UCHU
XII
"Saa ngapi sasa?" Bibiane alimwuliza
Willy Gamba.
"Imefika saa sita na nusu sasa", Willy
aliMjibu.
Walikuwa tayari wana saa moja ndani ya
kambi hii ya kijeshi na bado walikuwa
hawajapata tatizo lolote. Sasa ndio
walikuwa wanaanza kutega mabomu
kwenye bweni la mwisho ili baada ya
hapo kama itawezekana watafute namna
ya kutoka nje, kwani mabomu waliyokuwa
wameyatega na kuyaprogramu kwa saa
ya Willy ili kuyalipuwa lazima wawe
mbali, maana yalikuwa na uwezo wa
kuharibu kambi nzima na vitu vyote
vilivyomo kama yangefanya kazi kama
ilivyotarajiwa. Wakati wanafikiri hivi,
ghafla taa za kiwanja cha ndege
zikawashwa.
"Aha, kumbe ule ni uwanja wa ndege!"
Willy alinong'ona.
"Ndio, unafikiri zile ndege za kijeshi
zinaruka kutokea wapi!", Bibiane ambaye
naye hapo awali alikuwa hajui uwanja
ulikuwa wapi, alijibu.
"Kwanini wanawashwa taa wakati huu?",
Willy alijiuliza.
Wakiwa wameduwazwa na kitendo hiki na
wakiwa sasa wameondoka kwenye ukuta
wa bweni la mwisho na kujibanza kwenye
kivuli cha lori kubwa la jeshi lililokuwa
limeegeshwa pale, Bibiane alijibu.
"Huenda ndege za kivita zinatolewa ili
zikashambulie mahali ama ndege ya Jean
inataka kutua".
"Nafikiri hilo la pili ni sawa. Hii itakuwa
raha sana mimi kukutana uso kwa uso na
huyu bwana yako", Willy alikejeli Bibiane
akafadhaika.
"Si bwana yangu tena, bwana yangu ni
wewe Willy, maana wewe ndiyo uko na
mimi sasa, sema, fanya kila unachotaka
nifanye", Bibiane alijibu kwa sauti ya
mahaba. Willy alimwangalia, kisha
akamshika na kumbusu.
Mara wakasikia king'ola na askari
wakatoka na kuanza kuelekea kwenye
kiwanja cha ndege.
"Hapa kuna hatari, nafikiri
wametushitukia", Willy alisema huku ile
kengere yake ya hadhari ikilia kichwani
mwake. Kisha akaendelea. "Kinachotokea
hapa ni sisi kutoka ndani ya kambi hii.
Wataanza kutusaka sasa hivi".
Mara tena wakasikia mwungurumo wa
ndege na magari sita aina ya Landrover
ya wazi yakiwa yamebeba askari
yakielekea karibu na uwanja, yalipokaribia
yakasimama. Kisha, yakafika magari
mengine mawili aina ya Landcruiser GX
nayo yakasimama pale vilevile kusubiri ile
ndege itue. Pale kwenye uwanja mkubwa,
vikosi vya askari vilizidi kujipanga kwa
ajili ya mapokezi.
Ile ndege ilipotua watu wanne walitoka
ndani ya Landcuiser zilizokuwa
zimesimama kando na kusogea karibu ili
kuilaki ile ndege. Wakiwa bado
wamefichwa na kivuli cha lile Lori
walitumia viona mbali vyao na
kuwaangalia kwa makini wale watu
waliotoka kwenye yale magari.
"Yule aliyetangulia ni Col. Marcel
Bazimaziki, huyu ndiye kamanda mkuu
wa majeshi yote ya Akazu. huyo wa
kushoto ni Kapten Nkubana aliyekutoroka
Kigali, ndiye aliyetumwa kuniua, kumbe
naye keshafika huku. Wa kulia ni
kamanda Morris huyu ni mkuu wa vikosi
vya kukodiwa ambavyo vinafundisha
majeshi ya Akazu. Huyu wa nyuma
simfahamu".
Ndege ilisimama na milango ikafunguliwa
na watu wakaanza kutoka. Jean ndiye
alikuwa wa kwanza kutoka ndani ya
ndege hii.
"Aha huyu ndiye Jean nafikiri?", Willy
aliuliza.
"Bila shaka huyo ndiye Jean, ambaye
ndiye mzizi wa fitina katika Rwanda. na
yule anayemfuatia ni Anatoile Kabuga,
huyo ndiye kiongozi wa Akazu, anayefuata
ni Jenerali Kasongo, kamanda wa majeshi
ya Rais wa Zaire, rafiki mkubwa wa Jean,
anayetokea sasa pale mlangoni ni Col.
Gatabazi na huyo anayetokea mwisho
simfahamu, maana sijawahi kumuona",
Bibiane alieleza.
"Asante, sijui bila wewe ingekuwaje,
umefanya kazi yangu iwe rahisi kiasi
fulani".
"Ni kweli, lakini ungetumia njia nyingine,
wewe si wa kushindwa jambo".
Baada ya kutoka ndani ya ndege, kundi la
Jean liliingia ndani ya zile Landcruiser
wakaondoka huku wakisindikizwa askari
kwa ulinzi mkali.
"Unadhani watakuwa wanaelekea wapi
sasa?", Willy alimuuliza Bibiane.
"Sijui, nilitegemea huenda wanataka
kuzungumza na vikosi vilivyofanya
gwaride pale uwanjani, lakini
wameondoka moja kwa moja kuelekea
upande ambao ndiko kuna lango kuu.
Huenda wanakwenda kupumzika kwa
kamanda Morris, nyumba na ofisi ya
kamanda Morris iko juu ya hicho kilima,
huwezi kuona ukiwa hapa kwa vile
kumefichika kwa miti", Bibiane alieleza.
Kati ya magari yaliyobeba askari moja
halikuendelea na msafara isipokuwa
lilielekea kwenye gwaride. Gari hilo
lilipofika hapo lilisimama na watu
waliotoka ndani walikuwa Nkubana na
askari wengine watano. Kisha Nkubana
akaanza kuhutubia hilo gwarinde na
kikosi kimoja wapo kikapiga hatua moja
mbele na vingine vikatawanyika. Willy na
Bibiane hawakuelewa nini kilikuwa
kinaendelea.
"Lililopo ni sisi kuondoka hapa kambini
haraka iwezekanavyo. Vinginevyo
tutakamatwa hata kabla hatujamaliza kazi
iliyotuleta", Willy alieleza.
"Mimi bila kummaliza huyu Jean siendi
kokote ng'o", Bibiane alijibu kwa hasira.
"Lazima ufahamu kuwa hatuwezi
kukabiliana na watu wote hawa, lazima
kutumia akili ya ziada, wewe unajua
katika kazi yetu hii swala ni kuendelea
kuishi; lazima uhakikishe unajilinda ili
ubaki salama. Hapa tukitaka kuanza
mapambano ni sawa na kujinyonga sisi
wenyewe. Pili ili tuweze kulipua mabomu
tuliyotega ni lazima tutoke nje kabisa ya
eneo hili, la sivyo sisi pia tutakuwa
tumejiteketeza pamoja na adui", Willy
alimuasa Bibiane kisha wakaona wale
askari wa kikosi wanakabidhiwa silaha na
kuelekea kwenye seng'enge ya ua wa
kambi.
"Ehe, umeona kazi hiyo, hawa jamaa
wanategemea tutakuja hapa, lakini
hawajui kama tumeingia ndani na kazi
imefanyika", Willy alieleza.
"Lakini wakifika pale tulipoingilia lazima
watajuwa tuko ndani", Bibiane alijibu.
"Ndio sababu nikasema tutafute njia
tutoke humu ndani", Willy alisisitiza.
Wakati wote Willy alikuwa akipanga mbinu
za kuweza kutoka ndani ya kambi hii
wakiwa salama.
"Hebu nifuate tuangalie hali ikoje upande
wa lango kuu", Willy alimwambia Bibiane.
"Kule hatuwezi kupita, afadhari tuwahi
palepale mahali tulipotumia mwanzo",
Bibiane alisema na Willy akamuunga
mkono na kuona alikuwa na mawazo
sahihi hivyo, haraka haraka wakaelekea
sehemu waliyokuwa wameingilia, huku
askari wa doria wakizidi kujipanga na
kupewa silaha ili kuzidi kujipanga kando
ya ua huu wa seng'enge wakiwa tayari
kulinda kambi yao. Ile tembetembea ya
hawa askari kiasi fulani iliwasaidia sana
akina Willy na Bibiane kutobainika
mapema kwani walikuwa wamevaa
mavazi ya kijeshi kama wale askari.
Nkubana na watu wake waliweka ulinzi
mkali upande la lango kuu wakiamini
kuwa Willy angeweza kujaribu kuingia
pale kambini kwa kutumia lango kuu.
Hakuna askari wala kiongozi katka kikosi
chicho aliyefikiri kuwa adui wangeweza
kupitia sehemu nyingine yoyote kwani
waliamini kwamba hakuna kitu ambacho
kingeweza kupita ua ulioizunguka kambi
hii. Hivyo, hata hawakuweka askari
kuzunguka ua ilikuwa ni kwa hadhari tu.
Kumbe kitu ambacho hawakujua ni
kwamba teknolojia yotote inaweza
kushindwa na teknolojia nyingine yenye
maarifa ya juu zaidi. Willy alikuwa ndani
na tayari alikuwa ametega mabomu kila
upande.