SEHEMU YA 20
ILIPOISHIA:
Nilichoweza kukifanya, ilikuwa ni kuoga tu, usingizi mzito ukanipitia palepale kwenye kochi nilipokaa ili kupumzika kidogo kabla ya kurudia yale mazoezi kama Bonta alivyoniambia. Nilipokuja kuzinduka, tayari kulikuwa kumeshaanza kupambazuka, nikajishangaa imekuwaje?
SASA ENDELEA...
Nilijaribu kuinuka pale nilipokuwa nimelala lakini mwili ulikataa kabisa, viungo vyote vilikuwa vinauma mno. Ilibidi nitulie kwanza, nikashusha pumzi ndefu na kujikaza kiume, nikafanikiwa kusimama huku nikihisi kama mwili wangu unataka kupasuka kutokanana maumivu.
Ni hapo ndipo nilipoelewa ni kwa nini Bonta aliniambia kwamba nikifika natakiwa kuyarudia mazoezi yote kwanza kabla ya kulala. Kwa kuwa bado ilikuwa ni mapema sana, ilibidi nijikaze na kuanza kufanya mazoezi mepesi ili kulainisha viungo. Nilianza kwa kurukaruka taratibu, machozi yakawa yananitoka kutokanana maumivu.
Kadiri nilivyokuwa nazidi kurukaruka, maumivu yalianza kupungua na sasa viungo vikawa vinaanza kulainika, miguu ikaanza kukunjika vizuri, mikono nayo ikawa inaweza kukunjika kwa urahisi.
Nilianza kukimbiakimbia mle ndani na baada ya mwili kukaa sawa, nilirudia mazoezi yote tuliyofanya jana. Japokuwa ilikuwa bado ni asubuhi sana na kulikuw ana baridi, mwili wangu ulikuwa ukitokwa na jasho kama maji. Angalau sasa nilianza kujisikia vizuri, nikaenda bafuni kuoga kisha nikaanza kujiandaa.
Saa kumi na moja na nusu za alfajiri, tayari nilikuwa nimemaliza kujiandaa, nikatoka na kuanza kuelekea kituoni, nikapanda gari na safari ya kuelekea kambini ikaanza. Mpaka nafika, tayari ilikuwa ni saa moja kasoro za asubuhi, watu wengi tayari walikuwa wameshafika wakiendelea na kazi zao.
Kati ya wote tuliokuwa kwenye mazoezi jana, tulikuwa tumefika wanne tu, na wenzangu wote walikuwa wakichechemea kutokana na maumivu. Ile mbinu ya kufanya mazoezi asubuhi ilinisaidia sana kwa sababu angalau mimi ndiyo nilionekana kuwa ‘fiti’ japo bado mwili ulikuwa unauma kwelikweli.
Bonta aliponiona, alikuja kunisalimia huku akiwa na uso wa tabasamu, tukapeana ‘tano’ pale maana hiyo ndiyo ilikuwa salamu yetu kubwa, akaniuliza naendeleaje? Ilibidi nimsimulie kilichotokea, akacheka sana lakini akaniambia kwamba nimemfurahisha sana kwa ukakamavu niliouonesha.
Wale wengine waliendelea kufika mmojammoja na kila aliyekuwa anafika, ungeweza kudhani anaumwa kwa jinsi walivyokuwa wakiugulia maumivu. Wote tulipotimia, tulipelekwa kwenye chumba cha chini kwa chini, ambacho kilikuwa na vifaa vya kufanyia mazoezi kama ‘gym’.
Kumbe vile vyuma pale juu vilikuwa kama geresha tu, kule chini kulikuwa na sehemu kubwa ya kufanyia mazoezi ikiwa na vifaa vyote muhimu. Jamaa mmoja ambaye mara kwa mara nilikuwa namuona na Bonta, ambaye alikuwa na mwili mkubwa kwelikweli, alikuja na kuanza kutufanyisha mazoezi.
Tofauti yake ni kwamba alitufanyisha mazoezi ya kawaida tu ya kujenga mwili, na akatusisitiza kwamba tukiendelea vizuri, na sisi tutakuwa na miili iliyojengeka vizuri kimazoezi kama yeye alivyokuwa.
Niligundua pia kwamba hata mwili wa Bonta, ambao ulikuwa umejengeka vizuri sana, ilikuwa ni kwa sababu ya mazoezi maana alikuwa na kifua kipana, mikono mikubwa yenye misuli na tumbo lililotengeneza kile vijana wanachoita ‘six pack’.
Baada ya kufanya mazoezi kwa karibu saa nzima mfululizo, tulipewa muda wa kupumzika kisha tukaenda kunywa chai.
Kumbe mlemle ndani kulikuwa na kantini ambayo sikuwahi kuigundua, wahudumu wake wote walikuwa wanaume, tukapata kifungua kinywa cha nguvu kisha tukaambiwa tujiandae kwa safari ya kwenda Kazimzumbwi kumalizana na Mamba.
Watu waliposikia jina la Mamba, kila mmoja alionekana kupoteza uchangamfu usoni maana tulikuwa tunajua shughuli pevu tunayoenda kukutana nayo. Kabla hatujaondoka, kila mmoja wetu alipewa ‘ovaroli’ kama yale wanayovaa mafundi, tukavaa na kuingia ndani ya gari.
Kama ungetuona, ungeweza kudhani labda ni mafundi wa kampuni fulani wanaenda kazini lakini kumbe ilikuwa tofauti kabisa. Tulipanda kwenye magari mawili tofauti na yale tuliyotumia jana yake, na safari ya kuelekea msituni ilianza. Tulipofika, tulimkuta tayari Mamba na timu yake wameshafika, wanatusubiri, tukajipanga harakaharaka na bila kupoteza muda, kazi ikaanza.
Asubuhi hiyo tulianza kwa mazoezi ya shabaha tukiwa tumevaa maovaroli yetu, tukawekewa vitu kama sanamu za watu, zilizokuwa na michoro ya maeneo tunayotakiwa kulenga shabaha.
Alianza kwa kutufundisha kwa maelekezo kwanza huku akituonesha pia kwa vitendo, akatuelekeza sehemu za muhimu za kulenga, akatuelekeza maeneo ambayo ukimpiga mtu, unampunguza kasi ya kupambana na wewe lakini pia akatuelekeza maeneo hatari ambayo ukimpiga mtu hawezi kupona.
“Tunapoingia kazini, lazima mjue kwamba lengo letu siyo kuua watu wasio na hatia, kama tumetumwa mzigo fulani basi muhimu ni kuhakikisha mzigo unapatikana bila kusababisha vifo vya watu wasio na hatia, wananchi siyo adui zetu, adui zetu sisi ni polisi,” alisema, nikashtuka sana kusikia maneno hayo.
Kumbe wakati wananchi wa kawaida wakiwaona polisi kama ndiyo watetezi wao, kwa upande wa wahalifu, polisi huwa ndiyo adui yao namba moja. Mamba alitufundisha kabisa kwamba tunapokuwa kwenye kazi, ukimuona polisi hakuna cha ‘msalia mtume’, ni lazima umuondoe vinginevyo yeye atakuondoa wewe.
Niliwafikiria polisi, nikauona ugumu wa kazi yao! Nikazifikiria familia zao, watoto wao, ndugu zao na kadhalika, nikajikuta nawaonea huruma sana.
Hata leo baada ya kupitia mambo mengi sana, ninachoweza kukisema ni kwamba miongoni mwa watu wanaofanya kazi kubwa sana na ambao serikali inatakiwa kuwafikiria sana kwenye suala la maslahi yao, ni polisi.
Nitakueleza baadaye matukio ambayo tulikuwa tukipambana na polisi na utakubaliana na mimi kwamba ni kazi ngumu sana inayohitaji wito na moyo wa kujitoa sana, unahatarisha maisha yako kwa ajili ya kuwalinda watu wengine na mali zao, unapambana na watu wanaofundishwa kwamba wewe ndiye adui yao namba moja! Inahitaji moyo sana.
Mafunzo yaliendelea kwa muda mrefu, ikafika zamu ya kuanza kufanya kwa vitendo kile tulichofundishwa. Wengi wetu tulikuwa na uwezo mdogo sana wa kulenga shabaha na kuna wakati nilimsikia Mamba akisema kwamba hawezi kujivunia kutufundisha kwa sababu anajua ndani ya siku chache tu, wote tutakufa.
“Mkikutana na polisi nyie hakuna atakayerudi hata mmoja! Lazima ujue kulenga siyo kufyatuafyatua tu risasi, mtakufa wote kama kuku,” alisema na kuanza upya kutuelekeza. Lilikuwa somo gumu lakini taratibu tulianza kuelewa, hasa kutokana na msisitizo aliokuwa anautoa.
Kingine nilichogundua ni kwamba kumbe kushika bunduki pekee hakuna maana kama hujui kulenga shabaha! Unaweza kuwa na bunduki na ukazidiwa ujanja na mtu mwenye mshale, cha muhimu zaidi ni kujua unapiga wapi na kwa sababu gani. Baada ya kujifunza shabaha, tulihamia kwenye mazoezi ya viungo, ‘mtiti’ ukawa ni zaidi ya jana yake.
“Wewe unakula nini! Mbona huliilii kama wenzako?” uzalendo ulimshinda Mamba na kuamua kuniuliza. Aliona kila zoezi analotoa, naenda naye sawa kwelikweli, sikumjibu kitu nikawa namtazama tu. Mbinu aliyonipa Bonta ilinisaidia sana. Siku hiyo ilipita, tukaendelea na mazoezi karibu kila siku kwa muda wa siku ishirini na moja.
Huwezi kuamini, baada ya kumaliza mafunzo hayo, tulikuwa ‘tumekwiva’ kwelikweli, hata siku niliyorudi nyumbani kwenda kuwasalimia na kuwapeleka fedha za matumizi, kila mtu alikuwa akinishangaa. Nilikuwa nimebadilika ghafla kutoka kwenye uvulana na kuingia kwenye uanaume.
Mwili wangu ulikuwa umejengeka vizuri kimazoezi, kifua kilikuwa kimepanuka, mikono imejaa na hata kutembea kwangu kulibadilika, nilikuwa kama ‘mjeshi’ flani hivi. Kule kuchekacheka nilikokuwa nao awali, kuliisha, muda mwingi nikawa niko ‘siriasi’ sana.
“Kwani umeingia jeshini nini mwanangu? Maana unatisha siku hizi,” mama aliniuliza, nikashindwa kujizuia kucheka, nikamdanganya kwamba mahali ninapofanya kazi, tunafanya kazi ngumu sana ndiyo maana nimebadilika, basi akawa ananishukuru sana kwa jinsi nilivyoweza kujitoa mhanga kwa ajili ya kumsaidia baba na kuisaidia familia yetu.
Aliniambia kwamba fedha ambazo nimekuwa nikiwatumia, zimesaidia sana kubadilisha maisha ya pale nyumbani na kwamba anajivunia kuwa na mtoto mwenye moyo wa uthubutu kama mimi.
Kuna wakati aliniambia wazi kwamba anajutia uamuzi wake wa mwanzo wa kunikataza kwenda mjini kwa sababu kama ningemsikiliza, tungeendelea kuzama kwenye umaskini na pengine tungempoteza baba mapema zaidi kwa kukosa fedha za kununua dawa na za matunzo.
Nilikuwa namuitikia tu mama lakini ndani ya moyo wangu nilikuwa najua ukweli wa kila kinachoendelea, na kama na yeye angekuwa anajua, kamwe asingeniruhusu nifanye nilichokuwa nakifanya. Basi nilikaa pale nyumbani mpaka mida ya kama saa sita za usiku, nikawaaga kwamba naondoka.
Kila mtu alishangaa na afadhali siku ile nyingine nilienda na Bonta mpaka pale nyumbani, wakawa wananiuliza nitaondokaje? Niliwajibu kwamba nimekuja na teksi ya rafiki yangu kutoka mjini na alikuwa ananisubiri stendi. Haikuwaingia akilini lakini mwisho hawakutaka kunikwaza hasa kutokanana mchango wangu nilioanza kuuonesha kwenye familia, nikaagana nao na kutoka.
Ni kweli nilikuwa nimekuja na teksi kutoka Dar es Salaam lakini nilimwambia dereva anisubiri pale stendi kwa sababu sikutaka niwe gumzo pale kijijini. Kusafiri na teksi kutoka Dar halikuwa jambo dogo. Basi nilienda mpaka stendi ambako nilimkuta dereva akiwa amelala kwenye siti yake, nikamuamsha na muda mfupi baadaye, safari ilianza.
Kwa mujibu wa sheria za bosi Mute, ilikuwa ni makosa kulala nje ya nyumbani kwako, kwa hiyo ilikuwa ni lazima nirudi mpaka Sinza, bila kujali nitafika saa ngapi. Tulisafiri mpaka Dar, yule dereva akanipeleka mpaka Buguruni kama tulivyokuwa yumekubaliana, nikamlipa fedha zake kisha nikapanda bodaboda mpaka nyumbani kwangu, Sinza.
Mpaka naingia ndani, ilikuwa ni karibu saa tisa za usiku, nikaoga na kwenda kulala maana asubuhi nilikuwa natakiwa kuwahi kazini. Nililala kidogo tu, alarm ya kwenye simu ikaniamsha maana niliitegesha iniamshe saa kumi na moja na nusu. Niliamka nikiwa mchovu, nikaenda kuoga na kuanza kujiandaa, nikaenda mpaka kazini.
“Leo kuna kazi usiku, bosi atawapa maelekezo,” aliniambia Bonta nilipoingia tu. Sikuwa najua ni kazi gani lakini moyoni nilijua kwamba kazi imeanza. Kweli mida ya kama saa nne hivi za asubuhi, Bosi Mute alituita kwenye chumba cha mikutano.
Kwa kawaida, alikuwa akiitisha kikao, watu wote wanaacha kila walichokuwa wanakifanya na kwenda kumsikiliza. Muda mfupi baadaye alikuja na kutangaza kwamba siku hiyo kutakuwa na kazi, akawataka watu wote wanaohusika na maandalizi kuhakikisha kila kitu kinakamilika haraka iwezekanavyo.
Watu wengi walionekana kumuelewa haraka, lakini mimi na wale wenzangu tuliomaliza mafunzo pamoja, tulikuwa gizani bado. Akawataka watu wote kutoka isipokuwa sisi ambao sasa tulikuwa tumebatizwa jina la Kikosi B.
Tulibaki tumekaa kwenye viti vyetu, watu wote walipotoka, akatutaka tusogee mbele kulikokuwa na kama ubao mdogo mweupe, akachukua ‘marker pen’ na kuanza kutuelekeza jambo. Kila mmoja akawa na shauku ya kusikia hiyo kazi inahusu nini?
“Leo saa kumi na mbili kwenye benki ya ...(akaitaja jina), kuna mzigo utateremshwa. Mnatakiwa kuhakikisha tunaupata mzigo huo kwa gharama yoyote na kuufikisha kambini kwa sababu ni wa kwetu,” alisema, moyo wangu ukanilipuka paah!
“Tunaenda kuvamia benki?” nilijiuliza nikiwa ni kama siamini. Aliendelea kutuchorea mchongo mzima unavyotakiwa kufanyika, na akasema hatutaenda wote, bali watachaguliwa wachache kati yetu watakaoungana na Kikosi A kwa ajili ya kazi hiyo. Moyoni nikawa namuomba Mungu nisiwe miongoni mwa watakaochaguliwa.
Je, nini kitafuatia?
Sent using
Jamii Forums mobile app