Riwaya: Sala ya Sarah

Riwaya: Sala ya Sarah

RIWAYA : SALA YA SARAH

MTUNZI : ALEX KILEO

SEHEMU YA HAMSINI NA NANE.

ENDELEA..................

Trigger alitoka mpaka nje ya hospitali na kuingia kwenye gari lake, akawasha na kuondoka.

Strategic alikuwa akishuhudua hayo yote, akaichukua simu yake na kumpigia Vin,

"Trigger ndio anatoka muda huu" Strategic aliongea,

"yupo peke yake?" Vin aliuliza,

"ndio yupo peke yake, ila mkononi ameshika bahasha" Strategic aliongea,

"wakati akiingia ulimuona nayo hiyo bahasha?" Vin aliuliza,

"hapana" Strategic alijibu,

"poa, nipo njiani nakuja" Vin aliongea na kukata simu.

Strategic akaendelea kukaa eneo lile huku akiwa makini sana kuangalia watu wanaotoka na kuingia.

********

Dada wa mapokezi wa eneo la hospital ndio alikuwa mtu wa kwanza kupata mshangao kwa kuwa hakumuona Dokta akitoka wakati muda wake wa kutoka ulikuwa umefika, na kawaida ya huyu Dokta uwa hachelewi kutoka hata kwa dakika, muda ukifika uondoka hapo hapo.

"Lydia, mbona leo Dokta amechelewa kutoka, au ana kazi?" Dada wa mapokezi alimuuliza mwenzake,

"kumbe bado hajatoka? Ila atakuwa ameshatoka bwana, yule mzee hawezi kuwepo mpaka muda huu" Mwenzake alijibu huku akiwa hana uhakika,

"bado bwana, si angepita kusaini hapa, mbona sioni sahihi yake? au leo amepitiwa?" Dada wa mapokezi alimbishia mwenzake huku akifungua kitabu cha maudhurio ya wafanyakazi,

"tatizo lako Anita wewe mbishi, ngoja nikuhakikishie" Mwenzake aliongea huku akielekea kwenye mlango wa Dokta, alipofika aligonga hodi ila hakujibiwa,

"yupo?" Dada wa mapokezi aliuliza,

"nagonga hodi sijibiwi" Mwenzake alijibu huku akirudia tena kupiga hodi,

"ebu sukuma mlango" Dada wa mapokezi alimshauri mwenzake ambaye nae alikubaliana na ushauri huo, akasukuma mlango na kutupa macho kwenye kiti cha Dokta ila hakumuona,

"si nilisema? Ameondoka" Mwenzake alipaza sauti kumuelekea dada wa mapokezi,

"basi leo kapitiwa, maana hata mlango uwa ahachagi wazi pindi akiondoka" Dada wa mapokezi aliongea, ila mwenzake hakumsikia, akili yake ilikuwa kwenye michilizi ya damu iliyokuwa ikionekana chini ya meza, akainama na kuchungulia, akauona mwili wa Dokta ukiwa umelala sakafuni na damu ikiwa imetapakaa, akapiga kelele na kumfanya mwenzake ashtuke, nae akaungana na mwenzie kwenda kushuhudia hicho kitu kilichomfanya mwenzake apige kelele, nae baada ya kuoneshwa akajikuta anapiga kelele na kufanya baadhi ya wagonjwa na wafanyakazi wa ile hospitali kujaa mlangoni ili nao waweze kuona ni kipi kimetokea kwenye chumba hicho cha Dokta.

*****************

Vin alifika eneo la hospital na kuegesha gari yake, kisha akatelemka na kuanza kuelekea ndani ya jengo la hospitali, alipofika usawa ilipo gari ya Strategic, Vin alimuoneshea ishara ya dole gumba na kumfanya Strategic atabasamu.

Vin akaingia ndani ya jengo la hospitali, ila alikuta hali tofauti, alikuta yule daktari aliyemchukua vipimo siku iliyopita akiwa amewekwa kwenye kitanda cha matairi na kufunikwa shuka mwili mzima, kwa maana hiyo alikuwa amekufa. Baadhi ya watu na wafanyakazi wengine wa ile hospitali walikuwa wakilia kwa uchungu, Vin akaonekana kuchanganyikiwa kidogo, akaelekea ilipo ofisi ya mapokezi na kuwakuta wadada wawili wakiwa na macho mekundu kuashiria walikuwa wakilia muda mfupi uliopita,

"poleni" Vin aliongea kwa upole,

"asante" wale wadada walijibu kwa pamoja,

"ni kitu gani kimetokea?" Vin aliuliza,

"hakuna anayeyajua, yaani tumekuta Dokta amepigwa tu risasi" Dada wa mapokezi alijibu,

"kwa hiyo huduma zimesitishwa?" Vin aliuliza,

"ulikuwa na shida gani?" Dada wa mapokezi alimuuliza,

"nimekuja kuchukua majibu yangu, nilipima jana" Vin aliongea,

"nenda katika chumba cha Dokta uliyempa maelezo" Dada wa mapokezi aliongea,

"chumba nadhani ndio hicho ambacho huyo Dokta aliyepata matatizo" Vin alijibu,

"kwa hapo itabidi usubiri utaratibu mwingine, maana polisi wamezuia watu kuingia kwenye kile chumba mpaka uchunguzi ukamilike, na isitoshe kila majibu ya wagonjwa uwa ndani ya ofisi ya daktari husika" Dada wa mapokezi alijibu,

"kwa hiyo hamjabahatika hata kumuona mtu aliyefanya tukio, hii hospitali si ina camera?" Vin aliuliza,

"polisi ndio watafanya uchunguzi, kuna mtu wanamsubiri, ila kwa sisi tunamuhisi kijana mmoja ambaye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuingia ofisi hiyo ya Dokta" Dada wa mapokezi alijibu,

"huyo mtu yukoje?" Vin aliuliza,

"mweupe mrefu, ana michoro mwilini, mkononi amejichora bastola" Dada wa mapokezi aliongea, ila kwa maelezo hayo tu, Vin alimtambua mtu huyo anaezungumziwa ni Trigger,

"atashikwa tu" Vin aliongea na kisha akawa anaelekea nje huku mawazo yakiongezeka na kujiuliza kwanini Trigger amemuua yule daktari?

Vin alitembea mpaka kwenye gari la Strategic na kuingia,

"mbona hatuambiani hapa hospitali kuna nini? Maana umemiagiza niangalie kama Sarah amefika, mara namuona Trigger, mara na wewe unakuja nakuona umepitiliza ndani. Au mzee mnataka aletwe hapa kwa matibabu zaidi?" Strategic aliuliza huku akitabasamu,

"Trigger ameua muda ambao ulimuona eneo hili" Vin aliongea kwa unyonge,

"ndio maana nimewaona polisi na baadhi ya watu wakipishana maeneo haya. Amemuua nani?" Strategic aliuliza,

"jana kuna vipimo nilikuja kupima hapa, sasa nahisi huenda Trigger alikuja kuchukua majibu kwa nguvu, na tena Dokta aliyekufa ni yule yule niliyekuwa nae jana, na nimeshtuka sana mara baada ya kukumbuka kuwa uliniambia kuwa Trigger ametoka na bahasha ya njano, huenda ndio majibu yangu hayo" Vin aliongea kwa upole,

"mbona sielewi, hivyo vipimo ni vya nini mpaka Trigger achukue majibu kwa kutumia bastola?" Strategic aliendelea kuhoji na kumfanya Vin akae kimya kwa muda na kujikuna kichwa,

"jana nilivyokuagiza ukamuue Sarah, tulikutana na Sarah kabla hujakutana nae wewe, na akanitolea damu na kudai mimi ni ndugu yake, na hii ni mara ya pili. Sasa mara baada ya kunipa ile damu, nikapita hospitali nikiwa na Trigger na kuchukua vipimo vya DNA, majibu ndio nilitakiwa nifuate leo. Ndio maana nikazuia kwanza usimuue Sarah mpaka nijue ukweli, na pia nikakutuma uje umuwinde Sarah hapa kwa maana anaweza kuja na kumshurutisha Dokta aandike majibu ya uongo ili aonekane ni ndugu yangu" Vin aliongea kwa utulivu na kumfanya Strategic ashushe pumzi nzito,

"wewe unahisi kwanini Trigger amewahi kuja kufuata majibu? Tena mpaka ametumia nguvu ya ziada?" Strategic aliuliza,

"sasa hapo ndipo napata mashaka, huenda kuna kitu anakificha. Wewe umekaa muda mrefu na Trigger na baba yangu, na wewe peke yako ndio nimetokea kukuamini na ndio maana nakushirikisha kwenye mambo yangu. Tafadhali sana naomba uniambie ukweli wowote unaoujua kuhusu mimi, kwa maana mimi sijakulia hapa, historia inaonesha nilienda marekani tangu nikiwa mtoto" Vin aliongea,

"dah, sijui nikuambiaje? Ila nilishawahi kuwasikia Harry na Trigger wakisema Taita sio baba yako, ni mjomba wako tu, ila hawakujua kama niliwasikia" Strategic alitoa habari nyingine mpya kwa Vin, hapo sasa kichwa cha Vin kikaparaganyika,

"hawajasema baba yangu ni nani?" Vin aliuliza,

"nilisikia wakisema kuwa wazazi wako walikufa kwenye tukio la nyumba kuungua na moto" Strategic aliongea na vin akakumbuka maneno ya Harry na Sarah kuhusu kifo cha wazazi wake,

"kingine unachokijua kuhusu mimi?" Vin aliuliza,

"hakuna zaidi mkuu" Strategic alijibu,

"sawa, basi we nenda kaendelee na shughuli zako, nikikuhitaji nitakutafuta" Vin aliongea huku akishuka kwenye gari ya Strategic,

"poa boss" Strategic alijibu,

"ila ukiwa na Trigger na mzee usiwaeleze kama umeniona au umekutana na mimi siku za karibuni, hiyo ni kwa ajili ya usalama wako tu, maana Trigger akijua unanisaidia kupata ukweli wangu, anaweza kukuua" Vin alimtahadharisha Strategic,

"sawa, haina shida" Strategic alijibu na kisha Vin akaelekea kwenye gari yake na kuondoka.

Strategic nae akawasha gari yake na kuiondoa eneo hilo la hospitali.

***********************

Sajenti Minja alipotoka uwanja wa ndege, alielekea moja kwa moja katika hospitali ambayo aliambiwa kuna mwili wa mtu ambaye ulikotwa chini ya daraja la taka umepelekea uko.

Sajenti Minja alifika hospitali na kuwakuta baadhi ya askari wakiwepo eneo hilo, aliwasalimu,

"uchunguzi wa mwili uliookotwa umeanza?" Sajenti Minja aliuliza,

"bado, ila wamemaliza muda huu kumtoa risasi mbili zilikuwepo kichwani mwake" Askari alijibu,

"zipo wapi?" Sajenti Minja aliuliza,

"twende" Askari yule aliongea huku akiondoka na Sajenti Minja akimfuata kwa nyuma.

Walielekea mpaka kwenye chumba kimoja kidogo na kuingia, yule askari akavaa mipira mkononi na kufungua kabati dogo ndani ya kile chumba na kutoa mfuko mdogo wa nylon, ulikuwa na risasi mbili.

Sajenti Minja nae akavaa mipira mkononi na kuitoa risasi moja, akaitambua kwa haraka sana, ni zile risasi anazozitumiaga Sarah,

"aliyeuawa mmemtambua?" Sajenti Minja aliuliza kwa pupa,

"jina lipo kwenye kitambulisho chake, anaitwa Harry William, ni mfanyakazi WA TaV Company" Askari alijibu na kumfanya Sajenti Minja apate mwanga sasa, alikuwa anamjua Harry vizuri, na alikuwa akijua kuwa hiyo company aliyokuwa akifanyia kazi ni company ya Taita,

"kwa hiyo baada ya familia yake kuuawa siku zilizopita, leo hii wamemuua yeye?" Sajenti Minja aliuliza na kufanya mwenzake asielewe anachokimaanisha.

"una maana gani?" Mwenzake aliuliza,

"kwa hilo jina ulilonitajia hapo, huyo marehemu ndiye yule mtu familia yake tuliyoikuta wote wamekufa kwa kupigwa risasi" Sajenti Minja aliongea,

"kwa hiyo huu ni muendelezo? Inaweza kuwa ni mauaji ya madai au visasi" Mwenzake aliongea,

"yote yanawezekana" Sajenti Minja aliongea na kuvua ile mipira mkononi na kuelekea nje ya kile chumba.

*******************

Vin alivyotoka hospitali, alielekea moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Taita, alivyofika hakugonga hodi, aliingia moja kwa moja sebuleni na kumkuta Taita na Trigger wakiwa wamekaa na juu ya meza kulikuwa na bahasha ya njano yenye jina lake, Vin bila hata ya kumsalimia mtu, akaenda moja kwa moja kuchukua ile bahasha, hapo Trigger na Taita wakapata wasiwasi,

"mko salama?" Vin aliuliza huku akikaa kwenye kochi na mkononi akiwa na ile bahasha ambayo Trigger aliichukua hospitali,

"safi tu" Trigger alijibu huku akiinuka kwenye kochi.

Vin akaitoa karatasi iliyokuwa ndani ya bahasha, Vin akaanza kusoma, kila neno alilokuwa akilisoma ndipo uso wake ulizidi kubadilika, ilionesha wazi hasira zilivyokuwa zinaongezeka.

"mzee, baadae kidogo" Trigger aliongea huku akianza kuondoka,

"unaenda wapi? Rudi Kaa hapa, leo mtanieleza ukweli wa haya majibu" Vin aliongea kwa hasira huku akiichomoa bastola yake na kumuelekezea Trigger..................

**********ITAENDELEA***********

the Legend☆
MOTO

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom