na wewe zaidi Darren. Hamna mahali nitakapokuwa huru na wewe kama hapa. Hutaki hilo, mpenzi?”
“Unajua nataka lakini mazingira mpenzi yana--”
Melissa akakamata mdomo wa Darren na kuunyonya. Alishajua amefanikiwa kumteka mwanaume huyo, hatakiwi kuongea zaidi. Akamchezea mpaka alipoona yeye kuwa inatosha sasa.
Lakini baadae, ikiwa ni kwenye majira ya saa saba usiku, Darren anashtuka kitandani na kujikuta yu peke yake. Anatazama kushoto na kulia pasipo kumwona mtu aletoka kulala naye. Anastaajabu! Anapatwa na hofu.
Akatoka kitandani na kuangaza sebuleni, hamna mtu. Akaangaza chumba cha kwanza, napo hakuambulia jambo. Ila akiwa humo anasikia sauti ya kitu kikigongwa kwa taratibu … Tih! Tih! Tih!
Anafuatisha masikio yake ajue wapi sauti hiyo inatokea, mwishowe anajikuta ndani ya chumba cha tatu. Ila anapofika humo, sauti hiyo hukata. Anatazama kila kona ya chumba hiko pasipo kuona lolote la kutia shaka.
Hatambui nini kinaendelea.
Anajaribu kuita kwa taratibu, “Melissa!” na mara umeme unazima anakuwa kizani. Inachukua kama sekunde mbili tu, umeme unarudi! Darren anapotazama mlangoni, anauona mlango ukiwa wazi, unacheza kwenda mbele na nyuma!
Moyo wake ukapiga kwa hofu. Akapiga moyo konde na kuufuata, kisha akachungulia huko nje. Hakuona jambo nyuma yake, lakini mbele yake, alipotazama vema, akaona kutakuwa na mtu huko. Kule sebuleni kulikuwa na mwanga aliouhisi ni wa runinga. Lakini kama hiyo haitoshi, aliona pia na kivuli cha mtu!
Akaita, “Melissa!” na kuuliza, “ni wewe?”
Ajabu kile kivuli kikaanza kucheza kikizungusha kichwa chake kushoto na kulia, kulia na kushoto kana kwamba mwehu!
“Melissa!” Darren akaita tena. Saa hii sauti yake ilikuwa inatikisika. Alikuwa amejawa na mashaka zaidi. Mashaka juu ya Melissa. Mashaka juu ya roho yake!
Basi hakuwa na namna. Alijivika uanaume akasonga mbele japo kwa hatua za kusita. Alipojivuta mpaka sebuleni na kuchungulia, hakuona kitu! Alipotazama kile kivuli ndipo akajua kinatokea kwenye mwanga wa nje, mwanga upenyao dirishani!
Akatazama huko dirishani, akamwona mtu ambaye kabla hajamtambua, upesi akatoka mwangani na kujificha!
“Ni nani wewe?” Darren akauliza akijitahidi kukaza sauti. “Ni nani wewe, jitokeze kabla sijakufyatulia risasi!” akatishia lakini isisaidie kitu. Hakuna mtu aliyejitokeza wala kunena na yeye.
Basi akaenda stoo upesi na kuchukua fyekeo. Akiwa amelishika vema mkononi, akafungua mlango na kwenda nje. Akaita, “Melissa!” kimya. “Melissa!” kimya.
Akaizunguka nyumba nzima lakini hakuona kitu. Akiwa amerudi pale pale dirishani, akaona kivuli tena, mara hii kikiwa kinatokea ndani na si nje kama ilivyokuwa hapo awali! Kivuli hicho kikiwa ni matokeo ya kuhakisiwa kwa mwanga wa runinga.
Basi haraka Darren akatazama ndani, lakini napo akiwa bado hajamwona mtu huyo vema, akapotelea koridoni!
Basi upesi akakimbilia ndani. Akatazama kushoto na kulia, hakumwona mtu. Akatazama koridoni, napo hakumwona mtu. Akahisi mtu huyo atakuwa ameenda vyumbani, basi akaanza kusonga kwenda huko. Chumba cha kwanza akafungua na kutupa macho. Hamna mtu!
Chumba cha pili aliposhika mlango tu, runinga ikazimwa sebuleni! Alirusha macho yake akaona ni kiza huko. Moyo wake ukaruka pigo. Akahisi sasa anapoteza nguvu mwilini.
Hajakaa vema, akahisi uzito machoni, mara kidogo akapotezaa fahamu akidondoka kama furushi!
Alipokuja kupata fahamu, kwa mbali, akajiona yu ndani ya shimo. Na kwa juu kuna mtu mwenye chepeo akimwagia mchanga humo shimoni! Akimwaga kifusi kwa kifusi!
**
Sent using
Jamii Forums mobile app