UCHU
SURA YA PILI
KAZI KWAKO
"Umesikia George Foreman amerudi ulingoni na
kutwaa ubingwa", Chifu aliuliza.
"Sikusikia tu, nimeona kwenye televisheni".
"Basi na wewe nataka urudi ulingoni", Chifu
anasema kwa tabasamu huku akiupaka mkate
wake siagi.
"Mimi! mimi nimeoa na mke wangu ana mimba.
Mchezo huo sifanyi, sifanyi ng'o".
Chifu anaangua kicheko kiasi cha kuwafanya
watu wote ndani ya chumba cha mkutano
wamwangalie.
"Kwani mimi sijui umeoa! Kwani mimi sijui mke
wako ana mimba! Najua, lakini nakutaka
ulingoni tena. Kwani George Foreman hana mke,
hana watoto, mbona karudi ulingoni", Chifu
aliendelea kusema kwa kebehi.
"Huenda alikuwa anataka pesa, huenda alikuwa
anatafuta sifa, mimi sitaki vitu vyote hivyo, sirudi
ng'o", Chifu alielezwa kwa busara.
"Sikiliza nikueleze kwanza. Mimi ndiye
niliyekuruhusu uache kazi na kukushauri uoe na
nisingependa uharibu ndoa yako. Najua
unampenda sana mkeo, sasa nasema nisikilize
kwa makini nikueleze, kama utakataa itanibidi
niingie mimi mwenyewe ulingoni", Chifu alijibu
kwa masikitiko kiasi cha kumfanya mwenzake
apoe hasira zake.
"Chifu, hebu nieleze kuna nini? Kitu cha maana
namna hiyo, kiasi cha kusema utafanya kazi
hiyo mimi nisipokubali? Unajua mimi siwezi
kukuruhusu wewe kufanya hivyo.
"Basi sikiliza".
Ilimchukua Chifu saa nzima kumweleza suala la
Rwanda na jinsi msimamo wa PAM
ulivyohusiana pamoja na vipengele vingine vingi
ambavyo hata akina Musoke wasingeweza
kumweleza maana hawavijui.
"Unafikiri Serikali ya sasa ya huko haiwezi
kufanya kazi hiyo", Chifu aliulizwa.
"Haiwezi. Inahitaji ujuzi wa hali ya juu kufanya
kazi hiyo, katika hali ya machafuko namna ile,
maana hata wao hawajui nani ni nani katika
nchi yao. Hawamwamini mtu yeyote na wao
hawaaminiki vilevile na kuweza kupata habari za
kina kama zinavyotakiwa, unahitajika ujuzi wa
juu sana. Na katika Afrika nzima kama si wewe
basi itanibidi mimi mwalimu wako nikaifanye.
"Umenipa mtihani mkubwa sana. Unafikiri kazi
kama hii inaweza kuchukua muda gani?".
Chifu alipoulizwa swali hili, moyo wake ilitulia
akijuwa kazi itafanywa.
"Inategemea na wewe mwenywe, wiki moja au
mbili, mwezi yote yategemea wewe. Kwani Pepe
atajifungua lini?".
"Bado ana miezi miwili".
"Nakutakia heri. Nafikiri utamaliza kazi kabla ya
hapo. Tafadhali, hafadhari iwe kitu cha kwanza
kwako maana huko kuna hatari nyingi, usifanye
mchezo kama unataka kumwona mtoto wako",
Chifu sasa alikuwa amebadilika na kumwasa
mwenzake.
"Nikifa utamlea wewe", Alijibu.
"Sasa nina miaka sabini, nitamlea miaka
mingapi mie", Chifu alijibu.
"Wewe ndiye uliyetaka, shauri yako, damu yangu
itakuwa juu ya kichwa chako".
"Pole sana. Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania
inaondoka saa tano na nusu kwenda Kilimanjaro.
Tiketi hii hapa, umepatiwa nafasi kwenye ndage
hiyo. Musoke mtaonana uwanja wa ndege,
atakuja kukupokea, si unamfahamu?".
"Ndio, namfahamu".
"Haya kwa heri. Ukirudi toka Arusha, kabla ya
kwenda Kigali, njoo unione nitakuwa tayari na
taarifa za kukusaidia kule".
"Asante, nitafanya hivyo.
Chifu alilipa wakaondoka.
ITAENDELEA