Riwaya: Taharuki

Riwaya: Taharuki

RIWAYA: TAHARUKI
Imeandikwa na HALFANI SUDY
SIMU 0652 212391

Hii ni sehemu ya Kumi na Moja

“Catherine na Grace tunawaachia huru, sitegemei kama mtamsimulia yeyote hiki kilichotokea usiku wa leo, iwe siri yenu kama bado mnapenda kuishi hapa duniani, mmeelewa?”
Baada ya siku tatu Jordan alizikwa katika makaburi ya Sinza, na siku hiyo jioni ndipo Martin aliipata nafasi ya kukaa meza moja na Catherine kumhoji juu ya kifo cha aliyekuwa mpenzi wake. Haikuwa rahisi hata kidogo kwa Martin kuipata nafasi hiyo, Catherine alikuwa tayari kuhojiwa na mtu yeyote yule juu ya kifo cha Jordan, lakini hakuwa tayari kabisa kuhojiwa na adui yake. Kuhojiwa na Martin kwake aliiona kama kejeli ambayo hakutaka hata kidogo kuishuhudia. Lakini kutokana na ushawishi wa baba Luteni Jenerali Madoshi yake ndipo Catherine alikubali kukaa meza moja na Martin kwa ajili ya mahojiano.
“Samahani sana Caatherine kwa kuuchukua muda wako, ninajua upo katika majonzi makubwa sana ya kufiwa na aliyekuwa mpenzi wako, najua uchungu hau....”
“Kijana, twende moja kwa moja katika lengo la kikao hiki” Catherine alisema kwa ukali huku akimwangalia Martin kwa macho ya dharau.
“Samahani sana Catherine, lengo langu lilikuwa ni kukupa pole, unaj....”
“Kijana ukiendelea na porojo zako nitakuacha peke yako hapa mezani, naomba twende katika kitu kilichokufanya umuombe baba ukutane na mimi” Catherine alisema kwa sauti ya ukali.
“Samahani sana Catherine kwa kukupotezea muda, nani unahisi itakuwa kahusika katika mauaji ya Jordan? ” Martin aliuliza swali kwa sauti ya kutojiamini.
Catherine alimwangalia Martin machoni kisha akasema, “Hakuna mtu yeyote ninayemhisi kahusika na kifo cha Jordan” Catherine alijibu.
“Umeishi na Jordan kama wapenzi kwa miaka mingapi?” Martin aliuliza.
“Miaka mitatu” Catherine alijibu kwa mkato.
“Katika maisha yenu ya mahusiano, je umeona kama Jordan ana maadui wowote ambao wanaweza kuwa wamefikia hatua hii ya kumuua?” Martin aliuliza tena huku akimwangalia usoni Catherine.
“Hapana, sijaawahi kumjua hata adui mmoja wa Jordan” Catherine alijibu huku sauti yake ikionesha kuwa alikuwa anakereka na maswali ya Martin.
“Catherine, nipo hapa mbele yako kuhakikisha tunawakamata wauaji wa mpenzi wako na kuijua sababu ya kumuua. Naomba ufanye kama leo ndio siku ya kwanza unakutana na mimi. Naomba usahau kabisa kuhusu kilichotokea siku ile ofisini kwa baba yako” Martin alisema kwa sauti ya kukereka.
“Nimeshakujibu” Catherine alijibu kwa kifupi.
“Catherine, najua kama kuna watu walikuja kukuteka nyumbani kwako katika ule usiku ambo Jordan aliuwawa...” Martin alisema kauli ambayo ilimshtua sana Catherine.
“Unasemaje wewe?” Catherine aliuliza huku akimtolea macho Martin kwa mshangao.
“Najua kwamba ulichukuliwa usiku na kupelekwa katika nyumba moja iliyopo huko Magomeni Mwembechai na kukutanishwa na rafiki yako Grace. Najua kwamba malengo ya watekaji kukuteka ilikuwa ni kuupata mzigo ambao ulikuwa nao wewe....”
“Martin...” Kwa mara ya kwanza Catherine aliliita jina la Martin kwa heshima kubwa badala ya ‘kijana’ kama alivyokuwa anamuita awali.
“.....na uliwaambia watekaji kuwa mzigo wao uliupeleka kwa Jordan, na bila shaka watekaji waliokuteka ndio waliomuua Jordan baada ya kuupata mzigo wao. Sasa ninataka kujua kila kitu unachokijua kuhusu huo mzigo?” Martin alisema huku akimwangalia Catherine kwa macho makavu.
“Umeyajuaje yote hayo Martin?” Catherine aliuliza kwa mshangao huku akimsogelea Martin.
“Naomba unijibu nilichokuuliza Catherine, kama hauko tayari niambie sipo tayari, na mimi hutaniona tena mbele ya macho yako kukuuliza chochote juu ya kifo cha Jordan” Martin alisema bila ya wasiwasi wowote.
“Martin, sijawahi kutegemea hata siku moja kwamba wewe ni mahiri kiasi hiki, u mpelelezi hodari sana ambaye umepiga hatua kubwa sana, hatua ambazo hakuna askari hata mmoja aliyeweza kupiga. Kila ulichosema Martin ni kweli ingawa sielewi umeyajuaje. Ni kweli nilitekwa usiku nyumbani kwangu na kupelekwa katika nyumba moja ambayo sifahamu ilikuwa maeneo gani kwakuwa nilikuwa nimefungwa kitambaa cheusi wakati nikipelekwa katika nyumba hiyo. Ni kweli ndani ya hiyo nyumba ambayo wewe unasema ipo Magomeni Mwembechai nilikutanishwa na Grace. Watekaji walinitishia kumuua Grace na kuniua kwa mateso makali endapo sitawaambia wapi ulipo mzigo wao, nami niliwaambia mahali nilipoupeleka mzigo.
Martin, Grace ni rafiki yangu wa siku nyingi sana, tulikulia katika mtaa mmoja na kusoma shule ya msingi na sekondari moja, lakini baadae tukatengana baada ya kumaliza kidato cha sita na mimi kwenda kusoma nje ya nchi. Nilikutana naye tena Grace miezi miwili iliyopita baada ya kupoteana zaidi ya miaka minne.
Siku ya tatu baada ya kukutana na Grace ndipo aliponiambia kuwa kwa sasa yeye alikuwa ni mwajiriwa wa jeshi la Polisi. Katika kujadiliana juu ya hiyo kazi yake aliniambia kwamba kwa kipindi hiko kulikuwa na kesi nzito alikuwa anaichunguza, kesi ambayo sio tu ilikuwa inahatarisha kazi yake lakini pia ilikuwa inahatarisha maisha yake. Aliniambia katiak uchunguzi wake amegundua kuwa kuna kiongozi mkubwa wa serikali alikuwa anajihusisha kwa siri na biashara haramu ya dawa za kulevya. Alichunguza nyendo za kiongozi huyo kwa zaidi ya miaka miwili na sasa alikuwa na ushahidi wote wa kuweza kumtia hatiani huyo kiongozi. Grace aliniambia katika uchunguzi wake alikuwa ameipata diski mweko ambayo ina ushahidi wote wa kumtia hatiani huyo kiongozi, ila aliniambia kuwa kwasasa anahisi yupo katika hatari baada ya watu wa viongozi huyo kugundua kwamba alikuwa anamchunguza bosi wao kwa siri, hivyo Grace alinipa mimi hiyo diski mweko niihifadhi kwa muda kabla yeye kuiwasilisha katika sehemu husika.
Kwa kweli ilinishitua sana taarifa aliyonipa Grace, lakini sikuwa na namna zaidi ya kulikubali ombi lake. Alinipatia hiyo diski mweko na kwenda kuihifadhi katika nyumba ya Jordan, huku nikimueleza kila kitu Jordan juu ya diski mweko hiyo.
Zilipita wiki mbili tangu Grace anipe hiyo diski mweko, ndipo ule usiku uliokuwa unauzungumzia wewe ulikuja. Walinivamia watu usiku na kuniteka, walinilazimisha niwape mzigo wao. Mzigo wenyewe ulikuwa ni ile diski mweko wenye siri za wauza dawa za kulevya” Catherine alisimulia kwa kirefu.
“Nashukuru sana Catherine kwa maelezo yako, hizi ndizo taarifa nikizozitaka kutoka kwako, sasa ninaenda kuwaangusha watu hawa na kuirudisha diski mweko mikononi mwa Grace, lazima watu wote wanaojihusisha na mtandao wa dawa za kulevya tuwatie mbaroni, wanaharibu sana vijana wa nchi hii ambao ndio nguvukazi ya Taifa” Martin alisema kwa hasira.
“Martin lakini umeyajuaje yote hayo?” Catherine aliuliza kwa shauku ya kutaka kujua.
“Nitakusimulia kila kitu siku moja.....” Martin alijibu kwa mkato na kuinuka kitini.
Catherine alibaki katika mshangao mkubwa wakati akimshuhudia Martin akiondoka bila ya kumuaga, tangu siku hiyo chembechembe za chuki za Catherine kwa Martin zilikufa, ukazaliwa upendo ambao hata Catherine mwenyewe hakujua umetokea wapi?

Je nini kitatokea? LAKO JICHO!

Sent from my Infinix X655C using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA; TAHARUKI
Imeandikwa na HALFANI SUDY
SIMU; 0653 212391

Hii ni sehemu ya Kumi na Mbili

Ilimchukua wiki mbili kwa Martin Hisia kuudondosha utawala wa wauza dawa za kulevya. Kitu kwanza alichofanya, alimsogeza karibu ndugu yake, Robby. Robby na Martin walikuwa ni ndugu, Robby alikuwa ni mtoto wa baba mdogo wa Martin. Martin alimuweka chini Robby na kumueleza madhara ya kitu alichokuwa anakifanya. Robby alimuelewa na kuungana naye kwa siri. Kwa kumtumia Robby alifanikisha kuipata diski mweko waliyoipora kwa Jordan na kuwaweka hadharani wauzaji wote wa dawa za kulevya, wakiongozwa na waziri wa nishati, John Dunda, ambaye ndiye alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa biashara hiyo. Robby pia alitambulisha Martin katika mtandao wa Bilionea Zawwiya, Martin alipokelewa na kuanza kufanya kazi na Bilionea Zawwiya huku akitengeneza mkakati wa kuudondosha mtandao huo.
Zilipita wiki tatu tangu Martin kusababisha kukamatwa kwa watu waliomuua Jordan kukamatwa, ukaribu wa Martin na Catherine ulikomaa na baadae kuzaa penzi, penzi ambalo lilikuwa tamu hadi asubuhi ambayo Catherine alipopigiwa kwa simu ya Catherine huku mpigaji akijitambulisha kwa jina la Sauti Simuni. Simu ilikuwa inatoka katika mtandao wa Bilionea Zawwiya ambao ulikuwa na ushirikiano na mtandao uliondoshwa wa John Dunda, ambao kwa sasa Martin alikuwa ndani yake, bila Bilionea Zawwiya kujua kwamba Martin alikuwa ni ‘double agent’
Daniel na Hannan walikutana katika meza moja ya pembeni kabisa katika baa ya Hongera, makutano hayo yalitokea baada ya Daniel kumpatia kazi Hannan ya kumpa taarifa juu ya Martin Mbaga.
“Hannan uliniambia kuwa kuna mambo umeyapata kuhusu Martin, ni mambo gani hayo?” Daniel aliuliza baada ya kusalimiana na Hannan.
“Ndio Daniel, nimeifanya kazi uliyonituma ya kumchunguza Martin, mchumba wake na Catherine. Nilichogundua ni kwamba, Martin Mbaga ni kijana mwenye umri wa miaka ishirini na tano, baba yake Martin ni mfanyakazi mstaafu katika kiwanda cha bia cha Ziro cha huko mkoani Morogoro, wakati mama yake ni muuguzi katika hospitali ya Maero iliyopo hukohuko mkoani Morogoro.
Kipindi cha utoto Martin alikuwa anapenda sana kuwa mwanasheria kabla ya baadae ndoto hiyo kubadilika bila ya hata yeye mwenyewe kutarajia. Martin ana mpenzi anayeitwa Monica lakini hawajabahatika kupata watoto, kwasasa Martin yupo nchini Kenya katika jiji la Nairobi kwa kazi maaalum” Hannan alisema kwa kirefu huku akimwangalia Daniel.
“Martin yupo jijini Nairobi kufanya kazi gani?” Daniel aliuliza tena.
“Kama nilivyosema awali Daniel, ndoto za Martin zilibadilika bila hata yeye mwenyewe kutarajia, kutoka kuwa Mwanasheria na kudondokea kuwa afisa usalama wa Taifa, na hii ndiyo kazi iliyompeleka Martin nchini Kenya, Martin yupo nchini Keny.....”
“Inatosha, inatosha Hannan. Wewe ni Hannan yuleyule, hujabadilika. Wewe ni mchawi wa kike wa kompyuta ambaye unaweza kuzisaka taarifa zozote, popote pale zilipo ulimwenguni na kuzileta mbele ya kioo cha kompyuta yako. Taarifa ulizosema kuhusu Martin Mbaga zote ni sahihi, mimi ninajua kila kitu juu ya ulivyosema, nilikupa kazi hii ndogo ili nijue kwamba bado u mweledi vilevile katika kusaka taarifa zilizofichwa, na nimethibitisha kwamba upo vizuri sana” Daniel alisema kwa hisia wakati Hannan akibaki anamwangalia tu.
“Nini lengo la kunipa kazi hii?” Hannan aliuliza huku akitabasamu.
“Umeuliza swali zuri sana, lengo la kukupa kazi hii ni kama nilivyosema awali, kukupima kama uwezo wako wa kusaka taarifa kwa njia za kiteknolojia upo vilevile?” Daniel alisema.
“Baada ya kujua kwamba uwezo wangu haujatetereka?” Hannan aliuliza tena.
“Baada ya kuthibitisha kwamba uwezo wako wa kusaka taarifa upo vilevile ni kukupa kazi, kazi ngumu pengine kuliko kazi zote tulizowahi kuzifanya katika maisha yetu ya kiuchunguzi. Kwa kifupi, kuna vitu visivyo vya kawaida vinaendelea katika nchi yetu, vitu ambavyo tuna dhima ya kuvizima kabla nchi yetu haijaingia katika taharuki.
Kama uchunguzi wako ulivyoonesha kuwa Martin ni afisa usalama wa Taifa, huo ni ukweli, Martin anaripoti kila kitu kwangu na hata hiyo kazi aliyoenda kuifanya nchini Kenya ni mimi ndiye niliyeiratibu.
Miezi kadhaa iliyopita, Martin alifanya kazi nzuri sana ya kuwadondosha wauza dawa haramu za kulevya, na kwa jinsi alivyoifanya kazi ile kwa umakini nikashawishika kumpa kazi hii. Sababu nyingine ya kumpa kazi hii na ile ya awali zina mahusiano. Ni mimi ndiye kwa makusudi nilimuingiza Martin katika maisha ya Catherine, nilimuingiza baada ya kuhisi kitu nilipohudhuria harusi ya mtoto wa Bilionea Zawwiya na yule mtoto wa waziri wa ulinzi. Nilialikwa katika harusi ile, lakini kama ujuavyo kwa sisi wapelelezi, tunafanya kazi ya kuilinda nchi yetu tuipendayo popote pale tutakapokuwa.
Wakati wa kutoa zawadi katika harusi ile mimi nilikuwa nimekaa nyuma kabisa ya ukumbi wa Kipanga. Nikiwa kule kwa nyuma ndipo nilipowaona watu wawili waliokuwa wamesimama nyuma ya spika kubwa za muziki, watu wale walikuwa wanaongea kwa kunong’ona huku mara kadhaa wakimwangalia Catherine aliyekuwa amekaa katika sehemu ambayo ilikuwa imekaliwa na watu maarufu. Pengine unaweza kuhisi ni jambo la kawaida tu kwa nyota kama Catherine kuangaliwa sana na wale watu wawili, lakini macho ya watu wale hayakuwa macho ya kawaida, yalikuwa na kitu ndani yake.
Ulipofika wakati wa Catherine kwenda kutoa zawadi kwa maharusi, ndipo nilipomuona mmoja ya wale watu waliokuwa nyuma ya spika akienda kwa mashaka katika siti aliyokuwa amekaa Catherine, kwa usiri mkubwa alibandika kitu katika kiti kile. Hisia zangu zilikuwa sahihi, macho ya watu wale hayakuwa macho ya kawaida, na hiyo ilithibitishwa na vitendo vyao.
Nilisimama kule nyuma ya ukumbi nilipokuwa nimekaa na kuanza kuwafatilia wale watu, kwa bahati mbaya wale watu kila mmoja alienda upande wake baada ya kuongea kwa takribani dakika tano. Hapo ilinipasa nianze kumfatilia mmoja kati ya watu wale, maana kama wahenga walivyosema miaka mingi iliyopita ‘Mtaka yote kwa pupa hukosa yote’.
Niliamua kufatilia nyendo za jamaa mmoja kati ya wale ambaye alikuwa mrefu kuliko mwenzake. Nakumbuka alikuwa amevaa suti nyeusi zilizomkaa vyema mwilini mwake, na chini alivaa viatu vyeupe aina ya moka. Kichwani alikuwa amevaa kofia aina ya pama nyeusi. Jamaa alitoka kule nyuma ya spika na kwenda kukaa katika siti iliyokuwa karibu na Bilionea Zawwiya, nilimuona wakipeana ishara za siri kila wakitazamana na Bilionea Zawwiya. Akili yangu ikanambia kwamba nisiyatoe macho yangu hata kwa sekunde moja kwa yule jamaa, ni yeye ndiye atakayenipeleka katika sehemu sahihi ambapo hisia zangu zinapahisi. Nikiwa nimekaa upande ambao nilikuwa nawaona kwa pamoja yule jamaa na Catherine, na muda ule ndio Catherine alikuwa anarudi na kwenda kukaa katika siti yake. Alivyokaa tu, nilimuona yule jamaa mrefu akinyoosha dole gumba kuelekea upande wake wa kushoto, kwa kasi nami macho yangu yalielekea huko, nilimuona mtu aliyekuwa akimpa ile ishara ya dole gumba, alikuwa ni yule jamaa waliyekuwa naye awali kule nyuma ya spika za muziki, ambaye yeye alikuwa amevaa suti nyeupe lakini mshono wake ukifanana na wa yule jamaa mrefu. Nilipomchunguza kwa umakini, yule jamaa mfupi mwenye suti nyeupe niligundua kwamba alikuwa ana visikilizio masikioni mwake vilivyounganishwa na simu yake, hapo ndipo lilinipata wazo kwamba jamaa walikuwa wameweka kifaa ambacho kitawaunganisha wao na Catherine, lakini hilo litawezekana endapo tu Catherine atavaa gauni alilolivaa siku ile ya harusi ambalo walikuwa wamelibandika kifaa maalum”
“Aisee! Hao jamaa walikuwa wanataka nini kwa Catherine?” Hannan aliuliza kwa sauti yenye hamaniko.
“Kusema ukweli hata mimi sikugundua kwa wakati ule ni kitu gani walikuwa wanakitaka kwa Catherine, ilinipasa kutulia huku nikifanya uchunguzi wangu kwa umakini ili kugundua lengo la wale majamaa.
Baada ya ile ishara ya dole gumba yule jamaa mrefu mwenye suti nyeusi alinyanyuka pale kitini na kutoka nje ya ukumbi wa Kipanga. Nami nilitoka nilipokuwa nimekaa na kumfuata kwa nyuma bila ya yeye kujua kama nilikuwa namfuatiliwa. Alivyotoka nje alienda moja kwa moja nyuma ya ukumbi, akatoa simu yake mfukoni na kuanza kuipiga, aliongea na hiyo simu kwa dakika zipatazo kumi kisha aliikata. Akaitia simu yake mfukoni na kuelekea upande ambapo kulikuwa na maegesho ya magari, akaingia kwenye gari aina ya Range Rover Vogue ya rangi nyeusi, akaiwasha na kulitia moto. Kwa haraka nilienda kwenye gari yangu na kuanza kumfatilia yule jamaa.
Kutoka Sinza Mori, katika ukumbi wa Kipanga mahali ilipokuwa inafanyika harusi ya Seif, jamaa alielekea barabara iliyokuwa inaelekea Sinza Bamaga. Alipofika makutano ya Bamaga alikata kushoto na kuelekea barabara iliyokuwa inaelekea Mwenge. Niliacha umbali mdogo nyuma yake ili iwe ngumu kwake kugundua kama nilikuwa namfuatilia. Alipofika kwenye taa za Mwenge alikata kushoto na kuifuata barabara ya Sam Nojuma. Nilifanya kama naelekea Tegeta ili asigundue kama namfuatilia, kisha niligeuza kwa mbele na kuendelea kumfatilia yule jamaa, jamaa aliendesha gari moja kwa moja hadi katika taa za Ubungo na kukata kushoto, akitembeza matairi ya gari yake katika barabara ya Morogoro. Nilishangaa sana, iweje azunguke namna ile wakati kulikuwa na njia rahisi tu ya kutoka kule ukumbini Sinza Mori na kuifuta barabara ya Shekilango na kuelekea alipokuwa anaelekea sasa, hapo nikagundua kwamba jamaa alijizungusha ili kugundua kama kuna gari lilikuwa linamfuatilia. Hapo ndipo nilipozidisha umakini kuhakikisha kwamba hagundui kama nilikuwa ninamfuatilia.
Jamaa alinyoosha moja kwa moja hadi Magomeni Mwembechai na kuegesha gari katika nyumba moja. Nilienda kuegesha gari kwa mbali kidogo kutoka ilipokuwa ile nyumba. Niliitoa simu yangu na kuitafuta namba ya Deus. Deus ni mmoja ya watu wangu anayefanya kazi katika wizara ya ardhi ambaye ninamtumia kupata taarifa za nyumba ninazotaka taarifa zake katika uchunguzi wangu. Nilimuambia Deus aniambia mmiliki wa ile nyumba, Deus alinambia kuwa kwa muda ule hawezi kufanya chochote mpaka kesho yake atakapoenda ofisini. Ilinipasa kusubiri maana hakukuwa na namna yoyote ili ya kumjua mmiliki wa nyumba ile.
Siku ile niliondoka bila ya kufanya chochote hadi ilipofika kesho, nitakapomjua mmiliki wa ile nyumba, nilipanga uchunguzi wangu juu ya wale watu uanze kwa mmiliki wa ile nyumba. Lakini pamoja na kuamua hivyo niliiona hatari iliyokuwa inamkabili Catherine bila ya yeye kujua, niliamua kumpa ulinzi Catherine pia bila ya yeye kujua. Ndipo ilipotokea nafasi ambayo Luteni Jenerali Madoshi aliponipa kazi ya kumpa adhabu Martin baada ya kufanya makosa. Nilimpa Martin adhabu ya kuwa karibu na Catherine ili ayalinde maisha yake dhidi ya wale watu ambao sikujua hasa lengo lao ni nini. Hivyo ndivyo nilivyowaunganisha Catherine na Martin.

Je nini kitatokea? LAKO JICHO!

Sent from my Infinix X655C using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA; TAHARUKI
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU 0652 212391

Hii ni sehemu ya Kumi na Tatu

Siku ile niliondoka bila ya kufanya chochote hadi ilipofika kesho, nitakapomjua mmiliki wa ile nyumba. Nilipanga uchunguzi wangu juu ya wale watu uanze kwa mmiliki wa ile nyumba. Lakini pamoja na kuamua hivyo niliiona hatari iliyokuwa inamkabili Catherine bila ya yeye mwenyewe kujua. Niliamua kumpa ulinzi. Ndipo ilipotokea nafasi ambayo Luteni Jenerali Madoshi aliponipa kazi ya kumpa adhabu Martin baada ya kufanya makosa. Nilimpa Martin adhabu ya kuutengeneza ukaribu na Catherine, lengo lilikuwa ni ili ayalinde maisha yake dhidi ya wale watu ambao sikujua hasa lengo lao ni nini. Hivyo ndivyo nilivyowaunganisha Catherine na Martin.
“Daah kumbe ndivyo mambo yalivyokuwa Daniel? Lakini bado nataka kujua Martin aligundua nini baada ya kumuweka karibu na Catherine?” Hannan alimuuliza Daniel kwa shauku kubwa.
“Kwanza haikuwa rahisi kwa Martin kuwa karibu na Catherine, lakini baada ya mkasa ule wa dawa za kulevya na hasa baada ya Jordan ambaye alikuwa mpenzi wa Catherine kufariki iliwezekana. Pia kumbuka katika mkasa ule Martin alitengeneza urafiki mkubwa sana na Robby licha ya kuwa ndugu yake. Akaanza kumtumia Robby kuiba siri za wale watu. Mpaka mwishowe Martin aliingia katika hilo kundi kwa kumtumia Robby, na baada ya kuingia kundini kwa bahati nzuri aliaminiwa hadi na Bilionea Zawwiya.
Ilimchukua miezi mingi kidogo ndipo Martin alipewa kazi ya kwenda kuupokea mzigo asioufahamu huko jijini Naorobi nchini Kenya. Kazi ambayo waliifanya yeye na Robby. Ulikuwa mchezo ulioratibiwa na mfanyabiashara mmoja maarufu nchini Kenya anayeitwa Meya wa Kimathi, na walipanga kumtumia Catherine katika kuusafirisha mzigo huo kutokea jijini Dar es salaam. Kulikuwa na sababu kuu mbili za kufanya hivyo; Sababu ya kwanza walijua kwamba itakuwa rahisi kwa Catherine kuupeleka mzigo nchini Kenya bila ya kashikashi yoyote kutokana na umaarufu wake.
Sababu ya pili ilikuwa ni ya kiusalama, walijua kwamba hata kama ikitokea kwa bahati mbaya Catherine akishindwa kuufikisha mzigo katika mikono husika na kukamatwa, wao watabaki salama, kwakuwa Catherine atakuwa hamjui ni nani aliyemtuma kuupeleka ule mzigo nchini Kenya.
Kazi ilifanyika na Catherine kufanikiwa kuufikisha salam mzigo nchini Kenya na kumkabidhi Robby, wakati huo Martin alikuwa amejificha ili asionekane na Catherine. Lakini ilitokea bahati mbaya sana, mzigo uliibiwa hotelini. Sisi lengo letu lilikuwa ni kujua ule mzigo ulikuwa una nini ndani yake lakini kwa bahati mbaya hatukufanikiwa. Sasa tumerudi hatua elfu moja nyuma, hatuna pa kuanzia kujua ule mzigo ulikuwa ni wa kitu gani? Hapo ndipo unapoingia wewe Hannan. Nimekushirikisha ili tusaidiane kujua wapi ulipo mzigo? Mzigo ulikuwa una kitu gani ndani yake? Na kina Bilionea Zawwiya wana jambo gani la siri linalowafanya wafanye mambo yao kwa gharama na tahadhali kubwa namna ile” Daniel alimaliza kumuelezea Hannan.
“Mfyuuu...aisee..” Hannan alipumua kwa nguvu, “ Kusema ukweli ingawa bado hamjaujua mzizi hasa wa mambo haya lakini mmefanya kazi kubwa sana. Kujua uhusika wa Bilionea Zawwiya katika mkasa huu kumetupa njia ya kuanzia. Bila shaka Bilionea Zawwiya anajua mzigo alioubeba Catherine una nini ndani yake? Anajua wana mpango gani mpaka wakafikia kufanya yote hayo kwa usiri mkubwa sana. Kama nina cha kushauri katika yote uliyonieleza Daniel, basi ni kuhakikisha tunamkamata Bilionea Zawwiya, ni yeye pekee ndiye atayetuambia wana malengo gani na nchi hii?”
“Umetoa ushauri mzuri Hannan, ingawa utekelezaji wa usahuri wako ni mgumu sana. Najua unafahamu kwamba katika nchi hii hakuna tajiri anayependwa kama Bilionea Zawwiya. Wananchi wameweka imani kubwa sana kwake kwa roho yake ya upendo anayowaonesha. Masikini wengi wa nchi hii wanamchukulia Bilionea Zawwiya kama mkombozi wa maisha yao. Amekuwa akisaidia sana masikini kwa kuwagharamikia matibabu hapa nchini na wakati mwengine kuwapeleka hata nje ya nchi. Bilionea Zawwiya amekuwa akitoa misaada isiyo na idadi kwa masikini wa nchi hii.
Hiyo mosi, lakini pili rais Mark Mwazilindi mwenyewe ni rafiki mkubwa sana wa Bilionea Zawwiya. Sote tunajua jinsi bilionea Zawwiya alivyochangia pesa nyingi kwa chama tawala katika uchaguzi uliomweka rais Mark madarakani. Mara kadhaa amekuwa akimsaidia rais Mark, chama na serikali yake katika kampeni mbalimbali za kitaifa, na hii imetengeneza urafiki ulioshiba kati yao. Hayo niliyoyasema na mengine ambayo sijayasema yanaleta ugumu sana kwa sisi kumkamata Bilionea Zawwiya. Rais Mark hawezi kuruhusu hilo litokee hata iweje. Hicho ulichokisema Hannan tulishakifikiria kwa upana wake tukiwa pamoja na Martin. Lakini pamoja na yote hayo tulifikia maamuzi kwamba ni wewe ndiye utakayetuletea Bilionea Zawwiya katika chumba cha mahojiano endapo itahitajika” Daniel alielezea kwa kirefu.
“Mmefikiria mimi ninaweza kufanya nini ili niweze kumleta bilionea Zawwiya katika chumba cha mahojiano?” Hannan aliuliza huku akimwangalia usoni Daniel.
“Njia tuliyoifikiria ni hii” Daniel alisema kisha akameza funda la mate, “Hannan unajua kwamba Bilionea Zawwiya ana mtoto mmoja tu wa kiume, anaitwa Seif. Bilionea Zawiya anampenda mtoto wake huyo kuliko kitu chochote kile hapa duniani. Kutokana na maelezo yangu ya awali ushafahamu kuna ugumu kiasi gani kumkamata Bilionea Zawwiya kwa kutumia vyombo vyetu vya dola. Tutazua taharuki kubwa sana, lakini tunaweza kumtumia Seif ili kumpata baba yake” Daniel alitoa ushauri wake.
“Bado sijakuelewa Daniel, mimi ninahusikaje hapo katika kumleta Bilionea Zawwiya katika chumba cha mahojiano kwa kumtumia Seif?” Hannan aliuliza kwa shauku kubwa.
“Ni hivi, tunaweza kumweka Seif katika himaya yetu kwa wewe kuingia katika maisha ya Seif. Hivyo tutamtumia Seif kumtia katika mikono yetu baba yake” Daniel alisema kwa uhakika.
“Bado sijakuelewa unamaanisha nini, Daniel?” Hannan alisema kwa mshangao.
“Njia ni moja tu kama tunataka tumpate Bilionea Zawwiya katika chumba chetu cha mahojiano, njia ni wewe kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na Seif....” Daniel aliacha kuongea na kumwangalia Hannan machoni.
Je nini kitatokea? LAKO JICHO!
Like & Comment & Share

Sent from my Infinix X655C using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA; TAHARUKI
Imeandikwa na Halfani Sudy
Simu 0652 212391

Hii ni sehemu ya Kumi na Nne

“Njia ni moja tu kama tunataka tumpate Bilionea Zawwiya katika chumba chetu cha mahojiano, njia ni wewe kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na Seif....” Daniel aliacha kuongea na kumwangalia Hannan machoni.
Ulipita ukimya wa sekunde saba baada ya Daniel kumwambia hayo maneno Hannan, Hannan alibaki kimya huku akimwangalia Daniel kwa macho ya ‘Sijakuelewa hata kidogo Daniel’.
“Ni ngumu sana hiyo Daniel, unajua Seif ameoa hivi karibuni, sioni namna rahisi ya kujipenyeza katika maisha ya kimapenzi kwa Seif katika kipindi hiki ambacho ndio kwanza anaifurahia ndoa yake changa” Hannan alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
“Hannan, pengine wewe mwenyewe hujijui vizuri uzuri ulionao, wewe u mzuri sana. Una uzuri ambao unaweza kumtingisha mwanaume yeyote yule rijali. Mimi ninaamini Seif yupo katika orodha ya wanaume rijali, hivyo itakuwa kazi rahisi sana kwako kama utaitumia vizuri karata yako ya uzuri. Ninaamini Seif atamsahau mtoto wa waziri Almas Fumbo kwa muda pindi tu utakapomuonesha kwamba unampenda na unahitaji kuwa na yeye” Daniel alimshawishi Hannan.
Hannan alitabasamu kutokana na maneno ya Daniel, kuambiwa yeye ni mwanamke mzuri haikuwa habari ngeni katika masikio yake, lakini ilikuwa habari ngeni kuambiwa maneno hayo na Daniel. Walijuana na Daniel na kufanya kazi pamoja kwa muda mrefu sana, lakini hakuna siku ambayo aliwahi kumuambia kwamba yeye ni mzuri. Ilikuwa ni kauli iliyoyafurahisha sana masikio yake, na bila kutegemea alijikuta amekubali kufanya kazi hii ngumu aliyopewa na Daniel.
“Sawa Daniel, nitafanya kama mlivyopanga wewe na Martin, tutamtumia Seif kutupeleka kwa baba yake” Hannan alisema kauli iliyomfurahisha sana Daniel.
“Nafurahi sana kwa kutukubalia ombi letu, nikwambie tu sasa tunaenda kuukata mzizi wa fitna, tunaenda kulifumbua fumbo lililofumbwa juu ya mizigo isiyoeleweka” Daniel alisema kwa furaha. Wakapeana mkono na Hannan ishara kwamba kazi ilikuwa imeanza.

Bilionea Zawiya alikuwa katika maktaba yake ya vitabu iliyokuwemo ndani ya jumba lake kubwa la kifahari huko Masaki. Mbele yake kulikuwa na vitabu vitatu vilivyotandazwa mbele ya meza yake. Vitabu viwili vilikuwa mbele ya kitabu kimoja kilichochukua umakini wa Bilionea Zawwiya. Pembeni ya meza aliyokuwepo kulikuwa na meza nyingine iliyobeba tarakilishi ambayo ilikuwa imewashwa, huku mbele yake kukiwa na shubaka kubwa lililojaa vitabu lukuki.
Bilionea Zawwiya alikuwa makini na kurasa ya mia mbili na tatu ya kitabu alichokuwa anakisoma. Ndani ya maktaba kulikuwa kimya, sauti pekee iliyokuwa inasikika ni mlio wa karatasi pindi tu pale atakapofunua kitabu kutoka kurasa moja kwenda kurasa nyingine. Miwani ya kusomea ya Bilionea Zawwiya ilikuwa imeyafunika macho yake mawili, miwani ikiyomsaidia kuyaona vizuri maneno na kusoma kwa utulivu mkubwa sana kitabu alichokuwa anakisoma. Akiwa katikati ya usomaji, simu yake maalum iliita. Mshtuko mdogo ulionekana katika sura yake baada ya kusikia mlio kutoka katika simu yake maalum. Aliiokota simu iliyokuwa imelala juu ya meza, akalisoma jina la mtu aliyekuwa anampigia simu.
‘GB’ Ndio jina lilivyosomeka katika kioo cha simu yake janja.
“Kuna nini GB?” Sauti nzito ya Bilionea Zawwiya iliuliza simuni.
“Mkuu, kuna taarifa mpya nataka nikupe, upo sehemu nzuri ya kuweza kuipokea?” Ginger Bites aliuliza.
“Unawea kunipa hiyo taarifa, nipo sehemu ambayo ninayoweza kuipokea “ Bilionea Zawwiya alisema kwa sauti yake nzito.
“Nimegundua kuwa kuna wasaliti miongoni mwetu” Ginger Bites alisema kwa uhakika.
“Ni nani hao?” Bilionea Zawwiya aliuliza.
“Martin na Robby wanatusaliti!” Ginger Bites alisema kwa uhakika.
“Umejuaje GB?” Bilionea Zawwiya aliuliza kwa sauti kubwa.
“Mkuu samahani kwa kusema hili, muda mrafu nilikuwa namtilia shaka Robby kuwa ni mtu aliyepandikizwa kwetu kwa ajili ya kupeleka taarifa zetu sehemu fulani. Nilianza kufanya uchunguzi wangu kimyakimya lakini siku zote sikuupata ushahidi wa kuthibitisha shaka yangu. Shaka yangu iliongezeka baada ya kuleta ombi lake kwetu la kumuingiza Martin kundini. Niliendelea kuwachunguza wote wawili bila ya wao wenyewe kujua. Baadae nilikuja kugundua kwamba Martin alikuwa ni afisa usalama wa Taifa na alikuwa anamtumia Robby ambaye ni ndugu yake wa damu kama mtoa taarifa kwake”
“Unasemaje GB?” Bilionea Zawwiya aliuliza kwa kuhamaki.
“Najua ni ngumu sana kwako Bosi kuamini, lakini huo ndio ukweli, na kwasasa nina ushahidi wote ambao nitakuletea hapo nyumbani kuthibitisha uchunguzi wangu.” Ginger Bites alisema.
“Hongera sana GB, umefanya kazi kubwa sana ambayo hakuna unachostahili zaidi ya zawadi kubwa sana. Nashukuru sana kwa kunipa taarifa hii kabla hao nyumbu hawajaleta madhara makubwa kwetu. Nategemea utakuja hapa jioni kuniletea huo ushahidi, lakini sisubiri hadi jioni kuchukua hatua, nitampa Meya wa Kimathi hizi taarifa kwaajili ya kuwakamata hao wasaliti. Kwa mara nyingine tena nasema ahsante sana kwa kazi kubwa ulioifanya, nategemea ujio wako hapa nyumbani jioni” Bilionea Zawiya alisema na kukata simu.
Alivyokata simu ya Ginger Bites, alimpigia simu Meya wa Kimathi. Baada ya salamu aliongea maneno nane tu...
“Martin na Robby wapelekwe katika Handaki la Siri” Kisha akakata simu kabla hata ya kujibiwa.
Bilionea Zawiya alirejea kukiinamia kitabu chake na kuendelea kukisoma kama hakijatokea kitu. Kitabu alichokuwa anakisoma kilikuwa kimeandikwa kwa lugha ya kingereza, kimeandikwa na mwandishi nguli wa Saikolojia kutoka nchini Uingereza anayeitwa Robert Hooks, jina la kitabu lilikuwa ni,
‘How to change the mind of the child to be a terrorist’

Shule ya msingi ya Vanilla ni miongoni mwa shule maarufu sana katika jiji la Dar es aalaam. Ingawa ilikuwa ni shule mpya lakini ufaulu mkubwa kwa wanafunzi wake wa darasa la nne na darasa la saba ulilifanya jina la shule hiyo lipae juu mithili ya tiara. Wazazi wengi waliwapeleka watoto wao katika shule hiyo kwakuwa watoto wengi walitamani kusoma katika shule hiyo. Kwa miaka mitatu mfululizo ilikuwa imeshika nafasi ya kwanza kwa wanafunzi wa darasa la saba kwa Tanzania nzima, huku wanafunzi wa darasa la nne wakishika nafasi ya kwanza kwa mara mbili mfululizo.
Ilikuwa ni shule iliyojitosheleza kimiundombinu, zana za kufundishia na walimu wa kutosha wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma. Nyota ya shule hiyo ilikuwa inang’ara mithili ya nyota nzuri ya asubuhi.
Siku ya jumatatu asubuhi, gari la shule ya Vanilla ilikuwa inawapeleka wanafunzi ishirini na tano shuleni, hii ni baada ya kuwakusanya wanafunzi hao majumbani kwao. Ndani ya gari kulikuwa na dereva, utingo na mlezi wa wanafunzi hao.
Wakati wakiwa katika maeneo ya Tegeta, mbele yao kulikuwa na magari mawili yaliyoziba barabara kuu huku madereva wa magari hayo wakiwa wanachungulia uvunguni mwa magari hayo. Dereva wa gari la Vanilla alivyoona hakuna pa kupita alisimamisha gari.
Ilichukua takribani dakika ishirini na tatu bado zile gari mbili zilizoziba njia hazikutoka barabarani. Foleni iliyoanza kama utani ilianza kuwa kubwa. Dereva wa gari ya shule ya Vanilla kuona zile gari zinachelewa kutoka pale barabarani alishuka ndani ya gari yake na kusogelea mahali ziliposimama zile gari mbili. Lilikuwa ni kosa la mwaka.............
Kilitokea kitendo cha ghafla ambacho hakikuweza kumpa muda wa kutafakari kwa yeyote yule aliyetaka kutafakari. Jamaa mmoja aliyekuwa amevaa nguo nyeusi na kofia kubwa nyeusi waliingia katika ile gari ya shule, sekunde ileile mtu mwingine ambaye alikuwa ameshika bastola mkononi aliingia katika ile gari kwa kutumia mlango wa kawaida. Watoto waliokuwa katika ile gari walianza kulia na kupiga kelele za kuomba msaada.
“Wote kimya, atakayethubutu kutoa sauti yake mbaya nampasua kichwa chake!” Yule jamaa aliyevaa nguo nyeusi alisema huku akiwaonesha wanafunzi ile bastola.
“Tuondoke!” Kisha akasema kumwambia yule aliyeingilia upande wa dereva. Dakika ileile gari moja iliyokuwa imeziba barabara ilisogea pembeni kulipisha lile gari la shule lipite. Safari ya kuelekea kusikojulikana ilianza.
Dereva wa gari la shule ya msingi Vanilla alibaki ameshika mikono yake yote miwili kichwani akiwa haamini kilichotokea. Hiyo ilikuwa ni saa kumi na mbili na nusu asubuhi.
Taarifa za kutekwa kwa gari la shule ya msingi Vanilla zilivuma mithili ya upepo wa kimbunga. Kutekwa kwa gari la wanafunzi ilikuwa ni habari mpya na ya kuogofya ambayo haikuwa imewahi kutokea katika historia ya jiji la Dar es salaam. Ingawa kila mmoja alisema lake lakini hakuna aliyekuwa anajua nini hasa dhamira ya watekaji hao.
Saa moja baadae, kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es salaam John Rondo alitokea mbele ya waandishi kuelezea kwa namna tukio la kutekwa kwa wanafunzi wa shule ya msingi Vannila lilivyotokea, huku akitoa rai kwa raia yeyote anayeweza kuwapa fununu juu ya utekaji huo kutoa taarifa katika kituo chochote cha Polisi kilichopo karibu yake, huku akitoa onyo kali sana kwa wote waliohusika na utekaji huo.
Wazazi wa watoto waliotekwa walikuwa katika simanzi kuu, haikuwa rahisi kwao kuvumilia tukio la kutekwa kwa watoto wao ambao haikujulikana wamepelekwa wapi?
Saa mbili baadae, mkuu wa jeshi la Polisi, IGP Felician Mwilenga alikuwa mbele ya vyombo vya habari kuwapa karipio kali kwa wote walihusika na utekaji huo, huku akiwaahidi kwamba ni bora wawaachie huru hao watoto wasio na hatia kwa maana hakuna pa kutokea.
Pamoja na vitisho vyote hivyo lakini jeshi la Polisi halikupata fununu yoyote kutoka kwa mtu yeyote juu ya mahali walipopelekwa watoto hao. Ilikuwa ni moja ya habari iliyomuogopesha kila mpenda amani nchini Tanzania.
Kutoka maeneo ya Tegeta jijini Dar es salaam, mahali lilipotokea tukio la kutekwa kwa watoto wa shule ya msingi Vanilla, taarifa za utekaji huo zikasafiri kwa kasi na kufika hadi Mikocheni, nyumbani kwa mpelelezi mahiri nchini Tanzania Daniel Mwaseba.
Yalikuwa majira ya saa moja na dakika tano wakati Daniel akitoka bafuni kuoga baada ya kutumia zaidi ya saa mbili akifanya mazoezi ya viungo. Alipofika tu chumbani, simu yake iliita, na mtu aliyekuwa anapiga simu yake alikuwa ni bosi wake katika kitengo cha usalama wa Taifa, DGIS Simon Madoshi, ambao watu wa kitengo hiko walizoea kumwita kwa jina la Chifu. Daniel alipoona tu kuwa simu inatoka kwa Chifu akajua kwamba kuna jambo.
“Hallo mkuu” Daniel aliita simuni huku akijifuta maji kwa taulo lake jeupe.
“Najua umesikia kilichotokea Daniel” Chifu alisema simuni kwa sauti nzito bila ya kuijibu salamu ya Daniel.
“Sielewi unazungumzia nini Chifu” Daniel alisema kwa sauti iliyokuwa inaashiria kuwa alikuwa haelewi chochote.
“Usinambie kwamba hujasikiliza taarifa ya habari na wala kuingia katika mitandao ya kijamii?” Chifu aliuliza kwa mshangao.
“Huo ndio ukweli wenyewe Chifu, nimeamka tu na kuingia katika chumba cha mazoezi, hapa ninatoka kuoga ndio simu inaita” Daniel alisema.
“Daniel kuna taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa kwamba gari la wanafunzi wa shule ya msingi Vanilla limetekwa leo asubuhi. Hadi sasa haieleweki ni nani aliyefanya utekaji huo na ana malengo gani? Ni zaidi ya saa mbili tangu tukio hilo litokee lakini haieleweki watoto hao wamepelekwa wapi?” Chifu alimuelezea kwa kirefu Daniel.
“Daah ni tukio la kwanza la utekaji wa namna hii kutokea katika nchi yetu, wameliteka sehemu gani hilo gari?” Daniel aliuliza huku mwili wake ukimsisimka.
“Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda Rondo gari limetekwa maeneo ya Tegeta, ndio lilikuwa limetoka kuwakusanya wanafunzi kwa ajili ya kuwapeleka shuleni” Chifu alielezea.
“Aiseee” Daniel alishangaa.
“Hilo mosi Daniel, ingawa ndani ya tukio hilo kuna kitu kinachoiogopesha sana serikali, inasemekana kuwa miongoni mwa watoto waliotekwa ni mtoto wa mwenyekiti wa chama cha upinzani cha CGN...”
“Joash Mkubwa!” Daniel alimalizia kwa sauti kubwa.
“Ndio”
“Daah lazima tufanye kitu kuhakikisha hao watoto wanapatikana haraka iwezekenavyo, namjua Joash Mkubwa, atalifanya tukio hili ni fimbo kali ya kuichapia serikali ya rais Mark” Daniel alisema.
“Hiyo ndio hofu yangu, na hofu hiyo anayo hata rais Mark Mwazilindi, nimetoka kuongea naye muda si mrefu, ameipa idara yetu kazi ya kuhakikisha watoto wote wa shule ya msingi Vanilla wanapatikana haraka tena wakiwa salama salmini, hataki kabisa kuona serikali yake inachafuka kwa tukio hili”
“Sawa mkuu, nitahakikisha tunawapata watoto wetu wakiwa hai” Daniel alisema kwa kujiamini.

Je nini kitatokea? LAKO JICHO.

Sent from my Infinix X655C using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA: TAHARUKI
Imeandikwa na HALFANI SUDY
SIMU 0652 212391

Hii ni Sehemu ya Kumi na Tano

“Sawa Daniel, hakikisha unampigia simu mwenzio kuhakikisha kwamba yupo salama” Chifu alisema kwa kifupi na kukata simu.
Alipomaliza kuongea kwa simu na Chifu, Daniel aliitafuta namba ya Martin katika simu yake na kuipiga, ilikuwa kama alivyosema Chifu, Martin alikuwa hapatikani hewani. Akaitafuta namba ya Hannan na kuipiga.

“Habari za asubuhi Daniel” Hannan alisalimia baada ya kupokea simu ya Daniel.

“Nzuri Hannan, najua ushasikia mambo yaliyotokea asubuhi ya leo hapa mjini......”

“Nimesikia Daniel, si kuhusu kutekwa kwa gari la wanafunzi wa shule ya msingi Vanilla?” Hannan aliuliza kabla Daniel hajamwambia ni kitu gani alichokuwa anamaanisha.

“Upo sahihi, ni kuhusu kutekwa kwa wanafunzi wa shule ya msingi Vanilla. Sasa Hannan tumepewa sisi kazi ya kuhakikisha watoto wote wanarudi salama majumbani mwao hiyo, tena wakiwa salama” Daniel alisema.

“Sawa Daniel, hata mimi nilikuwa natamani kazi hii ipewe idara yetu. Nillipata hisia mbaya sana pindi tu nilisikia tukio hili katika vyombo vya habari. Kwa kupewa idara yetu ninaamini tutaifanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa sana na tutaikamilisha kwa wakati” Hannan alisema bila ya wasiwasi wowote.

“Halafu kitu kingine Hannan, simu ya Martin haipatikani hewani tangu jana usiku. Nitakutumia namba yake uichunguze ili tujue mara ya mwisho ilikuwa hewani akiwa wapi? Chifu ana wasiwasi sana juu ya usalama wa Martin” Daniel alisema.

“Sawa Daniel, nitumie namba ya Martin. Nitajaribu kuangalia alikuwa wapi mara ya mwisho. Bila shaka hapo ndipo patakuwa sehemu pa kuanzia kuchunguza ni kitu kimemtokea Martin”

“Sawa, ninakutumia sasahivi. Ukimaliza kazi hiyo ninaomba tukutane katika mgahawa wa Cream saa tatu asubuhi, tuone tunaanzia wapi kuwarudisha wanafunzi wa shule ya msingi ya Vanilla” Daniel alimwambia Hannan.

“Sawa Daniel, nitakuwa katika mgahawa wa Cream muda huo” Hannan alikubali.

“Sawa” Daniel alisema na kukata simu.

Daniel alijifuta maji ingawa yalikuwa yameshaanza kukaukia mwilini. Akalisogelea kabati la nguo na kulifungua. Akachagua suruali ya dengrizi ya rangi ya samawati na fulana nyeusi iliyokuwa na mchoro wa nyota nyeupe kwa mbele. Chini alivaa raba nyeusi ambazo nazo zilikuwa na nembo ya nyota tano kwa pembeni, kichwani alivaa kofia aina ya kapelo ya rangi nyeusi pia, mbele ikiwa na mchoro wa mbwa mdogo. Alilifunga kabati na kwenda katika droo ndogo iliyoungana na kitanda, akaifungua na kutoa bastola mbili, akazipachika katika pande mbili za kiuno chake. Akauokota funguo wa gari ulikuwa umelala juu ya kiti cha mbao na kutoka nje. Nje ya nyumba akaingia katika gari aina ya Alterza ya rangi nyeusi na kutoka nayo nje ya nyumba yake.

Saa tatu kamili ilimkuta katika mgahawa wa Cream uliopo katikati ya jiji la Dar es salaam. Alimkuta Hannan akiwa amechagua meza moja iliyokuwa pembezoni kabisa mwa mgahawa wa Cream. Hapo ndipo mahali hukutana mara zote Daniel anapomwambia wakutane katika mgahawa huo.

Juu ya meza, iliyotengenezwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia mti wa mpingo, kulikuwa na bilauri iliyokuwa na sharubati ya chungwa ndani yake. Hannan alikuwa anauvuta mrija ulioingizwa ndani ya sharubati hiyo kwa madaha.

Hannan alikuwa amevaa suruali ya dengrizi ya rangi ya nyeusi. Juu, alivaa fulana ya rangi ya pinki yenye vimdoli viwili vya rangi nyeupe. Chini, alikuwa amevaa raba nyepesi za rangi nyeupe. Alikuwa ana mwili wa kike mdogomdogo ambao ungekufanya umhusudu sana kwa jinsi alivyoweza kuutunza vyema.
Alivuta tena funda la sharubati ya chungwa, akauangalia mkono wake wa kushoto uliokuwa umevaa saa kutoka kampuni ya Casio. Ilikuwa ni saa tatu na dakika mbili, dakika mbili zaidi ya muda waliokubaliana na Daniel. Aliangaza macho yake katika mlango wa kuingilia, ndipo alipomuona Daniel akiingia ndani ya mgahawa wa Cream bila ya wasiwasi wowote. Hannan alitabasamu huku akimwangalia Daniel akielekea katika aliyokaa.

“Karibu sana Daniel, kwa mara ya kwanza leo nimekuwahi” Hannan alisema huku akisimama na kumkumbatia Daniel.

“Ahsante sana Hannan, na hongera kwa mara ya kwanza kunitangulia katika miadi” Daniel alisema huku akicheka.

“Umependeza sana leo..” Hannan alisema wakati wakiwa wameachiana na Daniel.

“Nawe umependeza pia...” Daniel alisema huku akikaa kwenye kiti.

“Ahsante Daniel. Tuache hayo tuelekee moja kwa moja katika kazi iliyopo mbele yetu. Nilifanikiwa kupekua na kufanikiwa kujua mahali pa mwisho ilipokuwa hewani simu ya Martin...” Hannan alisema.

“ilikuwa sehemu gani?” Daniel aliuliza kwa pupa.

“Kusema kweli yametokea majibu ya kushangaza sana, kwa mara ya mwisho simu ya Martin ilikuwa hewani saa mbili zilizopita katika jiji la Paris huko nchini Ufaransa”

“Unasemaje?” Daniel aliuliza kwa nguvu.

“Ndio majibu yaliyokuja, nilijaribu kumpigia simu rafiki yangu anayefanya kazi katika mtandao wa simu wa Teltel ili naye ajaribu kuitafuta namba hiyo. Naye alikuja na majibu hayohayo” Hannan alisema.

“Imewezekana vipi hiyo Hannan?” Daniel aliuliza.

“Kinachonijia katika akili yangu sio kitu kizuri kwa Martin, ninaomba unisamehe kwa kusema hivi, ila ninahisi Martin hayupo sehemu salam” Hannan alisema huku sauti yake ikiwa imeambatana na hofu.

Daniel alibaki akimwangalia tu Hannan, alikubaliana kwa asilimia zote na maneno ya Hannan lakini hakuwa tayari yawe ndio ukweli. Kwasasa alikuwa anamhitaji Martin kuliko wakati wowote ule. Alikuwa anamuhitaji katika kazi kubwa iliyopo mbele yake ya kuhakikisha wanawaokoa watoto waliotekwa wa shule ya msingi Vanilla. Alikuwa anamhitaji kwaajili ya kumalizia walichokianza kuhusu mzigo usioeleweka wa Bilionea Zawiya na wizi mkubwa wa madini ya Tanzanite, hivyo hakutaka kabisa kukubaliana na ukweli wa taarifa kuwa Martin hayupo sehemu salama kwa sasa.

“Unawaza nini Daniel?” Hannan alimuuliza Daniel alipomuona akiwa amezama katika dimbwi la fikra.

“Kauli yako kuwa Martin hayupo sehemu salama imeniogopesha sana Hannan. Katika vitu ambavyo nitajilaumu siku zote za maisha yangu ni kuona Martin anaingia katika hatari bila ya kufanya juhudi yoyote ile ya kumuokoa”

“Ninaelewa unavyojisikia Daniel, ninaelewa hata unachotaka kufanya kwaajili ya Martin. Lakini hauwezi kufanya unachowaza kufanya kwa wakati huu. Mbele yetu tuna kazi ngumu na kubwa sana za kufanya” Hannan alisema huku akimwangalia Daniel.

“Umejua kuwa ninafikiria kwenda nchini Kenya kumuokoa Martin?” Daniel aliuliza kwa mshangao.

“Ndio, nimejua ulikuwa unafikiria hivyo, lakini itakuwa ni ngumu kwa wewe kwenda nchini Kenya huku ukiacha jukumu ulilopewa na Chifu la kuwatafuta watoto waliotekwa na watu wasiojulikana. Ninakushauri tulimalize hili kwanza. Lakini hata hivyo haya ni mawazo yetu tu kuwa Martin yupo katika matatizo, pengine yupo sehemu fulani akiwa salama salmin” Hannan alisema.

“Nimekuelewa Hannan. Sasa yatupasa kutafuta pa kuanzia katika safari ya kuwaokoa watoto wetu waliotekwa. Nilipoongea na Chifu aliniambia kuwa idara yetu imepewa dhamana ya kushughulikia jambo hili lakini kwa kushirikiana na jeshi la Polisi, pia amenambia kuwa miongoni mwa watoto waliotekwa ni mtoto wa Joash Mkubwa”

“Mtoto wa Joash Mkubwa naye ametekwa?” Hannan aliuliza huku sura yake ikiwa katika mshtuko mkubwa.

“Ndio Hannan, na kutekwa kwa mtoto wa Joash Mkubwa kumeongeza hofu sana kwa maana hatujui yule jamaa ataibuka kwa mtindo gani. Lakini tujue tu kwamba kwa mtindo wowote ule atakaoibuka nao utakuwa sio salama kwa serikali ya rais Mark. Yatupasa kuhakikisha jambo hili linamalizika wakati huuhuu ambao Joash Mkubwa akitafuta mtindo wa kuja nao” Daniel alielezea kwa kirefu.

“Nimekuelewa Daniel, sasa mimi nilipiga hatua kidogo baada ya kusikia kuwa watoto wa shule ya msingi Vanilla wametekwa. Nilichugundua katika uchunguzi wangu mdogo ni kuwa, ndani ya gari lililotekwa kulikuwa na watu ishirini na saba ingawa lilitakiwa liwe na watu ishirini na nane; watoto wadogo ishirini na tano, dereva, utingo na msaidizi wa watoto. Ila tukio lilivyotokea dereva aliachwa wakati alipotoka garini kwenda kuziangalia gari mbili zilizokuwa zimeharibika barabarani na kuziba njia. Hivyo mpaka sasa jumla ya watu ishirini na saba walitekwa na hawajulikani walipo. Tuna sehemu mbili ambazo tunaweza kuzitumia kwa kuanzia uchunguzi wetu, kwanza kwa kwenda kumhoji dereva wa gari ya watoto ambaye inasemakana yupo katika kituo kikuu cha Polisi, kwa ajili ya mahojiano na jeshi la Polisi. Sehemu ya pili katika uchunguzi huu ni kuzichunguza hizo gari mbili zilizoziba njia, bila shaka zinahusika moja kwa moja katika tukio la utekaji” Hannan alitoa maoni yake.

“Umewaza vizuri sana Hannan. Hayo maeneo mawili uliyoyasema ni ya kuyazingatia sana, kwa huyo dereva na hizo gari mbili zilizoziba njia. Sasa ninaomba tugawane majukumu, wewe ufuatilie taarifa zote kuhusu huyo dereva, kabla hujaenda kufanya naye mahojiano huko Polisi. Mimi nitaenda eneo lilipotokea tukio kujua zaidi kuhusu hizo gari mbili. Ninaomba tufanye kazi hii kwa uharaka mkubwa lakini bila ya kupoteza umakini. Tukutane nyumbani kwangu baada ya saa mbili kupeana taarifa juu ya tuliyoyapata. Endapo mmoja wetu akichelewa kufika sehemu ya kukutania baada ya muda tuliokubaliana basi tujue kuna tatizo limetokea kwake, na lazima tutafute namna ya kumsaidia”

“Nimekuelewa Daniel, nitafanya kila kitu kama ulivyoagiza, nina imani tunaenda kufanikisha hili na watoto wetu tutawaokoa wakiwa salama” Hannan alisema.

Baada ya maongezi yaliyodumu kwa takriban dakika kumi na tano, waliagana kwenda kufanya kazi waliyopangiana. Hiyo ilikuwa saa tatu na nusu.

Hali ilikuwa ya majonzi makubwa sana katika nyumba moja huko Mbagala Kilungule. Familia ya mzee Mboto ilikuwa katika majonzi makubwa sana baada ya mtoto wao mkubwa wa kiume kuingia matatani na vyombo vya dola.

Saa nne na dakika kumi asubuhi, gari ndogo aina ya Toyota Mark X iliegeshwa mbele ya nyumba hiyo. Watu wachache waliokuwa wamekaa katika kibaraza cha nyumba ya mzee Mboto, macho yao yalielekezwa barabarani ili kumuona mtu atakayeshuka katika gari hiyo. Ingawa kwa siku hiyo, kuwasili kwa magari ya aina mbalimbali katika nyumba hiyo halikuwa jambo la kushangaza, na hii ilitokana na mtoto mkubwa wa nyumba hii kukamatwa baada ya gari alilokuwa anaendeshwa kutekwa na watu wasiojulikana. Hivyo mara kwa mara yalikuwa yanakuja magari mbalimbali kwaajili ya kumpa pole dereva mwenzao.

Raba nyeusi iligusa ardhi ya Kilungule, kabla ya mwili wa dereva wa gari hilo dogo kutoka garini. Dereva wa gari alikuwa mwanamke mrembo, kwa kumkadiria alikuwa hazidi hata miaka ishirini na tano. Kadirio la umri wake lilithibitishwa na umbo lake dogo. Mwanamke alifunga mlango wa gari yake na moja kwa moja alielekea katika nyumba ya mzee Mboto.

“Habari zenu wakubwa, shikamoni” Mwanamke alisalimia watu wote kwa ujumla.

Wengine waliitikia salamu ya yule mwanamke, huku wengine wakibaki wakimtolea macho mwanamke yule mrembo.

“Samahanini kwa kuwavamia bila ya taarifa” Mwanamke alianza kwa kuomba radhi, ”Ninaitwa Hannan nilikuwa nina shida na mwenyeji wa nyumba hii”

“Karibu sana, mimi ndio mwenyeji wa nyumba hii” Mzee mmoja wa makamo alisema kwa sauti ya huzuni huku akimwangalia Hannan.

“Nafurahi kukufahamu mzee, samahani ninaomba tuongee pembeni kama inawezekana” Hannan alisema kwa kujiamini.
Mzee Mboto alitoka katikati ya kundi la watu na kuelekea nyuma ya nyumba, Hannan naye alimfuata kwa nyuma. Watu wengine wote macho yao yalielekea kule walipoelekea mzee Mboto na Hannan.

“Samahani mzee kwa kukutoa mahali pale, kama nilivyojitambulisha awali, mimi ninaitwa Hannan, ni afisa wa jeshi la Polisi kutoka idara maalum. Nimekuja hapa kwa ajili ya kukuhoji machache kuhusu dereva wa gari la shule ya msingi Vanilla ambaye nimeambiwa anaishi hapa” Hannan alisema huku akinyoosha kitambulisho chake alichokuwa amekishika mkononi.
Mzee Mboto alimwangalia Hannan kwa macho ya uwoga kisha akasema, “Karibu sana binti yangu, nadhani hapa sio sehemu sahihi sana ya kunihoji, tungeenda sebuleni nadhani ingefaa zaidi” Mzee Mboto alisema bila ya kufanya jitihada zozote za kukiangalia kile kitambulisho alichokishika mkononi Hannan.

“Usiwe na wasiwasi, hata hapa patafaa, nina maswali machache tu ambayo ninaweza kukuuliza nawe ukanijibu hapahapa” Hannan alisema huku akimwamgalia machoni mzee Mboto.

“Sawa, karibu binti yangu”

Hannan aliingiza mkono wake katika mfuko wake wa suruali na kuwasha kifaa cha kurekodia sauti, aliporidhika kuwa kimeanza kurekodi aliuliza swali, “ Ninaomba unitajie majina yako matatu, kabila na uhusiano wako na dereva wa gari ya shule ya msingi Vanilla lililotekwa leo”

“Kwa majina ninaitwa John Joseph Mboto, kabila langu ni mmatumbi kutoka huko Kilwa Kipatimu, katika mkoa wa Lindi uliopo kusini mwa nchi hii. Erick ni mtoto wangu pekee wa kiume” Mzee Mboto alijibu.

“Una watoto wengine zaidi ya Erick?” Hannan aliuliza.

“Ndio, nina watoto wa kike sita, na mtoto wa kiume mmoja, ambaye ndiye Erick”

“Erick anaishi hapa?”

“Hapa ndio nyumbani kwa Erick, mimi ninaishi nyumba ile pale” Mzee Mboto alisema huku akiionesha kwa kidole cha shahada nyumba iliyokuwa mbele ya nyumba ya Erick.

“Samahani mzee kwa kuuchukua muda wako, najua upo katika kipindi cha majonzi baada ya mwanao kuingia katika matatizo, nikwambie tu haya yatapita endapo ukweli utajulikana, Ninaomba unipe nafasi ya kunijibu maswali yangu kadhaa ambayo bila shaka yatakuwa ni mwanga kuwajua wahalifu waliowateka wanafunzi na mwanao Erick kuwa huru”

“Ahsante sana binti yangu, mimi nipo tayari kutoa ushirikiano wowote ule ilimradi tu Erick wangu awe huru” Mzee Mboto alisema kwa sauti ya majonzi.

“Kwanza ninataka kujua kuhusu Erick, umri wake, familia yake na mambo mengine yanayofanana na hayo”

“Erick ana umri wa miaka thelathini na tano., ameoa na ana watoto wawili. Yeye na familia yake wanakaa katika ile nyumba uliyotukuta, amejenga mwenyewe ile nyumba kwa mshahara anaolipwa huko kazini kwake. Erick ni kijana mkimya sana, ninaweza sema tabia ya ukimya alizaliwa nayo kwa maana yupo hivyo tangu akiwa mtoto. Ukimya wake umemfanya awe na marafiki wachache sana, lakini rafiki yake mkubwa ni John Dukuu. Erick na John ni marafiki walioshibana haswa kiasi kwamba Erick alivyopata hii kazi iliyomletea matatizo alimfanyia mpango John, na kwa bahati nzuri naye aliajiriwa kama utingo katika gari analoendesha Erick. Erick anaipenda sana familia yake pengine kuliko kitu chochote kile. Hayo ni machache ambayo ninaweza kuelezea kuhusu mwanangu” Mzee Mboto alisema.

“Je Erick alishawahi kufanya kosa lolote lile ambalo likampeleka katika vyombo vya dola?” Hannan aliuliza.

“Kwakweli sikumbuki. Sikumbuki kabisa kama Erick alishawahi kupelekwa kituoni kwa kufanya kosa lolote lile. Hajawahi kufanya kosa lolote, na leo ndio kwa mara ya kwanza anapelekwa kituoni” Mzee Mboto alijibu.

“Sawa mzee Mboto, nashukuru sana kwa ushirikiano wako, ninaomba twende ndani, nina maswali kidogo ya kumuuliza mke wa Erick” Hannan alisema.

“Sawa binti yangu, ila ninaomba sana ujitahidi ili kumsaidia Erick, anateseka Polisi bila ya hatia” Mzee Mboto aliomboleza kwa sauti yake ya kizee.

“Usiwe na wasiwasi baba yangu. Endapo mtanipa nafasi ya kuweza kupata fununu juu ya waliowateka wanafunzi wa shule ya msingi Vanilla, basi ninakuahidi Erick atakuwa huru na kuendelea na majukumu yake”

Walitoka kule pembezoni mwa nyumba na kuelekea ndani, sebuleni, waliwakuta wakina mama wanne.

“Mama Adrian, kuna mgeni wako hapa” Mzee Mboto alisema huku akimwangalia mwanamke mmoja aliyekuwa amejifunga kanga huku akiwa amembeba mtoto mdogo mgongoni.

“Sawa baba, karibu sana mgeni” Mama Adrian alisema huku akifanya jitihada za kunyanyuka katika kochi la mbao.
Mama Adrian alifuata korido ndefu huku Hannan akifuata kwa nyuma. Huku akiwa anatembea macho ya Hannan yalifanya kazi ya kuzunguka huku na kule kutafuta chochote kile kitakachomsaidia katika uchunguzi wake. Hadi mama Adrian anasimama, Hannan hakuwa ameona chochote kile.

“Karibu sana mgeni” Mama Adrian alisema huku akimgeukia Hannan, alikuwa amesimama mwisho kabisa wa ile nyumba yenye korido ndefu.

“Samahani dada, mimi ninaitwa Hannan, ni askari wa jeshi la Polisi kutoka idara maalum. Nipo hapa kukuhoji mambo machache ambayo yatatusaidia katika kesi inayomkabili mumeo” Hannan alisema huku akimuonesha kitambulisho chake cha kazi alichokuwa amekishika kwa mkono wake wa kulia.

“Karibu sana” Mama Adrian alisema huku macho yake mekundu yakikiangalia kile kitambulisho alichokishika Hannan.

“Bila shaka Erick ni mumeo?”

“Ndio”

“Mna watoto wawili?”

“Ndio”

“Adrian na nani?”

“Adrian na Adriana”

“Mlioana mwaka gani?”

“Miaka mitano sasa imepita?”

“Unamjua rafiki mkubwa wa mumeo?”

“Ndio”

“Anaitwa nani?”

“John”

“Erick ana rafiki mwingine mkubwa zaidi ya John?”

“Hapana”

“Kwa siku za hivi karibuni Erick hajaanzisha urafiki na mtu mwengine yeyote?”

Mama Adrian alisita baada ya kusikia swali hilo, alimwangalia Hannan kwa macho ya mshangao kisha akajibu,”Alianzisha, lakini sidhani kama atakuwa anahusika na ...........”

“Anaitwa nani?” Hannan alimkatisha mama Adrian.

“Mume wangu alinitambulisha jina lake lakini nimelisahau”

“Alikuwa yupoje?” Hannan aliuliza huku akitoa karatasi na kalamu mfukoni kwake. Alikandamizia ukutani na kuanza kuchora kufuatana na maelezo ya mama Adrian.

“Alikuwa mrefu wastani, ana rangi ya maji ya kunde, sura yake ya duara yenye macho makubwa. Alikuwa na ndevu nyingi alizozichonga kwa mtindo wa O. Pamoja kwamba hakuwa mrefu sana lakini alikuwa na umbo lililojazia kama wabeba vyuma. Ninachokumbuka kingiiine hakuwa na nywele hata moja kichwani” Mama Adrian alielezea mwonekano wa rafiki mpya wa Erick.

“Anafanana na huyu?” Hannan alisema huku akimuonesha mama Adrian picha aliyokuwa ameichora baada ya maelezo ya mama Adrian.

“Ndiye mwenyewe!” Mama Adrian aling’aka kwa sauti kubwa huku macho yake yakionesha uwoga mkubwa. Hannan alimchora vilevile rafiki mpya wa Erick kutokana na maelezo ya mama Adrian.

“Huyu rafiki mpya akija walikuwa wanaongea nini na mumeo?”

“Kusema ukweli mimi hawakunihusisha katika mazungumzo yao, na ilionekana kuwa walikuwa hawataki hata kidogo nisikie walichokuwa wanakizungumza, maana mara kadhaa walikuwa wananyamaza kimya nikikaribia walipo”

“Hakuna neno lolote lile ulilowahi kulisikia wakilitaja katika mazungumzo yao?”

“Kwakweli hakuna” Mama Adrian alisema baada ya kuwaza kidogo.

“Vipi tabia ya Erick ilibaki ileile hata baada ya kukutana na huyo mgeni wake mpya?”

Mama Adrian alionesha mshangao mkubwa kuliko wa awali, alimwangalia Hannan huku akimshangaa, kisha alijibu kwa sauti ya kuchoka,

“Tabia ya Erick ilibadilika....”

“Ilikuwaje?”

“Kiasili mume wangu ni mkimya sana. Tabia ambayo kila mmoja anaijua kwamba anayo, lakini baaada ya kuanza kuja yule mgeni tabia ya ukimya ya Erick iliongezeka maradufu. Mara kadhaa nilimuuliza kama ana matatizo kutokana na mabadiliko hayo ya tabia lakini alisema kuwa hakuwa na tatizo”

“Amekuja hapa nyumbani kama mara ngapi huyo mgeni?”

“Mmmh amekuja kama mara tano au sita”

“Unakumbuka lini ilikuwa mara ya mwisho kuja hapa?”

“Jana usiku” Mama Adrian alijibu bila ya kufikiria.

“Amekuja tena baada ya haya matatizo yaliyompata mumeo?”

“Hajaja, pengine hajapata taarifa kama Erick yupo katika matatizo”

“Sawa, ninashukuru sana kwa ushirikiano wako. Ninaomba namba yako ya simu ili niweze kukupigia endapo kutakuwa na chochote cha ziada nitakachokitaka kutoka kwako” Hannan alisema huku akimpa simu yake mama Adrian.

Mama Adrian alichukua simu ya Hannan na kuandika namba yake ya simu, kisha alimrejeshea simu yake.

“Kwa usalama wa mumeo usimwambie mtu mwingine yeyote kuhusu huyo rafiki mpya wa mumeo” Hannan alisema wakati akiichukua simu yake.

Walirejea tena sebuleni, Hannan aliwaaga wale kina mama waliokuwa pale sebuleni ambao kwa sasa walikuwa wameongezeka, akaenda barazani na kumuaga mzee Mboto, kisha alienda kwenye gari yake, akawasha na kuondoka.
Kutoka Mbagala Kilungule alienda kusimamisha gari yake katikati ya uwanja wa Mbagala Zakheim. Aliitoa ile karatasi yenye picha ya rafiki mpya wa Erick, akatoa simu yake mfukoni na kwenda upande wa kamera, akaipiga picha ile picha. Kisha akaiingiza katika mfumo maalum wa utambuzi ili kumtambua mtu aliyopo katika ile picha. Mfumo ulianza kuzunguka.

‘Ginger Bites’ Ndio jina lililotokea chini ya picha ile, huku picha zingine mbili za huyo Ginger Bites zikionekana kwa chini.

“Ginger Bites!” Hannan alisema kwa sauti kubwa. “Ulikuwa unafuata nini nyumbani kwa Erick?” Hannan alijiuliza huku akiliingiza jina la Ginger Bites katika mfumo maalum wa kuchunguza kazi za watu.

“Hisia zangu zinaniambia kuwa haukuwa wa bure urafiki wa ghafla wa Ginger Bites na Erick” Hannan aliwaza wakati mfumo ukitafuta taarifa zaidi kuhusu Ginger Bites

Hisia za Hannan zimemuhisi vibaya mtu anayeitwa Ginger Bites, je hisia za kwako zimemuhisi vipi Ginger Bites? Tuwe wote katika mwendelezo wa TAHARUKI kutoka kwa mwandishi HALFANI SUDY.

Sent from my Infinix X655C using JamiiForums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom