Riwaya: Saa za Giza Totoro

Riwaya: Saa za Giza Totoro

SEHEMU YA 06



ILIPOISHIA:
Nilitafuta sehemu nzuri, upande wa nyuma kabisa wa shamba hilo kubwa, nikajificha na kuanza kupanga namna ya kwenda kutimiza azma yangu. Ilikuwa ni lazima nimuokoe Saima kwa gharama yoyote, hasa ukizingatia kwamba ndani ya tumbo lake, alikuwa na kiumbe, mwanangu mtarajiwa, ambaye angekuja kuyabadilisha kabisa maisha yangu na kunifanya na mimi nianze kuitwa baba.
SASA ENDELEA...
Nikiwa bado palepale mafichoni, usingizi ukikizonga kichwa changu kutokana na ukweli kwamba sikuwa nimelala hata kidogo usiku kucha, nilisikia muungurumo wa pikipiki zaidi ya moja kutokea upande wa nyuma wa shamba kubwa.
Nilijiweka sawa, ‘chuma’ changu nikakikamata vizuri mkononi kwa ajili ya chochote kwani japokuwa nilikuwa sehemu ambayo naujua isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kuniona, nilikuwa nafahamu vizuri jinsi Mute anavyoendesha shughuli zake. Alikuwa na intelijensia ya hali ya juu pengine kuliko hata vyombo vingi vya usalama.
Nikiri kwamba japokuwa ni kweli nilikuwa na matatizo makubwa na Mute, lakini ni yeye ndiye aliyenifundisha kila kitu nilichokuwa nakifanya. Nikiwa kwake, ndiko nilikojifunza kutumia bunduki, mbinu za mapigano ya mwilini au kwa kitaalamu ‘martial arts’, kutumia silaha nyingine mbalimbali na sehemu muhimu unazotakiwa kuwa nazo makini unapotaka kupigana na mtu, iwe ni silaha au kwa mikono.
Unajua tofauti kubwa kati ya raia wa kawaida na askari aliyepitia mafunzo, ni kwamba raia wa kawaida unaweza kuwa unajua kwamba ukimpiga ngumi usoni adui yako, utampasua na kumtoa damu au kumng’oa meno lakini hutaweza kuzuia asiendelee kupambana na wewe lakini askari anajua kabisa akikupiga sehemu gani, unaweza kudondoka na kupoteza fahamu papo hapo, au pengine kufa kabisa.
Sikuwa askari lakini kwa mafunzo niliyoyapata bila hiyari yangu nikiwa chini ya mikono ya Mute, nilikuwa na ujuzi pengine kuliko hata askari wenye mafunzo ya kawaida na pengine hiyo ndiyo sababu iliyofanya niwe tishio kwa watu waliokuwa wananijua.
Licha ya yote hayo, bado kuna kosa kubwa sana alikuwa amelifanya Mute kwenye maisha yangu, kwa sababu kwanza mbinu zilizotumika mpaka nikawa mfuasi wake, hazikuwa sahihi, unajua kazi hizi za hatari bora mtu aamue mwenyewe kuwa mtu mbaya lakini siyo kuingizwa ukiwa hujui chochote na ndiyo maana chuki yangu kwake ilikuwa kubwa mno kiasi cha kujiapiza kwamba siku nikikutana naye, lazima nitautoa uhai wake, tena kwa mikono yangu mwenyewe.
Kule upande wa nyuma wa shamba lile nilikokuwepo, kulikuwa na njia ndogo ambayo nakumbuka kabla mimi na Mute hatujaingia kwenye haya matatizo makubwa, tulikuwa tukiitumia kuingia na kutoka mle shambani hasa kwenye ‘misheni’ maalum ambazo zinatakiwa kufanyika kwa usiri mkubwa.
Muungurumo ulizidi kusogea, na mimi nikawa najaribu kunyanyua shingo yangu kutoka pale kwenye maficho yangu, kujaribu kutazama ni nini kilichokuwa kinaendelea.
Nikashtuka kuona pikipiki kubwa tatu zikija kwa kasi kubwa, na kati ya hizo, ya kwanza ilikuwa na watu wawili, nyingine ilikuwa na watu wawili na nyingine ilikuwa na watu watatu.
Kwa jinsi nilivyokuwa naujua utendaji kazi wa vijana wa Mute, nilijua pale lazima kuna mtu ametoka kutekwa au kuna jambo lisilo la kawaida limetokea kwa sababu pia kulikuwa na sheria nyingine inayoagiza kwamba mnapoenda kwenye kazi, lazima pikipiki moja ibebe watu wawili, dereva na abiria ambaye kimsingi ndiye aliyekuwa akikaa na silaha ili likitokea la kutokea, dereva yeye kazi yake iwe ni kukimbia na yule abiria wa nyuma kazi yake iwe ni kujihami.
Ilikuwa ni makosa pikipiki kuwa na dereva peke yake au kuwa na zaidi ya watu wawili kwa hiyo nikajua lazima kuna jambo. Kama muda ule ndiyo walikuwa wakiwasili pale Kibaha, maana yake ni kwamba walikuwa wamefanya tukio usiku wa manane na eneo la mbali lililowalazimu kutembea umbali mrefu ili kuwahi kuukwepa mkono wa kisheria.
Basi macho yangu yote niliyaelekeza kwenye ile pikipiki iliyokuwa na watu watatu kwa sababu kwa hesabu zangu, nilijua kwamba lazima pikipiki zote zilikuwa na watu wawili kama ilivyo kawaida, sasa huyu mtu wa tatu ni nani? Nikawa natafuta majibu.
Nilipoitazama ile pikipiki vizuri, niligundua kwamba yule mtu wa tatu, alikuwa mwanamke na kwa jinsi ilivyoonesha, ni kama alikuwa ameteswa kwa muda mrefu kwani hata kukaa mwenyewe hakuweza, badala yake mtu aliyekuwa nyuma yake ndiyo akawa amemshikilia. Kwa maana hiyo ni kwamba alikuwa amekalishwa katikati, mbele dereva na nyuma mtu mwingine.
Pia nguo zake zilikuwa zimelowa kwa damu na wakati nazidi kukazia macho, moyo wangu ulinilipuka mno baada ya kugundua kwamba blauzi aliyokuwa amevaa, japokuwa ilikuwa imelowa damu, ilikuwa ikifanana sana na blauzi ya kipenzi cha moyo wangu, Saima.
Kumbukumbu zangu zilinionesha kwamba ndiyo aliyokuwa amevaa siku ya mwisho wakati anatekwa na kuchukuliwa kwa nguvu kutoka kule nyumbani, kabla ya baadaye nyumba yenyewe kuchomwa moto.
“No! Haiwezekani, haiwezekani,” nilisema huku nikitetemeka kuliko kawaida. Nilijisikia uchungu usiomithilika ndani ya moyo wangu, kwa nini wamfanyie vile Saima wangu?
Amewakosea nini mpaka wamteke na kumtesa kiasi kile? Kama shida ya Mute ilikuwa ni mimi, kwa nini asinichukue na kwenda kunifanya chochote anachokitaka? Kwa nini wamfanye vile Saima, tena akiwa na ujauzito wangu?
Wamasai wana kitu kinaitwa mori! Yaani kijana wa Kimasai akipandisha mori, anaweza hata kupambana na simba na akamuua kwa mikono yake.
Basi na mimi japokuwa sikuwa Mmasai, nilijikuta nikipandwa na mori, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida, mwili nikahisi ukiwa na nguvu za ajabu, hofu yote ikaniisha na nikajiapiza kwamba ama zangu, ama zao! Nife mimi, au wafe wao wote lakini siwezi kukubali kumuona Saima wangu katika hali ile.
Japokuwa pale nilipokuwa nimekaa palikuwa ni juu kidogo, kwenye tawi la mti mkubwa, nilijirusha mpaka chini na cha ajabu hata sikufikiria mara mbili nitadondokea sehemu gani, kwa bahati nzuri pale chini palikuwa pameliwa matuta ya viazi, kwa hiyo ikawa ahueni kwangu.
Kishindo cha kuruka kwangu, kiliwashtua wale vijana wa Mute, nikamuona mmoja akiwapa ishara wenzake, wale waliokuwa wamembeba Saima wakazidi kuongeza kasi huku wale wengine wakigeuza pikipiki zao na kutazama kule nilikokuwepo, ambako ndiko kishindo kilipotokea.
Nilitambua kwamba malengo yao ni kuhakikisha misheni ya kumuingiza Saima ndani ya lile shamba inafanikiwa na ndiyo maana wale wengine waliongeza mwendo na sasa wakawa wamekaribia kwenye geti dogo la nyuma, huku wale wengine wakijiandaa kukabiliana na chochote kilichokuwa kinataka kuvuruga misheni yao.
Kwa sababu tayari nilishajua lengo lao, na mimi niliamua kupiga hatua moja zaidi kichwani mwangu, na kuhakikisha nazuia Saima asiingizwe mle ndani. Kwa kawaida, bunduki ikiwa na risasi, ili ufyatue risasi ni lazima kwanza uzivute risasi kwenye chemba kisha ndiyo uvute ‘trigger’ ili kuruhusu risasi itoke.
Na kisheria, kama bunduki haitumiki, risasi hazitakiwi kukaa kwenye chemba kwa sababu ni hatari sana, zinaweza kukulipukia hata wewe mwenyewe kwa bahati mbaya endapo ukigusa ‘trigger’ hata kwa bahati mbaya.
Kama umewahi kufuatilia kwa makini, hata kwenye filamu za mapigano, kabla mtu hajafyatua risasi, ni lazima kwanza aikoki bunduki au bastola yake, kile kitendo cha kukoki ndiyo kinachozivuta risasi kutoka kwenye ‘magazini’ na kuziingiza kwenye chemba.
Ni kitendo ambacho kinachukua sekunde kadhaa tu, lakini kwa akili ya mtu kama mimi, ninapokuwa na ‘bomba’ mkononi, sekunde moja pekee ilikuwa inatosha kufanya tukio la kushangaza. Maana yangu ni kwamba, wakati mimi nilishaikoki bunduki yangu na kuzijaza risasi kwenye chemba, wale wafuasi wa Mute bado walikuwa hawajafanya hivyo kwa sababu nilikuwa ni kama nimewashtukiza.
Kwa hiyo ule muda wa sekunde kadhaa za kushuka kwenye pikipiki, kuweka sawa bunduki zao na kuzikoki, ulitosha kunifanya niwe nimeshawatangulia mbele hatua kadhaa, kwa hiyo nilichokifanya, nilimlenga yule dereva aliyekuwa anaongeza mwendo kuelekea kwenye lile geti dogo.
Nadhani nilichokifanya hawakukitegemea kabisa kutokana na jinsi nilivyoweza kufanya ‘timing’ sahihi ya muda, basi yule mwenzao alipiga yowe kwa nguvu, pikipiki ikayumba na kupoteza mwelekeo, wakadondoka kama mzigo. Nilijua lazima Saima naye anaweza kuumia lakini ilikuwa ni bora nusu shari kuliko shari kamili.
Kilichofuatia baada ya hapo, ilikuwa ni mvua ya risasi, mitutu zaidi ya minne ilielekezwa kwangu, kila mmoja akawa ananifyatulia risasi. Wasichokijua wengi ni kwamba vita ya kurushiana risasi siyo sawa na kupigana ngumi, kwamba wewe unarusha na mwenzako anarusha kwa wakati huohuo! Ilikuwa ni lazima kutumia akili, mwenzako akiwa anakushambulia wewe unaji-cover kwenye eneo ambalo risasi haziwezi kukupata, kisha na yeye akizubaa kidogo na wewe unashambulia kwani pale unakuwa umeushika uhai wako mkononi, akifanya uzembe kidogo tu, basi unakuponyoka.
Sasa sijui ni kwa sababu ya ‘kupaniki’ au nini, wale wafuasi wa Mute ambao nilikuwa naamini kwamba nao wanazo mbinu kama nilizonazo mimi, walikuwa wakishambulia tu bila ku-take cover.
Kwa hiyo nilichokifanya kabla risasi ya kwanza haijafyatuliwa, niliwahi kuruka na kulala chini, nyuma ya matofali ambayo ilionesha yalisalia wakati wa ujenzi wa ukuta, kwa hiyo risasi zote zilikuwa zikiishia kwenye matofali hayo, wakawa wananishambulia huku wakinisogelea ‘kibwegebwege’, nikaona huo ndiyo muda wa kukamilisha kile kilichonifanya nifunge safari mpaka eneo hilo.
Ghafla niliinuka huku ‘bomba’ likiwa mkononi, kidole kikiwa kwenye ‘trigger’, nikazichekesha kwa mtindo wa kufagia kutoka kushoto kwenda kulia lakini ghafla nilihisi kitu kikipenya kwenye mwili wangu, damu zikaruka kama bomba lililopasuka, ghafla nikaanza kuhisi kama kizunguzungu.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 07

ILIPOISHIA
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kumbe tayari ilikuwa ni usiku lakini sikupata majibu hapo ni wapi na huyo mtu aliyekuwa akinisogelea ni nani. Kabla sijapata majibu, nilishtukia nikimulikwa na mwanga mkali usoni.
SASA ENDELEA...
“Umeamka?” sauti nzito ya yule mtu ilisikika ikinihoji huku akiwa bado ananimulika usoni, nikawa najaribu kujizuia lakini kwa kuwa mikono yangu ilikuwa imefungwa kwa nyuma, nilishindwa kufanya chochote kuuzuia mwanga ule, nikapata wazo la kufumba macho.
“Umefanya kazi nzuri sana leo,” alisema mwanaume huyo huku akizima ile tochi aliyokuwa ananimulika nayo, kisha akanisogelea pale kwenye kitanda nilipokuwa nimefungwa, akatoa kisu kidogo na kukata kamba nilizokuwa nimefungwa mikononi, akamalizia na miguuni.
Nilijaribu kuinuka huku nikiwa nimemkazia macho kwa sababu bado sikuwa najua yeye ni nani, nimefikaje hapo na kwa nini ananiambia maneno hayo. Kumbukumbu za tukio la mwisho kabla sijapoteza fahamu zilinifanya niwe kama nimechanganyikiwa.
“Hebu tulia kwanza, utajitonesha kidonda chako bure,” alisema mwanaume huyo huku akinionesha kwa ishara kwenye bega langu la upande wa kushoto, nikajitazama na kushtuka kuona nimefungwa bandeji kubwa.
“Una bahati sana, ingeshuka chini kidogo ilikuwa inaenda kukupiga kwenye moyo, mshukuru sana Mungu kwamba iliingia kutokea mbele, ikapita katikati ya mfupa wa bega na kutokea upande wa pili,” alisema mwanaume huyo ambaye sasa niliweza kumuona vizuri uso wake.
Nilishtuka kutokana na maelezo aliyokuwa ananipa, harakaharaka nikakumbuka kuhusu tukio la kurushiana risasi lililotokea kabla ya baadaye kuhisi kitu cha baridi kikipenya na kuingia kwenye mwili wangu, na baadaye kupoteza fahamu kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Nini kilitokea na nimefikaje hapa?”
“Ina maana hujui ulichokifanya?” alisema mwanaume huyo huku akinitazama, tabasamu hafifu likiwa limechanua kwenye uso wake. Nilihisi bado nipo kwenye hatari kubwa kwa sababu hata jinsi mwanaume huyo alivyokuwa akinitazama, ilionesha kama kuna kitu kinakaribia kutokea.
Nilichokifanya, japokuwa bado nilikuwa najisikia maumivu makali hasa pale kwenye mkono, nilianza kupiga hesabu za namna ya kumtoroka mwanaume yule.
“Unataka kutoroka si ndiyo?” aliniuliza mwanaume huyo, nikashtuka kugundua alijuaje kilichokuwa ndani ya kichwa changu, nikawa natingisha kichwa kuonesha kwamba siyo kweli.
“Unatakiwa kuniamini, niliamua kukusaidia kuanzia kipindi ambacho hukuwa na fahamu, kama ningekuwa na nia mbaya na wewe si ningeshafanya ninachotaka kukifanya?”
“Wewe ni nani?”
“Hunijui mimi Snox? Ina maana umenisahau?” alinijibu kwa kunitaja jina langu, nikajikuta nikizidi kuchanganyikiwa. Nikawa namtazama usoni huku nikijaribu kuvuta kumbukumbu zangu lakini bado sikuweza kumkumbuka kirahisi. Nadhani na yeye aligundua kwamba sijamtambua kabisa, ikabidi avue mzula aliokuwa ameuvaa na kunisogelea.
Ni hapo ndipo nilipomtambua! Huyu alikuwa miongoni mwa vijana wa Bosi Mute na jina lake alikuwa akiitwa Siza, nakumbuka aliajiriwa siku za mwishomwisho kabla mimi sijaamua kuachana na kazi hiyo na kuamua kuwa raia mwema baada ya kuchoshwa na aina ya maisha niliyokuwa naishi.
“Umenikumbuka sasa!”
“Nakufahamu.”
“Uliyaokoa maisha siku ile Ubungo, na kiukweli nilibaki na deni kubwa ndani ya moyo wangu, nilihuzunika sana niliposikia umeondoka lakini nikamshukuru Mungu kwa kuamua kukubadilisha,” alisema mwanaume huyo, kauli ambayo iliufariji sana moyo wangu.
“Najua upo kwenye wakati mgumu sana mdogo wangu, siku zote nimekuwa nikikuamini na naamini hata hili utalishinda kwa ujasiri mkubwa,” alisema huku safari hii akinipigapiga begani kama dalili ya kunifariji.
Nilikumbuka kuhusu tukio alilokuwa akilizungumzia na jinsi nilivyomuokoa! Nilijikuta nikisisimka sana mwili kwa sababu mwenyewe nilishasahau au pengine nilichukulia kama ni tukio la kawaida tu lakini kumbe bado Siza alikuw akilikumbuka tukio hilo na kuamua kunilipa kwa wema.
Waliosema wema hauozi hawakukosea, unajua unaweza kutenda wema pengine hata kama mpo kwenye tukio baya ambalo ni chukizo mbele ya Mungu na wanadamu, lakini kama umelifanya kwa nia njema kabisa, basi ipo siku litakuja kukurudia, hata kama atakayekufanyia wema siyo yule ambaye wewe ulimfanyia, unaweza kurudishiwa wema wako kwa namna ya tofauti kabisa. Nitakuja kuelezea kuhusu tukio hili la mimi na Siza baadaye lakini ni miongoni mwa matukio ya ujambazi yaliyowahi kuitingisha nchi na kuweka historia ya aina yake.
Wakati mwingine ni suala la kumshukuru Mungu tu kuona mpaka leo bado niko hai kwa sababu ama kwa hakika nimepitia mambo mengi sana kwenye hii dunia.
“Chuma changu kiko wapi?” nilimuuliza swali hilo ili niwe na uhakika na usalama wangu.
“Hiki hapa,” alisema huku akichukua bunduki yangu ambayo kumbe alikuwa ameihifadhi chini ya kile kitanda nilichokuwa nimelalia, akanipa kwa adabu, tena kwa kutumia mikono yote miwili. Nikainamisha kichwa kidogo kama ishara ya kumshukuru.
“Vipi kuhusu Saima?”
“Bado yuko chini ya mikono ya Bosi Mute.”
“Hapa ni wapi na nini kilichotokea?” nilimuuliza, akashusha pumzi ndefu na kunitazama, akanipigia saluti ambayo sikuelewa anamaanisha nini. Akaniambia yeye ndiye aliyekuwa zamu alfajiri ya asubuhi iliyopita na alishuhudia jinsi nilivyowapiga ‘ambush’ vijana wa Mute waliokuwa wakimuingiza Saima kwenye ngome hiyo.
“Mimi ndiye niliyekuwa getini na nilikuwa na taarifa tangu usiku kwamba kuna mzigo utafikishwa kambini alfajiri lakini sijui nini kikatokea wakachelewa kidogo.
“Wakiwa wamekaribia, niliwaona kutokea kwenye mnara wa mlinzi wa geti la nyuma, nikawa nawafuatilia wanavyosogea kama ilivyo kawaida ya kazi yetu,” alisema Siza na kuendelea kunieleza kwamba alifungua geti alipoona wamekaribia lakini ghafla akashtushwa na milio ya risasi zilizoanza kufyatuliwa kama mvua.
“Ilibidi nifunge geti na kufuatilia ni nini kilichokuwa kinaendelea lakini mpaka tunatoka nje,watu wote walikuwa chini, kila mmoja akiwa amechakazwa kwa risasi na cha ajabu, hakukuwa na mtu au watu waliofanya shambulio hilo baya, watu wote wakaamini kwamba lazima kuna watu wameshambulia na kukimbia lakini mimi nikawa mgumu kuamini kwa sababu aina ya upigaji wa risasi niliousikia ulikuwa tofauti.
“Kwa hiyo wakati wenzangu wanahangaika na wenzao ambao walikuwa na hali mbaya sana, wengine wakimkamata Saima na kumrudisha ndani, mimi niliamua kutoka na kulichunguza vizuri eneo la tukio na ndipo nilipokuona ukiwa umelala chini ya mti, damu nyingi zikiwa zimekutoka na kukufanya upoteze fahamu.
“Nikaamua kukubeba begani na kukimbia kuelekea porini kwa lengo la kutafuta nafasi nzuri ya kukusaidia bila mtu yeyote kujua chochote kinachoendelea na namshukuru Mungu nilifanikiwa na ndiyo maana leo upo hapa!
“Hapa ni Kibaha, Machinjioni na hatupo mbali sana na kambini,” alisema Siza, maelezo ambayo yalinifanya sasa nielewe ni nini kilichokuwa kimetokea.
“Vipi Mute anasemaje baada ya lile tukio?”
“Bado hajajua ni nani aliyehusika, ila kimsingi amechanganyikiwa sana, yaani amekuwa kama mbogo,” alisema Siza.
“Vipi kuhusu Saima wangu?”
“Yuko salama na bahati nzuri mimi na Teddy ndiyo tuliopewa jukumu la kumhudumia. Alikuja akiwa an hali mbaya lakini sasa hivi anaendelea vizuri, bado sijamwambia chochote kuhusu wewe ingawa mwenyewe anaonekana kama kuna kitu anakijua lakini hataki mtu yeyote ajue!
“Inaonesha alikuona ulivyokuwa unarushiana risasi pale getini na suala hilo limemchanganya sana kichwa chake. Kwani anajua kwamba wewe ni mzee wa bomba!”
“Mimi siyo mzee wa bomba Siza, wewe mwenyewe unajua kwamba hayo mambo nilishaachana nayo.”
“Anajua kwamba umewahi kupitia hii kazi?”
“Hajui chochote!”
“Ndiyo maana! Sasa nakushauri, utakapopata nafasi ya kuzungumza naye, mueleze ukweli awe anajua, pengine utamsaidia kumtuliza kichwa chake. Unajua kiumri mimi ni mkubwa kuliko wewe Snox, najua umuhimu wa hiki ninachokwambia.”
“Lakini mimi sifanyi tena hii kazi? Nimeshakuwa raia mwema hivi sasa.”
“Ungekuwa raia mwema usingefanya kile ulichokifanya pale getini! Ungewaacha wakupige risasi na kukuua! Ulichokifanya ni uthibitisho kwamba uwezo wako unazidi kuongezeka kila kukicha! Nani anayeweza kupambana kwa uwezo mkubwa kiasi kile na kuwaangusha watu wote? Wewe ni kamanda,” alisema huku akipiga tena saluti, nikaona kama ananichanganya kichwa.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 08



ILIPOISHIA:
“Ungekuwa raia mwema usingefanya kile ulichokifanya pale getini! Ungewaacha wakupige risasi na kukuua! Ulichokifanya ni uthibitisho kwamba uwezo wako unazidi kuongezeka kila kukicha! Nani anayeweza kupambana kwa uwezo mkubwa kiasi kile na kuwaangusha watu wote? Wewe ni kamanda,” alisema huku akipiga tena saluti, nikaona kama ananichanganya kichwa.
SASA ENDELEA...
“Namtaka Saima!”
“Unafikiri itakuwa rahisi kama unavyofikiria? Umefanya kazi na bosi Mute, unajua ni mtu wa aina gani.”
“Sijali chochote, namtaka Saima kwanza mengine yatafuatia.”
“Nenda kamchukue kama unaweza.”
“Ninaweza nandiyo maana nipo hapa,” nilimjibu kwa kujiamini, akanitazama usoni kisha akatingisha kichwa kama anayepingana na nilichokuwa nakisema.
“Mute ameshajua kwamba wewe ndiye uliyesababisha maafa makubwa kwa kuwapiga risasi vijana wake, unajua anawaza nini kuhusu wewe hivi sasa?”
“Sijali, ninachokitaka ni Saima wangu kwanza kisha mimi na yeye tutamalizana.”
“Basi kwa taarifa yako, ameagiza uuawe mahali popote utakapoonekana. Anasema mwanzo alijua unaweza kubadilika na kurudisha moyo wako nyuma lakini kwa kitendo kilichotokea, amebadilisha mawazo, anataka ufe.”
“Mimi pia nataka afe, na nitahakikisha namuua kwa mikono yangu.”
“Sikia Snox, usifanye maamuzi kwa hasira. Kwa hali uliyonayo hivi sasa, unatakiwa kwanza kukaa na kuuguza jeraha lako huku ukipanga mipango ya namna ya kurudi, utakapokuwa tayari mimi nipo tayari kukusaidia.”
“Nashukuru kwa msaada wako, ahsante sana Siza,” nilimwambia huku nikimpa mkono, naye akanipa wake, nikautumia kama ‘sapoti’ ya kusimama kutoka pale kitandani. Tukakamatana mikono kikakamavu kama kawaida yetu. Ghafla nilisikia maumivu makali pale kwenye lile jeraha la mkono, Siza akanituliza na kunitaka nikae, nikafanya hivyo.
“Huwezi kupambana ukiwa na hali kama hiyo, kaa utulie! Hapa ni sehemu salama, nitakulinda!” alisema Siza, nikamtazama usoni, na yeye akanitazama, macho yetu yakagongana na kweli alionesha kumaanisha alichokuwa anakisema.
Nilitikisa kichwa kuonesha kumkubalia, akaniambia nimsubiri anatoka kidogo lakini akanionya kutotoka nje. Alitoka na kuniacha mle ndani huku nuru ya mshumaa ikinisaidia kutazama vizuri mazingira. Lilikuwa ni jengo kubwa kama ghala fulani hivi ambalo halitumiki, na kulikuwa na vifaa vingi vya kilimo vikiwa vimehifadhiwa.
Niliendelea kuchunguza vizuri na katika utafiti wangu, nilibaini kwamba kuna uwezekano mkubwa ghala hilo likawa ni miongoni mwa maghala nisiyoyajua ya Bosi Mute kwa sababu alikuwa amejitanua sana maeneo ya kibaha, akijifanya anajishughulisha na kilimo cha kisasa.
Moyoni nilikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wangu, hasa kutokana na Siza kuniambia kwamba Bosi Mute alikuwa ameagiza niuawe baada ya tukio lile la kuwashambulia vijana wake na kujaribu kumtorosha Saima. Hata hivyo, kauli alizoniambia Siza kwamba nisiwe na wasiwasi atanilinda, zilinifanya kidogo niwe na amani.
Kilichonipa ujasiri zaidi, ni uwepo wa silaha yangu, nikaichukua pale nilipokuwa nimeiweka baada ya kuridhikana maelezo ya Siza, nikaikumbatia na kuibusu, nikawa naitazama huku mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu.
“Lazima nitakuokoa Saima, tena haraka kuliko unavyotegemea,” nilisema, nikaibusu tena bunduki yangu na kuiweka pale kitandani, upande wa kichwani kisha nikajilaza, mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu.
Nilikuwa nasikiamaumivu makali pale kwenye jeraha la mkononi lakini kwa kuwa haikuwa mara yangu ya kwanza kupata majeraha makubwa mwilini mwangu, tena ya risasi, nilijikuta nikipata nguvu za kuendelea kuvumilia maumivu hayo.
Kumbukumbu zangu zilinirudisha nyuma mpaka siku ya kwanza nilipokutana na Bosi Mute ambaye kama nilivyosema, ndiye aliyenifanya nikaingia kwenye kazi hiyo ya hatari kwelikweli.
***
Nakumbuka ilikuwa ni tarehe za mwishomwisho za mwezi Desemba, mwaka 2014, wakati maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya yakiwa yamepamba moto. Tofauti na familia zote ambazo zilikuwa zikiendelea na maandalizi ya sikukuu, kwetu sisi hali ilikuwa tofauti.
Nyumba yote ilikuwa imegubikwa na huzuni kubwa kutokana na hali ya kiafya ya baba ambaye alikuwa anaumwa sana, akiwa amefikia hatua ya kukata kauli. Tulishafanya kila kitu kama wanafamilia kuokoa maisha ya baba, alishatibiwa sana Hospitali ya Taifa ya Muhimbili bila mafanikio, tulishauza karibu mashamba na viwanja vyetu vyote kuokoa maisha ya baba, lakini yote ilikuwa ni kazi bure.
Hali ya kiafya ya baba ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele na ikafika mahali, hata hospitali kwenyewe tukaambiwa tujaribu kutafuta mbinu nyingine kwani ilionesha matibabu ya hospitalini hayawezi tena kumsaidia baba.
Kwa waliowahi kuuguza, watakuwa wanaelewa hali mnayokuwa nayo ndugu pale mnapoambiwa na madaktari kwamba jaribuni kuhangaika kwa njia nyingine kwani matibabu ya hospitalini yameshindikana. Kama hujawahi kufikwa na hali kama hiyo, maana yake huwa ni kama mnaambiwa mchukueni ndugu yenu akafie nyumbani.
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwetu, hatukuwa na cha kufanya zaidi ya kumchukua baba hospitalini akiwa na hali mbaya na kurudi naye nyumbani, Msanga, Kisarawe Mkoa wa Pwani.
Kiasili sisi ni wenyeji wa Kanda ya Ziwa, Mkoa wa Mara kwenye eneo liitwalo Kiabakari na huko ndiko tulikozaliwa ingawa baadaye katika pilika za maisha, baba alipata kazi kwenye mashamba ya korosho ya Mhindi mmoja kwa sababu kitaalamu baba alisomea mambo ya kilimo, tukahama kutoka Mara na kwenda Msanga na kujenga makazi yetu ya kudumu hapo.
Baba ndiye aliyekuwa kiongozi wa familia na maisha yetu yote tulikuwa tukimtegemea kwa hiyo kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja alipokuwa anaumwa, maisha yetu yalikuwa ya tabu sana.
Basi tukiwa hapo nyumbani, baadhi ya ndugu kutoka Mara walikuja, tukawa tunashirikiana kumsindikiza baba katika siku za mwisho za uhai wake, kwa hiyo pale nyumbani palikuwa ni kama pana msiba. Majirani na jamaa zetu nao walikuwa nasi bega kwa bega, wanaoishi jirani wakawa wanakuja na kuondoka huku wengine wakihamia hapohapo nyumbani kwa sababu sote tulikuwa tunajua lolote linaweza kutokea wakati wowote.
Hali ilipozidi kuwa ngumu pale nyumbani, wakati mwingine tukishinda njaa au kutegemea misaada ya ndugu, jamaa na marafiki, niliamua kuchukua uamuzi mgumu.
“Utaondokaje mwanangu wakati hali ya baba yako unaiona?”
“Sasa mama, unafikiri tutaendelea na maisha haya mpaka lini? Kuna dawa baba aliandikiwa aendelee kutumia akiwa nyumbani, zote zimeisha na hakuna fedha za kuzinunua tena, ndugu ndiyo kama hao unavyowaona, hakuna mwenye msaada zaidi ya kututegemea sisi, sina namna mama ngoja nikajaribu kutafuta hata kibarua mjini.”
“Kibarua gani mwanangu wakati hata elimu huna, umeishia form two kwa sababu ya kukosa ada, ingekuwa baba yako ameanza kuumwa ukiwa umemaliza form four angalau ningekuruhusu, utaenda kufanya kazi gani mjini?”
“Mama mimi ni mwanaume.”
“Sawa lakini wewe bado ni mdogo sana Kenny, mimi siwezi kukuruhusu mwanangu, kaa tu hapahapa nyumbani tutajua cha kufanya,” alisema mama akiwa na uso wa huzuni, macho yake yakiwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu.
Kiukweli japokuwa alinisihi sana, mimi nilishakuwa na uamuzi wangu na miongoni mwa tabia ambazo wazazi wangu walikuwa hawazipendi kabisa, ni suala langu la kuwa na misimamo yangu. Tangu nikiwa mdogo, nilikuwa na hulka moja kwamba nikishaamua kung’ang’ania kitu, lazima nikifanye hata kama nikikatazwa kiasi gani.
Basi japokuwa kwa nje nilionekana kama nimemuelewa mama, moyoni nilishaapa kwamba lazima niende Dar es Salaam. Uzuri ni kwamba kutoka Msanga mpaka Dar es Salaam siyo mbali sana, nikazugazuga pale nyumbani na nilipopata upenyo tu, niliondoka kimyakimya bila kumuaga mtu yeyote.
Nilienda moja kwa moja mpaka stendi ya Msanga, huku mfukoni nikiwa sina hata senti tano. Nilipofika, nilijichanganya na abiria wengine waliokuwa wakisubiri usafiri na moyoni nikawa najisemea liwalo na liwe!
Mara lilikuja gari, likateremsha abiria waliokuwa wakitoka mjini na kugeuza, abiria wote wakalikimbilia, na mimi nikajichanganya. Muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa nimepanda, tena nilifanikiwa kupata na siti, nikakaa huku nikiwa sijui nitamjibu nini kondakta atakapoanza kudai nauli.
Basi muda mfupi baadaye, safari ilianza. Mbele kidogo, kondakta alianza kukusanya nauli na alianza na abiria waliokuwa mbele, taratibu akawa anasogea kule nyuma nilikokuwa nimekaa, mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio. Aliendelea kukusanya nauli mpaka aliponifikia, akagongagonga safaru alizokuwa amezishika mkononi, kama wanavyofanya makonda wa daladala wanapodai nauli.
“Nitakupa mbele!” nilijibu kwa kujiamini, akanitazama usoni, na mimi nikawa ‘siriasi’ kisha akaendelea kuchukua nauli kwa abiria wa upande wa pili. Mbele kidogo, kuna abiria walikuwa wanashuka, basi akaacha kupokea nauli na kwenda kuwafungulia mlango.
Waliposhuka safari iliendelea, akarudi tena kuendelea kukusanya nauli na alipomaliza, alinigeukia tena.
“Hapoo!”
“Si nimekwambia nitakupa mbele?” nilijibu kijeuri, akanitazama tena kisha akarudi mlangoni. Safari iliendelea abiria wakawa wanashuka na kupanda na hatimaye tukawa tumekaribia Gongo la Mboto ambapo kimsingi ndiyo mwisho wa magari yanayotoka Pwani, akanifuata tena na safari hii, alikuwa amekuja kisharishari kabisa.
“Nitakupa wakati wa kushuka,” nilimwambia, akaona kama namletea masihara kwenye kazi. Akanikomalia nimlipe, na mimi nikawa nakomaa kwamba nitakupa wakati wa kushuka, zogo kubwa likaibuka kiasi cha kufanya abiria wengine waingilie.
Wengine walikuwa wananipigia kelele mimi kwamba nini kinachonizuia kumpa nauli yake? Wengine wakawa wanampigia kelele konda kwamba kwa nini asisubiri mpaka nitakapokuwa nashuka.
“Mimi hapa sina nauli lakini kuna ndugu yangu ananisubiri stendi, yeye ndiye atakayelipa,” nilisema katikati ya lile zogo, konda akazidi kuwa mbogo kiasi cha kufikia hatua ya kunikunja, tukaanza kuvutana.
Yeye alikuwa na mwili mkubwa na kimsingi ndiye aliyekuwa na haki, kwa hiyo alinidhibiti kisawasawa, abiria wengine wakawa wanamsihi aniachie lakini akakomalia kwamba hawezi kuniachia mpaka nilipe, ndani ya gari ikawa ni vurugu mtindo mmoja.
Tayari tulishawasili Gongo la Mboto, basi akanivuta kutoka pale kwenye siti na kuanza kunitoa nje huku akifoka kwamba nikamuoneshe huyo atakayenilipia nauli, vinginevyo atanikomesha. Niliogopa sana, nikawa hata sijui mwisho wangu utakuwa nini. Alinishusha huku akiwa bado amenikwida kwa nguvu, watu wakajaa, abiria wengine waliteremka kwenye gari na kuja kujaribu kutuamulia.
“Kwani unamdai shilingi ngapi jamani? Basi mimi namlipia,” alisema mama mmoja wa makamo huku akitoa noti ya shilingi elfu kumi, kwa hasira konda alinitingishatingisha, akanizibua kofi la nguvu na kunisukuma, nikapepesuka na kwenda kudondokea kwenye mtaro, wahuni wa stendi wakawa wanacheka huku abiria wengine wakianza kumjia juu konda kwamba kwa nini amenipiga wakati tayari msamaria mwema alishatoa fedha.
Pale nipodondoka, nilijikuta nikipandwa na jazba kali mno, ni kweli nilikuwa nimemfanyia uhuni lakini hakupaswa kunipiga na kunidhalilisha kiasi kile mbele za watu. Nikaokota jiwe na kunyanyuka kwa kasi ya kimbunga, hakuwa na habari na mimi tena, akawa anamhesabia yule mama aliyenilipia chenji.
Nilipenyapenya na kumfikia na bila kuuliza, nilimtwanga na lile jiwe kichwani kwa nguvu, damu zikaruka kwa wingi na watu wakaanza kupiga kelele, hapohapo nilijichanganya kwa abiria wengine na kuanza kutimua mbio. Hakukubali, akawa ananifukuza kama faru aliyejeruhiwa.
Je, nini kitafuatia?

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom