RIWAYA : SALA YA SARAH
MTUNZI : ALEX KILEO
SEHEMU YA HAMSINI NA TATU.
ENDELEA..................
Askari walizidi kusogelea mlango wa sebule ya Sarah huku mikononi wakiwa silaha nzito. Ila kabla hawajaufikia mlango, mlango ulifunguliwa na akatoka babu yake Sarah na kutembea kuelekea getini,
"Mikono juu" Askari mmoja aliongea kwa amri ila babu yake Sarah hakuonesha kujali, alizidi kupiga hatua kuelekea getini,
"weka mikono juu mzee, ina maana husikii?" Yule Askari aliuliza ila safari hii aliipaza sauti yake huku akiamini atamuogopesha mzee yule, ila wala yule mzee hajateteleka, alizidi kupiga hatua kulisogelea geti. Askari yule akaona anafanyiwa dharau kubwa sana, ikambidi atoke kasi kumuelekea mzee, alipofika alimpiga kikumbo na yule mzee akaanguka chini, kisha yule askari akamgeuza yule mzee tumbo chini, mgongo juu na akaichukua mikono ya yule mzee na kuifunga pingu, kisha akamnyanyua,
"wewe si unajifanya jeuri" Askari aliuliza huku akimsukuma yule mzee na kutoka nae nje ya geti,
"sasa wewe vipi? Mbona mmemkamata msamalia mwema?" Polisi ambaye alikuwa kiongozi wa msafara wa polisi aliuliza na kumfanya yule askari aliyemshika mzee ashangae,
"ametoka ndani, tumempa amri amekataa kutii" Askari aliongea,
"huyu ndiye aliyetupigia simu na kutupa taharifa za kuwepo muharifu hapa, alafu sio mara moja, mara zote huyu ndiye anayetupa taharifa za muharifu" Kiongozi wa kikosi kile aliongea na kumfanya babu yake Sarah asikie uchungu kwa mara ya kwanza juu ya kauli ile, kwa kuwa aliijua alikuwa anamchoma mjukuu wake,
"mfungue pingu hiyo" Kiongozi wa kikosi alitoa amri kisha askari akatii na kumfungua pingu mzee,
"mmechelewa mbona, yule binti ameshaondoka tayari" Babu yake Sarah aliongea huku akimuangalia kiongozi wa kikosi kile,
"dah, ameelekea upande gani?" Kiongozi wa kikosi aliuliza,
"sijui, kwa kuwa mimi nilikuwa ndani, sikuweza kujua ameelekea uelekeo gani?" Babu yake Sarah alijibu na kumfanya kipindi hicho Sajenti Minja alikuwa anafika, askari wote wakampigia saluti akiwemo kiongozi wa kikosi kile cha polisi.
"mmefanikiwa kumkamata?" Sajenti Minja aliuliza huku akisimama jirani na babu yake Sarah,
"mzee anadai ameshaondoka" Kiongozi wa kikosi alijibu,
"hawa wazembe sana, nimewapigia simu muda mrefu ila ndio wamekuja sasa hivi, sijui wanamuogopa yule mwanamke?" Babu yake Sarah aliongea huku akijifanya amekasirika,
"Dokta Pendo yupo ndani?" Sajenti Minja alimuuliza babu yake Sarah,
"ndio, yupo" Babu yake Sarah alijibu,
"chukua kikosi chako na uondoke, mmeshakosea, mnapopigiwa simu mnatakiwa mfike kwa wakati" Sajenti Minja aliongea kwa amri kwa maana alihisi kama Dokta Pendo yupo ndani, basi hata Sarah atakuwa ndani.
Baada ya Sajenti Minja kutoa amri, wale askari walijilusanya na kuondoka zao huku baadhi ya askari wakilalamika chini chini kwa kitendo cha Sajenti Minja cha kuingilia kazi yao na mwisho akawafukuza bila kuwapa uhuru wa kufanya upekuzi kwenye nyumba ya Sarah.
Sajenti Minja alisimama mlangoni pale getini mpaka alipohakikisha gari ya polisi imepotea machoni mwake, kisha Sajenti Minja akaingia moja kwa moja mpaka sebuleni na kumkuta Sarah na dokta Pendo wakiwa wamekaa, kwanza wote walishtuka mara baada ya mlango kifunguliwa.
"vipi, upo salama?" Sajenti Minja aliuliza huku akichuchumaa kwenye miguu ya Dokta Pendo na wakati huo babu yake Sarah nae alikuwa akiingia ndani,
"ndio umekuja kumkamata Sarah?" Dokta Pendo aliuliza huku akimuangalia Sajenti Minja,
"wameshaondoka" Babu yake Sarah alijibu,
"kwanini ulimchukua Dokta Pendo hotelini bila kunipa taharifa?" Sajenti Minja aliuliza huku akimgeukia Sarah ambaye muda wote alikuwa kimya kwa maana alikata tamaa mara baada ya polisi kuizunguka nyumba yake, na aliamua atulie tu sebuleni huku akisubiri litakalomkuta, kwa hiyo babu yake aliposema askari wameondoka, ulikuwa muujuza mkubwa sana kwa Sarah.
"wewe si nimekuuliza? Unaniletea kiburi" Sajenti Minja aliuliza kwa hasira huku akimtazama Sarah,
"taratibu basi, kwani yeye kumchukua Dokta Pendo hotelini kuna ubaya gani, hawa si ni marafiki? au wewe unataka kuvunja ushoga wao?" Babu yake Sarah alijibu na kumfanya Sajenti Minja ashtuke, hakutegemea kama yule mzee anaweza kumtetea Sarah, Sajenti Minja akamgeukia mzee huku sura yake ikionesha mshangao wa wazi,
"siongei na wewe mzee, alafu leo mbona unamtetea sana Sarah, si alikuwa adui yako huyu, nasikia hata hawa askari niliowafukuza uliwaita wewe?" Sajenti Minja aliuliza huku akicheka na Dokta Pendo nae alikuwa akicheka ila kwa kujificha jificha,
"bwana wewe, binadamu tumeumbwa kukosea" Babu yake Sarah alijibu huku akiwa anaangalia chini,
"sasa Sarah itabidi twende kituoni, kwani ile kesi bado inaendelea na pia kumbuka kuwa una kesi nyingine ya mauaji, siku ile unatoroshwa kuna askari alikuwa" Sajenti Minja aliongea,
"na wewe nawe, kila kitu polisi, yaani kitu kidogo polisi, utadhani ulizaliwa uko?" Dokta Pendo aliongea huku akionekana hajapenda maongezi ya Sajenti Minja,
"hata mimi anamiudhi, Sarah mjukuu wangu uwe unachagua marafiki, sasa huyu mtu umemtoa wapi?" Babu yake Sarah huku akiwa anamuangalia Sajenti Minja kwa hasira na kumfanya Sajenti Minja acheke,
"Sarah huyu mzee ni babu yako, sitaki unijibu hilo, ila ninachokifanya kujua ni kuwa je, Taita ni mjomba wako?" Sajenti Minja aliuliza huku akimtazama Sarah,
"sio mjomba wake" Babu yake Sarah alijibu na kumfanya Sajenti Minja amuangalie,
.
"mzee kumbuka wewe ndiye uliyeniambia kuwa mwanao alimuoa dada yake Taita, na mwanao ndiye baba yake Sarah, sasa kwa nini unakanusha swali langu, au hujui kuwa huyu Sarah ndiye yule mjukuu wako anayeishi uingereza?" Sajenti Minja alimuuliza babu yake Sarah huku akijua kuwa babu yake Sarah atashangaa,
"ndio unanitambulisha au? Mbona najua muda mrefu tu kuwa huyu ni mjukuu wangu" Babu yake Sarah alijibu na kumfanya Dokta Pendo aangue kicheko,
"mzee miyeyusho kweli. Sarah hujanijibu, Taita ni mjomba wako?" Sajenti Minja alirudia swali lake,
"ndio, ni mjomba wangu?" Sarah alijibu, Sajenti Minja akatingisha kichwa kukubaliaba na Sarah,
"kuna kitu kimoja unanificha, wewe ni mpiganaji mzuri sana, wa ngumi na mtumiaji mzuri sana wa silaha, je haya mafunzo umeyapata wapi?" Sajenti Minja aliuliza na kumfanya Sarah ashushe pumzi nzito,
"Mimi ni mwanajeshi" Sarah alitoa jibu lililomshangaza kila mtu ndani mule,
"wa kambi gani?" Sajenti Minja aliuliza huku akificha mshangao wake,
"sio wa hapa, mimi ni raia wa uingereza" Sarah alijibu na kumfanya Sajenti Minja akumbuke kitu, alikumbuka let lile tukio la kupambana na mwanamke ndani ya ile nyumba iliyoungua na akakumbuka zile risasi mbili alizoziokota na kuzifanyia uchunguzi na kugundua kuwa zinatumiwa na jeshi la uingereza,
"kuna matukio mengi sana umeyafanya, yakiwemo ya utekaji, je ni vibaya nikikutia hatiani?" Sajenti Minja aliuliza,
"na wewe nawe unaona sifa kuwatia watu ndani" Dokta Pendo aliongea,
"nyie kaeni kimya, hapa ni mimi na Sarah tu" Sajenti Minja aliongea kwa ukali na kufanya Dokta Pendo atulie,
"unataka kuniweka hatiani? Ni sawa, ila naomba muda kidogo" Sarah aliongea kwa kujiamini,
"muda? Muda wa nini, unatakiwa uondoke na mimi muda huu" Sajenti Minja aliongea,
"ngoja nikuambie kitu, yaani wewe hapo ulipo, huwezi kunifanya chochote hata nikiamua kutokwenda polisi, na nilivyokuomba muda nimetumia busara tu, kwa hiyo niache nikamilishe mambo yangu kwanza" Sarah alijibu,
"unatupangia kazi sio, kumbuka hapa sio uingereza" Sajenti Minja aliongea,
"angalia chini ya meza" Sarah aliongea na kumfanya Sajenti Minja achungulie chini ya meza, na kipindi hicho babu yake Sarah nae alitaka kuchungulia ila Sarah alimzuia.
Sajenti Minja alipochungulia aliona mabomu mawili chini ya meza, Sajenti Minja akarudi taratibu kwenye kiti,
"ningekuwa mkorofi, ni muda sana ungekuwa umeshakufa, eidha kwa ulichokiona chini ya meza, au siku ile ulipotuona na dokta Pendo kwa mara ya kwanza, maana nilikushambulia ukapoteza fahamu, ila nikakuacha, elewa sipo hapa kumdhuru mtu, nipo hapa kudili na wanyama" Sarah aliongea ila Sajenti Minja alikuwa na wasiwasi kutokana na alichokiona,
"naomba niondoke" Sajenti Minja aliongea huku akiinuka,
"afadhali, nenda tu baba" Babu yake Sarah aliongea ila Sajenti Minja hakuongea kitu, Sajenti Minja akaondoka huku akitafakari neno ka Sarah alilosema anadili na wanyama.
"kwani uko chini ya meza kuna nini, mbona Minja alivyochungulia amekuwa mpole?" Dokta Pendo aliuliza,
"chungulia" Sarah aliongea huku akitabasamu na kumfanya babu yake achungulie, kidogo akimbie,
"hayana madhara, nimeweka kutisha watu tu" Sarah aliongea huku akiinuka katika kiti,
"shoga nirudishe hotelini" Dokta Pendo aliongea,
"nitakurudisha jioni, ngoja tule tushibe, nitakurudisha jioni ninapoenda kumalizana na Harry" Sarah aliongea huku akipotelea chumbani.
*******************
Mishale ya usiku, Trigger na Vin walikuwa ndani ya geti la Harry, na chini alikuwa mlinzi wa geti ambaye kwa muonekano wa haraka ilionekana amepoteza maisha au amepoteza fahamu,
"twende ndani, huyu tayari" Vin aliongea huku wakielekea ndani, walipofika hawakugonga hodi, wakasukuma mlango na kuingia, wakamkuta mke wa Harry akiwa na watoto wake,
"vipi shem, mbona unatutisha kwa namna ulivyoingia?" Mke wa Harry aliongea huku akitabasamu,
"jamaa tumemkuta?" Trigger aliuliza bila kujibu swali la mke wa Harry,
"ametoka, aliniambia anaweza asirudi leo" mke wa Harry alijibu,
"alikwambia anapoenda?" Vin aliuliza,
"hapana, kwani vipi? mbona mnanitisha?" mke wa Harry aliuliza,
"Harry amemuua Taita, kwa hiyo anatafutwa" Vin aliongea huku akimtazama mke wa Harry ambaye alikuwa amekamata mdomo kwa mshtuko,
"tupo hapa kulipa kisasi" Trigger aliongea na kumshangaza zaidi mke wa Harry,
"kivipi?" Mke wa Harry aliuliza huku machozi yakimtoka,
"maliza mchezo, Harry atakuwa amekimbia nchini tayari" Vin aliongea kwa sauti ndogo iliyomfikia vyema Trigger, Trigger akachomoa bastola yake na kuwamiminia risasi familia ya Harry, hakuna aliyebaki hai, wote walikufa,
"sasa wewe wahi Kiwanja cha ndege ukaangalie kama utamuona Harry, acha mimi niendelee kusubiri hapa, huenda atarudi" Vin alimwambia Trigger,
"poa mkuu" Trigger aliongea kisha akatoka zake nje na kuondoka zake.
Kipindi Trigger anaondoka, ndicho kipindi Sarah alikuwa anaingia ndani kwa kupitia ukuta, alivyotua tu ndani akaangaza macho na kuweza kuuona mwili wa mlinzi ukiwa umelala, Sarah akajua kuna uvamizi ulifanyika muda uliopita, Sarah akapata wasiwasi huku akiamini huenda ni Aisha ndio mvamizi.
Sarah akaufikia mlango wa sebuleni na kuingia, ila alichokiona ndicho kilichomstua, aliikuta miili ya watu ikiwa imelala na imetapakaa damu, macho ya Sarah yaliangukia kwenye mwili wa mtoto mdogo wa kike, kipenzi chake,
"princess!!" Sarah aliongea huku akiukimbilia mwili ya yule mtoto, alipoufikia akaubeba na kuutingisha huku akilia, alikuwa na uchungu sana, alilia huku akiamini huu mchezo umefanywa na Aisha,
"umekuja kumuua Harry au umekuja kumtuma?" Vin aliingia pale sebuleni huku akiongea maneno hayo na kumfanya Sarah ashtuke,
"ni nani aliyemuua huyu mtoto?" Sarah aliuliza kanakwamba hakuona maiti nyingine hapo sebuleni,
"na wewe unamfuata uko alipo muda si mrefu" Vin aliongea huku akiichomoa bastola yake na kufanya Sarah aamini kuwa huyu ndiye aliyefanya mauaji hayo, Sarah akachomoa kisu na kumrushia Vin, Vin akayumba kidogo kwa lengo la kukikwepa kile kisu, Vin alipokaa sawa alishuhudia teke kali likiupiga mkono wake na kufanya aiangushe bastola yake. Vin akagundua kuwa kiumbe anayepambana nae ana kasi ya ajabu sana. Vin akaamua kutumia mbinu za kujiami, yaani awe anapigana huku anarudi nyuma, Sarah akaligundua hilo, kwa kasi ile ile Sarah aliruka teke jingine kali, Vin akapiga hatua moja nyuma na Sarah akamkosa, Sarah akatua mbele ya Vin, Vin akaachia ngumi kali, Sarah akaidaka kisha Sarah nae akaachia ngumi kali, ikampata Vin usoni, Vin akaanza kuona nyota nyota, Sarah akatumia mwanya huo na kumpiga ngumi nyingi za haraka haraka, Vin akaenda chini,
Vin akajiinua na sarakasi nyepesi, akaokota pasi iliyokuwa hapo sebuleni na kumtupia Sarah, Sarah akakwepa, Vin akachukua king'amuzi na kumrushia Sarah, Sarah akainama, alipoinuka akakutana na ngumi ya Vin ikiwa imemlenga uso, Sarah akaidaka na kuunyongorota mkono wa Vin na kumfanya Sarah awe nyuma ya Vin huku akiwa ameushika mkono wa Vin kwa nyuma,
"nakuua mshenzi wewe ili kuilipa damu ya huyu malaika uliyemuua bila ya sababu" Sarah aliongea kwa hasira huku akiichomoa bastola yake, Vin alikuwa hana la kufanya, alibanwa vibaya sana.
Wakati Sarah akiwa amemshika namna ile Vin, Sarah kuna kitu alikiona kwenye mkono wa Vin, kilimshtua Sarah, aliona madoa mawili meusi kwenye mkono au Vin, tena yapo eneo lile lile kama lililopo doa lake, Sarah akajikuta amepoteza ujasiri wa kumfyatulia risasi Vin,
"Sebastian" Sarah aliita huku akimuachia Vin, Vin akashanga, ila hakutaka kujali Sarah anachofanya, Vin akamtupia ngumi nzito Sarah, Sarah hakuizuia ingawa alikuwa na uwezo wa kujikinga, ngumi ile ikatua kwenye pua ya Sarah, Vin akarusha ngumi nyingine, Sarah akamdaka mkono,
"Sebastian mimi ni dada yako, usinipige" Sarah aliongea kwa upole huku akimuachia mkono Vin, Vin akaona Sarah kama amechanganyikiwa, Vin akarusha teke na Sarah akaudaka mguu wa Vin na kumsukuma chini, Vin akadondoka
"Mimi ni dada yako, tusipigane" Sarah aliongea kwa ukali ila Vin hakuna alichojua, Vin akainuka na meza ya kioo na kumtupia Sarah, Sarah akakwepa na sasa Sarah akaamua aondoke, aliona akiendelea kukaa pale, Vin atamjeruhi na yeye hakutaka kupigana na mdogo wake.
"nitakutafuta Seba" Sarah aliongea na kisha akaanza kuondoka kwa mwendo wa taratibu bila hata kuangalia nyuma, alivurugwa akili kwa kumgundua mdogo wake.
Wakati Sarah akiondoka bila wasiwasi wowote, Vin aliimkimbilia bastola yake na kuiokota, aliamini muda huo ndio muda wa kutekeleza ahadi aliyompa baba yake (Taita).
Wakiwa wameachana umbali wa hatua kumi tu, Vin alimnyooshea Sarah bastola, ubaya Sarah hakuwa na habari na alikuwa akiendelea kutembea tu kuelekea nje.
Vin akatoa tabasamu la ushindi, hakujua anayetaka kumuua ni dada yake, Vin akiwa amelenga usawa wa kichwa cha Sarah, Vin alimfyatulia Sarah risasi, na kisha Sarah akaanguka chini................
**********ITAENDELEA**********
the Legend☆