Riwaya: Saa za Giza Totoro

Riwaya: Saa za Giza Totoro

SEHEMU YA 09

Nilipenyapenya na kumfikia na bila kuuliza, nilimtwanga na lile jiwe kichwani kwa nguvu, damu zikaruka kwa wingi na watu wakaanza kupiga kelele, hapohapo nilijichanganya kwa abiria wengine na kuanza kutimua mbio. Hakukubali, akawa ananifukuza kama faru aliyejeruhiwa.
SASA ENDELEA...
Nilitimua mbio kwa kadiri ya uwezo wangu, watu wakawa wanapiga kelele kwa nguvu huku nao wakikimbilia kule tulikokuwa tunaelekea.
Licha ya kukimbia kwa kadiri ya uwezo wangu, yule konda bado alikuwa akija kwa kasi ya kimbunga, nikashtukia akinikata mtama wa nguvu kutokea nyuma, nikaruka na kudondoka chini kama mzigo, ile najaribu kunyanyuka tena alinifumua teke jingine kwa nguvu, nikaanguka tena, akaja na kunikalia kifuani.
“Muache inatosha jamaa! Oyaa anaua huku,” nilisikia mtu akipiga kelele lakini konda hakutaka kuniachia, alianza kunivurumishia ngumi za usoni, nikajua nisipofanya kitu kweli anaweza kuniua.
Sijui kwa nini watu wengine wanakuwa na roho mbaya kiasi hiki, yaani amenikata mtama, nimedondoka na kuumia, ameona haitoshi, amenipiga tena teke na kuja kunikalia na kuanza kunitwanga ngumi za usoni kama anapigana na mtu mzima mwenzake.
Aliponipiga ngumi ya kwanza, niliona kama nyotanyota, akanipiga nyingine, nikaanza kuhisi vitu vikichuruzika kwa wingi puani na mdomoni, akawa anataka kunipiga ngumi nyingine, nikapata akili ya haraka.
Niliudaka mkono wake mzito na kumpindua kwa staili ya kuunyonga mkono kama nataka kuuvunja, akadondoka chini mzimamzima. Kufumba na kufumbua, niliokota jiwe lingine kubwa lililokuwa pembeni ya pale nilipoangukia, nikalinyanyua kwa jazba huku nikipiga kelele.
Nililishusha kwa nguvu zangu zote na kama asingepata akili ya kukwepa, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Kitendo kile kilimshangaza kila mtu kwa sababu kilitokea kwa kasi kubwa mno. Kwanza nadhani hata yeye mwenyewe aliogopa kwa jinsi nilivyounyonga mkono wake na kumuangusha wakati yeye ndiye aliyekuwa amenikalia kifuani. Kitendo cha kumkosakosa na lile jiwe, kilizidi kumpa woga, akajua kweli naweza kuyakatisha maisha yake.
Akiwa bado amepigwa na butwaa, nililiokota tena lile jiwe, huwezi kuamini aliponiona nikijitayarisha kulivurumisha tena, alikurupuka na kuanza kukimbia, na mimi sikutaka kumuacha, nikawa namkimbiza huku nikitafuta upenyo wa kumtwanga nalo. Kibao kikawa kimegeuka.
Maumivu niliyokuwa nayahisi baada ya kunipiga ngumi za uso, yalinifanya niwe kama mwendawazimu, sikujali kwamba alikuwa mkubwa kuliko mimi, nilitaka na mimi nimshikishe adabu. Nilipomkaribia, nililivurumisha tena kwa kasi kubwa, akawahi kulikwepa, likaenda kupiga nguzo ya umeme, watu wakawa wanapiga kelele kwa nguvu.
Sikukubali, niliokota lingine lakini wakati nainuka, nilishtukia mtu akinikamata kwa nyuma, nikageuka na kutaka kummalizia hasira zangu, kufumba na kufumbua nikajikuta nimekamatwa na zaidi ya watu wanne, wote wakinisihi niachane naye kwani naweza kupata kesi ya kuua.
Yule konda alikimbia mpaka kwenye gari, akapiga bodi kwa nguvu akimuamrisha dereva wake kuondoa gari, kweli akaliondoa kwa kasi huku watu wakicheka na wengine wakishangilia.
“Mngemuacha amkomeshe, hawa makonda wamezoea sana kuonea abiria,” alisema mtu mmoja huku wengine wakiendelea kunisihi nitulie. Kwa jinsi nilivyokuwa na hasira, hasa baada ya kumuona amefanikiwa kuondoka na kukimbia, zilinifanya niwe nalia kwa jazba kama mtu aliyepandisha mashetani.
“Punguza hasira mdogo wangu,” alisema yule mwanaume aliyekuwa amenikamata mikono kwa nguvu akiendelea kunisihi. Haikuwa kazi nyepesi kunituliza kwani hakuna kitu ambacho nilikuwa siwezi kukubaliana nacho kama kuonewa.
Basi wasamaria wema walifanikiwa kunitoa eneo hilo, wakanipeleka kwenye duka moja la dawa ambalo pia walikuwa wakitoa huduma za vipimo na kuchoma sindano. Nikaingizwa ndani ambapo harakaharaka nilisafishwa damu zilizokuwa zinaendelea kunitoka, nikapewa dawa za kupunguza maumivu na angalau sasa nikawa najisikia vizuri.
“Kwani unaelekea wapi?” mmoja kati ya wale watu walionipeleka pale kupata huduma ya kwanza aliniuliza.
“Nimekuja town kutafuta maisha,” nilijibu bila hata kumtazama usoni, nikawa naendelea kujichua pale usoni kwa kipande cha barafu nilichopewa ambacho nilielezwa kwamba kitasaidia kukata damu zisiendelee kutoka puani.
“Una ujuzi gani kichwani?”
“Mbona unaniuliza maswali mengi,” nilisema huku nikimgeukia. Bado nilikuwa na hasira na nilimuona kama kila mtu ni mbaya kutokana na kilichotokea.
“Nguo yako imelowa damu, hebu nisubiri nikuchukulie hata jezi hapo nje! Usitoke, kaa hapahapa,” alisema huku akiinuka. Alitoka na aliporudi, alikuwa na jezi ya Simba mkononi ambayo ilionesha ameinunua hapo nje, akanirushia na kuniambia nibadilishe na kuivaa.
Nilimshukuru, nikavua lile shati nililotoka nalo nyumbani ambalo kweli lilikuwa limelowa damu, nikajifutafuta vizuri na kuivaa ile jezi, akaniambia lile shati chafu nilitupe kwenye ‘dust bin’, jambo ambalo nililifanya.
“Lengo langu ni zuri tu mdogo wangu! Nimefurahishwa na ujasiri ulioonesha wa kukabiliana na yule mshenzi na ndiyo maana nipo hapa kukusaidia,” alisema mwanaume huyo. Nikamtazama vizuri usoni.
Alikuwa ni mtu wa makamo, akiwa amevalia koti la suti, ndani akiwa na fulana na shingoni akiwa na cheni kadhaa zinazong’ara na chini akiwa amevaa raba. Alionesha kuwa mtu ambaye anajimudu kidogo kimaisha, nikashusha pumzi ndefu na kuendelea kumtazama mwili wake uliokuwa umejazia, akionesha wazi kwamba ni mtu wa mazoezi.
“Unaonaje tukawa na mazungumzo kidogo baada ya kutoka hapa? Usiwe na wasiwasi, mimi nitakulinda.”
“Sihitaji kulindwa, naweza kujilinda mwenyewe.”
“Hizo hasira umerithi kwa nani?” aliniuliza huku akichekacheka, sikumjibu chochote zaidi ya kujiinamia huku nikiendelea kuugulia maumivu ambayo sasa yalikuwa yamepungua sana.
Hata sijui nani alilipia ile huduma niliyoipata pale lakini baadaye, yule mwanaume ambaye bado sikuwa namjua ni nani na kwa nini ameamua kunisaidia, aliniambia tuondoke, nikainuka na kumfuata.
Nilichokigundua, kumbe hakuwa peke yake, alikuwa na wenzake kama watatu hivi ambao hata pale eneo la tukio niliwaona. Wenzake walikuwa wamekaa upande wa mbele wa lile duka na ilivyoonesha ni kama hawakuwa wanataka watu wajue kama wapo pamoja maana hata sisi tulipotoka, nao waliinuka mmoja baada ya mwingine na wakawa wanakuja nyuma yetu.
“Hawa ni akina nani?” nilimuuliza yule mwanaume.
“Wako wapi?”
“Hao wanaokuja nyuma yetu?” nilimuuliza swali ambalo lilimfanya anitazame usoni na kutabasamu. Umegunduaje kama wanatufuata?” alinijibu huku akitabasamu. Basi kule nje watu bado walikuwa wamekusanyika kwa makundi makundi na waliponiona nimetoka, wengine walianza kupiga miluzi huku wengine wakishangilia.
“Umeshakuwa staa!” alisema yule mwanaume huku akinigeukia, nikashindwa kuelewa anamaanisha nini.
Mbele kidogo, tuliingia kwenye gari dogo lenye vioo vya giza (tinted), akanielekeza kukaa siti ya pembeni ya dereva wakati yeye akikaa nyuma ya usukani.
Muda mfupi baadaye, wale wanaume wengine ambao nilishawahisi kama wanatufuata kwa nyuma, nao waliingia na japokuwa gari lilikuwa dogo na wao kila mmoja alikuwa na mwili mkubwa, waliweza kutosha kukaa wanne kule nyuma.
“Dogo anataka kuwajua nyie ni akina nani?”
“Aah tusamehe mzee, usije kutuchenjia kama ulivyomchenjia konda,” alisema mmoja, wote wakacheka sana na wakawa wananisalimu kwa kunipa mikono ningongesheane nao, watoto wa mjini wanaipa kupeana tano.
“Usiwe na wasiwasi, hawa ni marafiki zangu na upo kwenye mikono salama,” alisema yule dereva huku akiondoa gari. Akaniuliza tena kama ni kweli nataka kazi.”
“Ndiyo nataka kazi braza,” nilimwambia, safari hii kwa upole na nidhamu kwa sababu nilishaona kweli ana nia ya kunisaidia.
“Tutakupeleka kwa bosi wetu, naamini huwezi kukosa kazi ya kufanya, hasa tukimsimulia ulivyotaka kumwaga ubongo wa konda wa daladala,” alisema, wenzake wote wakacheka sana na kugongesheana mikono.
Moyoni nilikuwa na hofu lakini sikutaka sana kuitanguliza hofu yangu maana ni kweli nilikuwa natafuta kazi na kilichotokea ilikuwa ni kama zari. Basi tuliingia kwenye barabara ya lami na safari ya kuelekea mjini ikaendelea, wakawa wanapiga stori za hapa na pale na kucheka kwa nguvu.
Je, nini kitafuatia?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 10

ILIPOISHIA:

Basi tulienda mpaka mbele kidogo, kwenye kituo kilichochangamka sana ambacho baadaye nilikuja kugundua kwamba panaitwa Mombasa. Kwa wenyeji wa Gongo la Mboto watakuwa wanapajua vizuri. Basi dereva akapunguza mwendo na kutoka kwenye barabara ya lami, akaingia mpaka kwenye maegesho ya baa moja iliyokuwa jirani na barabara.
“Shuka mdogo wangu tukainue mioyo yetu,” alisema yule dereva huku akinipigapiga begani, watu wote wakashuka na mimi nikashuka, ‘aka-lock’ milango yote kisha wakatangulia na kuanza kupandisha kwenye ngazi za kuingia kwenye hiyo baada, na mimi nikawa nawafuata.
Tulipoingia kwenye baa hiyo, waliongoza moja kwa moja mpaka kwenye chumba kilichokuwa kimejitenga, ndani kabisa ambapo mlangoni kilikuwa na maandishi yaliyosomeka VIP. Wakati tunapita, karibu watu wote waliokuwa ndani ya baa ile, waliacha kila walichokuwa wanafanya na kuanza kututazama.
Sikuelewa haraka kwa nini hali hiyo imetokea lakini sikutaka kuwa na haraka ya kujua mambo. Basi tuliingia mpaka kule ndani, wakaja wahudumu wa tatu wa kike waliokuwa wamevalia kihasarahasara, wakawa wanasalimiana nao kwa kukumbatiana na kupeana mabusu.
Ilionesha ni kama wanafahamiana kwa jinsi walivyokuwa wanachangamkiana. Muda mfupi baadaye, meza ilikuwa imejaa vinywaji, kuanzia pombe kali, bia za kawaida na pakti mbili za sigara. Kwa fujo hizo ilionesha kwamba walikuwa na fedha za kutosha, nikawa nashangaashangaa tu.
“Unakunywa pombe gani?” aliniuliza yule mwanaume ambaye alikuwa amekaa pembeni yangu. Kwangu mimi alikuwa ndiyo mwenyeji wangu kwani angalau alinionesha roho nzuri tangu aliponikuta katikati ya timbwili na yule konda.
“Fanta orange!” nilisema, wote wakacheka na kugongesheana mikono.
“Unakunywa Fanta kwani wewe mgonjwa? Utatujazia nzi bure hapa! Kunywa hii,” alisema huku akifungua chupa ndogo ya bia yenye rangi ya kijani. Aliifungua kwa kutumia chupa nyingine na kuiweka mbele yangu.
Niseme ukweli kwamba katika maisha yangu sikuwa nimewahi kunywa pombe hata mara moja, kwa hiyo huo ulikuwa mtihani mkubwa kwangu.
“Hiyo wala siyo chungu na haieleweshi, kunywa uchangamke,” alisema huku wenzake wakiendelea kucheka. Nikajikaza kisabuni na kuishika, nikapeleka mdomoni na kupiga funda moja. Ni kweli haikuwa chungu sana kama nilivyokuwa nasikia lakini sikuipenda ladha yake, nikaendelea kujikaza na kumeza.
Ndani ya dakika zisizozidi kumi, walikuwa wameshamaliza pombe zote pale mezani kwani staili yao ya kunywa ilikuwa ni fujo tupu, mtu akishika chupa ya bia haishushi mpaka iishe, wakachangamka sana huku moshi mwingi wa sigara ukinipa wakati mgumu sana.
Mpaka wanamaliza, mimi ya kwangu hata nusu haikuwa imefika, wakainuka na kuniambia niwasubiri hapohapo wanakuja, aliitwa mhudumu mmoja na kukabidhiwa eti anilinde.
“Akimaliza muongezee na akitaka chakula mhudumie, tunakuja sasa hivi,” alisema yule mwenyeji wangu huku akinipigapiga begani, nikawa natingisha kichwa kukubaliana naye. Walipotoka, nilimuomba yule mhudumu anihamishie kule nje kulikokuwa na hewa maana chumba chote kilikuwa kimejaa moshi wa sigara.
Alinisaidia kubeba chupa yangu ya bia, akaenda kuniwekea kwenye meza ambayo haikuwa na mtu, basi watu wakawa wananitazama kwa macho ya wiziwizi huku wakiwa ni kama wananong’onezana jambo.
Sikuwajali sana, nilihisi wananitazama jinsi ninavyoinywa ile bia kwani kiumri bado nilikuwa mdogo. Niliendelea kunywa taratibu huku safari hii nikijitahidi kutoonesha ushamba.
Dakika kama tano hivi baadaye, wote tuliokuwa ndani ya baa hiyo tulishtuka baada ya kusikia milio ya risasi, watu wote wakaacha kila walichokuwa wanakifanya, wengine wakainuka harakaharaka na kuanza kuangalia uwezekano wa kukimbia.
Sikuwa nimewahi kusikia milio ya risasi zaidi ya kusikia tu kwa watu wakihadithiana lakini iliposikika tu, nilijua lazima ndiyo risasi hizo nilizokuwa nikisikia tu kwa watu. Ilivyoonesha, milio hiyo haikutoka mbali sana na pale tulipokuwepo.
Muda mfupi baadaye, ukimya ulitawala, kwa mbali likaanza kusikika gari likija kwa kasi kubwa huku muungurumo wake ukiwa mkubwa kama yale magari ya mashindano, kila mtu akawa anatazama barabarani kutaka kutazama ni gari gani lililokuwa linapita kwani ilionesha kuna uhusiano wa gari hilo na milio ya risasi iliyosikika.
Katika hali ambayo iliniacha mdomo wazi, nilishuhudia lile gari tulilokuja nalo likiingiakwa kasi kwenye maegesho ya pale baa tulipokuwa tumekaa. Akashuka yule mwenyeji wangu na kupanda ngazi harakaharaka, akaelekea moja kwa moja kule kwenye kile chumba walichoniacha.
Niligundua kwamba kwa vyovyote atakuwa ananitafuta mimi, basi nikasimama harakaharaka na kumfuata.
“Tuondoke!” alisema huku kijasho chembamba kikiwa kinamtoka. Sikupata hata nafasi ya kumuuliza chochote, nikawa namfuata nyumanyuma akielekea kwa haraka pale kwenye gari, watu wote wakawa kimya kabisa. Alifungua mlango na mimi harakaharaka nikaingia.
Ndani ya sekunde chache tu, alilitoa lile gari kinyumenyume, akafunga breki kali na kuzungusha usukani kwa nguvu, akakanyaga mafuta na kuganya gari liondoke kwa kasi mithili ya yale magari ya mashindano. Wenzake kule nyuma walikuwa kimya kabisa, mara kwa mara wakigeuka kutazama walikotoka.
Mbele kidogo kulikuwa na taa za kuongozea magari na licha ya taa nyekundu kuwaka kuonesha magari yaliyokuwa yakitokea kule tulipokuwepo yanatakiwa kusimama, dereva alicheza ‘faulo’ moja ya hatari ambayo nusura isababishe ajali, akakata kona na kuingia upande wa kulia kwenye barabara ambayo hata sikuwa najua inaelekea wapi, akakanyaga mafuta kwa nguvu na kufanya watu wote walioshuhudia jinsi alivyopita pale kwenye mataa akiwa haamini kilichotokea.
Mwendo aliokuwa akienda nao ulikuwa unatisha kwelikweli, nikajishikilia vizuri kwenye kiti kwa sababu sikuwahi kupanda kwenye gari linaloendeshwa vibaya kama hilo. Ndani ya dakika chache tu, tulikuwa tayari tumefika mbali sana, nje kabisa ya mji.
Mbele kidogo alipunguza mwendo na kukata kuingia kwenye barabara nyembamba upande wa kushoto, safari ikaendelea kwa kasi kubwa na kuishia mbele ya geti kubwa la chuma ambapo alipiga honi mara mbili, likafunguliwa na gari kuingizwa ndani kisha geti likafungwa.
Hakusimama, aliendelea kukanyaga mafuta mpaka kwenye geti la pili ambalo lilifunguliwa, akaingiza gari na kupaki ndani ya kama ‘godauni’ kubwa, tukateremka huku mimi nikigeuka huku na kule kushangaa mandhari ya eneo hilo.
Lilikuwa ni godauni kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na watu kadhaa wakifanya kazi za ufundi wa kuchomelea vyuma huku wengine wakiwa bize kutengeneza magari mengi yaliyokuwa ndani ya godauni hilo.
“Twende huku,” alisema yule mwanaume, tukawa tunatembea kwa kasi kuelekea ndani zaidi ya lile godauni. Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba wale wanaume walikuwa na begi ambalo hata sikujua ndani yake lina nini lakini katika kumbukumbu za awali, sikuwaona mahali popote wakiwa na begi.
Ndani ya kichwa changu, nilishahisi kwamba begi lile lina uhusiano mkubwa na tukio la kusikika kwa milio ya risasi na ule mwendo tuliokuja nao mpaka ndani ya eneo hilo lililokuwa limezungushiwa ukuta mrefu kwa nje.
“Huyu ni nani na ameingiaje humu ndani?”
“Huyu ni mgeni wa bosi.”
“Mbona sina taarifa zake,” alisema mlinzi aliyekuwa kwenye geti la kutokea kwenye lile godauni upande wa ndani kabisa.
“Hili lipo kwenye mikono yangu, nimeshakwambia ni mgeni wa bosi,” alisema yule mwenyeji wangu kwa sauti ya kibabe, mlinzi ambaye alishaonesha dalili za kutaka kunizuia nisipite, alishusha bunduki yake na kusogea pembeni kutupisha, tukaingia.
Kwa kule ndani, kulikuwa na nyumba kama tatu hivi, zilizojengwa kisasa kama makazi ya watu wenye fedha zao. Yaani usingeweza kuamini kama hapo ni wapi kwa sababu mazingira ya kule nje kabisa ya geti, ndani ya geti, ndani ya godauni na kwenye nyumba hizo, yalikuwa tofauti kabisa.
“Utamweleza bosi kama ulivyonieleza mimi.”
“Kuhusu nini?”
“Kuhusu kazi! Mweleze moja kwa moja, usipindishe maneno,” aliniambia kwa sauti ya kunong’ona wakati tukikaribia kwenye mlango wa vioo wa kuingilia kwenye moja kati ya nyumba zile. Pale nje ya mlango palikuwa na ile mashine maalum inayotumika kukagua watu wanaoingia maeneo yenye ulinzi, kama uwanja wa ndege.
Kulikuwa na wanaume watatu wenye miili mikubwa waliovalia sare maalum ambapo walikuja na vikapu maalum vya plastiki, wakawa wanamsogezea kila mmoja. Kilichotokea kilinishtua mno, kumbe kati ya wale watu tuliotoka nao Gongo la Mboto, ni mimi pekee ndiyo sikuwa na silaha, kila mtu alikuwa na bunduki.
Mwenyeji wangu ndiye aliyekuwa wa kwanza kutoa ya kwake, tena siyo bastola bali bunduki kubwa iliyokuwa imekatwa mtutu na kitako na kuwa fupi. Alinitazama kisha akawa ni kama ananikonyeza hivi, nilishindwa kuelewa anamaanisha nini.
Basi wote walikabidhi silaha zao kisha wakakaguliwa kwa kile kifaa maalum chenye uwezo wa kugundua kama una chuma chochote mwilini, mmoja kati ya wale wanaume akabonyeza namba fulani ukutani na mlango ukafunguka.
Tuliingia ndani ambako kulikuwa na watu wengine kadhaa wakiendelea na kazi zao, huyu yuko bize na kompyuta, mwingine anapekuapekua mafaili, yaani ilikuwa ni ofisi kabisa. Tulipita kwenye ofisi kadhaa, tukatokea kwenye ofisi kubwa yenye vioo kila upande, mlango mkubwa ukafunguka wenyewe na tukaingia mpaka ndani.
Wote waliinama kwa heshima na kusimama kwa kujipanga, yule aliyekuwa amebeba begi akasogea mbele hatua kadhaa na kuliweka juu ya meza kisha akarudi kujipanga kama wenzake, nikawa natetemeka kuliko kawaida.
Kwa muda wote huo, yule mwanaume ambaye bila hata kuuliza nilijua ndiye bosi mwenyewe, alikuwa akihangaika kuwasha sigara kubwa au maarufu kama ciger huku mkononi akiwa anabofyabofya simu yake ya bei mbaya.
Ilipowaka, alivuta na kutoa moshi mwingi kisha akawatazama mmoja baada ya mwingine bila kuzungumza chochote na macho yake yakatua kwangu, akayagandisha huku akiwa ni kama ananishangaa.
Je, nini kitafuatia?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 11

ILIPOISHIA:
Ilipowaka, alivuta na kutoa moshi mwingi kisha akawatazama mmoja baada ya mwingine bila kuzungumza chochote na macho yake yakatua kwangu, akayagandisha huku akiwa ni kama ananishangaa.
SASA ENDELEA...
Nilimuona yule mwenyeji wangu akimsogelea bosi kwa unyenyekevu, akainama pembeni yake kisha akawa ni kama anamnong’oneza kitu fulani. Nilijua kabisa lazima atakuwa anampa taarifa zangu, naye akawa ananitazama kwa kunikazia macho.
Hakutingishika wala kujibu chochote, baada ya kumalizia kuzungumza naye, alirudi pale alipokuwa amesimama na kujipanga na wenzake, nikaona yule bosi akininyooshea kidole kisha akanipa ishara kama anayeniita.
“Huku nikitetemeka, nilisogea huku nikiwa makini kumtazama. Aliwapa ishara wale wengine wote kutoka, mle ndani tukabaki mimi na yeye tu, akanionesha kwa ishara sehemu ya kukaa, jirani na pale alipokuwa amekaa na ‘kukunja nne’ huku akiendelea kuvuta ‘ciger’.
Kwa zaidi ya dakika tano nzima hakuzungumza chochote zaidi ya kuendelea kuvuta sigara huku akitoa moshi mwingi angani, akawa anabofyabofya simu yake na wakati mwingine akiandikaandika vitu kwenye laptop yake ya kisasa, zile zenye kama alama ya ‘epo’ kwa nyuma, wenyewe wanaziita ‘Mac Book’.
“Unaitwa nani!” aliniuliza kwa sauti nzito ya kukwaruzakwaruza.
“Naitwa Kenny!”
“Bonta ameniambia taarifa zako, unahitaji nikusaidie nini?”
“Naomba kazi bosi, kazi yoyote tu hata ya kufagiafagia bosi, baba yangu anaumwa sana, dawa zake zimemuishia na yeye ndiye pekee tuliyekuwa tunamtegemea, nisaidie bosi nipo tayari kufanya chochote,” nilisema huku machozi yakianza kunitoka.
“Unalia nini sasa? Wewe ni mwanaume unatakiwa kuwa na roho ngumu,” alisema huku akikaa vizuri pale kwenye sofa alilokuwa amekalia, akaendelea kuchezea simu yake huku akinitazama mara mojamoja.
“Baba yako anaumwa nini?”
“Anaumwa sana, madaktari wamesema hawaoni ugonjwa na hivi tunavyoongea amekata kauli, yaani wa leo wa kesho!” nilisema huku nikijisikia uchungu mkali sana ndani ya moyo wangu. Kiukweli nilikuwa nahitaji bosi huyo anionee huruma na kunisaidia.
“Umesoma mpaka darasa la ngapi?”
“Form Two, nililazimika kuacha baada ya baba kuanza kuumwa na hivyo kukosa mtu wa kunilipia ada, nataka nikipata kazi nije nijisomeshe mwenyewe,” nilisema kwa adabu.
“Hebu chukua huu mzigo, mwaga fedha zote mezani kisha uanze kuzipanga kulinganana thamani, noti za shilingi elfu kumi zitenganishe upande wake na za elfu tano kisha utazihesabu,” alisema huku akinioneshea lile begi lililokuwa pale mezani kwake.
Ni begi hilo ndiyo tuliloingia nalo na wale niliokuwa nimeongozana nao wakamkabidhi, nilishtuka sana kugundua kwamba kumbe lilikuwa limejaa mabunda ya fedha.
Mpaka hapo sasa nilikuwa nimeshaanza kupata picha ya kinachoendelea, kwa sababu niliunganisha matukio ya milio ya risasi kusikika, wale wanaume kuja pale waliponiacha kwa kasi kubwa, kunichukua kwenye gari, kuondoka kwa kasi kama ya magari ya mashindano na mwisho kukabidhi mzigo kwa bosi.
Harakaharaka nilianza kufanya kazi aliyonipa yule bosi kwa sababu niliamini hiyo ndiyo inaweza kuwa tiketi ya kupata msaada kutoka kwake. Nilianza kwanza kwa kufungua fedha zote zilizokuwa kwenye mabunda, kisha nikawa natenganisha, noti za shilingi elfu kumi naziweza sehemu yake na za elfu tano mahali pale.
Nikiri kwamba achilia mbali kuzishika, katika maisha yangu sijawahi kuona fedha nyingi kiasi hicho. Yalikuwa ni mabunda makubwamakubwa, yakiwa yamefungwa kwa ‘rubber band’, yakiwa na mchanganyiko wa noti za aina mbili tu, za elfu tanotano na za elfu kumikumi.
Baada ya kumaliza kupanga, nilianza kuhesabu, nikawa nachanganyachanganya hesabu kutokana na mchecheto niliokuwa nao.
Ilibidi anielekeze namna ya kuhesabu, akaniambia niwe nahesabu moja moja, yaani nihesabu idadi ya noti nyekundu ni ngapi kisha nihamie zile za elfu tano. Nilihesabu mpaka zote zikaisha, yeye akawa anaandika kila kiasi ninachomwambia.
Kulikuwa na noti za elfu kumikumi, elfu tano na mia nne ambazo ukizipigia hesabu, ni karibu shilingi milioni hamsini na nne, na kulikuwa na noti nyingine za elfu tanotano karibu elfu tatu. Kilikuwa ni kiwango kikubwa mno cha fedha ambacho kama nilivyosema, sikuwahi kukishika katika maisha yangu.
Baada ya kumaliza kuhesabu, alinielekeza namna ya kuzipanga, nikawa nazifunga vizuri kwenye mabunda ya shilingi milioni kumikumi. Baada ya kumaliza, alinielekeza kukaa palepale nilipokuwa nimekaa awali kabla ya kuianza kazi hiyo.
“Hii kamnunulie baba yako dawa na kutimiza mahitaji mengine madogo, unatakiwa kurudi hapa kesho asubuhi na mapema, utaondoka na Bonta,” alisema huku akinipa bunda lililokuwa na karibu shilingi laki tatu.
Sikuyaamini macho yangu, niliinua mikono juu kamaishara ya kumshukuru Mungu, machozi ya furaha yakawa yananitoka nikiwa hata sijui nimshukuru vipi Mungu wangu. Basi Bonta, yule mwenyeji wangu aliitwa na kupewa maelekezo ambayo mimi sikuyasikia, kisha akanipa ishara kwamba nimfuate.
“Vipi bosi anasemaje?”
“Ameniambia unisindikize twende nyumbani nipeleke hizi hela za kumnunulia baba dawa kisha turudi kesho asubuhi,” nilimwambia kwa furaha.
“Nilikiwambia bosi wetu hana noma, cha msingi ni uaminifu tu na kubwa hutakiwi kumweleza yeyote kuhusu chochote unachokijua, kuanzia tulivyokuokoa kule mpaka ulivyokuja kuonana na bosi,” aliniambia huku tukitembea harakaharaka kutoka nje ya lile godauni kuelekea nje kabisa.
Nilimuahidi Bonta kwamba nitatunza siri zote na nitafanya kazi zote kwa bidii na kwa moyo wangu wote. Tulitoka mpaka kule nje kabisa ambapo Bonta alichukua pikipiki moja kubwakubwa hivi, akanipa ishara kwamba nipande, kweli nikafanya hivyo kissha tukaenda mpaka kwenye geti kubwa la kutokea ambapo alisaini kwenye daftari maalum kisha tukatoka.
Safari hii alikuwa akiendesha pikipiki kwa mwendo wa kawaida tu, tukaondoka nikiwa hata sijui tunaelekea wapi lakini breki ya kwanza ilikuwa ni Kipawa. Sikuwa napajua lakini mwenyewe ndiyo aliyeniambia kwamba panaitwa hivyo, siyo mbali sana na uwanja wa ndege.
Aliipitisha pikipiki yake kwa mafundi, akaiacha hapo kisha tukaelekea nyumbani kwake. Licha ya umri wake kuonesha kwamba anastahili kuishi na mke na watoto, Bonta alikuwa anaishi peke yake, kwenye nyumba ya vyumba vitatu iliyokuwa na kila kitu ndani kwa ndani.
Ilikuwa ni nyumba nzuri yenye vitu vingi vya thamani ndani, kulikuwa na televisheni kubwa ukutani, masofa ya kisasa na vitu vingine vingi lakini kasoro yake ni kwamba kulikuwa kuchafu, yaani vitu havikuwa na mpangilio.
“Unaweza kunisaidia kufanyafanya usafi mdogo wangu, ngoja mimi nikatafute msosi,” aliniambia na kiukweli, kutokana na mambo yote aliyonifanyia, moyo wangu ulikuwa mweupe kabisa kumsaidia chochote anachokitaka. Kwa jinsi tulivyolelewa kwenye familia yetu, nilikuwa na uwezo wa kufanya shughuli zote za nyumbani.
Kwa hiyo nilianza kufanya usafi mle ndani, nikafagia vyumba vyote, nikakusanya nguo zote chafu zilizokuwa zimetupwatupwa ovyo mle ndani na kuziweka kwenye kapu la nguo chafu, nikafunua mapazia yote ili hewa iingie na kuweka kila kitu sawa.
Baada ya hapo, nilianza kupiga deki na nilianzia kwenye chumba alichokuwa analala. Nikiwa nasogeza kitanda ili nifanye usafi mpaka chini, nilikutana na kitu ambacho sikukitegemea. Kulikuwa na bunduki iliyokatwa kitako, ikiwa imefungwa kwenye uchago wa kitanda.
Nilipatwa na hofu mwanzo, lakini baadaye nilipatwa na shauku ya kutaka kuitazama vizuri zaidi. Katika maisha yangu sikuwa nimewahi kuigusa bunduki hata mara moja, hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza, nikawa naichunguza vizuri huku nikitetemeka. Nikiwa naendelea kuishangaa, nilisikia mlango wa nje ukiguswa, harakaharaka nikairudisha mahali pale na kuendelea na usafi.
Bonta alipoingia, nilijifanya kama sijaona chochote, akawa anachekelea jinsi nilivyomsafishi
a nyumba yake vizuri. Aliweka chakula mezani na alikuwa pia amenunua chupa kadhaa za pombe kali, nyingine akaweka kwenye friji na akaniambia nimalizie usafi kisha ndiyo tule, yeye akawa anaendelea kunywa pombe kali.
Nilimalizia kufanya usafi na kumfuata, tukala pamoja chakula lakini yeye tayari alikuwa ameshaanza kulewa kwani hata mazungumzo yake yalikuwa hayaeleweki.
“Inabidi ukaze moyo mdogo wangu, hii kazi ngumu sana na ya hatari lakini inalipa,” aliniambia kwa sauti ya kilevi, nikamuuliza kazi gani, akacheka sana.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 12

“Usiwe na haraka, kila kitu utakijua kwa undani kabisa, unachotakiwa ni kuwa na subira,” alisema, sikutaka kuhoji sana kwa sababu kama angenitazama usoni angeweza kugundua jinsi nilivyokuwa na hofu baada ya kuiona ile bunduki.
Kiukweli ni kwamba nilikuwa nimekosa sana amani baada ya kuiona ile bunduki, moyoni nikawa najiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Hata hivyo sikutaka sana kujali sana kuhusu kilichokuwa kinaendelea au nilichokuwa nakishuhudia, cha msingi kwangu ni kwamba nilikuwa nimefunga safari kutoka kijijini kwetu kwa ajili ua kuja kutafuta maisha na sasa kulikuwa na kila dalili kwamba nipo kwenye sehemu ambayo ndoto zangu hizo zinaweza kutimia bila wasiwasi kwa hiyo sikutaka kujishughulisha na mambo yasiyonihusu.
Baada ya kumaliza kufanya usafi, tulikula chakula na baada ya hapo Bonta aliniambia na mimi niende nikaoge, nikafanya hivyo na baada ya kumaliza tulipumzika kidogo mpaka majira ya kama saa mbili hivi za usiku.
“Tuondoke, umesema kwenu ni kijiji gani?” aliniuliza Bonta, nikamweleza kwamba kunaitwa Msanga lakini nilishangazwa na uamuzi wake wa kutaka tuondoke usiku huo. Nilipoona giza limeanda kuingia nilidhani labda ataniambia tulale mpaka kesho yake, lakini nikakumbuka kwamba bosi alikuwa amesema tunatakiwa kurejea kesho yake asubuhi.
“Saa hizi?”
“Ndiyo! Kwani hapo Msanga kuna umbali gani?” alisema huku akijiandaa ikiwa ni pamoja na kuvaa gloves maalum za kuendeshea pikipiki kwenye mikono yake. Basi sikuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana naye.
Muda mfupi baadaye tulitoka na safari ya kuelekea Msanga ilianza kwa kutumia pikipiki yake kubwa ambayo ndiyo tuliyokuja nayo kutoka kule ofisini kwa bosi ambako mpaka wakati huo sikuwa najua kunaitwaje.
Wakati tunaondoka alikuwa akiendesha pikipiki kwa mwendo wa kawaida lakini kadiri tulivyokuwa tunazidi kusonga mbele ndivyo alivyokuwa akizidi kuongeza kasi, ukizingatia kwamba pikipiki hiyo ilikuwa ikipiga kelele sana, nilijikuta nikikosa amani mno ndani ya moyo wangu.
Pikipiki ilikuwa inakwenda kwa kasi kubwa na sikuwa na sehemu ya kushikilia zaidi ya kumshika Bonta mwilini, naye akawa anazidi kuichochea huku kwenye kona akiilaza utadhani tupo kwenye mashindano. Vile vibia nilivyokunywa viliyeyuka kutokana na hofu niliyokuwa nayo.
Ilifika mahali nikaona ni bora nifumbe macho nisiwe naona kilichokuwa kinaendelea kwani kiukweli mwendo aliokuwa akienda nao ulikuwa wa kutisha kwelikweli.
“Tunaelekea kwa wapi hapa?” aliuliza Bonta, swali lake likanifanya nifumbue macho, sikuamini kuona kwamba tayari tumeshafika Msanga. Yaani kwa mwendo tuliokuwa tukienda nao, hata kwa mtu ambaye angesafiri kwa gari asingeweza kufika kwa muda huo.
Nilimuelekeza na kweli muda mfupi baadaye tayari tulikuwa tukipita kwenye njia ya kuelekea nyumbani lakini safari hii tulikuwa tukienda kwenye mwendo wa taratibu kwa hiyo hata muungurumo ulikuwa wa chini. Safari iliishia nje ya nyumba yetu ambapo Bonta aliniambia kwamba natakiwa kuhakikisha ikifika saa sita, tunaianza safari ya kurejea Dar.
Nilimshangaa sana. Yaani tumeondoka Dar usiku, halafu tunatakiwa kusafiri tena usiku huohuo kurudi Dar, kivipi? Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu.
Yeye aliniambia kwamba haingii ndani na badala yake anaomba nimuoneshe sehemu kwenye baa ili awe anakunywa moja moto moja baridi. Nilimwambia nitajisikia vibaya sana kama hataingia kuwasalimu wazazi wangu, hasa baba yangu ambaye alikuwa hoi kitandani. Ilibidi akubali, akavua zile gloves zake, kofia kubwa aliyokuwa amevaa na koti kubwa sasa akawa na mwonekano wa kawaida ambapo tuliingia ndani.
Mshtuko walioupata ndugu zangu, ulikuwa mkubwa sana, kwanza kwa sababu niliondoka bila kuaga lakini pia muda ambao tuliingia haukuwa wa kupokea wageni, hasa kijijini kwetu. Ilikuwa ni tayari saa tatu kasoro za usiku.
Mama alinikimbilia na kunikumbatia, akawa ananitazama usoni huku akiwa ni kama haamini. Alikuwa na maswali mengi kuanzia mahali nilipokuwa kwa nini nimechubukachubuka usoni, huyo niliyekuwa naye ni nani na usiku huo tumetoka wapi lakini niliamua kumnyamazisha kwa kutoa burungutu la fedha na kumpa.
“Hizi ni kwa ajili ya kumnunulia baba dawa pamoja na kununua mahitaji mengine ya hapo nyumbani, nimepata kazi na natakiwa kwenda kuanza kesho asubuhi huko Dar. Tunaondoka usiku huuhuu nimekuja tu mara moja kuwaletea fedha,” nilimwambia mama asiwe na wasiwasi wowote na mimi, niko kwenye mikono salama na nitajitahidi kuwakumbuka mara kwa mara.
Nakumbuka mama alilia sana, sikujua analia nini lakini katika kilio chake alinishukuru saba kwa nilichokifanya kwa sababu fedha zilikuwa zikihitajika sana kipindi hicho kuliko wakati mwingine wowote na bahati nzuri, ndani ya muda mfupi tu nilikuwa nimeweza kwenda kuzitafuta na kuzipeleka.
Japokuwa hakusema lakini nilimuoa mama alivyokuwa akijivunia kuwa na kijana mimi, alinichukua na kwenda naye mpaka chumbani alikokuwa amelala baba, nilipiga magoti na kumuombea kwani baba hakuwa na uwezo wa kutambua chochote kilichokuwa kinaendelea. Hakumjua mtu aliyekuwa akiingia wala aliyekuwa anatoka.
Nilipata uchungu sana ndani ya moyo wangu na nilijiapiza kwamba nitafanya kila kinachowezekana kuhakikisha namsaidia baba, kwa muda woye huo, Bonta alikuwa amekaa sebuleni akiwa na ndugu zangu wengene wakipiga stori za hapa na pale, akiwasimulia kilichokuwa kinaendelea jijini Dar es Salaam na wao wakimpa stori za hapa na pale kuhusu kilichokuwa kinaendelea pale kijijini.
Nilitoka na kwenda kumchukua Bonta, tukaingia chumbani alikokuwa amelala baba ambapo naye alipiga magoti na kumuombea kwa Mungu kwa imani yake kisha akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi na kumpa mama kwa ajili ya kusaidia vitu vidogovidogo katika kumuuguza baba.
Japokuwa mwenyewe alikiona kitendo hicho kama kidogo na cha kawaida lakini ndani ya moyo wangu kilinifanya nijisikie tofauti sana. Kiukweli kuanzia muda huo, nilimuona Bonta kuwa zaidi ya ndugu kwangu. Ni yeye ndiye aliyenipokea kwa mara ya kwanza katika mazingira magumu sana ambayo alinikuta nikiwa kwenye ugomvi mkubwa na kondakta wa daladala.
Lakini ni yeye pia ndiye aliyenikutanisha na bosi na sasa ni yeye ndiye aliyekuwa akiongea nami wakati tukimtazama baba ambaye ama kwa hakika hali yake ilikuwa mbaya sana. Tulitoka chumbani na kwenda sebuleni ambapo mama aliagiza tuandaliwe chakula. Tulikula na baadaye tuliendelea na stori za hapa na pale, ilipofika majira ya kama saa sita kasoro, tuliaga kwamba tunaondoka, kila mtu akatushangaa.
“Mnaondokaje usiku namna hii?”
“Tuna usafiri wetu mama, isitoshe kama nilivyosema kesho ndiyo siku yangu ya kuanza kazi kwa hiyo hatuwezi kulala huku,” nilimwambia, akawa mgumu sana kukubali lakini ushawishi wa Bonta ulimfanya aamini kwamba nitakuwa kwenye mikono salama.
Basi tulitoka na safari ya kurejea jijini Dar es Salaam ilianza. Kama ilivyokuwa wakati tunakuja, Bonta alikuwa akiendesha pikipiki kwa fujo, yaani usipoinama, ule upepo unavyopiga unajikuta uso wote ukiwa umejawa na machozi. Hakuwa anajali mashimo wala mawe na uzuri ni kwamba pikipiki ilikuwa na nguvu, kwa hiyo akawa anafukia tu.
Saa sita kama na dakika arobaini hivi, tayari tulikuwa tumeshafika Gongo la Mboto, mimi mwenyewe sikuamini, Bonta akazidi kuichochea pikipiki yake na muda si mrefu tayari tulikuwa tumewasili Kipawa. Mpaka nashuka kwenye pikipiki na kuingia ndani kwake kulala, miguu yote ilikuwa ikitetemeka huku masikioni nikiwa nasikia mvumo wa sauti ya pikipiki.
Nilifika kwenye sofa na kujibwaga, Bonta akafungua friji na kutoa chupa ya pombe kali, akapiga funda moja na kunimiminia glasi moja, akanipa na kuniambia kwamba nipige funda moja nitajisikia vizuri ndani ya moyo wangu na kupunguza uchovu, jambo ambalo kweli nililifanya.
Japokuwa nilikunja uso kutokana na ukali wa pombe hiyo, lakini ndani ya moyo wangu nilijisikia poa kabisa kwa sababu ule uchovu wote uliyeyuka. Bonta akaingia chumbani na alipotoka, aliniambia mimi nilale yeye anatoka kidogo, akanielekeza kufunga milango yote, akaondoka na pikipiki yake.
Niliporudi kule chumbani, kitu cha kwanza ilikuwa ni kukagua kama ile bunduki ipo palepale lakini cha ajabu ni kwamba haikuwepo. Kwa tafsiri nyepesi ni kwamba Bonta alikuwa ameichukua, sasa amekwenda nayo wapi usiku wote huo? Sikuwa na majibu.

Tuendelee
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom