Riwaya: Una nini Melissa?

Riwaya: Una nini Melissa?

SteveMollel

JF-Expert Member
Joined
Jul 12, 2015
Posts
8,803
Reaction score
25,449
Habari zenu, nimekuja tena ndugu yenu kwenye riwaya hii fupi ya UNA NINI MELISSA? Nashukuru kwa wale wote waniungao mkono, wajuazo raha zilizo ndani ya story tamu. Haya sasa tufunge mkanda tuanze.

Kwa wale wajawa na hofu za mapema, mkae mbali ati. Msije sema hamkuonywa. Natamani niwatag wote lakini siwezi, kwa wale niwakumbukao basi mtaita na wengine Madame S Shunie Tumosa koncho77 Ilankunda1234
 
*UNA NINI LAKINI MELISSA?


*Simulizi za series*


Darren alipotazama saa yake ya mkononi akatambua wazi kuwa amekawia. Akasonya akijivuta toka kwenye kitanda. Ilikuwa ni saa tatu asubuhi na alitakiwa kufunga safari mnamo saa kumi na mbili asubuhi. Tafakari. Haraka akaelekea bafuni kukoga na asipake mafuta wala kuchana nywele, akavaa na kujiondokea kwenda kituoni akapande basi.

Alipofika huko, akalazimika kusubiri kwa lisaa limoja kabla hajapata basi analotakiwa kulipanda. Alipolikwea, akaenda nyuma kabisa ya basi na kuketi akilaza kichwa chake dirishani, basi ule usingizi alioukatiza, ukamsomba tena na kumfanya alale fofofo mpaka kuchuruza mate.

Akalala kwa lisaa limoja kabla hajashtuliwa na simu yake mfukoni. Simu ilikuwa inatetemeka na kutoa sauti kwa pamoja. Akaichomoa na kuitazama akiwa amefichama macho yake kama mtu aliyemulikwa na mwanga mkali usoni. Akaona ni Melissa kiooni! Melissa mpenzi wake.

Kabla hajapokea, akasafisha koo lake na kufanya zoezi la kuzungumza asigundulikane ametoka kulala, kisha,

“Melissa …”

“Umelala, Darren?” Ilikuwa ni kauli ya kwanza toka kwa mwanamke huyo. Japo Darren alijitahidi kuficha, bado haikusaidia. Ikambidi tu atabasamu.

“Sijalala, Melissa.”

“Mbona sauti yako kama ya mtu aliyetoka kulala?”

“Masikio yako tu. Mimi niko kwenye basi sasa, hausikii?”

“Unaenda wapi, Darren?”

“Kwa bibi!”

“Mbona hukunambia?”

Darren akapiga kofi paji lake la uso. “Nilisahau, Melissa. Nisamehe.”

“Unarudi lini?”

“Nadhani keshokutwa. Sitakaa sana huko.”

“Keshokutwa ndo’ hutokaa?”

“Melissa, ni baada ya siku moja tu ambayo ni kesho. Kuna umbali gani hapo?”

Kukawa kimya kidogo. Sauti ya Melissa ikaguna alafu ikasema, “Sawa. Safari njema, Darren!”

“Ahsante, mpenzi.” Darren akakata simu na kuegesha kichwa chake dirishani ila mara hii hakulala tena bali akitazama yanayoendelea huko nje ya basi. Angalau usingizi ulikuwa umekwisha japo bado macho ni mazito. Alipiga mihayo mara kadhaa hapa na pale.

Basi kichwani mwake, kwa kukosa cha kufanya, akaanza kuwaza mambo kadhaa, haswa ya huko anapoelekea. Huko kijijini, countryside, kutembelea nyumba ya marehemu bibi yake.

Kichwani mwake akapata kuona picha ya bibi yake kipindi yu hai. Namna alivyokuwa mcheshi na mchangamfu lakini pia mkarimu. Akajikuta akitikisa kichwa kwa masikitiko. Hakika atamkumbuka sana. Na pengo lake ni wazi litaonekana. Alikuwa anawapa sababu ya wao kutembelea kijijini lakini hivi baada ya kifo chake, hakutakuwa na safari hiyo tena, aliwaza Darren. Hata wazazi wake wameshakaa na kuamua kuwa nyumba hiyo ya marehemu iuzwe.

Hakupenda hilo lakini hakuwa na namna. Hakujua ni nini wazazi wake waliwaza kichwani mpaka kufikia maamuzi hayo, ila kwa uono wake yalikuwa ni maamuzi ya kipumbavu. Ya kipumbavu sana!

Akajikuta akisonya mwenyewe na kutikisa kichwa. Akasonya tena na kutikisa kichwa kabla hajaamua kuachana na mawazo hayo na kupekua simu yake kubwa. Akapekua ghala lake la picha na video kisha akazama mtandaoni

Kwa umbo, Darren alikuwa ni kijana mrefu mwenye mwili uliojengeka vema. Nywele zake nyeusi, uso wake mrefu, macho yake yamechongoka kana kwamba ya nyoka, lips zake nyembamba na kidevu chake chembamba kimefunikwa na ndevu.

Ni mtaalamu wa mifugo, Veterinarian ama vet kwa ufupi. Lakini mbali na kazi yake hiyo hobby yake kubwa ni kuogelea. Ila mara kadhaa apatapo muda hupenda pia kusoma vitabu na kuangalia tamthilia.

Kwakuwa alikuwa tayari ana kazi yake na umri wake, 25, ulikuwa unamruhusu kutoka nyumbani, basi alifanya hivyo. Alipanga katika jiji la California, ambapo palikuwa karibu na eneo lake la kazi, lakini pia karibu na mpenzi wake Melissa.

Melissa, mwanamke mwembamba chotara wa kilatini na kizungu, alikuwa ni mfanyakazi katika supermarket moja ndani ya jiji la California. Alikuwa ni mwanamke mzuri haswa. Macho yake yangekufanya uzame mtaroni ukimtazama. Tabasamu lake lingekufanya usahau kumdai ulichomkopa.

Nywele zake ni laini kama hariri ya sufi. Cheko lake ni kama ndege wa asubuhi huko msituni. Mwendo wake ni wa madaha akiona huruma kukanyaga ardhi. Na zaidi umbo lake, aliloliteka toka kwa mama yake mlatini, lingekufanya ukawa mdhaifu wa maungio ya mwili. Si kwamba alikuwa na umbo kubwa, hapana! Ila mwanamke ambaye kila kiungo chake kimekaa pahala pake, na si kuparamiana.

Kila kitu kilikuwa ‘balanced’. Mungu alitenda. Na huenda wewe ungemwona mwanamke wa kawaida, tena sana, ila kwa Darren, huyu alikuwa ndiye alfa na omega. Hakuwahi kumwona mwanamke kama huyu.

Kila anapomtia machoni lazima ahisi vinyweleo vyake vimesimama, moyo wake unaruka pigo, na mate yanamkauka mdomoni! Anamwona kila siku lakini bado hajamzoea. Na kama ukimuuliza nini lengo lake maishani, basi atakwambia la kwanza ni kumwoa Melissa. La pili ni kumwoa Melissa na la tatu ni kumwoa Melissa!

Lakini kuna kitu hajafahamu kuhusu Melissa. Na kuna kitu pia hajafahamu kujihusu yeye pia. Hawezi kumwoa Melissa. Na Melissa hawezi kuolewa na yeye. Huenda jambo hili likawa ni gumu sana kwa Darren, ila ndiyo uhalisia wenyewe.

Pengine mtu angekuja na kumwambia hilo angemwona ni adui, na angempa ushahidi wa mahusiano yao yaliyodumu kwa miaka miwili. Lakini bado isingetosha kupinga ukweli. Watu hawa hawawezi kuwa pamoja! Si ardhini, majini ama hewani.

Ninayekuambia haya naitwa Byron. Si mtu wa maana sana ila ni muhimu ukalishika jina langu kwa manufaa ya huko mbeleni. Na vipi kuhusu mwonekano wangu? … Mimi ni mwanaume mwenye miaka sabini na nane. Kichwani nimejawa na mvi. Mkononi mwangu nabebelea fimbo ya kunisaidia kutembea maana miguu yangu imechoka na mwili wangu umevikwa joho rangi ya kahawia.

Hayo yanakutosha. Mengine utayajua kadiri na muda.

Baada ya kuchoma masaa matatu njiani, Darren alishuka toka kwenye basi na kuanza kujongea upande wake wa kaskazini. Alipotembea kwa takribani dakika kumi, akawa amefika mbele ya nyumba zee ya marehemu bibi yake. Hapo alikuwa ana kazi moja tu ya kufanya, nayo ni kusafisha nyumba hiyo ipasavyo.

Nyumba hii ilikuwa na vyumba viwili tu, ila uwanja wake wa nje ndiyo mpana. Hivyo basi Darren akaona ni stara akaanza kusafisha nje kwanza, alafu huko ndani, hamna shida, atapafanyia kazi ambayo alifahamu fika haitamchukua zaidi ya lisaa.

Akateka fyekeo na jembe. Akavuja jasho kwa muda wa masaa matatu kabla hajawa hoi na kwenda ndani kuoga, kula na kupumzika. Kesho yake akamalizia huko nje, na keshokutwa yake, akawa anahusika na ndani tu. Akapasafisha kwa kufyagia na kudeki.

Akiwa anasafisha chumba cha bibi yake, ndipo akakutana na picha kadhaa za zamani. Katika picha hizo, akamwona bibi na babu yake wakiwa vijana, pamoja pia na mama yake angali mdogo. Akafurahi sana. Akaketi kitandani akiendelea kuangalia picha hizo.

Lakini katika moja ya picha hizo, kuna ambayo ilimshangaza Darren. Kulikuwa na watu wanne pichani wote wakiwa ni mabinti. Binti mmoja alimtambua kuwa ni bibi yake, wa pili hakumtambua kabisa, wa tatu pia, ila wa nne alimtambua baada ya kumtazama vema, lakini hakuamini.

Binti huyo wa nne alikuwa ni Melissa!

“Hapana,” akajisemea mwenyewe akitikisa kichwa. Akaigeuza picha na kuitazama kwa nyuma, ilikuwa imeandikwa mwaka kwa peni, mwaka 1956! Darren akatahamaki.

Akafikicha macho yake na kuangaza tena. Hakuna kilichobadilika. Melissa alikuwa pichwani! Picha moja na bibi yake wakiwa ujanani.

Darren Akadhani amewehuka.

**



Sent using Jamii Forums mobile app
 
*UNA NINI LAKINI MELISSA? -- 02*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA
Mama akatoa macho kwa mshangao. “Hapana!” akakanusha akitikisa kichwa. “Hapana, mpenzi. Ni hatari!”

“Huoni ni hatari akiendelea kutokujua?” Baba akauliza. Mama akatazama chini akiwa na sura ilonywea. Alikuwa anahofia.

Alikuwa anatakiwa kuhofia.

ENDELEA
Hakusema jambo mpaka pale Baba alipomshika bega na kumwambia kwa upole, “nikamwambie? Niruhusu nifanye hivyo!”
Mama akatikisa kichwa. “Hapana, Gerald. Si muda sahihi hivi sasa. Ni mapema sana. Tungoje kidogo tafadhali.”
Baba akamtazama asiseme jambo bali kushusha pumzi ndefu puani na kisha akajiendea zake ajiandae kuoga. Muda si mrefu, Darren akaaga anakwenda. Mama akamwomba sana ile picha ya Bibi lakini Darren akagoma kumpatia. Kwa kumpoza akamwambia kuwa atamrudishia kesho kutwa yake.
“Nakuahidi mama,” Darren akaapa kabla hajaenda zake. Alinyookea nyumbani kwake kisha akampigia simu Melissa akimwomba aje nyumbani kwake kwani kuna dharura.
Kama baada ya lisaa, Melissa akawa amefika hapo. Alikuwa amevalia topu nyeupe na jeans nyeusi. Alipendeza. Tuseme hata akivalia gunia mwanamke huyu hupendeza kutokana na umbo na uzuri wake.
Akamkumbatia Darren na kisha akamjulia hali kwa tabasamu pana. Lakini akafanikiwa kuona jambo usoni mwa Darren. Mwanaume huyo hakuwa sawa.
“Kuna tatizo Darren?” akauliza kwa sauti yake ya chini.
Darren ndipo akatoa picha ile, picha ya Bibi yake na wale wenza, na kumwonyeshea Melissa. “Melissa huyu ni wewe?”
Kwa mwanzoni Melissa akapigwa na butwaa. Mtu alikuwa akifanana naye vilivyo. Ilikuwa ni ajabu. Akachukua kama dakika mbili akitazama picha ile kisha akamuuliza Darren, “umetoa wapi picha hii?”
“Kwa Bibi yangu,” Darren akajibu. “Yule niliyekuambia kumhusu.”
“Yule marehemu?” Melissa akauliza upesi. Brian akatikisa kichwa. “ Ndiye huyo huyo!”
“Na yeye ni yupi kati ya hawa?”
“Huyu hapa!” Darren akaonyeshea kwa kidole. “Hapa ni mnamo miaka ya alfu moja mia tisa na hamsini!”
Melissa akaendelea kuitazama ile picha kana kwamba mtu anayekumbuka jambo. Darren akamuuliza, “Vipi Melissa? Umemtambua huyo mtu?”
Melissa akatikisa kichwa akiendelea kutazama ile picha alafu nwishowe akairejesha mikononi mwa Darren na kusema, “Anafanana na mimi sana!”
“Ndio! Hata mimi nilishangazwa sana ndiyo maana nikaibeba nije nikwonyeshe!”
Melissa akawa amenyamaza kimya. Macho yake yalionyesha yu mbali kifikra. Darren akamtazama na kumwita mara mbili kabla mwanamke huyo hajashtuka na swali, “Unaweza ukanipeleka huko kwa Bibi yako?”
“Amefariki!” Darren akamjibu akimtolea macho. “Au wataka kuona kaburi?”
“Twende hivyo hivyo!” Melissa akasihi. “Sidhani kama kutakuwa na shida, Darren!”
Darren akafikiri kidogo kisha akamwambia wataenda huko mwisho wa wiki kwani atabanwa na kazi hapa siku za usoni.
“Darren,” Melissa akaita akijitengenezea kumtazama mwanaume huyo. “Naomba, nipo chini ya miguu yako, tafuta siku ya karibuni. Mpaka mwisho mwingine wa wiki ni mbali sana!”
Darren akashangazwa na hitaji hilo la ghafla. “Melissa, ni haraka mno! Vipi kuhusu rat—”
“Tafadhali, Darren!” Melissa akanong’ona kwa huruma. Macho yake yalipoa na uso wake ukiwa kama ule wa mtoto aombapo kitu. Darren akashindwa kukataa. “Sawa, basi tufanye keshokutwa.”
“Kwanini sio kesho?” Melissa akauliza kwa upole. Darren akamtazama kwanza mwanamke huyo, alafu punde uso wake ukawa mgumu, “Melissa kwani kuna nini huko kitakachopotea tukikawia?”
“Darren, ungalikuwa wewe umefanana na mtu pichani hivi usingelipata hamu ya kujua?”
“Sawa,” Darren akalegea. “Tutaenda huko hiyo kesho.”
Basi baada ya hapo wakafanya mpango wa chakula, wakawasha pia na runinga watazame baadhi ya filamu. Wakachoma hapo masaa mpaka kiza kilipoingia. Wakala na kuendelea kutazama runinga wakiwa wanapeana mabusu na maneno matamu.
Usiku ulipokuwa mkubwa zaidi wakaenda kitandani, na kabla ya kulala ‘wakanyooshana migongo’. Wakachoka sana na basi usingizi ukawakwapua kwa upesi sana wasidumu hata lisaa.
Wakiwa wamelala, ni saa tisa ya usiku, ghafla Melissa anaamka na kuketi kitako kitandani. Kuna jambo linamtatiza kichwani. Anamtazama Darren, yu hoi hajielewi. Basi anatoka kitandani na kwenda kuifuata ile picha ya Bibi pale mezani.
Akaiteka kwa mikono yake membamba kisha akairejea kuitazama kwa macho yake makavu pamoja na kiza. Baada ya sekunde mbili, akasema kwa kunong’ona, “Tabitha … Cassandra … Bessie.!”
Akisema majina hayo akawa anamtazama mmoja baada ya mwingine. Punde akasikia Darren akijigeuza kitandani, upesi akatazama. Mwanaume huyo hakuwa ameamka. Bado alikuwa kwenye lindi kubwa la usingizi. Melissa akaachana naye na kuendelea kutazama ile picha, mwishowe akaiweka kifuani mwake akiwa na uso wa mawazo.
“Tabitha, nangoja jua lichomoze,” akasema hivyo na basi akarejea kitandani mwake na kulala.
Masaa yakazidi kusonga mpaka kufikia majira ya saa kumi na moja. Hapo Darren akashtuka toka usingizini na kuangaza. Alidhani pengine amekawia. Akafungua dirisha na kutazama nje, bado kiza. Basi kabla hajajirudisha kitandani akaenda chooni kwa haja ndogo.
Alipotoka huko, kama bahati tu, akajikuta macho yake yakiangukia mezani pale alipoacha picha yake. Akasonga karibu na kuitazama tena picha ile akitumia msaada wa taa ndogo ya mezani.
Akajikuta anatabasamu kumwona mtu mithili ya Melissa. Ila alipoitazama picha hiyo zaidi akagundua yule Melissa wa pichani alikuwa ana kovu dogo chini ya goti lake la kushoto. Aliweza kuona hivyo maana gauni lilikuwa limeishia magotini.
Basi kwa hamu ya kutaka kujua akamsogelea Melissa kitandani kisha akamtazama mguu wake wa kushoto. Hapo akaona kovu lile lile la kwenye picha! Ni kovu dogo ambalo hakupata hata kulijua kwa muda wote huo ambao amekuwa na Melissa kwenye mahusiano.
“Inawezekanaje?” akajiuliza. Akairejesha picha ile mezani kisha akazima taa na kurejea kitandani. Akalala nyuma ya mgongo wa Melissa aliyekuwa amelala kiubavu na kidogo akapitiwa na usingizi.
Ila hapo Melissa akafungua macho. Macho yake yalikuwa makavu tofauti na mtu atokaye usingizini. Melissa hakuwa amelala. Melissa alisikia na kuona kila kitu ambacho Darren ametoka kukifanya.
Hakufanya kitu na badala yake akalala. Asubuhi ya saa moja kamili wakaamka na kujiandaa kwa ajili ya safari. Kufikia saa tatu tayari wapo kwenye basi wakienda kijijini, countryside.
Walipopoteza masaa matatu barabarani wakafika kituoni. Wakatembea kwa ufupi kabla ya kufika kwenye nyumba kubwa ya Bibi. Hapo Melissa akasimama kuitazama nyumba hiyo kwa umakini. Naye Darren aliyekuwa ametangulia mbele ikamlazimu amrejelee, akatabasamu akimwambia, “Ndiyo hapa! … ni pazuri, sio?”
“Ndio, ni pazuri!” Melissa akajibu pasipo kumaanisha kwa uso wake, wakazama ndani. Humo akang’aza sana macho, ndani ya nyumba nzima na pia huko nje kana kwamba mtu anayetaka kununua akitaka kubaini madhaifu.
Walipokuwa nje, akamwomba Darren amwonyeshe kaburi la Bibi yake. Naye Darren pasipo ajizi, akampeleka magharibi ya mbali ya nyumba hiyo na kumwonyeshea, “Ndiyo hapa!”
Melissa akasoma kibao cha kaburi. Kilisomeka kwa jina la Cecilia Goodwin. Akauliza, “hili ndilo jina la bibi yako?”
“Ndio,” Darren akamjibu.
“Ahsante. Tunaweza tukarudi ndani.”
Wakarudi huko na Darren akampatia Melissa picha za Bibi yake. Kwa taratibu akazitazama moja baada ya nyingine.
“Sikumwona mtu huyo tena,” alisema Darren. “Yupo kwenye picha moja tu.”
Melissa asiseme kitu akaendelea kukagua picha zile. Alipomaliza akamkabidhi Darren na kisha akalaza kichwa chake kochini. Darren akazirejesha picha hizo na kisha kujumuika na Melissa hapo sebuleni.
Usiku ulipowadia, Melissa akamnong’oneza Darren kwenye sikio lake la kulia, “Nakuhitaji mpenzi.”
Darren akamtazama mwanamke huyo kwa kukodoa, “Melissa, tumefanya jana tu!”
Melissa akang’ata lips zake na kulegeza macho. “Kwani kuna ubaya, mpenzi?” akauliza akiweka kiganja chake kifuani mwa Darren.
“Hamna ubaya ila si kawaida yako.”
Melissa akatabasamu. Akafungua kifungo kimoja cha shati la Darren. “Sasa nitafanya nini na ingali u karibu yangu, tena tukiwa wapweke wenye nafasi?” akateta kwa sauti ya puani.
Darren asijibu, mwanamke huyo akaanza kubusu kifua chake na hatimaye akatimiza adhma yake. Darren akawa hoi kana kwamba amelima ekari za mbaazi. Hata alipojilaza hapo kochini akawa kama mfu!
Basi Melissa akajivalia nguoze na kisha akaelekea stoo. Huko akateka chepe na kutoka ndani ya nyumba kisha akaelekea moja kwa moja kule mashariki ya mbali kukuta kaburi la Cecilia Goodwin, bibi yake Darren.
Hapo kabla hajafanya chochote akaita kwa kunong’oneza, “Tabitha!”
Kisha akaanza kuchimba kaburi.


**

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom